Search
Close this search box.

Bajeti Wizara ya Kilimo Inaakisi Umuhimu wa Kilimo Tanzania?

Kilimo cha umwagiliaji inaonekana ni eneo la kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita katika Sekta ya kilimo

subscribe to our newsletter!

Sekta ya Kilimo imeendelea kuwa ndiyo sekta nyeti kwa uchumi wa nchi na kwa maisha ya Mtanzania mmoja mmoja, ambapo kwa mwaka wa 2021 imeweza kuchangia asilimia 26.1 ya pato la Taifa, imetoa ajira kwa Watanzania takribani asilimia 65.6 na kuchangia malighafi za viwanda vya ndani kwa asilimia 65.

Siyo hivyo tu, katika Sensa ya mwisho ya kilimo iliyofanyika nchini inaonesha kuwa kati ya jumla ya kaya milioni 7.837 zinazojishughulisha na kilimo, zaidi ya kaya milioni 3.49 zilitegemea mauzo ya mazao ya chakula kama chanzo kikuu cha mapato ya kaya.

Licha ya mchango huu mkubwa wa sekta sekta ya kilimo, kwa mwaka wa fedha 2023/24 Sekta ya Kilimo ukijumuisha kilimo cha mazao, ufugaji na uvuvi imetengewa bajeti ambayo ni sawa na 3% tu ya bajeti nzima ya Serikali  kwa mwaka 2023/24, hii ni kinyume na Azimio la Malaba ambalo Tanzania imelidhia linalotaka  nchi za Afrika kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya hii nyeti.

Pamoja na ufinyu huu wa bajeti ya sekta ya kilimo kwa ujumla, tukiangazia bajeti mahususi ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa Bungeni inaonesha kuna viashiria chanya vinavyoonesha namna Serikali imeamua kutilia mkazo sekta hii ambayo imekuwa kama uti wa mgongo wa taifa.

Hii inatokana na ukweli kwamba bajeti ya kilimo imeendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa mwaka hadi mwaka tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani, kutoka bilioni 294.1  mwaka 2021/22 hadi bilioni 751.1 kwa mwaka 2022/23. Kwa mwaka 2023/24 bajeti imefikia  bilioni  970.78  ambayo ni sawa ongezeko la asilima 29.24% ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2022/23.

Katika hali ya ufikishaji fedha kwenye miradi, hadi kufika April 2033 kiasi cha 73.22% ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Wizara ya Kilimo iliiidhinishwa na kutolewa.

Katika uchambuzi wa The Chanzo, tumeyaangazia mambo matatu tu; umwagiliaji, usalama wa chakula na upatikanaji wa mbolea kwa kuwa ni moja ya maeneo ambayo yametajwa sana na wadau mbalimbali wa kilimo.

Kilimo cha Umwagiliaji

Kilimo cha umwagiliaji inaonekana ni eneo la kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita katika Sekta ya kilimo kwani asilimia 38 ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2023/24  imetengwa kwa ajili ya Tume ya Umwagiliajji.

Bajeti ya kilimo kwa kulinganisha na fedha za umwagiliaji

Kiasi hiki cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya umwagiliaji ni mara 29 ya kiwango cha Bajeti kilichotengwa kwa ajili ya umwagiliaji mwaka 2020/21 ambapo Serikali ilitenga jumla ya sh 12,801,180,000 tu sawa na 6% ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huo wa fedha.

Tanzania ina eneo la hekta milioni 29.4 linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo mpaka hivi sasa ni  hekta 727,280.6 tu sawa na asilimia 2.5 ndizo ambazo zinatumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Ongezeko la uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji umelenga kufikia lengo la Serikali la kuwa na hekta milioni 1.2 zinazomwagiliwa hadi kufika mwaka 2025. Lakini, lengo hili linaweza lisifikiwe katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kwa kuwa licha ya ongezeko hili la fedha la kukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya umwagiliaji bado jitihada kubwa inahitajika kiuwekezaji.

Kwani kukamilika tu kwa idadi ya miradi 69  iliyopangwa katika mwaka wa fedha 2022/23 kutaongeza hekta 95,005 tu za umwagiliaji endapo utekelezaji wake utakuwa ni kwa asilimia 100, hivyo kufanya hekta za umwagiliaji kuwa 822,285.6. Lakini, hadi kufika Aprili 2023, mikataba 48 tu yenye thamani ya Shilingi 234,127,200,000 sawa na 70% ya lengo la kujenga na kukarabati miradi 69 ya umwagiliaji ndiyo ilisainiwa.

Lakini katika kuongeza ufanisi wa kilimo cha umwagiliaji Wizara imetoa taarifa ya kuajiri watumishi 321 katika ofisi 121 za umwagiliaji, ambapo kati yao 121 ni waandisi kilimo, mafundi sanifu 100 na maafisa kilimo 100. Hatua hii inaweza kuongeza ufanisi wa utekelezaji na usimamizi wa miradi ya umwagiliaji iliyopo na inayoendelea kujengwa.

Kwa ujumla ili kuhakikisha Tanzania inatoka katika kilimo cha kutegemea mvua, ikizingatia mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea, ni muhimu sana Serikali kuendelea kuwekeza fedha nyingi zaidi katika eneo la umwagiliaji ili uzalishaji wa kilimo hususani mazao ya chakula uwe ni wa uhakika.

Usalama wa Chakula

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, kwa mwaka 2022/23 Tanzania imejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 114, hii ni kutokana na uzalishaji wa chakula kufikia tani 17,148,555 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 15,053,299.

Licha ya ziada kubwa ya uzalishaji wa chakula, Katika kipindi cha mwaka 2022/23 Watanzania waliendelea kushuhudia ongezeko la bei za vyakula ambapo hadi kufika Machi 2023 mfumuko wa bei za chakula ulifikia asilimia 9.7 ukilinganisha na asilimia 6.5 Machi 2022.

The Chanzo inaona ziada ya chakula haikuweza kupelekea kushuka kwa bei za vyakula sokoni kwa sababu ya gharama za kulima hususani mbolea kuwa juu katika msimu wa 2021/22, kupanda kwa bei za mafuta na ongezeko la mauzo ya nje ya vyakula ambayo kwa mwaka 2022 yalifikia tani 1,195,649.

Katika mwaka wa fedha 2023/24 Wizara kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) imepanga kununua tani 400,000 za mahindi na mchele kama mojawapo ya njia ya kuimarisha akiba ya chakula ambayo kwa sasa ni tani 159,870.216. Hii ni hatua nzuri katika kuimarisha akiba ya chakula lakini pia itawapa soko la uhakika wakulima wa mazao ya chakula.

Upatikanaji wa mbolea za viwandani

Mbolea za viwandani ni moja ya pembejeo muhimu sana katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, hususani katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula. Pamoja na umuhimu huu, Tanzania ni tegemezi wa mbolea ya viwandani kutoka nje.

Hali ya upatikanaji wa mbolea

Kati ya tani 819,442 za mbolea zilizopatikana katika kipindi cha mwaka 2022/23, tani 617, 079 ziliingizwa kutoka nje ya nchi sawa na asilimia 75%, tani 75,399 zilizalishwa na viwanda vya ndani na tani 75,399 ilikuwa ni bakaa ya mwaka 2021/22.

Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali ilitenga takribani asilimia 20 ya matumizi ya Wizara hii kwa ajili ya ruzuku za mbolea ili wakulima waweze kupata pembejeo hii kwa bei nafuu.

Lakini hadi kufika April 2023, ni tani 342,729.500 tu za mbolea zenye ruzuku zilisambazwa kwa wakulima 782,553 kati ya wakulima 3,050,621 waliandikishwa. Hii ni sawa na asilimia 26 tu ya wakulima walioandikishwa ndiyo walinufaika na mbolea hizi. Kiwango hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na uhalisia wa uhitaji.

Mgawanyo wa mbolea ya ruzuku

Pia uchambuzi wa The Chanzo umebaini kwamba asilimia 74 ya mbolea hizi za ruzuku zilipelekwa katika mikoa mitano ya Ruvuma, Mbeya, Njombe, Songwe na Iringa. Mikoa hii ni moja ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mahindi na mchele, pengine Serikali ilipeleka zaidi mbolea haya maeneo ili kuinua uzalishaji wa mazao haya ya chakula.

Mbolea ya ruzuku kwa kila mkoa

Kwa mwaka wa fedha 2023/24 ruzuku ya mbolea imeendelea kuwa kipaumbele cha Wizara ya Kilimo licha ya Waziri kutotaja kiasi mahususi kilichotengwa kwa ajili hiyo. Lakini kwa bajeti ya ujumla ya kilimo ni dhahiri kwamba mbolea ya ruzuku haitaweza kuwafikia wakulima takribani milioni 3 waliojiandikisha kwa mwaka wa fedha uliopita.

Lakini kuanza kufanya kazi kwa kiwanda cha mbolea cha  Itracom Fertilizers Ltd  jijini Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka inatoa matumaini juu ya uzalishaji wa ndani wa mbolea pamoja na upatikanaji wake kwa bei nafuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *