Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.
Sasa, tunapozungumzia mabadiliko ya tabianchi, na tumeshaona kwamba ni kweli kuna mabadiliko ya tabianchi, na ushahidi upo kwa hapa Tanzania mabadiliko ya tabianchi yanatokezea.
Tunaposema kwamba inabidi tuchukue hatua kukabiliana nayo, ina maana tunaangalia kwamba haya mabadiliko ya tabianchi yana athari gani? Mabadiliko ya tabianchi yana athari tofauti kwa jamii tofauti duniani kutegemeana na sababu mbalimbali.
Sisi hapa kwetu [Tanzania], kwa sababu mabadiliko ya tabianchi ambayo tunayaona sana ni kupungua kwa kiasi cha mvua, yaani mvua kunyesha nje ya msimu ambao tumeuzoea, na ukame kuongezeka, hiyo inakuwa na athari sana katika maisha yetu na katika uchumi wetu kwa sababu maisha yetu sisi kama Watanzania yanategemea sana tabianchi na hali ya hewa.
Shughuli zetu za kujikimu kimaisha, kama ambavyo tunafahamu, takwimu zinaonesha, asilimia 65 ya nguvu kazi ya Watanzania iko katika sekta ya kilimo, halafu takwimu nyingine zinaonesha kwamba asilimia kubwa ya kilimo chetu kinategemea mvua, kinategemea mazingira yetu jinsi yalivyo.
Kwa hiyo, huu utegemezi wetu katika tabianchi ya eneo kwa ajili ya kufanya kilimo chetu ndiyo inapelekea kwamba tunaathirika zaidi.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua
Ndiyo maana kumekuwa na uhaba wa chakula katika maeneo tofauti tofauti. Kumekuwa na njaa. Ina maana hata kile tunachokizalisha kwa ajili ya kwenda kuuza nje ya nchi kuweza kujipatia fedha ambazo zitasaidia katika maendeleo tofauti tofauti inakuwa inaathiriwa kwa sababu hiyo.
Hiyo ni eneo mojawapo, kwamba watu wetu wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo na kwa sababu kilimo chetu ni kilimo ambacho kinategemea sana hali ya hewa, ama tabianchi, kinaathiriwa kwa kiasi kikubwa na hivyo wananchi pamoja na taifa tunaathirika.
Utalii, usafirishaji
Lakini vilevile sekta zetu zingine za uchumi zinaathirka. Sekta nyingine ambayo inachangia sana katika uchumi ni sekta ya utalii. Kuna makadirio yanayosema kwamba, kwa mfano, ile theluji katika Mlima Kilimanjaro itaenda kupungua.
Kwa hiyo, kuna wanao jiuliza je, ile theluji katika Mlima Kilimanjaro ikipungua watalii wataendelea kuja ama watashindwa kuja?
Lakini pia hizi mvua zinazonyesha nadhani kila mtu anafahamu kumekuwa na matukio ya madaraja kukatika kutokana na mafuriko sehemu tofauti tofauti Tanzania katika miaka ya hivi karibuni kuliko hata kipindi cha nyuma.
Mwaka huu [wa 2023] peke yake tu tulisikia daraja kwenye hii njia ya kuunganisha Chalinze, Pwani na Segera, Tanga kuna daraja limekatika pale.
Sasa kama miundombinu kama hiyo inaathiriwa ina maana hata sekta ya utalii na usafirishaji wa watu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine itaathiriwa vilevile na uchumi wetu unategemea sana sekta ya utalii.
Zanzibar, kwenye visiwa vya Unguja na Pemba, kuna watafiti ambao walionesha kwamba kuna kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari ambacho kimepelekea mmomonyoko katika maeneo ya pwani kwenye fukwe zetu, ambayo ile nayo imeharibu miundombinu, imeharibu vivutio vingine vya utalii ambayo itaenda ikiathiri hii sekta ya utalii.
Nishati
Lakini vilevile masuala ya nishati na nishati yetu tunategemea sana uzalishaji kwa kutumia maji.
Mabwawa haya ya kuzalisha umeme sasa jinsi ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanapelekea kupungua kwa mvua na hivyo kupungua kwa kiasi cha maji ambacho kinakwenda katika mito yetu ndivyo ambavyo tumekuwa tukifahamishwa mara kwa mara kwamba kumekuwa na kupungua kwa uzalishaji umeme ndiyo maana kumekuwa na mgao wa umeme.
SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?
Kwa hiyo, bila ya kuangalia njia mbadala za kupata nishati, utegemezi wetu katika nishati ambao unatokana na maji, ina maana tunaendelea kuathirika na sekta ya nishati ikiathirika ina maana na sekta nyingine zinazotegemea nishati ya umeme zitaendelea kuathirika. Kwa hiyo, maisha ya watu pamoja na uchumi wa taifa utendelea kuathirika.
Lakini vilevile kuna ushahidi wa tafiti ambao unaonesha kwamba haya mabadiliko ya tabianchi ambayo yamepelekea ukame, kuongezeka kwa joto katika baadhi ya maeneo hapa Tanzania na mvua kunyesha imepelekea, kwa mfano, mbu kuweza kuishi katika maeneo ambayo zamani walikuwa hawaishi na hivyo kupelekea kuibuka kwa malaria katika yale maeneo.
Kiwango cha malaria ambacho kinaripotiwa maeneo kama ya Kilimanjaro, maeneo ya Iringa, na maeneo mengine ni tofauti na miaka iliyotangulia na hii inasemekana ni kutokana na kuongezeka kwa joto katika yale maeneo na kuongezeka kwa joto kumetokana na haya mabadiliko ya tabianchi.
SOMA ZAIDI: Nini Kinadhihirisha Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania?
Lakini vilevile hizi mvua zinaponyesha nyingi na kusababisha maafa zinapelekea pia kuongezeka kwa homa za matumbo, kipindupindu, nakadhalika. Kwa hiyo, bila kujipanga, haya mabadiliko ya tabianchi yanaenda kuathiri pia sekta ya afya na hivyo kuathiri nguvu kazi, maisha ya watu, na uchumi kiujumla.
Na sekta zetu nyingine pia katika nchi yetu ya Tanzania zinaenda kuathirika kwa sababu tuna utegemezi katika mazingira yetu katika hali ya hewa yetu na katika tabianchi.
Kwa hiyo, hizo ndizo sababu zinapelekea kwamba ni lazima tuzungumzie haya mabadiliko ya tabianchi kwa sababu yana athari kwa mtu mmoja mmoja mpaka kwa kitaifa, lazima tuyafahamu, ili tuweze kuchukua hatua stahiki za kukabiliana nayo.
Sasa hayo niliyoelezea yalikuwa ni yale ambayo tunaweza tukasema kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zile athari ambazo ni za moja kwa moja. Lakini kuna athari nyingine ambazo siyo za moja kwa moja.
Utegemezi
Na nimesema kwamba ni kwa kiwango gani tutaathirika na athari za mabadiliko ya tabia nchi inategemea na ile wanayoita exposure yetu, utegemezi wetu katika tabianchi na hali ya hewa ya eneo. Ikibadilika, basi tunaweza kuathirika.
Lakini vilevile ni kwa kiwango gani tutaathirika inasababishwa vilevile na hali yetu ya kiuchumi iliyopo, au hali yetu ya umaskini, pamoja na mifumo tuliyonayo, hiyo pia inachangia.
Kama tuna uchumi mzuri, watu wana kipato kizuri, ina maana hata zikitokea hizi athari za mabadiliko ya tabia nchi tunaweza tukakabiliana nazo.
Tuchukulie mfano kwamba mvua zimenyesha, zimeharibu shamba la mtu. Lakini kwa hali ya umaskini wa yule mtu, hana uwezo wa kwenda kununua tena mbegu na kwenda kuzipanda tena.
SOMA ZAIDI: Wananchi Mkuranga Walia Na Athari Za Mabadiliko Tabia Nchi
Kwa hiyo, ataathirika sana, lakini angekuwa na uchumi mzuri, ina maana angeweza kwenda kununua mbegu nyingine akaja akapanda, akafanya kilimo cha umwagiliaji, na maisha yake yakaenda vizuri.
Kwa hiyo, hali zetu za kiutamaduni, za kiuchumi, za kisiasa, zinachangia kwa kiasi gani sisi tutaathirika na haya mabadiliko ya tabianchi.
Migogoro
Lakini pia mabadiliko haya ya tabianchi yenyewe yanaenda kuongeza athari katika matatizo mengine ambayo tayari tunayo katika jamii. Kwa mfano, tunafahamu kwamba kumekuwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Kumekuwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima tu wadogo wadogo na wakulima wakubwa, watu wanaoenda kutafuta maeneo ya uwekezaji, nakadhalika.
Sasa mabadiliko ya tabianchi yanapelekea baadhi ya watu kuweza kuondoka katika maeneo fulani ambayo yale maeneo yameathirika zaidi na kwenda katika maeneo mengine.
Wanapofanya hivyo wanaenda kule kunakuwa na ushindani wa zile rasilimali ambazo zinapatikana kule.
Lakini kadri ambavyo kipato cha mtu mmoja mmoja na kaya kinavyoenda kuathirika inaweza kuchochea vilevile athari nyingine katika jamii.
Unyanyasaji dhidi ya wanawake au ukatili wa kijinsia, kwa mfano, unaweza kusema, unaweza ukaongezeka kwa sababu ya migogoro ambayo itatokea ya jinsi ya kutumia rasilimali ama maliasili zilizopo ndani ya familia na katika kitaifa vilevile.
Kwa hiyo, wale ambao wanaonekana kwamba ni wanyonge watazidi kuwekwa kando kwa sababu zile maliasili, ama zile rasilimali, zimezidi kuwa muhimu katika kuweza kukabiliana, ama kuweza kustahimili, athari zinazotokana na haya mabadiliko ya tabianchi.
Hapa Tanzania tunafahamu kabisa kwamba, kwa mfano, kuhama hama kwa wafugaji na kwenda katika maeneo ambayo ni ya wakulima kunachangiwa, kwa kiasi fulani, na haya mabadiliko ya tabianchi.
Lakini vilevile kunachangiwa na sera na sheria ambazo ni mbovu pamoja na utekelezaji wake ambao unapelekea watu kulazimika kuhama na kule wanakoenda kushindwa kutatua migogoro ambayo inaibuka na hivyo matatizo kuweza kuongezeka.
Kwa hiyo, kuna muingiliano baina ya yale matatizo ambayo tunayo katika jamii zetu na haya mabadiliko ya tabianchi.