Search
Close this search box.

Utafiti wa Kijenetiki Wabainisha Asili ya Waswahili wa Afrika Mashariki

Waswahili wa Afrika Mashariki wanatokana na mwingiliano kati ya wanawake wa Kiafrika na wanaume kutoka Iran na India, watafiti wasema.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Utafiti wa vinasaba vya karne nyingi umebainisha asili ya Waswahili wa mwambao wa Afrika Mashariki, ukionesha kwamba mchangamano wa ustaarabu miongoni mwa watu hao umetokana na, kwa kiwango kikubwa, mchanganyiko kati ya wanawake wa Kiafrika na wanaume wa Persia, ambayo ni Iran ya sasa.

Kwenye utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la Nature, watafiti walichambua vinasaba vya watu wapatao 80 kutoka maeneo matano tofauti nchini Tanzania na Kenya, vinasaba ambavyo umri wake ni kuanzia takriban miaka 1250 mpaka 1800, Baada ya Kristo (BK).

Zaidi ya nusu ya vinasaba vilivyokutwa kwenye watu hao vilionesha wanatokana na wanawake wenyeji wa mwambao wa mashariki wa Afrika, huku mchango mkubwa pia wa vinasaba hivyo ukitoka bara la Asia, ambapo asilimia 90 vilitokana na wanaume kutoka Iran na asilimia 10 kutoka India.

Baada ya mwaka 1500 BK, sehemu kubwa ya vinasaba kutoka bara la Asia vilitokana na vyanzo vya Kiarabu, utafiti huo uliofanywa na watafiti kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali duniani umehitimisha.

Mwambao wa Waswahili wa Afrika Mashariki unaanzia mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kwa upande wa kaskazini, mpaka kisiwa cha Kilwa, nchini Tanzania, kwa upande wa kusini. Pia, hujumuisha sehemu za Kenya na Malawi na visiwa vya Zanzibar na Comoro.

Waswahili wa zamani kutoka kwenye miji kama Mombasa na Zanzibar walisafirisha bidhaa kutoka sehemu za ndani za Afrika kama vile pembe za ndovu, dhahabu pamoja na watumwa kwenda vituo mbalimbali katika Bahari ya Hindi. 

Pia, wanatajwa kuwa Waislam wa kwanza miongoni mwa Waafrika kusini mwa Jangwa la Sahara. 

Esther Brielle, mwanajenetiki kutoka Chuo Kikuu cha Harvad na mmoja wa watafiti kwenye utafiti huo anasema kwamba uwepo wa upendeleo wa kijinsia kwenye mchanganyiko kati ya watu wa Afrika na wa Asia kunaibua maswali juu ya mipangilio ya kijamii na majukumu ya kijinsia yaliyokuwepo zama hizo.

SOMA ZAIDI: Sifa Kedekede Zamwagwa Dunia Ikiadhimisha Siku ya Kiswahili

“Kwa upande mmoja, una wanaume kutoka Persia [Iran] wakichanganyikana na wanawake wa Kiafrika, kitu kinachoweza kuonesha kukosekana kwa usawa wa kijinsia, huku kundi la wanawake likionekana kuwa na hadhi ya chini,” Brielle alinukuliwa na mtandao wa Reuters akisema. 

“Hata hivyo, katika hili, kwa sababu watu wa Kibantu kutoka Afrika Mashariki mara nyingi huegemea umamani, inaonekana wanawake wa Kiafrika walikuwa na uhuru zaidi wa kuchagua wenza wao wa kuanzisha nao familia,” aliongeza Brielle kwenye mkutano huo na wanahabari.

“Na hali inaonekana ilikuwa kwamba familia kubwa za kibiashara kutoka Afrika na Asia ziliunda mafungamano ya kifamilia yenye maslahi ya kiuchumi,” aliongeza.

Watafiti wanasema kwamba inawezekana pia kwamba wanawake wa Kiafrika na jamii zao waliamua kuanzisha familia na wafanyabiashara au watoto wa kifalme kutoka Persia ili kukuza mitandao ya kibiashara kati ya wafanyabiashara wa Afrika na Persia.

Utafiti huo unaonesha kwamba watu wenye asili ya Afrika na Asia walianza kuchangamana katika eneo la mwambao wa Afrika Mashariki kuanzia kwenye miaka ya 1000 BK. Matokeo ya kijenetiki yanaakisi asili ya mchangamano ya Waswahili.

Lugha yao ya Kiswahili ina asili ya Kiafrika, Uislam, ambayo ndiyo dini yao kuu, ulikuja kutoka Mashariki ya Kati, na vyakula vyao vinaonesha kuathiriwa na vyakula vya Kihindi na sehemu nyengine na ukanda wa Mashariki ya Kati.

Stephanie Wynne-Jones, profesa wa akiolojia ya Kiafrika kutoka Chuo Kikuu cha York, Uingereza, na mtafiti mwenza kwenye utafiti huo, alisema kwamba mizizi ya lugha ya Kiswahili inaenda nyuma zaidi ya miaka 1,500 kama sehemu ya familia ya lugha za Kibantu.

“Hii inadhihirisha asili ya uenyeji wa hii jamii [ya Waswahili] na inatuonesha kwamba jenetiki za Kipersia hazikuwa sehemu ya ukuaji wa ujumla wa watu hawa,” Reuters ilimnukuu Wynne-Jones akisema.

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

Utamaduni wa Kiswahili ulifikia kilele chake kati ya karne ya 12 na 15, ukiporomoka baada ya uvamizi wa Mreno kwenye karne ya 16.

“Taarifa hizi za kijenetiki zinatoa maelezo mapya ambayo yanakosoa mitazamo ya awali ya kikoloni iliyokuwa ikihusisha asili ya Waswahili na maendeleo yao na kuwasili kwa wageni,” alisema Brielle.

Kumekuwa na mjadala wa siku nyingi miongoni mwa wasomi kuhusiana na asili ya Waswahili ingawaje Waswahili wa sasa wamekuwa na historia ya simulizi inayokumbatia mizizi ya Kiafrika na Kiasia. 

Kwa mfano, moja kati ya simulizi hizi zinahusisha kuanzishwa kwa himaya ya Kilwa na kuwasili kwa mtoto wa mfalme kutoka Persia, au Iran ya leo.

Chapurukha Kusimba, mwanaanthropolojia kutoka Chuo Kikuu cha South Florida, Marekani, na mtafiti mwenza wa utafiti huo, alisema ni kitu kinachofurahisha kwamba matokeo ya utafiti wao yanaendana na historia ya wenyeji wa mwambao wa Afrika Mashariki.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha mchango wa Afrika, na kwa kweli Uafrika kwenye Kiswahili, bila kuondosha mchango wa Persia na India,” Kusimba alinukiliwa na Reuters akisema.

One Response

  1. Utafiti wa uwasili ndio shina la tumbuko la msahili . Kulengana na utafiti huu yaonyesha walikuwa waasili kwanza ambao walikuwa wako maendeo ya mwambao wa pwani ambao ni wabajuni . Kisha ndio tukachanganya damu na waridhiwa waliokuja kutoka sehemu mbali mbali .
    Kulengana Vave ambao nihistoria ya wabajuni yasema , Tulitoka t’ini kwa miyi stini . Utafiti wastahilo ujaze mapungufu ya uwasili kisha ndio ufidie mapungufu ya waridhiwa ndio tupate wadhawa .
    Shukran kwa utafiti huu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *