The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CCM Yadaiwa Kupora Ardhi ya Wanakijiji Kilimanjaro

Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho yadaiwa kukodisha kinyemela ardhi ya kijiji yenye ukubwa wa takriban ekari tano kwa mtu binafsi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wakazi wa kijiji cha Mangio, kilichopo wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wameiandikia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiitaka ieleze kwa nini iliondoa shauri lao mahakamani kuhusu mgogoro wao na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wanayoishutumu kupora ardhi yao na kuikodisha kwa mtu binafsi.

Kwenye barua yao hiyo ya Mei 8, 2023, na ambayo The Chanzo imeiona, wanakijiji hao wanasema walifungua shauri hilo mwaka 2017, Mahakama Kuu, Moshi, kabla ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ijiunge kwenye shauri hilo mwaka 2022, na kuliondoa mahakamani Novemba 2022 bila ya kuwashirikisha.

“Tumesikitishwa sana na hatuafikiani na maamuzi uliyoyachukua,” inasema barua hiyo yenye majina na sahihi za watu 83. “Ni kwa sababu zipi, kimantiki na kisheria, zilizokusukuma wewe kufanya maamuzi peke yako ya kufuta shauri bila kutushirikisha sisi wananchi?”

“Ni kwa sababu zipi, kimantiki na kisheria, uliamua kufuta shauri mahakamani kabla Mahakama haijatatua mgogoro wetu?” inaendelea barua hiyo ambayo nakala pia imetumwa Wizara ya Katiba na Sheria. “Sisi [wanakijiji] tuchukue hatua gani za kisheria ili tupate haki yetu?”

Barua ambayo wanakijiji hao waliwasilisha kwa wakili wa serikali

The Chanzo iliiandikia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikitaka kufahamu kama imepokea barua hiyo ambapo ilijibu kwamba wameipokea na tayari wameanza kuifanyia kazi.

Kiini cha mgogoro

Kiini cha mgogoro kati ya wanakijiji hao na Jumuiya ya Wazazi CCM ni ardhi yenye ukubwa wa takriban ekari sita ambayo wanakijiji hao waliitoa mwaka 1976 kwa ajili ya upanuzi wa shule ya msingi iliyokuwepo kijijini hapo. Mwaka 1986, ilijengwa Shule ya Sekondari ya Mangio katika eneo hilo.

Hata hivyo, mnamo mwaka 1991, wanafunzi wa kwanza walifika Kidato cha Nne katika shule hiyo lakini hawakufanikiwa kufanyia mitihani katika kituo hicho kwa sababu sekondari hiyo haikuwa imesajiliwa, hali iliyowakuta tena wanafunzi wa Kidato cha Nne kwa mwaka 1992.

SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao

Hali hiyo iliwalazimu wananchi kutoka vijiji vilivyojenga shule hiyo kuanza mchakato wa kutafuta taasisi ambayo ingeisajili shule hiyo na kuendelea kuiendesha, huku umiliki wa ardhi ukibaki kwa vijiji. Ndipo mwaka 1993 Jumuiya ya Wazazi CCM walipokabidhiwa shule hiyo na kuisajili kwa ajili ya kuiendesha.

Hata hivyo, mnapo Januari 12, 2016, jumuiya hiyo iliwahamisha wanafunzi wote waliokuwa wakisoma katika shule hiyo baada ya kushindwa kuiendesha, ikikubaliwa kwamba shule hiyo ikabidhiwe kwa Serikali kwa ajili ya kufungua Kidato cha Tano na Sita au apewe mwekezaji aiendeshe kwa manufaa ya kijiji.

Jumuiya ya Wazazi CCM, katika hali iliyowashangaza wanakijiji hicho, haikuikabidhi shule hiyo kwa Serikali, badala yake ilimpatia mtu binafsi anayejulikana kwa jina la Yusuph Mfinanga ambapo nyaraka za Mahakama zinaonesha alipatiwa kwa Shilingi milioni 81.

Ndipo wanakijiji wa Mangio, hapo mwaka 2017, walipofungua kesi dhidi ya Jumuiya ya Wazazi CCM katika Mahakama Kuu ya Moshi, Kitengo cha Ardhi, ambayo, hata hivyo, iliondolewa mahakamani hapo Novemba 2022 bila ya hukumu kutolewa, hali iliyowaacha wanakijiji na maswali mengi.

Kinyemela

Moja kati ya wanakijiji waliozungumza na The Chanzo kwa sharti la kutotajwa majina yao wakisema wanahofia usalama wao alidai zoezi zima la kuhamisha ardhi hiyo kutoka kwa wanakijiji kwenda kwa Mfinanga lilifanyika kinyemela, huku akisema hakuna kumbukumbu zozote za malipo.

“Hii kesi imekaa zaidi ya miaka mitano mahakamani [na] hakuna mahali mzee Yusuph Mfinanga ametoa risiti ya kulipia hizo fedha,” kilisema chanzo hicho.

“Hata Jumuiya [ya Wazazi CCM] haikutoa [risiti],” aliendelea mwanakijiji huyo. “Angekuwa nayo, [Mfinanga] angeleta kama ushahidi. Lakini hakuna mahali Jumuiya imetoa kwamba tulipokea fedha hizi. Ina maana ni fedha zilizoliwa na wajanja tu.”

SOMA ZAIDI: Apigania Haki Yake ya Ardhi Kwa Miaka 36 Bila Mafanikio

The Chanzo ilimtafuta Mfinanga kwa njia ya simu kumuuliza alipataje haki ya kuendesha ardhi ambapo aligoma kutoa jibu lolote, akimtaka mwandishi awatafute watu kutoka Jumuiya ya Wazazi CCM.

“Waulize watu wa CCM, mimi sijui,” Mfinanga alisema. “[Hao wananchi] walikwambia wananinadai mimi? Wanawadai CCM. Sasa nasema hivi, wapigie watu wa CCM. Mimi siwezi kuongea lolote juu ya mambo yao.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Wilaya ya Mwanga, Hamza Mwanga, alikataa kuzungumzia suala hilo, akidai yeye siyo msemaji wa jumuiya hiyo.

“Ukitaka mtu sahihi, mpigie Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, ndiye mtu sahihi ambaye atakuelekeza uipigie tume ya chama inayomiliki maeneo hayo,” Mwanga aliiambia The Chanzo. Juhudi za kumpata Katibu Mkuu, hata hivyo, hazikuzaa matunda.

Siyo kesi pekee

Hata hivyo, hii siyo kesi pekee inayohusisha migogoro ya ardhi kati ya CCM na jumuiya zake mbalimbali na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwenye ripoti yake ya mwaka wa fedha 2020/2021, kwa mfano, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alionesha kwamba ndani ya mwaka huo kulikuwa na jumla ya mashauri 108 katika Mahakama mbalimbali nchini, 86 kati yao yakihusu ardhi, baina ya CCM na wananchi.

Pia, mnamo Februari 15, 2023, Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, iliiamrisha Bodi ya Wadhamini ya CCM na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusitisha shughuli zote katika eneo lenye mgogoro kati yao na Kanisa Katoliki mkoani humo.

SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama

Bernard Baha ni Mratibu wa Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA), jukwaa linalojihusisha na utetezi kwenye eneo la ardhi, ambaye ameiambia The Chanzo kuwa suala la migogoro ya ardhi kati ya CCM na wananchi lipo na linaendelea katika maeneo mengi nchini na ambayo mpaka sasa bado halijapatiwa ufumbuzi.

“Ni kesi ambazo tunakutana nazo sana kwenye shughuli zetu,” Baha aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum.

“Nadhani namna nzuri ya kutatua kesi hii mahususi [ya Mangio], ni muhimu kuangalia makubaliano ya awali yalikuwa ni yapi haswa, kama yalifanyika kisheria au la,” Baha aliongeza. “Hiyo itakuwezesha kujua kama mtu aliyepo sasa kwenye eneo analikalia kihalali au ametumia ujanja ujanja tu.”

Walaumiwe viongozi?

Malalamiko haya ya wanakijiji cha Mangio yanakuja wakati ambapo Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amewataka viongozi wa Serikali na chama hicho tawala kuchukua juhudi za makusudi kutatua migogoro ya ardhi inayowaathiri wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

SOMA ZAIDI: Mgogoro Kati ya Wakulima, Wafugaji Wanukia Songwe

Akizungumza wilayani Mvomero, mkoani Morogoro hapo Januari 29, 2023, kwenye muktadha tofauti, Chongolo alisema kwa kiwango kikubwa migogoro ya ardhi nchini husababishwa na viongozi wa chama na Serikali katika juhudi zao za kupigania maslahi binafsi.

“Sisi viongozi ndiyo wenye jukumu la kutatua changamoto [za migogoro ya ardhi], viongozi tukinyooka, na tukasimamia sheria ya nchi, kwa sababu hakuna kijiji kisicho na mpaka kwani yote imeanishwa, hakutakuwa na shida,” Chongolo aliwaambia wananchi.

“Ukiona kuna shida [kati] ya kijiji na kijiji, ujue viongozi wenyewe ndiyo wanashida.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts