Mbali na kumaanisha uondoaji madarakani viongozi wa Serikali, hususan kwa kutumia nguvu, neno mapinduzi, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, pia lina maana ya mabadiliko ya haraka ya mbinu au hali, kwa mfano, katika kilimo, elimu nakadhalika.
Leo, Januari 12, Zanzibar inaadhimisha miaka 59 ya mapinduzi yalioiangusha Serikali ya mseto ya vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na kumaliza pia utawala wa kifalme katika visiwa hivyo.
Ni siku ambayo shughuli za kitaifa na kichama (kwa kusema chama, namaanisha Chama cha Mapinduzi – CCM), zitapambwa kwa kaulimbiu ya Mapinduzi Daima, ambapo viongozi watasema Mapinduziiiiii, na wafuasi wao wataitikia Daimaaaaaa!
Kwa bahati mbaya sana, siku hii mara nyingi hupita bila kufanyika kwa tafakuri pana ya safari ya miongo hiyo sita ambayo Zanzibar imekuwa jamhuri, hususan kwenye eneo la ustawi wa wananchi wa kawaida wa Zanzibar.
Ni kwa namna gani, kwa mfano, CCM na Serikali yake visiwani humo inatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Mapinduzi Daima, kwenye maeneo kama vile uchumi, elimu, sayansi na teknolojia, siasa na nyanja nyengine zinazoathiri maisha ya kila siku ya Mzanzibari?
Mbali na kuondokana huko na utawala wa kifalme, ni nini Mzanzibari wa kawaida leo hii, husasan wale waliozaliwa miaka ya 1980 au 1990, ambao habari za mapinduzi wamezisoma vitabuni, wanaweza kukiangalia na kuwa na fahari na tukio hilo la kihistoria?
Maisha ya Wazanzibari yameimarika kwa kiasi gani tangu utawala wa kifalme uondoke Zanzibar, au ndani ya miaka takriban 60 ya utawala wa CCM visiwani humo?
Jibu langu mimi, ambalo limejikita kwenye uzoefu zaidi badala ya utafiti, ni kwamba hali ya sasa ni mbaya zaidi kuliko ile aliyoiacha Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuliko ilivyo sasa.
Mnyonge mnyongeni …
Ni ukweli usiopingika kwamba kipindi cha miaka minane ya utawala wa Mzee Karume, hadi alipouawa 1972, kwa sehemu kubwa, kilikuwa ni kipindi cha hofu, ikiaminiwa kwamba wapambe walimpotosha, na hata kumtia wasiwasi, kwamba alikuwa na maadui.
Matokeo yake, vigogo kadhaa wa ASP, wengi wao wakiwa ni wajumbe wa baraza la kwanza la mawaziri, “walipotea” katika mazingira ya kutatanisha, hali iliyosadiki ule usemi kwamba mapinduzi hula hata watoto wake!
SOMA ZAIDI: Othman Masoud: Mapinduzi ya Zanzibar Siyo Milki Ya Wachache
Lakini, kama Waswahili wanavyosema, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Tukiyaweka kando yote hayo, Mzee Karume alifanya mengi linapokuja suala la kuboresha uchumi wa Zanzibar na ustawi wa watu wake.
Hata linapokuja suala la kisiwa cha Pemba, ambacho Serikali nyingi zilizofuatia zimekuwa zikikitenga, Mzee Karume alikiweka karibu sana, akichukua hatua kama vile kuwapeleka baadhi ya mawaziri wadogo wakafanyie kazi zao huko, akiwemo waziri mdogo wa elimu.
Tukiwa tunaadhimisha mapinduzi leo hii, tuna wajibu wa kujisomea historia ya kweli, na kuyadhukuru mazuri na mapungufu ya pande zote za kisiasa, vyenginevyo ni kuipinga historia.
Tukirudi kwenye kaulimbiu ya Mapinduzi Daima, ni lazima tujiulize ni kwa namna gani siasa za Zanzibar zimekuwa za kimapinduzi, zenye kulenga kuwanufaisha wananchi wa visiwa hivyo?
Kwa mtazamo wangu ni kwa kiwango kidogo sana, huku siasa zikigeuka za chuki na fitna na kuwaumiza Wazanzibari badala ya kuwanufaisha.
Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, aliingia madarakani baada ya uchaguzi wa 2020 huku jamii ikiwa imegawika sana, huku, kama ilivyo kwa chaguzi zote visiwani humo tangu 1995, madai ya wizi wa kura yalisindikizwa na machafuko ya kisiasa.
Uchaguzi huo, naweza kusema, uliyazima matumaini ya maridhiano yaliyotarajiwa.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), moja kati ya jaribio la kuzifanya siasa za Zanzibar kuwa za kimapinduzi, ikaingia majaribuni baada ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo kugoma kushiriki. Ni busara tu ya viongozi wake ndiyo zilizoikoa SUK visiwani humo.
SOMA ZAIDI: Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?
Mapinduzi Daima, kwa hiyo, yanamtaka Dk Mwinyi kumaanisha anachosema linapokuja suala la kutafuta maridhiano ya kweli visiwani Zanzibar.
Hiyo ni pamoja na kuacha kuwarejesha madarakani watu ambao rekodi zao zinaonesha hawafurahishwi na siasa za kimapinduzi, badala yake wanavutiwa na siasa za chuki, uhasama na mifarakano.
Nao viongozi wa upinzani, hususan wa chama cha ACT-Wazalendo chenye wafuasi wengi visiwani, wanapaswa kujipambanua zaidi na kuzingatia matarajio yaliyokuwepo wakati wa uongozi wa mwanasiasa mahiri hayati Maalim Seif Shariff Hamad badala ya kurudia hayo kwa hayo majukwaani.
Tutoke ndani ya boksi
Zanzibar inaadhimisha miaka 59 ya mapinduzi lakini wakati umefika kutoka ndani ya boksi. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutaweza kutokomeza uhasama wa miongo mingi na kufungua ukurasa mpya.
SOMA ZAIDI: Nini Hasa Kilipelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
Nihitimishe safu hii kwa kutoa wito kwamba ni muda muafaka sasa kwa Serikali ya Zanzibar na CCM kuitafsiri kaulimbiu ya Mapinduzi Daima tafauti, kwamba iwe ni kaulimbiu inayoipa Serikali morali ya kuwaletea maendeleo zaidi Wazanzibari.
Hii ni kwa sababu, kimsingi, kila hatua ya kuwaletea watu maendeleo katika elimu, afya, makaazi na ajira ni mapinduzi katika jamii.
Kung’ang’ania tafsiri ya kaulimbiu ya Mapinduzi Daima kwamba CCM Zanzibar ilishika dola kwa mtutu wa bunduki, na hivyo haiwezi kuiachia kwa sanduku la kura, ni kujiangamiza.
“Mapinduzi yana maana yake, na maana kubwa siyo ugomvi,” aliwahi kusema Amani Abeid Karume, Rais wa sita wa Zanzibar. “Mapinduzi ni uhuru wetu sote. Hakuna mwenye kumiliki mapinduzi.”
Ni ujumbe makhsusi, ujumbe mzito kwa jamii ya Wazanzibari. Tutafakari pamoja!
Mohammed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.