Riwaya ya A Walk in the Night ya mwandishi wa Kiafrika ya Kusini Alex La Guma ni hadithi inayoangazia madhila ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi wanayoyapitia watu wa jamii ya watu weusi nchini Afrika ya Kusini, maarufu kwa Madiba au Bondeni.
Madhila yanayosimuliwa katika simulizi hii yanaakisi siku za nyuma kabisa katika historia ya taifa hili lenye visa, mikasa, na habari nyingi zenye kusisimia. Ni simulizi ya miaka kati ya 1948 hadi 1994, kwani hizi ndiyo zilikua zama za utawala wa kibaguzi uliosimamiwa na makaburu.
Alex La Guma, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi raia wa Afrika ya Kusini, ni mwandishi mahiri wa hadithi na tamthiliya ambaye alizaliwa mnamo Februari 20, 1924, na kufariki Oktoba 11, 1985.
Matabaka
Kabla msomaji hajaanza kuisoma hadithi hii, yafaa kuelewa kwamba Afrika ya Kusini ilikuwa na mjumuiko wa matabaka matatu kwa mujibu wa utofauti wa watu na rangi zao.
Tabaka la kwanza ni wazawa halisi wa Afrika ya Kusini. Hawa ni watu weusi ambao ni wengi nchini humo na ndiyo wanaodharaulika, kukandamizwa, na kudhulumiwa haki zao. Hawa ndiyo tabaka la chini kabisa.
Watu hawa huishi mitaa yao peke yao na hawaruhusiwi kuchangamana na wengine. Wanaishi katika dimbwi la umasikini na ukosefu mkubwa wa huduma za kijamii katika mitaa yao. Katika simulizi hii ya A Walk in the Night, hawa hufahamika zaidi kama blacks, au watu weusi.
Kundi la pili katika simulizi hii ni watu ambao ama ni weupe (lakini siyo wazungu) au wengi wao ni mashombe, hawa wakiwa ni wale ambao wamechanganya wazazi wao, kwa maana mzazi mmoja anakuwa mzungu na mwingine anakuwa Mwafrika.
Tabaka hili huchukuliwa kama watu wa tabaka la kati na walipata haki kwa namna ambayo siyo kwa kiwango cha juu wala siyo kwa kiwango cha chini bali ni kwa kiwango cha kati.
SOMA ZAIDI: Zuhura Yunus: Nafahamu Hisia Zitakazoibuliwa na Kitabu Changu
Katika simulizi hii, hawa hufahamika zaidi kama the coloured. Kwa mujibu wa msanii maarufu wa uchekeshaji wima na raia wa hukohuko Bondeni Trevor Noah, katika kitabu chake alichokiita Born a Crime, katika jamii ya watu wanaofanya ubaguzi wa rangi, kundi hili la mashombe ndilo hupata taabu zaidi kwani hubaguliwa na watu weusi wenzao na pia wazungu huwadharau kwa madai kwamba wao siyo wazungu kamili.
Kundi la tatu ndilo kundi la wazungu halisi, au the whites. Hawa ndiyo wanaoifaidi keki ya taifa, ndiyo watu wa tabaka la juu kabisa nchini humo. Wanaishi mitaa yenye hadhi ya juu na yenye huduma lukuki za kijamii kama vile umeme, maji, barabara nakadhalika. Hawa ndiyo wenye maamuzi makubwa katika jamii yote.
Mickey
Kwenye hadithi ya A Walk in the Night, La Guma amemtumia kijana Michael ‘Mickey’ Adonis ambaye ni shombe wa Kizungu na Kiafrika kama mhusika mkuu.
Mickey anafukuzwa kazi katika kiwanda cha kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba ambako yeye alikua kama mashine opareta. Msimamizi, au foreman, anayemfukuza kazi Mickey ni Mzungu. Sababu ya kumfukuza kazi ni ya kibaguzi haswa.
Mickey aliomba ruhusa ya kwenda maliwatoni. Mzungu akagoma kumpa ruhusa hiyo na kudai aendelee kuchapa kazi. Mickey akajibizana na boss yule na huo ndiyo ukawa mwisho wa kibarua chake.
Mickey alilipwa posho yake na stahiki zingine muda uleule kisha akaanza safari kwa treni kutoka kazini kwake hadi mtaani kwake District Six. Kwa hasira alizonazo juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu aliotendewa, Mickey anavuta sigara bila kukoma.
Ni mwendo wa kuwasha kuvuta, kumaliza na kuwasha nyingine. Nani anaweza kuikabili sonona ya kufukuzwa kazi katika ulimwengu huu uliojaa mahitaji mengi ya pesa na heshima?
Kabla hajafika District Six, Mickey anashuka mtaa wa Hanover ambao unakaliwa na mashombe pamoja na wazungu wachache. Hapo anaingia katika mgahawa wa Moreno na kupata chakula cha jioni.
SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?
Akiwa hapo anatokeza kijana Willie Boy ambaye si rafiki yake damdam bali wanafahamiana kwa sababu matatizo yanawaunganisha. Waswahili husema waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba. Mickey anamsimulia swahiba huyu wa mchongo madhila aliyokutana nayo kazini kwao siku ile.
Willie Boy anasikitika na kujiapiza kwamba kamwe hatakubali kufanya kazi na Wazungu kwani wao wanachojua ni kuwaamrisha Waafrika, kazi kazi kazi tu. Mickey ni mkarimu sana, hivyo anampatia pesa kidogo Willie Boy ili akanunue sigara na ‘dagga’ kama inavyo maanishwa bangi katika simulizi hii.
Willie Boy ni mhuni chokoraa ambaye haachi kitu. Ukabaji, uvutaji, na unywaji wa pombe yeye ni kanyaga twende tu.
Mickey anaelekea ghetto kwake. Akiwa anaukaribia mlango wa ghetto anakutana na Uncle Doughty akiwa anatembea kwa kushika ukuta kutokana na ulevi chakari alionao. Babu huyu anamkaribisha Mickey chumbani kwake ili wapige kilevi.
Mauaji
Wakiwa chumbani, Mickey akapewa chupa ya mvinyo na kuanza kuinywa kwa pupa na kutaka kuimaliza chupa yote. Uncle Doughty akamsihi Mickey asimalize ulabu wake na hapo mabishano yakaanza na kusababisha kipigo cha teke kwa Uncle Doughty hadi akafa palepale ndani.
Kabla ya kuuawa, Uncle Doughty alimsihi Mickey maneno ya upendo, mshikamano na kuthamini utu wa binadamu. Alimwelezea kwamba yeye alikua mcheza filamu maarufu na ameizunguka dunia yote kwa kazi hiyo.
Akamwambia Mickey kwamba licha ya umaarufu huo, wazungu wenzake wamemtenga na kumfukuza mitaa yenye hadhi kwa vile tu ana maradhi ya kisukari, mlevi chakari na pia amezeeka mno. Hapa tunaona jinsi ubaguzi wa rangi unavyoenda mbali zaidi kwa kuwabagua hata wazungu wenyewe kwa wenyewe.
Baada ya kufanya mauaji ninayoyaita si ya kukusudia, Mickey anajilaumu sana, japo ipo sauti inamwambia mauaji yake ni halali kwani wazungu siyo watu wema na ndiyo waliomletea shida na kutangatanga bila kazi hata yeye.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah
Hii ni roho ya kisasi, yaani Mickey anawachukia Wazungu na kumuua mmoja wao kisa amefukuzwa kazi na Mzungu. Mickey anajificha ghetto kwake, wasiwasi unamzidia na kuamua kupotelea gizani kujaribu kukwepa mkono wa sheria.
Ghafla anakuja Willie Boy mwenye alosto ya kuvuta sigara au pombe. Anagonga mlangoni kwa Mickey bila majibu na hivyo anaamua kuingia chumbani kwa Uncle Doughty ambako anamkuta amelala hajielewi.
Anaamua kukimbia na kupotelea kusikojulikana lakini kabla hajafanya hivyo anakutana na Abrahams anayetafuta kibiriti ili awashe sigara yake.
Mickey kwenye mgahawa wa Wahindi. Akiwa pale anajitokeza kijana mdogo Joe ambaye Mickey anamfahamu kama chokoraa, au mtoto wa mtaani, ambaye ni mchangamfu na anajielewa.
Anakumbuka siku moja alimpa pesa Joe na akagundua yuko tofauti na watoto wengine wa mtaani. Joe havuti sigara wala hanywi pombe. Yeye huendesha maisha yake kwa kuokota samaki waliotelekezwa na wavuvi ufukweni mwa bahari.
Kutelekezwa
Mickey anamhoji Joe kuhusu historia yake ambapo alieleza kwamba yeye ametelekezwa na wazazi wake. Alianza baba yao, mama akabaki pamoja na wadogo zake.
Mama akashindwa kulipia pango la nyumba na hatimaye akamwambia Joe na wadogo zake wahamie kijijini kwani maisha ya mjini yalikuwa yameshawashinda. Joe hakukubaliana na hoja ya mama yake kwa madai kwamba tatizo lililopo nchi nzima ni ubaguzi wa rangi na matabaka katika jamii.
SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?
Anaamini kwamba shida hii haikwepeki kwa kuadilisha makazi bali kwa kupambana au kuwaelimisha wale wanaoihusudu.
Wanajitokeza vijana watatu mbele ya Mickey. Hawa ni vijana wa mtaani ambao kiufupi wameunda genge lao la wahuni. Hapa wanamtafuta rafiki yao mmoja aitwae Sockies ili akasome ramani wakati wakidhamiria kwenda kuvunja nyumba na kuiba.
Joe anawajua vijana hawa na anaamua kumsihi Mickey asije kujiunga na wahuni wale kwani yeye ni kijana anayejielewa.
Mbaroni
Taarifa za mauaji zimewafikia polisi waliokua doria usiku ule. Konstabo Raalt na dereva Andries wanasogea eneo la tukio na kuwahoji wananchi juu ya taarifa zitakazosaidia kubaini wauaji.
Abrahams anajitokeza na kueleza kwamba amemuona kijana akiwa anatoka chumba cha marehemu. Polisi wanaanza kumsaka muuaji kwa mujibu wa ushahidi wa mavazi na muonekano wa nje wa kijana huyo.
Kwa bahati mbaya sana, aliyeonekana pale si Mickey bali ni Willie Boy, yule aliyeombwa kibiriti. Andries na Raalt hawana maelewano mazuri. Raalt ni mkali mno hasa kwa wahalifu weusi.
Amekuwa akiwapora fedha zao, akiwapiga kwa ukatili na hata kutumia risasi kuwajeruhi. Huyu naye anaonekana ni mwenye kisasi kwani anaonewa mno na mkewe mwenye kisirani naye. Hapa tunaona muendelezo wa roho ya kisasi.
Willie Boy anaelekea kwa mama mkorofi Gipsy. Anaomba akopeshwe pombe ya kienyeji na kuahidi kulipa siku chache baadaye. Akiwa anaendelea kunywa pombe yake, wanaingia mabaharia Wazungu wakiwa na wasichana wa Kiafrika.
Mmoja wa wasichana wale ni Nancy ambaye anafahamiana na Willie Boy. Nancy anapiga soga na Willie Boy, baharia mmoja anamnunilia Willie Boy pombe kali, wanapishana maneno kisha ugomvi mkubwa unazuka.
Gipsy anampiga Willie Boy na kumpora kisu chake ambacho alikua anaenda kumchoma nacho Mzungu yule. Willie Boy anatolewa kwenye Bar ya Gipsy na baada ya hapo anakutana na Mr. Green, mlevi wa kutupwa ambaye anamkaba na kumlazimisha ampe pesa. Kisasi kinaendelea hapa, yaani Willie Boy amepigwa na Gipsy, hasira zake anazimalizia kwa Mr. Green.
Mr. Green ni mzee wa mjini. Kabla hajakabwa na Willie Boy alikua bar na dereva teksi wakibadilishana stori za hapa na pale. Katika stori zao waliokua wanazungumzia hali mbaya ya ubaguzi wa rangi nchini mwao.
Ubaguzi wa rangi
Wakakubaliana kwamba ubaguzi wa rangi na ukatili wa mtu na mtu haupo tu nchi za magharibi bali hata katika nchi za Kiafrika hali bado ni mbaya. Akatolea mfano wa ugomvi baina ya Flippy Isaacs na Cully Richards.
Flippy alifungwa jela kwa kosa la kuvunja na kuiba. Akiwa jela akapewa taarifa kwamba mkewe anashiriki mapenzi, au anachepuka, na Cully Richards muuza bucha. Baada ya kumaliza kifungo chake Flippy akaenda buchani kwa Cully Richards na kuleta shida. Cully Richards alimkata mapanga na kumuua Flippy Isaacs palepale.
Willie Boy anakamatwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya Uncle Doughty. Andries anamlaumu Konstabo Raalt kwa kumjeruhi Willie Boy kwa risasi hali ya kuwa walikua na nafasi ya kumkamata bila kutumia nguvu kupita kiasi.
Konstabo Raalt anadhihirisha ukatili wake kwa kumchelewesha kumpeleka Willie Boy hospitali huku akiwa anavuja damu kama kuku aliyechinjwa na kuachiwa.
Inaguswa simulizi ya Grace Lorenzo na Franky Lorenzo. Franky anaambiwa na mkewe kwamba tayari ana ujauzito na hivyo ajiandae kupokea mtoto wao wa tano. Franky anachanganyikiwa kwa mawazo na baada ya kumlaumu mkewe kwa nini asitumie vidonge kama wanavyofanya wanawake wengine, naye anamjibu apunguze kuhitaji kila siku.
Wawili hawa wanaishi kwenye chumba kimoja, kitanda kimoja, watoto wanne!
Mwisho kabisa anaonekana Mickey akiwa pamoja na genge la wahuni. Anaenda kuvunja na kuiba.
Wosia wa Joe haukusaidia kitu. Franky na Gracy Lorenzo bado ni masikini, Joe anaonekana ufukweni mwa bahari akiokota samaki waliooza.
Siraji Ally Hokororo ni mwalimu wa sekondari na msomaji wa vitabu kutoka Arusha, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia allysiraji07@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.