The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Amnesty International Yaishutumu Tanzania Kukiuka Haki za Binadamu Loliondo

Serikali yaiita ripoti hiyo “uzushi.”

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeishutumu Serikali ya Tanzania kukiuka haki za binadamu za wenyeji wa Loliondo, Arusha, kwenye zoezi la kumega ardhi inayodaiwa kuwa ni ya kijiji kwa ajili ya kupanua pori tengefu la Loliondo hapo Juni 10, 2022.

Zoezi hilo lililohusisha Serikali kuchukua kilomita za mraba zipatazo 1,500 kutoka kwa ardhi ya kijiji inayokisiwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4,000 lilichochea mtafaruku baina ya wenyeji wa Loliondo, wengi wao wakiwa ni kutoka kabila la Wamaasai, na maafisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo polisi.

Wenyeji kadhaa walijeruhiwa baada ya maafisa polisi kufika eneo hilo kujaribu kuzuia wenyeji hao wasipinge zoezi hilo, huku askari mmoja aliyetambulika kwa jina la Garlus Mwita Garlus akiuwawa. Jumla ya viongozi 20 wa Kimaasai walishtakiwa kwa mauaji hayo, kesi ambayo Serikali iliiondoa mahakamani hapo Novemba 22, 2022.

Kwenye ripoti yao hiyo waliyoitoa Juni 6, 2023, Amnesty International imeishutumu Serikali kuwanyanyasa wenyeji wa Loliondo kwenye zoezi lake hilo, ikidai Serikali ilitumia nguvu pasipo na sababu za msingi, kuhamisha wenyeji kwa nguvu, na kuwakamata na kuwaweka kizuizini kiholela.

Amnesty wanadai kwamba zoezi hilo liliwaacha wenyeji wa Loliondo wapatao 70,000 bila maeneo ya kulisha mifugo yao, ambayo ni shughuli kubwa ya kiuchumi wanayoitegemea kuendesha maisha yao ya kila siku na kusaidia familia zao.

SOMA ZAIDI: Kuondolewa Wakazi Loliondo: Kama Siyo Machozi Yao, Kipi Kitazuia Operesheni ya Serikali Dhidi ya Wakazi Hao?

Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International Afrika Mashariki, amenukuliwa kwenye taarifa ya shirika hilo akisema kwamba zoezi hilo lilihusisha uhamishaji wa watu kutoka kwenye maeneo yao bila ridhaa yao kama sheria na taratibu za kimataifa zinavyotaka.

“Serikali ya Tanzania inapaswa, kwa haraka sana, itambue na kutekeleza haki za Wamaasai kwenye maeneo yao ya asili na maliasili zingine,” Chagutah alinukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema. “Serikali ni lazima iheshimu matakwa ya sheria za kimataifa.”

Upotoshaji

Hata hivyo, Serikali imekanusha vikali kwamba zoezi lake hilo la Juni 10, 2022, lilihusisha ukiukwaji wa haki za binadamu, huku Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro akibaisha kwamba askari waliokuwepo eneo hilo walikuwa watulivu licha ya kukabiliwa na hatari kutoka kwa wenyeji waliokuwa wanapinga mpango huo.

Akizungumza na BBC Swahili hapo Juni 6, 2023, Ndumbaro pia alikanusha kwamba zoezi hilo lilihusisha uhamishwaji wa watu kutoka kwenye maeneo yao ambayo wamekuwa wakiishi siku nyingi.

“Kuna habari nyingi za upotoshaji kuhusu ardhi na wakazi wa Loliondo,” Ndumbaro alinukuliwa akisema. “Hakuna mtu atakayetolewa kwenye eneo hilo, na Serikali haina mpango wa kuwaondoa au hata kutumia nguvu yoyote dhidi ya wakazi wa Loliondo.”

SOMA ZAIDI: Kashfa ya Loliondo Inatuonyesha Kwamba Uhifadhi Tanzania Upo Kwa Malengo ya Kibiashara, Siyo Kulinda Mazingira

Hata hivyo, Juni 10, 2022, wakati tukio hilo lilipotokea, picha na video zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha wenyeji wa Loliondo wakiwa na majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya miili yao.

Video nyingine pia zilionesha wenyeji wa maeneo hayo wakiwa katika taharuki ya kulinda usalama wao, huku milio ya kufyatuliwa kwa risasi ikiwa inasikika kutoka kwenye video hizo pia.

Kwenye ripoti yao hiyo iliyopewa jina la ‘We Have Lost Everything: Forced Evictions of the Maasai in Loliondo, Tanzania,’ Amnesty International imeishutumu Serikali kuwapiga risasi na mabomu ya machozi wenyeji waliokuwa wanapinga mpango huo, ikisema jumla ya majeruhi 40 walipatikana kutokana na vitendo hivyo.

Kwenye vurugu hizo pia alipotea mzee wa Kimaasai mwenye umri wa miaka 84, aliyetambulika kwa jina la Oriaisi Pasilance Ng’iyo, ambaye mpaka sasa hajulikani alipo. Kwa mujibu wa Amnesty, Serikali imekana kumshikilia.

Kukimbia makazi

Amnesty pia wanadai kwamba vurugu hizo zilipelekea wenyeji wengi kukimbia makazi yao na kutafuta hifadhi maporini, ikiwemo kwenye misitu na hifadhi za taifa.

Wengine pia walikimbilia nchini Kenya, kwenye eneo linaloitwa Narok, ambapo kwa mujibu wa Amnesty mpaka kufikia Mei 2023, jumla ya familia 60 za wenyeji wa Loliondo walikuwa wakiishi huko.

Amnesty International imeitaka Serikali kufanya uchunguzi huru na wa wazi juu ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wenyeji wa Loliondo, ikiwemo kifo cha Mwita, askari polisi aliyeuwawa kwenye hamkani hizo, na watu ambao mpaka sasa hawajajulikana walipo kama Mzee Ng’iyo.

Mnamo mwaka 2022, Serikali ilisema uamuzi wake huo wa kumega ardhi hiyo inayodaiwa kuwa ya kijiji ulitokana na nia yake ya kuhifadhi maeneo ambayo wanyama huzaliana, ambayo Serikali ilidai mara nyingi yamekuwa yakivamiwa na wafugaji.

Kwa siku za hivi karibuni, Serikali imejikuta katika wakati mgumu wa kutetea maamuzi yake huko Loliondo na Ngorongoro, ambako nako inaendesha zoezi la kuwahamisha wenyeji wake na kuwapeleka Tanga kwa madai kwamba kuongezeka kwa idadi ya watu huko kunahatarisha eneo hilo ambalo ni hifadhi ya taifa.

SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo wa Kile Kinachoendelea Ngorongoro

Baadhi ya wenyeji kutoka maeneo haya, wakiungwa mkono na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu ya nje na ndani ya nchi, wamekuwa wakizikosoa juhudi hizo za Serikali, wakisema siyo shirikishi na zinafanyika katika mazingira ya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, shutuma ambazo Serikali, hata hivyo, imeendelea kuzikanusha.

Lukelo Francis ni mwandishi wa habari kutoka The Chanzo, Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *