The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mgogoro Kati ya Wakulima, Wafugaji Wanukia Songwe

Wakulima walalamika wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba; wafugaji wasema hawana pa kulisha mifugo yao.

subscribe to our newsletter!

Songwe. Mgogoro unanukia kati ya wakulima wa mazao mchanganyiko na wafugaji katika tarafa ya Songwe mkoani hapa kufuatia malalamiko kutoka kwa wakulima kwamba wafugaji wamekuwa wakivamia mashamba yao nyakati za usiku na kulisha ng’ombe wao.

Malalamiko hayo kutoka kwa wakulima yamekuwa ni ya siku nyingi, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, kuandaa mkutano wa hadhara na wakulima hao hapo Mei 22, 2023, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufanyia kazi malalamiko hayo.

Wakizungumza kwa hisia kali kwenye mkutano huo, wakulima walisema hali hiyo imekuwa ikiibuka kila mwaka kuanzia Machi hadi Juni ambapo mifugo ambayo wamiliki wake hawajulikani huingia kwenye mashamba yao na kula mazao yao.

Wakulima hao ambao hufanya shughuli zao katika Bonde la Mwambani, wamedai kwamba wafugaji hao huingiza mifugo yao kwenye mashamba yao nyakati za usiku, wakizitaka mamlaka husika kuingilia kati na kuwaondoshea usumbufu huo.

Ignas Sinkala, 61, ni moja kati ya wakulima hao waliolalamikia hali hiyo, huku akidai wafugaji hao wamekaa kishari kwani hutembea na silaha kama visu wakati wanapofanya shughuli zao za ufugaji, hali anayodhani siyo ya kawaida.

Sasa kisu cha nini?

“Ukienda bondeni huko mtu anachunga ng’ombe ana fimbo na kisu, sasa kisu cha nini?” alihoji Sinkala, baba wa watoto sita kutoka kijiji cha Mwambani.

“Kuchunga ng’ombe kunahitaji fimbo basi, sasa kisu cha nini?” aliendelea kuhoji. “Kwa hiyo, kwa kweli tunashida sana hapa, yaani tunashida sana na wenzetu wafugaji tunawapenda lakini Serikali imetuletea watu ambao hawatupendi.”

Magolot Kapondola ni mkulima anayejihusisha na kilimo cha mpunga na mahindi katika Bonde la Mwambani ambaye alisema kwenye mkutano huo na Mkuu wa Wilaya kwamba alikuta mahindi yake yameliwa na kuharibiwa na ng’ombe muda mfupi tu baada ya kutoka shambani.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali Inataka Wafugaji Watumie Mfumo wa Utambuzi Mifugo wa Kieletroniki?

“Hii hali kusema ukweli inatuumiza,” Kapondola, 48, alisema kwenye mkutano huo. “Si mchukii mfugaji, naichukia mifugo. Mifugo ikae sehemu inayotakiwa. Tunaiomba Serikali, watafutieni nao [wafugaji] sehemu ya kukaa na sisi tubakie na mashamba yetu.”

Sadick John Chikundu, mkulima wa alizeti, mpunga, na mahindi katika Bonde la Mwambani, aliujulisha mkutano huo kwamba haitakuwa na maana kwa wakulima na mamlaka kupambana na wafugaji.

Chikundu alishauri mapambano yaelekezwe kwa viongozi wa Serikali wanaodaiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu kuingia kwenye mashamba yao.

“Shina lipo ndani kwenye wilaya yako hapo, [Mkuu wa Wilaya],” Chikundu, 30, alisema kwenye mkutano huo.

“Ili kudhibiti hili suala, cha kwanza inatakiwa wewe ukae na viongozi wako, na ikiwezekana wale wafugaji waitwe, huenda wakakusaidia kujua nani anayesababisha sisi [wakulima] kuteseka hapa,” aliongeza mkulima huyo.

Malalamiko haya yamekuja licha ya kuwepo kwa katazo linalowataka wafugaji kutoshusha mifugo yao kutoka milimani kwenda bondeni kipindi cha masika mpaka Julai 30, katazo ambalo, hata hivyo, baadhi ya wafugaji wamekuwa wakilikiuka.

Mifugo itakula wapi?

The Chanzo ilimuuliza Lushona Paulo Makula, Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Songwe, anayazungumziaje malalamiko hayo ya wakulima, ambapo alikiri kuwa ni malalamiko ya msingi yanayotokana na baadhi ya wakulima kukaidi agizo la kutoshusha mifugo mabondeni.

Hata hivyo, Makula alisema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wafugaji hawana sehemu ya kulisha mifugo yao, huku akilalamika kwamba Serikali imeshindwa kuwatengea wafugaji maeneo mahususi ya kulisha mifugo yao.

SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama

“Tuna malisho yaliyokuwa yametengwa lakini yako kwenye makaratasi tu,” Makula alisema kwenye mahojiano hayo. “Yale maeneo tayari yalishatelekezwa na yakavamiwa na watu wa makazi. Tujiulize, mifugo itakula wapi?”

Akizungumza kwenye mkutano huo na wakulima, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, alisema tayari Serikali imeunda timu itakayochunguza tuhuma za rushwa ili kuruhusu wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

“Tumebaini kwamba katikati yetu viongozi kuna ambao wametusaliti, kama mnavyosema wananchi,” Itunda alisema.

“Sasa, tumeanza vikao vya ndani ili kabla ya kuanza pambano na adui wetu ni lazima tuwe wote safi. Wasaliti tuwajue,” aliongeza. “Tumeunda tume kupitia wenzetu wa TAKUKURU, ili wafanye uchunguzi kujua na nani wanatusaliti.”

Migogoro kati ya wakulima na wafugaji imekuwa ikiendelea kwa miaka mingi mkoani Songwe, huku lawama, kwa kiwango kikubwa, zikielekezwa kwa viongozi wa vijiji na vitongoji wanaodaiwa kupokea hongo na kuchochea migogoro hiyo.

Tatizo kubwa

Hata hivyo, Songwe siyo sehemu pekee ya nchi inayokabiliwa na migogoro isiyokwisha kati ya wakulima na wafugaji, kwani migogoro kama hiyo imekuwa ikiripotiwa sehemu nyingine mbalimbali za nchi.

Mnamo Disemba 26, 2022, kwa mfano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza wakuu wa wilaya wote nchini kufanya vikao na wafugaji kutoka maeneo husika ili kuweka namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kutambua mifugo yao na kuweka zuio la mifugo mingine kuingizwa katika wilaya hizo.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tanzania Inahitaji Sera Mpya ya Mifugo, Uvuvi?

Hata hivyo, kwenye tathmini yake ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini iliyoitoa Novemba 11, 2022, chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kilihusisha migogoro hiyo na utungaji wa sera na sheria za ardhi kwa malengo ya kibiashara badala ya kumlinda mwananchi.

ACT-Wazalendo iliishauri Serikali kuharakisha na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha, na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano.

“Mamlaka za halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi,” chama hicho kilipendekeza.

“Vilevile, mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji yaimarishwe, kusimamiwa, na kujengewa uwezo ili yaweze kushugulikia, kuamua, na kutatua masuala ya ardhi katika maeneo yao kwa wakati,” ACT-Wazalendo ilishauri kwenye tathmini yake.

Asifiwe Mbembela ni Mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *