The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jinsi Sakata la Ndizi Kuzuiliwa Kuingia Zanzibar Lilivyoibua Mjadala wa Muungano 

Tukio hili limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii, huku watu mbalimbali akiwemo mfanyabiashara ambaye ndizi zake zilikamatwa wakihoji muktadha mzima wa Muungano.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Katika hali ya kushangaza ndizi zimeweza kuibua mjadala wa muda mrefu wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Ndiyo, ndizi hizi hizi za kula. Wakati mijadala mingi ya Muungano huwa mikali kwa upande wa Zanzibar, wakati huu mjadala umekuwa mkali zaidi upande wa Tanzania Bara.

Sakata zima lilianza Februari 1, 2023, pale Veronica Mwanjala, mfanyabiashara mdogo aliyesafirisha ndizi tenga 30 kutoka Tanzania Bara kuelekea Zanzibar, kutoa malalamiko kuwa mamlaka za Zanzibar zimekamata mzigo wake wa ndizi visiwani humo.

Taarifa za mfanyabiashara huyo zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, akilalamika: “Nilipata tenda kwenye hoteli mbili Zanzibar, lakini badala yake nilizuiliwa bandarani.”

Baada ya mzigo wa Veronica kuzuiliwa aliambiwa arudi Februari 2, 2023, ambapo alikutana na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Mifugo na Biashara wa Zanzibar, Shamata Shaame Khamis aliyefika bandarini. Baada ya mahojiano, Veronica aliruhusiwa kuchukua ndizi zake pamoja na kulipa faini ya Sh50,000.

Hata hivyo, Veronica anadai kwamba mambo hayakwenda sawa baada ya makubaliano hayo na Waziri kwani afisa aliyekuwa akisimamia jambo hilo pale bandarini hakumruhusu aondoke na ndizi hizo kwa kushikilia msimamo wa kuwa ndizi kutoka Bara haziruhusiwi kuingia Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Shamata alithibitisha kutokea kwa tukio hili na kueleza kwamba zuio la mazao ya migomba toka bara lipo toka mwaka 2017.

“Uhitaji [wa ndizi] upo ila kwa mujibu wa sheria zilizopo haturuhusu kuingiza ndizi kwa sababu ya kuzuia ugonjwa ulioshambulia migomba [ya Tanzania bara],” amesema.

Khamis alienda mbali zaidi akieleza kuwa Veronica hakuwa na kibali chochote cha kuingiza ndizi kutoka Tanzania Bara na hakutoa ushirikiano wa kutosha kwa mamlaka pale walipomhitaji ama azirejeshe Tanzania Bara au ziharibiwe huku akishuhudia.

Mjadala wa muungano

Tukio hili limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii, huku watu mbalimbali akiwemo mfanyabiashara Veronica wakihoji muktadha mzima wa Muungano.

“Nalalamika na ninapata shida kwamba hii ni nchi moja yenye Muungano,” Veronica alisikika akiongea katika video iliyokuwa ikisambaa katika mtandao wa Twitter.

“Kama ndizi za Bara zinapigwa marufuku Zanzibar, nini maana ya muungano?” Aliuliza mmoja wa watumiaji wa mtandao wa Twitter kwa jina la DevotaTweve.

Wadau wengine wameendelea kusambaza tangazo la kuzuia ndizi kutoka Tanzania Bara.

“Mmeenda mkakamata ndizi mtu anaweza hisi ni kitu kikubwa kumbe ni ndizi tu, magendo yanatoka wapi Tanganyika na Zanzibar yaani Tanzania?” anauliza mtumiaji  mwingine wa mitandao kwa jina la DennisBenedict.

Akiongea na waandishi wa habari Hawa Ahmad Iddi, ambaye ni mkaguzi wa mazao na karantini Bandari ya Malindi Zanzibar, anasema ni tatizo la ‘mawasiliano’ baina ya mamlaka za Zanzibar na Tanzania bara juu ya vitu gani hasa vinazuiliwa.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *