The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sekta Isiyo Rasmi Yadaiwa Kutokuwa Rafiki Kwa Wanawake wa Kitanzania

Licha ya kuwa na asilimia 60 ya nguvu kazi nchini sekta isiyo rasmi mazingira yake yamekuwa si wezeshi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Eliaika Mtui ni mama wa mtoto mmoja. Elimu yake ni darasa la saba. Mara tu baada ya kumaliza elimu hiyo, familia yake haikuwa na uwezo wa kumuendeleza kielimu hivyo aliaanza kufanya kazi za ndani ili kuweza kumudu gharama za maisha. 

Kutokana na kazi zake za ndani, Eliaika, 53, alifanikiwa kupata mtaji uliomuwezesha kuweza kuanza kufanya biashara akianzia biashara zake huko Arusha, akinunua nguo za mtumba na kutembeza mitaani kama machinga.

Mnamo mwaka 1999 Eliaika alihamia Dar es Salaam kwa ajili ya kuja kuendelea kufanya biashara zake, akianza kufanya biashara katika maeneo ya Manzese, kisha Urafiki na mpaka hivi sasa anafanya biashara Kariakoo, eneo maarufu la kibiashara jijini hapa.  

Biashara yake kubwa anayoifanya ni kuuza viatu. Mama huyu anapanga viatu pembezoni mwa barabara akisubiri wateja wanaopita njia waweze kununua.

Mnamo mwaka 2000, Eliaika alifanikiwa kumpata kifungua mimba wake ambaye amemlea na kumsomesha mpaka chuo kikuu bila mkopo wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na biashara hizo ndogo ndogo. Lakini pia amefanikiwa kujenga nyumba yake kwa kudunduliza kile akipatacho katika biashara. 

Mama huyu ni mmoja kati ya akina mama wengi waliopo maeneo mbalimbali nchini ambao ni sehemu ya watu wanaopatikana katika sekta isiyo rasmi, sekta ambayo licha ya kuwa na idadi kubwa ya Watanzania mazingira yake hayajawahi kuwa rafiki kwao mpaka hivi leo.

Akizungumza leo Januari 27, 2023, katika mdahalo ‘Morning Breakfast’ unaoandaliwa na taasisi ya Policy Forum, Eliaika alieza kuwa yeye kama mfanyabiashara mdogo ambaye yupo katika sekta isiyo rasmi haijawahi rahisi kufanya shughuli zake kutokana na mazingira na changamoto ambazo toka awali amekuwa akikabiliana nazo. 

“Hatuna sehemu rasmi za kufanyia biashara kwa sababu tunatoka sehemu moja tunaenda sehemu nyingine maana ni kukimbizana,” alisema mama huyo kwenye mjadala huo. 

“Kwa mfano, tulitoka Manzese tukapelekwa Urafiki, Urafiki mpaka ukaanze moja ina maana unatengeneza mahali pa kujikimu [kwanza] pakae sawa. [Mpaka] upange biashara kile kimtaji kinaisha wakati mtaji wetu sio mwingi,” alilalama mama huyo.

SOMA ZAIDI: Nini Kifanyike Kuboresha Mfumo wa Kodi 2023?

Eliaika alieleza kwamba wafanyabiashara wengi wadogo mitaji yao imekuwa ni kuanzia Sh100,000 mpaka Sh150,000, huku mara nyingi bidhaa zao zikichukuliwa na mamlaka za jiji kwa kile kinachodaiwa wanafanya biashara katika sehemu zisizo rasmi. 

“Wanasema ni viongozi wa wamachinga, kwa hiyo wanachukua vitu vyetu ina maana kwenda kuvikomboa tena kule mpaka utoe hela au vingine vinapotea, kama wanachukua hatuwezi kujua lakini kwa kukomboa unakuta wanakwambia toa Sh50,000 [au] toa Sh20,000,” anasema Eliaika.

Mama huyo alienda mbali zaidi na kubainisha kuwa hata wakati wa ugawaji wa meza kwa wafanyabiashara katika eneo la Karikaoo wao ambao ndiyo walengwa wanaotakiwa kuzipata wamekuwa hawapati meza hizo. 

Badala yake viongozi wao ndiyo huzipata na kuanza kupangisha kwa gharama ambazo ni vigumu sana kwo kuweza kuzimudu. 

“Hata wale waliopangiwa zile meza mimi naona ni wale wanaojiita viongozi na wale viongozi ina maana wamepangisha siyo wao wanaofanya biashara,” alisema Eliaika. “Wanakuja wanakwambia tunapangisha 150,000 sasa kama unauwezo wanakwambia miezi sita unalipia ndiyo unafanya biashara.”

“Walengwa kama walengwa wale ambao wanapanga chini kabisa, au wenye kupewa zile meza, hawapewi ina maana wale viongozi unakuta wanachukua zile meza wanajimilikisha halafu wanapangisha,” alieleza mama huyo.

Tatizo ni nini?

Dominic Ndunguru ni Mkurugenzi Mtendaji wa Open Mind Tanzania, taasisi inayofanya kazi na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi. 

Akizungumza wakati wa mjadala huo unaofanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, Ndunguru alisema kwamba licha ya kwamba asilimia 60 ya nguvu kazi nchini inapatikana katika sekta isiyo rasmi sekta hiyo haijaweza kukua kutokana na sababu kadhaa.

SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Ajenda Kuu ya Wakulima Wadogo Wanawake Barani Afrika

“Moja ya sababu hizi ni ukosefu wa mazingira yaliyobora ya kufanyia biashara,” alisema Ndunguru. “Hili mama [Eliaika Mtui] amelieleza vizuri sana, ambacho ni kitu kikubwa sana kinawakumba wafanyabiashara wengi.”

“Namba mbili ni kutambuliwa pamoja na mikopo, biashara nyingi bila kukopa [haiwezekani] kutoka kiwango kimoja kwenda kiwango kingine. Ni ngumu kwa kutegemea tu mtaji wako binafsi kufanikiwa hapo.

“Namba tatu ni siasa. Siasa pia imekua ikiathiri sana masuala ya sekta isiyo rasmi, hasa kuna ule msemo usinigusie wapiga kura wangu. Sasa hii pia imekuwa ni changamoto pia hata kwenye kuongeza mapato wakati mwingine Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapanga mipango ya kuweza kutanua mapato lakini mwanasiasa fulani anaona hawa watu wangu wakianza kubanwa kidogo itakuwa changamoto.

“Mwisho ni suala la sera na mifumo tumeona kuna huo mkanganyiko wa machinga ni nani, sekta isiyo rasmi ni nani, mjasiriamali ni nani,” alisema Ndunguru.

Mipango ya Serikali

Judith Matage ni Afisa Biashara kutoka Manispaa ya Temeke ambaye alisema kwenye mjadala huo uliofanyika katika Hoteli ya Four Points by Sheraton kwamba Serikali inatambua mchango wa sekta isiyo rasmi na imekuwa ikiwekaa mazingira mazuri yatakayohakikisha yanawakomboa wanawake na makundi mengine yaliyopo katika sekta hii.

“Serikali kuanzia ngazi ya taifa mpaka ngazi ya Serikali za Mitaa imekuwa ikifanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kwamba kwanza inamtambua na inamkwamua mwanawake,” Matage.

SOMA ZAIDI: EAC Yatakiwa Kuboresha Sera, Sheria Kusaidia Wajasiriamali Wanawake Mipakani

Matage anatolea mfano wa jitihada zinazofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake Jinsia na Makundi Maalumu kuanzia katika bajeti zake kwani imekuwa ikitenga fungu kwa ajili kutoa mikopo ili kuwakwamua wanawake wanaopatikana katika sekta isiyo rasmi.

“Lakini pia hii Wizara [ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake Jinsia na Makundi Maalumu] ukiangalia mwaka huu wa 2022/2023 ilitenga Shilingi milioni 600 kwa ajili ya kutoa hii mikopo kwa wajasiriamali. Ikatenga bilioni 45 kwa ajili ya kuwaundia miundombinu ya kuwawezesha wamachinga.

“Bado ikaja ikatenga Shilingi milioni 107 kwa ajili ya kuwafunza wale viongozi wa wamachinga lakini ukija mpaka ngazi ya Serikali ya mtaa kila halmashauri huwa inatenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kina mama, vijana na walemavu,” alisema Matage.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *