The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunawezaje Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi?

Ni muhimu Tanzania kuendesha shughuli zake za kiuchumi kwa namna inayopunguza utegemezi wake kwenye tabianchi, ikiwemo kufanya kilimo cha umwagiliaji.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji. 

Mbinu kubwa za jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinawekwa katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni ile inayoitwa kuzuia, ama mitigation, yaani kuzuia mabadiliko ya tabianchi yasiendelee kutokezea.

Na hii, kwa uchache, ni kwamba inachukuliwa ili tuweze kupunguza kiasi cha hewa ukaa, na hewa nyingine ambazo zinasababisha mabadiliko ya tabianchi, tupunguze uzalishaji wake kwa kubadilisha mifumo yetu, iwe ni katika viwanda, [au] iwe ni katika usafirishaji tutumie, kwa mfano, nishati mbadala, nishati ambazo hazizalishi hewa ya ukaa. Kwa hiyo, ni katika kupunguza tatizo lisiendelee kuongezeka.

Lakini kwa sababu tatizo lipo, na tunakabiliana nalo, mbinu nyingine ya kukabiliana nayo ni adaptation, yaani kukabiliana na tatizo ambalo tayari linatokea. 

Kwa sababu tayari tumeshajua mvua zinanyesha nje ya msimu, tayari tunajua kwamba vipindi vya ukame vitaongezeka kwa nchi zile ambazo ni za kaskazini, inafahamika kabisa majira yale ya baridi, baridi itakuwa kali zaidi na majira ya joto vipindi vya joto vitakuwa ni vya juu zaidi kuliko ilivyozoeleka, je, tunakabiliana nayo vipi?

Mbinu hizi zinategemea na mchango wa nchi husika katika kusababisha tatizo. Haina mantiki sana kwa nchi kama Tanzania kuwekeza zaidi katika kuzuia, kwa sababu uzalishaji wetu wa hewa ukaa, pamoja na hizo gesi nyingine, uko chini sana ukilinganisha na nchi nyingine, hasa nchi ambazo zimeendelea. 

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua

Kwa hiyo, sisi kwa rasilimali zetu chache tulizonazo, rasilimali fedha nakadhalika, inatupelekea tuangazie zaidi katika namna ya kukabiliana, yaani adaptation kwa sababu sisi kutokana na hali yetu kiuchumi, mifumo yetu ya kitaasisi kuwa duni uwezo wetu wa kukabiliana unakuwa ni mdogo. 

Lakini vilevile, maisha yetu yanategemea zaidi vyanzo, ama shughuli, ambazo zinaathiriwa zaidi na masuala ya hali ya hewa pamoja na mabadiliko ya tabianchi, kwa mfano, kilimo, uvuvi, ufugaji, nakadhalika.

Kwa hiyo, sisi ni lazima, tunalazimika, kuwekeza zaidi katika adaptation, yaani kukabiliana na hayo mabadiliko ya tabianchi. Sasa ni mbinu gani ambazo zinaweza zikatumika inategemea na kwenye sekta [husika].

Sasa nitagusia tu katika zile sekta ambazo ni kubwa na zinazogusa uchumi wetu na maisha ya watu wengi katika taifa letu. Tukianza na kwenye kilimo, moja kwa moja inaonesha kabisa kwanza, inabidi tuwe na kilimo ambacho siyo tegemezi sana katika misimu ya mvua. 

Kilimo cha kisasa

Na kilimo hicho kinajulikana kwa majina tofauti tofauti lakini kuna aina ya kilimo ambayo inajulikana kwa jina la climate-smart agriculture, yaani kutokana na mabadiliko ya tabianchi tuwe na kilimo ambacho kinaendana na hayo mabadiliko.

Na kilimo hicho ni kilimo kile ambacho kinaangalia hali ya ikolojia ya lile eneo, ili kuweza kuamua ni mazao gani ambayo yatalimwa pale, yanayoendana na ile hali pale. 

Kwa sababu tunajua kabisa ukame utaongezeka, ina maana ili kukabiliana na hiyo hali ya ukame ni vizuri kupanda aina ya mazao ambayo yanastahimili kuliko kupanda mazao ambayo unajua katika ukame hayawezi kustahimili. 

SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?

Na mazao haya yanafahamika kwa mfano mtama, mihogo, karanga, nakadhalika. Lakini mazao kama mpunga na mahindi, ambayo ndiyo mazao yetu ya chakula, pamoja na ngano yenyewe, yanaathiriwa kwa urahisi zaidi na ukame.

Kwa hiyo, ili tuweze kukabiliana nayo ni lazima tufanye mabadiliko pia katika mazao ambayo tunayalima. Lakini hata katika yale mazao tunaweza kutumia mbinu tofauti tafouti kuweza kuwa na teknolojia, kwa mfano, hizi wanaita hybrid seeds, mbegu ambazo zimeboreshwa kimaabara ili kuweza kukabiliana na hali ya ukame. 

Kwa hiyo, hata kama ni mbegu za mtama lakini zinakuwa mbegu za mtama ambazo zinaweza kustahamili ukame zaidi kuliko zile mbegu za asili ambazo tumezizoea. 

Lakini vilevile tuwekeze zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa takwimu zilizopo ni kwamba tuko chini ya asilimia 10 ya matumizi ya eneo ambalo tunaweza tukalitumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, hii ni fursa nyingine na kuna mbinu nzuri tu za kufanya kilimo cha umwagiliaji. 

Kuna hii wanaita drip irrigation, ambapo wanaweka mipira maji yatoke kidogo pale tu kwenye ule mmea na siyo kutapanya maji katika eneo lote. Hizo ni mbinu ambazo kwa sababu tunategemea sana katika sekta ya kilimo zinaweza zikatumika na zikasaidia na tusisubiri mpaka mvua zinyeshe.

SOMA ZAIDI: Nini Kinadhihirisha Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania?

Yale maji yatakayokusanywa, tutakayoyavuna, hata kama mvua zitanyesha nje ya msimu, itanyesha katika muda mfupi tuweze kuyavuna yale maji na kuyahifadhi, tuweze kuyatumia kwa ajili ya kufanya kilimo cha umwagiliaji. Hiyo ni mbinu nyingine. 

Uhifadhi wa mazao

Mbinu nyingine ni kuboresha namna  tunavuna na kuhifadhi mazao yetu katika sekta hii ya kilimo. 

Mara ya mwisho takwimu ambazo niliziona ilionesha kwamba uharibifu, ama kupotea, kwa mazao kunakosababishwa na mbinu duni za uvunaji na uhifadhi wa mazao yetu kunapelekea kupoteza mpaka asilimia 40, nadhani, ya mazao yetu kwa sababu tunatumia mbinu duni za kuvuna, tunapoteza mazao na mbinu duni za kuhifadhi.

Kiasi kwamba unakuta, kwa mfano, maeneo ya Tanga kama Muheza [na] Segera kipindi cha msimu wa machungwa, machungwa ni mengi na yanaoza. Wakati yale yangeweza kuchakatwa, yakahifadhiwa, au yakasafirishwa kwenda kuwa chakula mahali pengine nchini. 

Kwa hiyo, unakuta kwamba kuna mazao kama hayo ambayo yangeweze kutengeneza kipato, yangeweza kuwalisha watu maeneo mengine, lakini kutokana na mbinu duni tulizonazo inapelekea kwamba kuna kuwa na upotevu wa hali ya juu. Kwa hiyo, hiyo ni mifano ya mbinu ambazo tunaweza kutumia katika sekta ya kilimo.

SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania

Ukienda kwenye uvuvi vilevile, kuna mbinu ambazo zinaweza zikatumika za kuweza kuboresha sekta yetu ya uvuvi ili kuweza kutengeneza kipato kwa kaya moja moja, mvuvi mmoja mmoja, na mpaka kitaifa. 

Na mbinu nyingine zipo, na hasa katika makabrasha mbalimbali ya upande wa Serikali, unakuta kabisa zimeanishwa pale, zimewekwa, ni mbinu nzuri sana, ila tatizo lililopo linakuja kwamba utekelezaji wake ndiyo unakuwa unakwama, kwa sababu mifumo yetu ya kitaasisi bado inaonekana ni duni. 

Lakini vilevile, uwezo wa kifedha kuwekeza katika kuhakikisha kwamba baadhi ya hizo mbinu ambazo zimejaribiwa na kuonesha kwamba zina manufaa kuweza kufanyika katika kiwango kikubwa maeneo mengi nchini. 

Unakuta kwamba hakuna hizo rasilimali fedha za kutosha, kwa mfano, za kuweza kushawishi watu wengi waweze kuwekeza katika kutekeleza hizo mbinu mbalimbali ili kuweza kukabiliana na hayo mabadiliko ya tabianchi.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Apangua Hoja za Wanaopinga Uwepo wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi

Fursa kwenye gesi

Lakini vilevile, ukienda kwenye sekta yetu ya nishati, tunafahamu tuna gesi asilia, na tafiti zimekuwa zikifanywa na inaweza ikasaidia katika uzalishaji wa nishati ili tusiendelee kutegemea katika nishati ambayo inazalishwa kwa kutumia maji peke yake. 

Kiasi kwamba kama mvua zikipungua basi kwenye yale mabwawa maji yanapungua halafu tunakosa umeme, umeme ukikosekana, uzalishaji unakosekana [na] uchumi unazidi kudidimia. 

Tuna gesi asilia, tuna jua la kutosha, tuna upepo, vyote hivi vinaweza vikatumika. 

Na uzuri ni kwamba, kwa mfano, katika nishati inayotokana na jua, mbali ya kwamba tunafahamu kuna gharama kubwa ambazo zinakuwepo mwanzoni, lakini sasa hivi, nadhani, hakuna sehemu yoyote ambayo utaenda Tanzania, hata vijijini, ambako hutakuta watu wana paneli za jua hata kama ni zile ndogo tu za kuzalisha nishati ya jua.

Kwa hiyo, hilo ni eneo ambalo tayari tuna uwezo wa kutumia hizo teknolojia kwa haraka na kuweza kusaidia tofauti na kipindi cha nyuma.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Sisi vijana tunapaswa kukabiliana na hizo athari za mabadiliko ya tabianchi na kujifungu kuhusu hayo mabadiliko ili tuweze kupana suluhisho pamoja kwasababu umoja ni nguvu pia sisi vijana nchi zetu zinatutegemeya sisi tu ili tuzitowe kwenye hizi janga . Asante sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts