Kwa Nini Wajawazito Wanakuwa na Tabia Zisizo za Kawaida?

Mtaalamu asema ni vichocheo vya homoni, aonya dhidi ya kula udongo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mkunga Mbobezi wa Masuala ya Afya ya Uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) Alex Nyaruchary amesema kwamba sababu ya wajawazito kuwa na tabia zisizo za kawaida ni kuwa na kichocheo cha progesterone miilini mwao, kichocheo kinachoathiri namna wajawazito wanavyojisikia.

Nyaruchary alibainisha hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hapo Aprili 3, 2023, ambapo alisema kwamba ni kawaida kwa wanawake kuwa na tabia zisizo za kawaida wakiwa wajawazito kwani kichocheo hicho kinazalishwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi hicho.

Tabia hizo zisizo za kawaida ni kama vile kuchukia baadhi ya vyakula; kupenda baadhi ya vitu, ikiwemo udongo na mkaa; kuchukia baadhi ya watu; na kuwa na tabia za kukasirika.

“Ni kwamba wakati wa ujauzito, akina mama wanakuwa wana kiwango kikubwa cha kichocheo kinachoitwa progesterone, hiki kichocheo kinakuwa kikubwa sana kipindi cha ujauzito,” alisema Nyaruchary kwenye mahojiano hayo.

“Kichocheo cha progesterone ndicho kinachochukua nafasi kuisaidia mimba ijishikize vizuri katika tumbo la uzazi na kuendelea kukua sasa katika kipindi chote cha ujauzito. Kwa hiyo, hiyo progesterone ndiyo inakuwa iko kazini kufanya kazi kusaidia kufanya ile mimba ikae vizuri ndani ya tumbo la huyu mwanamke.

“Sasa huyu mama anapokuwa na hicho kichocheo kwa namna hiyo kinaweza kikabadilisha hali yake ya namna anavyojisikia. Kuna wengine, wakati mwingine, wananuna. Ile ni kwa sababu kile kichocheo kinashusha ile hali yake, namna ambavyo anakuwa na hali ile. Kwa, hiyo inashusha ule uchangamfu.”

SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu

Nyaruchary anasisitiza kuwa tabia zinazofanywa na wanawake hawa katika kipindi hicho ni za mpito kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kimwili yanayowatokea akina mama hawa na kuitaka jamii kuelewa namna ya kuishi na wanawake wanapokua katika kipindi cha ujauzito.

Mabadiliko kwa akina mama hawa hutokea zaidi katika kipindi cha mwanzo cha miezi mitatu na wengine katika kipindi chote cha ujauzito, hivyo jamii inapaswa kuichukulia kawaida hali hiyo, Nyaruchary aliongeza.

“Unapokuwa na mke anajisikia namna hiyo, usimchukie, wala usione kama vile anafanya makusudi, ni mabadiliko ambayo yatachukua muda mfupi,” alisema mtaalamu huyo. 

“Na mara nyingine hayachukui muda mrefu, wengine ni miezi mitatu tu ile ya mwanzo. Baada ya kuwa sasa ameshazoea kile kipindi cha ujauzito kimeshakaa vizuri, kuanzia mwezi wa nne, wa tano, na kuendelea, yule mama sasa hali yake inabadilika, kwa sababu ilikuwa tu ni kipindi cha mpito,” ameongeza.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi

Nyaruchary ameshauri hatua za kuchukuliwa pindi zionekanapo tabia hatarishi, ikiwemo tabia ya kula udongo, mkaa na barafu, zinazoweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni.

“Kikubwa ambacho ninaweza nikaishauri jamii ni kwamba kwanza tuelewe kula udongo, yaani unaokota chini unakula, au mwingine, kwa mfano, kama wale wanaoishi kwenye nyumba ambazo ni za udongo, anaweza akawa anabandua kwenye nyumba halafu akawa anakula, kwanza tuelewe hivi siyo vitu vizuri,” anaonya mtaalamu huyo.
“Unaweza ukajikuta vile anavyoviokota na kula vikamsababishia minyoo huyu mama, na wakati mwingine kama vile nilivyosema ya kwamba vinaweza vikaathiri ufyonzwaji wa madini kwenye vyakula vingine tunavyokula. Kwa hiyo, mama anaweza akajikuta naye anapata utapiamlo pasipo kutarajia.
“Kwa hiyo, ninachoweza kuishauri jamii ni kuepukana na haya mambo. Kwa mfano, kula udongo, uepukane nayo, kula mikaa uepukane nayo, badala yake tafuta kitu ambacho unaweza ukatumia. Kwa mfano, mwingine anaweza akaamua anapokuwa amepata hamu ya kula udongo anaweza akaamua labda akanunua pipi akawa anakula. 

“Na ukiona kwamba unashindwa ni vizuri basi umtafute mtaalamu ili aweze kukupa ushauri zaidi.”

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts