Zanzibar. Mchoraji wa vibonzo mashuhuri nchini Tanzania Masoud Kipanya amesema hawezi kusema kwa asilimia 100 kama yuko huru kutekeleza sanaa yake hiyo, akibainisha kwamba akiamua kuwa huru kabisa “basi tutagombana [na] tutaudhiana” na watu mbalimbali.
Kipanya, ambaye jina lake halisi ni Ali Masoud, amesema hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hivi karibuni kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii.
“Kwenye nchi kama hii ya kwetu ambayo ndiyo kwanza inaendelea, bado kuna mambo mengi [ambayo] bado hayako sawa,” Kipanya, ambaye pia ni mtangazaji wa redio, alisema kwenye mahojiano hayo.
“Na hayako sawa kwa sababu kuna mazingira bado hayako sawa kwa sababu bado hatuko makini [kama nchi],” aliongeza msanii huyo ambaye vibonzo vyake vingi ni vya kisiasa.
“Kibinaadamu woga huwezi kuacha kuwa nao [kwenye kazi zako] kwa sababu lengo siyo kumtukana mtu, au kumdhalilisha mtu, lakini inapolazimika kutoa mchango wangu kwenye kulisema jambo kwa faida ya watu wengi, nalisema,” alisema Kipanya.
Akijibu swali ni wapi anapopata mawazo ya vibonzo vyake kwenye mahojiano hayo, Kipanya alisema mawazo yake yanatokana na maisha ya kidunia kwa ujumla wake, ndani na nje ya Tanzania.
“Kwa hiyo, ninachofanya mara nyingi huwa natoa mawazo kwenye maisha yetu ya kila siku ambayo tunayaishi, [huko] ndiko ambako napata mawazo ya katuni [zangu],” alisema mwanasanaa huyo aliyejipatia jina la ‘Kipanya’ kutokana na vibonzo vyake.
SOMA ZAIDI: BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania
Akiwa mmoja kati ya wachora vibonzo wenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania, vibonzo vya Kipanya, ambaye hupenda kujitambulisha kama mwana-umajumui wa Kiafrika, hufuatiliwa na watu wengi wanaoburudika na kuelimika kwa vibonzo hivyo.
Hata hivyo, kama kuna kitu kimoja kuhusu Kipanya ambacho mashabiki wake wengi wanaweza kukiri kuhusu yeye ni uwezo wake wa kuzificha jumbe za vibonzo vyake na kuiacha hadhira yake kwenye taharuki ya kujaribu kuzing’amua.
Kwenye mahojiano yake hayo na The Chanzo, Kipanya alisema hicho ni kitu anachokifanya kwa kukusudia ili kuchochea uwezo wa watu kufikiria.
“Sababu ya kwanza kubwa [ya kufanya hivyo] ni kupenda kufikirisha [watu] kwa sababu mimi naamini taifa lolote la watu ambao hawafikiri, natoa tu mfano, sisemi kwamba Tanzania hawafikiri, hapana, lakini jumuiya yoyote ile ya watu ambao hawataki kufikiria, basi ni rahisi kupata matatizo, ndiyo maana wanasema mwisho wa uwezo wako wa kufikiria ndiyo mwanzo wa matatizo yako,” alisema Kipanya kwenye mahojiano hayo.
SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?
“Nakumbuka juzi kuna utafiti ulikuwa umefanywa, ulikuwa unapima umri wa vijana kati ya miaka 13 hadi 16 hivi, walikuwa wanaangalia uwezo wa watu kufikiria, kutatua matatizo yao, kwa sababu ili utatue tatizo ni lazima uwe na uwezo wa kufikiria, tatizo linapokuja unalikabili na kulichukua vipi? Unalitafakari vipi? Unalichanganua vipi? Mpaka unakuja unatoa jawabu,” aliongeza Kipanya.
SOMA ZAIDI: Je, Serikali Inaifahamu Dhana ya Utamaduni Anuai?
Kipanya anaeleza kwamba kulingana na maisha ya binadamu yalivyo, kila tatizo linaloletwa lina suluhu yake lakini ni watu wachache, kwa maoni yake, wana uwezo wa kupata suluhu ya matatizo yao.
“Kwa hiyo, katuni ni moja kati ya vitu ambavyo vinachochea kutaka kufikiria,” anasema mchora vibonzo huyo. “Kitendo cha kujiuliza huyu hapa anamanisha nini ni mwanzo wa mchakato wa tafakuri.”
Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia najomar@live.com.