The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sheria za Uchaguzi, Vyama vya Siasa Kufanyiwa Marekebisho?

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inapendekeza hivyo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro hapo Jumanne, Aprili 11, 2023, alipokea Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Uchaguzi na Vyama vya Siasa Tanzania, huku Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ikibainisha mambo kadhaa ya kiuchaguzi na vyama vya siasa yanayopaswa kurekebishwa.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa jijini hapa na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji (Mstaafu) Januari Msoffe ilitokana na wito uliotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (Chama cha Mapinduzi – CCM) Neema Lugangira ambaye alilamikia namna mazingira ya kisheria yanavyokwamisha wanawake kushiriki kwenye siasa Tanzania.

Akichangia bungeni hapo Aprili 28, 2022, Lugangira alitaka Sheria ya Uchaguzi na ile ya Vyama vya Siasa, mtawalia, zifanyiwe marekebisho kwa kuzingatia masuala mbalimbali, ikiwemo mfumo wa uteuzi wa wabunge na madiwani wanawake wa viti maalumu na usawa wa kijinsia katika ngazi ya vyama vya siasa.

Akiwasilisha muhtasari wa taarifa hiyo kwa Dk Ndumbaro, Msoffe alisema kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa inatoa sharti kwa vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinakuza usawa wa kijinsia katika kuandaa na kutekeleza sera zake, uteuzi wa wagombea, na uchaguzi wa viongozi wake. 

Msoffe alisema kwamba sheria hiyo pia inatoa sharti kwa vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa vyama kuwa wazi kwa jinsia zote. 

“Pamoja na masharti haya, utafiti umebaini kwamba bado utekelezaji wa suala la usawa wa kijinsia katika Sheria ya Vyama vya Siasa umekuwa mgumu kutokana na baadhi ya vyama kutoweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi na kusababisha uwepo wa idadi ndogo ya wanawake katika uongozi wa vyama vya siasa,” Msoffe alisema. 

“Aidha, sheria hiyo haimpi Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia utekelezaji wa ujumuishaji wa jinsia ndani ya vyama vya siasa,” Msoffe alisema kuhusu utafiti wao huo uliotokana na maoni ya wadau mbalimbali.

Wadau hao, waliotoka mikoa 16 ya Tanzania, ni pamoja na vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mahakama ya Tanzania, na Chama cha Wanasheria Zanzibar.

Wadau wengine ni pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika, Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wabunge na madiwani wanawake wa viti maalum, Asasi za Kiraia, makundi maalum (Vijana, Wazee, Wanawake, Watu wenye Ulemavu), na wananchi.

Viti Maalum

Kwenye eneo la upatikanaji wa wabunge na madiwani wa viti maalum, utafiti umebaini kwamba baadhi ya vyama vya siasa, ambavyo tume haikuvitaja, havijaweka utaratibu wa wazi wa kuwapata wagombea wa ubunge na udiwani wanawake kwa nafasi hizo.

Hali hii inasababisha malalamiko na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa wabunge na madiwani hao, tume imebainisha.

SOMA ZAIDI: Viti Maalumu Vishindaniwe Kwa Wananchi

Msoffe alisema changamoto hizo ni pamoja na upendeleo, maslahi binafsi, ukabila, rushwa na rushwa ya ngono, katiba za vyama kuwabana wanawake, na mfumo dume. 

Nyingine ni kama vile tamaa ya madaraka, kutokuwa na ukomo wa viti maalum, kukosekana kwa uratibu mzuri na usimamizi wa wazi wakati wa uchaguzi ndani ya vyama vya siasa.

“Utafiti unaonesha kwamba changamoto hizo zinasababisha kuwepo kwa manung’uniko kutoka kwa wanawake kuwa haki inakuwa haitendeki kwa walio wengi,” aliongeza mwenyekiti huyo.

Akizungumza punde baada ya kupokea taarifa hiyo, Dk Ndumbaro alisema kinachofuata sasa ni taarifa hiyo kuwasilishwa bungeni ili wabunge na wananchi wapate fursa ya kujua kilicho ndani pamoja na kuijadili.

Hata hivyo, Ndumbaro, ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini (CCM), alisema Serikali itafanya kila linalowezekana kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi wa kisiasa, akisema kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitengwa kwenye nafasi hizo.

“Nafasi yao imekuwa finyu kutokana na tamaduni zetu, mila zetu lakini [pia] mtazamo juu ya mwanamke katika jamii,” Dk Ndumbaro alisema. “Matarajio ni kwamba mchakato wa mabadiliko ya sheria utaanzia [taarifa hii] ikishawekwa mezani, bungeni.”

SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?

Masuala mtambuka

Kwenye Taarifa yake hiyo ya Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Uchaguzi na Vyama vya Siasa Tanzania, tume pia imechambua ushiriki usioridhisha wa Watanzania kwenye chaguzi, hali iliyoihusisha na vyama vya siasa kutokutekeleza ilani na wagombea kutotimiza ahadi walizotoa kwa wananchi.

Sababu nyingine ni kama vile kuteuliwa kwa wagombea wasio chaguo la wanachama ndani ya vyama; dhana ya baadhi ya wagombea kudai kuibiwa kura; mazingira na umbali wa vituo vya kupigia kura; na ukosefu wa elimu endelevu ya uraia na elimu ya mpiga kura.

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Kenya Umekwisha. Tanzania Imejifunza Nini?

Tume pia iligusia malalamiko ya siku nyingi juu ya kutokuwepo kwa utaratibu unaowawezesha Watanzania walio nje ya nchi na wale walioko vizuizini kushiriki kupiga kura, ikiripoti kwamba wadau wameitaka Serikali kuliangalia jambo ili kupanua wigo wa demokrasia nchini.

Kwenye suala la uchaguzi kwa njia ya kielektroniki, tume imesema kwamba wadau wameshauri mfumo huu usitumike kwa sasa kwa sababu bado Tanzania haijaendelea kwenye eneo hilo, hali ambayo inaleta hofu ya usalama wa mchakato mzima wa upigaji kura, uhesabuji wa kura, na utoaji wa matokeo.

Sambamba na Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Uchaguzi na Vyama vya Siasa Tanzania, tume pia iliwasilisha kwa Serikali Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Utoaji Haki Katika Mahakama za Mwanzo Tanzania.

Mahakama za Mwanzo taaban

Kwenye utafiti wake, tume ilibaini kwamba Mahakama za Mwanzo zinakabiliwa na changamoto mbalimballi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wataalam wa lugha ya alama au wakalimani katika maeneo ambayo washukiwa hawajui Kiswahili; miundombinu isiyoridhisha; uhaba wa vyumba vya mahakama; nyumba za watumishi; na vitendea kazi.

Hali iko hivyo licha ya tume kubaini kwamba Mahakama za Mwanzo zinahudumia idadi kubwa ya wananchi ambapo kwa mwaka 2021, kwa mfano, takribani asilimia 70 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika Mahakama za Tanzania Bara yalikuwa katika Mahakama za Mwanzo.

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania

Idadi ya mawakili wa kujitegemea pia ni ndogo katika Mahakama za Mwanzo kuliko mahitaji ya huduma zao, Msoffe alibainisha kwenye taarifa yake. 

Aidha, idadi kubwa ya mawakili hao wanaendesha shughuli zao maeneo ya mijini, huku viwango vya ada za mawakili vikiwa bado ni vikubwa kulinganisha na uwezo wa wananchi walio wengi.

Tume imebainisha pia kwamba Mahakama za Mwanzo hazina mamlaka ya kisheria ya kupokea na kusikiliza mashauri ya mirathi ya Kikristo, hali inayowafanya wananchi wenye mashauri hayo kulazimika kufungua mashauri ya aina hiyo katika Mahakama za Wilaya. 

“Mazingira haya yanasababisha usumbufu na kuongeza gharama za kutafuta huduma katika Mahakama za Wilaya ambazo zipo wilayani ambapo baadhi zipo mbali na makazi ya wananchi walio wengi, hususan wanaoishi vijijini,” Msoffe alimwambia Dk Ndumbaro.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *