Mwanza. Katika mwalo* wa Mswahili jijini hapa, wanawake kadhaa wanaweza kuonekana wakishiriki kikamilifu katika zoezi linalolenga kuwanufaisha na faida zitokanazo na Ziwa Victoria, moja kati ya maziwa makubwa barani Africa, hususan kupitia uvuvi.
Kwa mtu yoyote anayefika hapa kwa mara ya kwanza, kitu cha kwanza atakachokiona ni wanawake, wa rika mbalimbali, wakishiriki katika uchakataji ambapo hupokea dagaa kutoka ziwani na kuwasafisha kabla ya kuwaanika.
Wanawake hawa huja hapa kila siku ya wiki, wakilazimika kuingia ziwani, muda mwengine maji yakiwafikia shingoni, ili kufuata dagaa na samaki, bidhaa zinazowasaidia kuendesha maisha yao na kuwawezesha kuhudumia familia zao.
Miongoni mwa wanawake hawa, The Chanzo inamuona Fatuma Swalehe, mama mfupi kwa kimo anayeonekana kuwa na umri wa miaka 60, akianika dagaa juani. Fatuma anasema anakuja hapa kila siku kuanzia saa 12 asubuhi na kuondoka saa moja jioni.
SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu
“Boti zinaweka nanga mbali sana, wanawake tunafuata dagaa na samaki mpaka huko, tunaloana hadi sehemu zetu za siri,” Fatuma alilama kwa mwandishi wa makala haya.
“Kina mama hapa mwaloni tunaenda maji ya mbali kutafuta samaki,” anaongeza mama huyo. “Unakuta mtumbwi wenye samaki wazuri upo mbali, inamlazimu [mwanamke] afike maji ya shingo.”
Fatuma ni moja tu kati wa wanawake wengi hapa walioamua kuvunja miiko na kuingia kwenye kazi ambayo kwa miaka mingi ilikuwa inatawaliwa na wanaume.
Ni wanawake ambao wameamua kukabiliana na changamoto mbalimbali ili kujenga maisha ya kujitegemea.
Mbali na uwepo wa akina Fatuma ambao kwa kiasi kikubwa hujikita kwenye uchakataji, wapo pia wanawake wanaomiliki boti zinazokwenda ziwani kufanya shughuli za uvuvi.
Hawa ni pamoja na Mwaka Juma anayefanyia shughuli zake katika kisiwa cha Gembele, moja kati ya visiwa kadhaa vinavyozunguka Ziwa Victoria.
Lakini wakati akina mama hawa wanajivunia jitihada zao zinazolenga kuwakomboa kiuchumi, kitu kimoja kinachojitokeza kwa dhahiri unapozungumza nao ni changamoto nyingi wanazozipitia na ambazo zinatishia kuwarejesha nyuma.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
Moja kati ya changamoto kubwa ambayo The Chanzo iliigundua, hususan kwa akina mama wenye boti ni kutokuwa na uwezo wa kuzipeleka ziwani boti hizo kwa uvuvi bila ya kuwashikirikisha wanaume.
Wanawake hawa hulazimika kuingia mkataba na wanaume ili kuifanya boti iweze kufanya kazi na mwisho wa siku kugawana kilichopatikana.
Hata hivyo, mpangilio huu kwa kiwango kikubwa huwaathiri wanawake na kuwanufaisha wanaume.
Pia, kuna hatari ya kuibiwa wavuvi ambapo muda mwingine wavuvi wanaowatumia wanaweza kuhongwa na mmiliki mwingine wa boti na wakawaacha akina mama hao na boti zao.
Lucy Kiranga ni Afisa Jinsia na Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Wanawake kutoka Shirika la Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi (EMEDO) lenye makao makuu yake jijini Mwanza.
Kutokana na kazi ambazo EMEDO imekuwa ikizifanya na wanawake hao, Kiranga anasema kwamba upatikani wa rasilimali kwa akina mama hao imekuwa ni changamoto kubwa na ya siku nyingi.
Kuna changamoto nyengine pia ambazo Kiranga anasema ni kubwa zaidi na zenye kutishia usalama na ustawi wa wanawake hao.
“Akina mama wanabakwa, wanachinjwa, wanaporwa pesa. Kuna kesi ya Bukoba mama alikatwa koromeo,” alisema afisa huyo. “Ilibidi viundwe vikosi maalumu vya ulinzi, na mwalo kuanza kufunguliwa muda wa kawaida na siyo usiku usiku.”
SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni
Kaimu Afisa Mfawidhi Kitengo cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Victoria katika Ofisi za Maliasili mkoa wa Mwanza Hamadi Stima aliiambia The Chanzo ilipotembelea ofisini kwake kwamba wanawake hao wanakibiliana na changamoto nyingi ambazo wao kama ofisi wanazitambua.
Kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanawake kwamba wamekuwa wakidhalilishwa na wanaume, ikiwemo kutolewa lugha chafu za matusi, na madai ya wavuvi kuegesha vyombo mbali ili waweze kuona maungo wa wanawake, Stima alisema hilo linaweza kutatuliwa kwa njia ya sheria.
“Ngazi za wilaya zinatakiwa waweke sheria kwamba kila mtumbwi ni lazima uguse nchi kavu ili kuweza kupunguza ghasia wanazopitia kina mama za kuingia kwenye maji,” alisema afisa huyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ilemela Sitta Singibala akizungumza na The Chanzo alisema kwamba changamoto wanazopitia wanawake watakuwa wanasaidiwa kama wavuvi wengine.
“Hizo changamoto zinawahusu wavuvi wote,” alisema Sitta. “Lakini sisi kama Halmashauri, huduma zozote wanapewa kama wavuvi wengine wa kiume. Kwa sababu hizo shughuli mtu anakuwa ameamua kufanya mwenyewe.”
*Sehemu ambayo shughuli za uvuvi hufanyika.
Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com.