The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zanzibar Imejiandaa Kiasi Gani Kukabiliana na Majanga ya Moto?

Miundombinu na mipango miji isiyo rafiki yatajwa kukwamisha uokozi wa haraka pindi majanga ya moto yanapotokea.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Kuna mawazo mkanganyiko baina ya waathirika wa majanga ya moto visiwani hapa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Zanzibar kuhusiana na uwezo na utayari wa mamlaka husika kwenye kukabiliana na majanga ya moto ili kuokoa maisha na mali za wananchi.

Kwa siku za hivi karibuni, Zanzibar imekuwa ikikumbwa na matukio mengi ya moto yanayopelekea upotevu mkubwa wa mali na maisha ya raia, huku takwimu kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji zikionesha kwa mwaka 2022 pekee, jumla ya matukio ya moto 205 yaliripotiwa kutoka sehemu mbalimbali za Zanzibar.

Licha ya kuwa matukio hayo kuwa ni pungufu ukilinganisha na yale yaliyotokea mwaka 2021 (327) au mwaka 2020 (251), sauti zimekuwa zikipazwa kuhusiana na matukio hayo yanayosababishwa, kwa kiasi kikubwa, na hitilafu za umeme, husasan kwenye kuwarudisha nyuma wananchi kimaendeleo na kupelekea kuwapoteza wapendwa wao.

Kwenye mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni, Msaidizi Mratibu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Makame Omar Mohamed, alisema kwamba kwenye matukio hayo 205 yaliyotokea Zanzibar, jeshi hilo lilifanikiwa kufanya uokozi kwa asilimia 75, hali aliyoieleza kama ni mafanikio.

“Kikosi kinajitahidi kutoa huduma na pia kufanyia kazi [ripoti za majanga] kwa wakati,” Mohamed alisema. “Na licha ya kuwepo kwa matukio hayo, bado Kikosi cha Zimamoto na uokozi kinaendelea na jitihada za makusudi za kupunguza majanga na maafa yanayoyotokana na moto.”

Tathmini hii ya Mohamed juu ya utayari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kukabiliana na majanga ya moto Zanzibar, hata hivyo, inatofautiana na ile ya watu ambao wamepoteza wapendwa wao na kushuhudia uharibifu mkubwa wa mali zao kutokana na matukio hayo.

Sikuweza kumuangalia

Asha Khamis alimpoteza binti yake wa mwaka mmoja baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi huko Mwanyanya, mkoa wa Mjini Magharib, Unguja, kushika moto na kupelekea uharibifu mkubwa kwenye nyumba hiyo Asha na ndugu zake waliyorithi kutoka kwa mama yao.

Asha, 29, aliieleza The Chanzo kwamba tukio hilo lilitokea mnamo Oktoba 2, 2022, ambapo hitilafu ya umeme ilitokea kwenye nyumba hiyo majira ya asubuhi, huku binti yake huyo akiwa amelala na yeye mwenyewe akiwa amekwenda dukani kununua vitu.

“Dada zangu hawakujua kama kulikuwa na mtoto mwingine amelala ndani,” Asha, ambaye amebaki na binti yake wa miaka minne, alisimulia.

“Walimtoa mtoto wangu yule mkubwa ambaye alikuwa anacheza ukumbini,” anaongeza mama huyo. “Wao walijua kuwa nimemchukua huyu mdogo dukani. Niliporudi nyumbani niliona moto, nikaona basi nimemkosa mwanangu.”

SOMA ZAIDI: ‘Usumbufu Ni Mkubwa’: Wajasiriamali Waichambua Mikopo ya ‘Inuka na Uchumi wa Buluu’

Ni imani ya Asha kwamba endapo kama watu kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wangefika bila kuchelewa, basi binti yake angelikuwa hai muda huu na kuendelea kuishi naye.

“Zimamoto walifika kwa kuchelewa, tayari moto ulikuwa umeshakuwa mkubwa na kushika kila mahali,” Asha alieleza kabla ya kuanza kulia na kushindwa kuongea. “Binti yangu alikuwa tayari ameshavimba na kuungua sana. Sikuweza hata kumuangalia.”

Naanza upya

Kama Asha alipoteza binti na kuingia gharama za kuifanyia marekebisho nyumba yao ya urithi, Said Mohammed Said kutoka Bububu, mkoa wa Mjini Magharib, Unguja, alifanikiwa kuikoa familia yake lakini nyumba yake yote iliteketea kwa moto.

Said, 30, alikuwa akiishi na mama yake mzazi, mke na watoto wawili kwenye nyumba hiyo ya kifahari ya vyumba vinne kabla tukio hilo ambalo hatakuja kulisahau maishani mwake liikumbe familia yake hapo Septemba 24, 2022.

“Nimepata hasara kubwa, zaidi ya [Shilingi] milioni 30,” Said aliiambia The Chanzo ambayo ilimkuta akiwa na mafundi wakianza kuijenga upya nyumba hiyo. “Nimeiondoa familia, ndiyo najenga tena upya.”

“Vitu vyote vilivyokuwemo ndani [ya nyumba] viliungua,” Said, anayejishughulisha na biashara ya chakula, aliendelea kueleza. “Maana yake naanza upya. Nimepoteza kila kitu. Lakini nashukuru familia imetoka salama. Zimamoto walifika ila ndiyo kwa kuchelewa.”

SOMA ZAIDI: ‘Nimeamua Kuacha Kesi, Nibaki na Binti Yangu’: Masaibu ya Waathirika wa Udhalilishaji Walemavu Zanzibar

Moto ni moja kati ya majanga mengi ambayo Zanzibar imeweka mipango na mikakati ya kukabiliana nayo.

Tathmini ya kitaifa ya kukabiliana na majanga visiwani humo ya karibuni kabisa ni ile ya mwaka 2008 ambayo, pamoja na mambo mengine, inabainisha sababu kadhaa zinazopelekea kuchelewa kwa juhudi za uokozi pindi matukio ya moto visiwani humo yanapotokea.

Miongozo kukiukwa

Kwa mujibu wa tathmini hiyo iliyofanywa kwa niaba ya Kamisheni ya Kupambana na Maafa Zanzibar, moja kati ya sababu hizi ni kutokufuatwa kwa kanuni na miongozo iliyowekwa kwa ajili ya kupunguza hatari za moto visiwani humo.

Kwa mfano, tathmini hiyo ilieleza kwamba ni nadra sana kwa majengo – ya umma na yale ya binafsi – kuwa na nyenzo na miundombinu ya kukabiliana na majanga ya moto, kama vile kuwa na sehemu za dharura za kutokea pindi moto ukitokea.

Licha ya kwamba tathmini hii ni ya mwaka 2008, inaonekana hali bado imeendelea kuwa hivyo kama inavyothibitishwa na Msaidizi Mratibu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Makame Omar Mohamed, ambaye amelalamikia suala hilo alipoongea na The Chanzo.

Mohamed anadhani kwamba kwa kiasi kikubwa changamoto hii imechochewa na Serikali kutokuzikazania taasisi zake kuwa na nyenzo hizi, hali ambayo anadhani inachochea kulifanya tatizo kuwa kubwa.

SOMA ZAIDI: ‘Hayatibu Ugonjwa Wowote’: Zanzibar Yatahadharisha Unywaji wa Maji ya Chemchemi Pemba

“Kwanza, Serikali yenyewe iweke mikakati ambayo itakuwa mikakati imara ya viongozi wanaoziongoza hizi taasisi kuona umuhimu wa taasisi zao kupambana na majanga,” alisema Mohamed.

“Kwa sasa hivi, tayari kuna maelekezo ya kuzitaka taasisi na ofisi zote za Serikali kupata mafunzo na ulazima wa kupata huduma kuhusu  kuzima, kujilinda, na kuchukua hatua pale majanga yanapotokea,” aliongeza.

Mipango miji holela

Lakini pengine sababu kubwa ya kuchelewesha uokoaji pindi matukio ya moto yanapotokea ni namna miundombinu ya barabara na mipango miji katika maeneo mengi ya Zanzibar isivyokuwa rafiki kwenye shughuli za uokoaji.

Hii ni changamoto ambayo pia imeorodheshwa kwenye tathmini hiyo ya mwaka 2008 iliyotajwa hapo juu ambayo inataja kubanana kwa majengo, mitaa membamba, na hali ya mitaa kutokufikiwa na magari ya zimamoto kama sababu inayoathiri juhudi za uokozi visiwani humo.

Tathmini hiyo pia ilibainisha kwamba visima vingi vya uzimaji moto, au fire hydrants kama vinavyojulikana kwa kimombo, vilivyowekwa Zanzibar kwenye miaka ya 1960 kwa sasa vimeharibiwa au vimevamiwa na makazi ya watu.

Kwa vile ambavyo vipo, tathmini hiyo ilisema kwa sasa na vyenyewe havifanyi kazi.

Suala hili la miundombinu kuwa kikwazo kwenye juhudi za uokozi halitambuliwi na mamlaka husika tu, bali hata wananchi wa kawaida wanalitambua na kuwapa hofu pia.

SOMA ZAIDI: Kada wa CCM Zanzibar Apotea Kwa Miaka Miwili. Familia Yataka Majibu

Issa Jecha ni mkazi wa Jang’ombe, mkoa wa Mjini Magharib, Unguja, ambaye alishindwa kueleza ni namna gani gari za zimamoto zinaweza kuingia kwenye mitaa ya mji huo kutokana na namna nyumba zake zilivyo banana sana.

“Kwanza, huku hata maji hakuna, na nyumba ziko pachapacha,” Jecha, ambaye kazi yake ni dereva wa daladala, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu. “Sasa hapo ni mtihani janga la moto likitotokea.”

Teknolojia ya kisasa

The Chanzo ilimuuliza Msaidizi Mratibu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Makame Omar Mohamed, licha ya uwepo wa changamoto hizi, mamlaka hiyo inahitaji nini ili iweze kuwa katika nafasi nzuri ya kufanya shughuli za uokoaji ambapo alisema kwamba upatikanaji wa haraka wa taarifa unaweza kusaidia shughuli za uokozi.

“​​Kwa mfano, mpaka sasa hivi, sisi tunapata taarifa kutoka kwa wadau na wananchi, ila huko kwenye nchi za watu, moto ukitokea teknolojia inakupa taarifa hapo hapo,” alisema Mohamed. “Kwa hiyo, hilo likifanyika, basi jitihada za uokozi nazo zitaimarika.”

“Kitu cha pili ni kuongezwa kwa vifaaa vya kutolea huduma zaidi,” aliongeza. “Licha ya sasa kuongezwa vifaa kama gari mbili ambazo zimeongezwa kwa ajili ya kutoa huduma lakini ni vyema kuwa na gari nyingi ili kuweza kuwafikia wananchi kwa haraka.”

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kupamba na Maafa Zanzibar, Makame Khamis Makame, aliieleza The Chanzo kwamba mamlaka hiyo inatambua changamoto zinazozikabili juhudi za uokozi visiwani humo, akisema Serikali iko mbioni kuzifanyia utatuzi.

“Majanga na maafa ni jambo ambalo hakuna anayepanga yatokee lakini kuna kila sababu ya kuchukua tahadhari za awali,” alisema Makame.

“Pamoja na mambo mengine, elimu pia ni muhimu kwenye uokozi,” aliongeza. “Ndiyo maana, sisi kama kamisheni tunatoa elimu, hususan kwenye masuala ya matumizi sahihi ya vifaa vya umeme na pia kuwafundisha wananchi juu ya kujilinda.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. A good article Najjat. Story ya Asha kupoteza mwanae inasikitisha sana. Serikali inapaswa kufanyiw kazi suala la mitaa ambayo haifikiki kirahisi angalau iwe na horse pipes za maji ya zima moto ili kukabiliana na dharura hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts