The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Saïd Hassane: Mbuyu wa Kikomori Umeanguka

Mwanaharakati huyo wa ukombozi wa bara la Afrika aliaga dunia hapo Disemba 2, 2022.

subscribe to our newsletter!

Mnamo siku ya Ijumaa, Disemba 2, 2022, Umoja wa Umajumui Mamboleo wa Afrika Huru yenye Mamlaka Kamili tulipokea kwa huzuni kubwa sana na majonzi yasiyo kifani habari za kifo cha Saïd Hassane Mohamed Jaffar Elmacelie kilichotokea nyumbani kwake Paris, Ufaransa.

Kifo cha shujaa huyu aliyekuwa mstari wa mbele katika nyanja zote za mapambano ya ukombozi wa kitaifa ni pigo kubwa sana kwa vuguvugu la harakati za ukombozi wa kifikra na mawazo katika visiwa vya Komoro.

Kama wanavyoeleza wanaharakati wenzake waliokuwa karibu naye sana, marehemu ameacha kwa kila mmoja wao urithi wa somo la uongozi wa kweli, ulio thabit, uliojengeka katika misingi ya uadilifu, uwazi, heshima, kujitolea, na uvumilivu.

Lakini ni nani hasa alikuwa Saïd Hassane Mohamed Jaffar Elmacelie? 

Alikuwa ni mwanaharakati ambaye mwelekeo wa mapambano yake umethibisha siku zote msimamo wake wa kusimama na kutetea ukweli, haki na uhuru.

Msanii aliyejitolea

Tokea mapema katika utoto wake, Saïd Hassane alianza kujitokeza kwa kuonyesha vipaji vyake kama msanii aliyejitolea. Wakati akiwa bado yuko skuli ya sekondari, Saïd Hassane alianzisha kikundi cha kwanza cha muziki wenye mahadhi ya Blues.

Haya yalitokea katika miaka ya 1960-1970, wakati wa kufunguka milango na kuingia nchini tamaduni mpya za kisasa. 

Akiwa anajitayarisha kufanya mtihani wa shahada ya mwisho wa masomo ya sekondari katika fani ya fasihi, katika skuli ya sekondari ya pekee iliyokuwepo visiwani Komoro wakati wa utawala wa kikoloni wa Kifaransa, Saïd Hassane alionesha mapenzi yake makubwa kwa muziki wa kisasa na wa kitamaduni. 

Alidhihirisha kipaji chake kwa kuweza kupiga ala mbalimbali, na kujishajihisha na uanzishwaji wa vikundi vyengine vya muziki. Ni katika wakati huu ndipo alipopewa, kwa mapenzi makubwa, jina la utani la Body.

Kufuatia uhuru wa visiwa vya Komoro, kwa agizo la Serikali ya Kisoshalisti iliyokuwepo madarakani wakati huo (iliyohamasishwa na fikra za kimapinduzi za Umajumui wa Kiafrika za Mwalimu Julius Nyerere), Saïd Hassane alitunga nyimbo ya taifa ya Komoro ambayo alimpa Abou Chihabi, mmoja kati ya wafuasi wake makini kabisa katika muziki, kuipiga. 

SOMA ZAIDI: Azali wa Comoro Anavyoendelea Kumdhibiti Rais wa Zamani Sambi Kifungoni

Pendekezo lake lilikubaliwa kwa shauku kubwa sana na Serikali mpya iliyokuwepo madarakani!

Katika miaka ya 1990, Saïd Hassane alianzisha katika jamii ya Wakomoro wa Ughaibuni Chama cha Wasanii wa Kikomoro kilichowashirikisha wasanii wakubwa wenye hadhi ya kimataifa kama vile Nawal, Gam Gam, El Badawi na wengineo.

Kwa pamoja, wakishajihishana na kutilia mkazo ushirikiano baina ya wasanii, kupiga

pamoja, na kupeleka mbele mshikamano kwa maslahi mapana ya jamii. 

Kutokana na matokeo ya kazi zao za usanii, Saïd Hassane alijidhihirisha kuwa mtu aliyevutiwa na muziki wa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, mtaalamu wa muziki na ala za muziki za Kikomoro, Bukini na Afrika Mashariki.

Msomi wa mstari wa mbele

Mnamo mwaka 1975, kufuatia uhuru wa visiwa vya Komoro na wito wa Rais msoshalisti Ali Soilihi Mtsachiwa, Saïd Hassane, akiwa mwandishi wa habari kijana, alikubali kuchukuwa jukumu la kuiongoza idhaa ya kimataifa ya Redio Komoro. 

Mpaka kufikia hapo, urithi aliouacha unaendelea kuonekana na kutambulika katika mbinu za kufanyia kazi na mikakati ya ushirikiano iliyolenga nchi za Afrika na Kambi ya Kisovieti (ya wakati wa USSR).

Wakati mtandao wa hujma wa Françafrique ulipofanikiwa kuyazima mapinduzi machanga ya visiwa vya Komoro kwa kumtumia mamluki Bob Denard kumuuwa Ali Soilihi, Saïd Hassane aliamua kuhajir na kuhamia nchini Ufaransa, ambako aliendelea na kazi yake ya uandishi wa habari kupitia vyombo na taasisi mbalimbali za habari. 

Taarifa zake katika medani za kisiasa na kijiografia ziliwasisimua wengi. Kwa miongo mingi, Saïd Hassane alikuwa maarufu kama mwandishi mahiri aliyejitolea, mwenye ujuzi wa hali ya juu wa masuala nyeti ya kimkakati wa kijiografia na kisiasa wa visiwa vya Komoro. 

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?

Saïd Hassane alijitokeza waziwazi kuonesha msimamo wake mkali dhidi ya fikra zenye lengo la kuvigawa visiwa vya Komoro, upotoshaji wa historia, mbinu za udanganyifu kwa lengo la kuurudisha ukoloni na dhidi ya ujanja wa mtandao wa hujma wa Françafricain kutumia watu kuiyumbisha nchi, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kisiasa.

Mnamo mwaka 1999, wakati wa kesi ya mamluki Bob Dernard iliyosikilizwa mjini Paris dhidi ya mauaji ya Rais Ahmed Abdallah, Saïd Hassane aliwashajihisha vijana wa Kikomoro wajitokeze kwa wingi mahakamani, kama alivyosema, ili waweze kuujuwa ukweli kwa kila ncha wa mauaji ya kisiasa.

Saïd Hassane hakusita kumshutumu vikali dhalimu Denard na kuikebehi kwa nguvu zake zote kashfa ya kesi iliyopangwa ili kumwachia huru “mamluki wa Jamhuri [ya

Ufaransa].”

Mpambanaji katika nyanja zote

Mchango mkubwa wa Saïd Hassane unaonekana zaidi katika medani ya mapambano ya kijamii na kisiasa. Alikuwa mwanaharakati aliyekuwa mstari wa mbele katika mapambano yote, nguzo isiyopingika ya jumuia za kiraia za kikomoro katika harakati zake za ukombozi.

Mnamo mwaka 1996 kulifanyika harakati za kuleta mwamko katika jamii dhidi ya hukumu ya kifo. Saïd Hassane alikuwa mstari wa mbele katika kuanzisha jumuia

mahsusi SOS-DEMOCRATIE na kusimamia mchakato wa kuanzishwa jarida lake la habari

Democratie-Infos.

Chombo ambacho kimejielekeza zaidi katika kutetea haki za kidemokrasia, na kuwa sehemu muhimu ya rejea, kama anavyopenda kukumbusha rais wake Abdourahmane Abana.

Mnamo mwaka 1998 kulifanyika harakati za kuwashajihisha wasomi watwania dhidi ya njama za kujitenga kwa kisiwa cha Nzuwani, zilizochochewa na vitimbakwiri vya Françafrique. 

Saïd Hassane alishiriki katika kuasisi jumuia mahsusi ya FRATERNITE COMORIENNE bega kwa bega na Profesa Ahmed Mohamed-Chamanga, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kutisha! 

Saïd Hassane alitumia nguvu zake zote kuwashajihisha wanadiaspora wa Kikomoro wamuunge mkono Chamanga katika mapambano yasiyo na uwiano. 

Juhudi zake zilizaa matunda kwani leo hatari ya kujitenga imetoweka. Hata hivyo, bado imebaki ni hatari ambayo inaweza wakati wowote ikawashwa upya na maadui wa umoja na mshikamano wa visiwa vya Komoro. 

Hatimaye, katika miaka ya 2005-2006, wakati jumuia za kiraia zilipoanza kupata nguvu na ufanisi katika harakati zao za kupigania na kulinda umoja wa mipaka, usiogawika, wa visiwa vya Komoro (katika mukhtadha wa uvamizi na ukaliwaji haramu wa kimoja katika visiwa vya Komoro, kisiwa cha Mayotte, na Ufaransa tokea mwaka 1976), Saïd Hassane alikuwa miongoni mwa waasisi wa Collectif Comores Masiwa Mané, taasisi iliyosimamia dhana muhimu kwamba nchi ya Komoro, kisheria, imeundwa na mkusanyiko wa visiwa vinne vikubwa.

Tokea mwaka wa kwanza wa kuundwa kwa taasisi hii, Saïd Hassane aliweza kuja na pendekezo la sheria iliyopitishwa na Bunge la Komoro, kuifanya Novemba 12 ya kila mwaka kuwa siku rasmi ya sikukuu ya kitaifa (ni siku ambayo visiwa vya Komoro Huru vilikubaliwa rasmi kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa, kufuatia Azimio la Umoja wa Mataifa.

Harakati za kimataifa

Baadaye, Saïd Hassane aliongoza kikundi cha ushirikiano wa pamoja kufanya kazi na taasisi na mashirika rafiki katika medani ya kimataifa. Hii ilipelekea

kuasisiwa kwa Kamati ya Kulinda Mipaka, Uhuru na Mamlaka Kamili ya Visiwa vya Komoro au Collectif de Défense de l’Intégrité et de la Souveraineté des COMORES (CDISCOM), kwa Kifaransa.

Kamati hii ilibeba na kuwakilisha nje ya visiwa vya Komoro, suala la ukombozi wa kisiwa cha Mayotte kutoka katika makucha ya ukoloni wa kifaransa, pamoja na lile la kuzitetea tunu za uhuru kamili wa visiwa vya Komoro. 

Kwa ajili ya kumbukumbu ya historia, jina hili lilipendekezwa wakati wa kikao cha pamoja

na rafiki Rock Wamytan, wakati huo akiwa Rais wa Chama cha Kisoshalisti cha Ukombozi wa Kitaifa wa Kanaky, Front de Libération National Kanaky Socialiste (FLNKS).

Saïd Hassane alibakia kuwa jungu kuu la mawazo ndani ya CDISCOM, iliyokuwa ikikusanya ndani yake viongozi wa taasisi na vyama vya kisiasa vilivyokuwa vikipinga ubeberu. 

Alikuwa na satwa kubwa ndani ya jumuia hii na kuweza kutoa uongozi thabit, ulio makini na usioyumba katika jamii, uliochanganyika na unyenyekevu, upeo mkubwa wa kuona na

kufahamu mambo, uwazi na ukarimu. 

Jumuiya ya CDISCOM inabeba mpaka leo kauli mbiu yake, iliyojengeka katika msemo maarufu unaotumika kuhitimisha machapisho yake mengi kwenye vyombo vya habari, inayoeleza kama ifuatavyo: Umoja wa kitaifa hauna mjadala, mipaka ya nchi haibadilishiki, na uhuru na mamlaka ya taifa hayawezi kuchezewa au kununuliwa kwa pesa.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Chini ya uongozi wake, na kufuatia kwa maelekezo yake ya kimkakati, vyombo vyengine vipya vya harakati vilichipuka kama vile COMITE MAORE, SULUHU, UKOMBOZI na kadhalika na kufanya kazi kwa pamoja ya kulinda uhuru na mamlaka kamili ya visiwa vyote vya Komoro.

Saïd Hassane alijitokeza na kuthibitisha katika maisha yake kuwa ni mtoto aliyechukuwa mguu wa babake, Mheshimiwa Said Mohamed Jaffar, kiongozi aliyetoa hotuba ya kuviingiza visiwa vya Komoro katika Umoja wa Mataifa hapo Novemba 12, 1975.

Pole na rambirambi

Wakati huu ambapo mpambanaji huyu wa aina yake, wa kupigiwa mfano, wa ukombozi wa Afrika ameiaga dunia hii kwenda kuungana kwa heshima na taadhima na wazee waliotangulia mbele ya haki, sisi, jumuia, vyama vya siasa na wanachama wa Umoja wa Umajumui Mamboleo wa Uhuru na Mamlaka Kamili ya Afrika, au l’Organisation Néo Panafricaniste de Souveraineté (ONS): 

Tunatoa, kwa dhati ya moyo wetu, mkono wa pole na rambirambi kwa aila ya marehemu pamoja na ndugu na jamaa zake na kuwahakikishia kwamba tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.

Tunatoa heshima zetu zote na kumkumbuka, kwa dhati ya nyoyo zetu, mzalendo huyu mkuu, mpambanaji asiyechoka wa uhuru wa Afrika.

Tunaamini kwamba Saïd Hassane ametoa mchango wake mkubwa usio na kifani na wa kupigiwa mfano katika harakati na anastahili kusherehekewa kitaifa na miongoni mwa wanaharakati wa ukombozi wa Afrika.

Tunamuombea awe katika waja wa darja ya juu ya utukufu, apate malazi mema na amani katika makaazi yake ya milele, kiumbe huyu aliesabilia maisha yake yote hapa duniani katika harakati za kuwakomboa binaadamu wenzake kutoka katika minyororo ya mabeberu na vitimbakwiri vyao.

Tunawaomba wanaharaki wa Peoples of Global Africa kumuadhimisha leo, kesho na daima. Buriani, Body, Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako na akulaze mahala pema peponi!

Salamu hizi zilichapishwa kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kifaransa na Umoja wa Umajumui Mamboleo wa Uhuru na Mamlaka Kamili ya Afrika. Zimechapishwa tena hapa kwa Kiswahili kufuatia ombi la umoja huo. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *