Suala la umri sahihi wa mtoto kumiliki simu ya mkononi huwa na utata, japo wataalamu na watafiti wa maendelo na makuzi ya watoto wanashauri kuwa mtoto wa kuanzia miaka 10 anaweza kumiliki simu.
Wapo watoto wengi tu wanaowahi na wengine kuchelewa kumiliki simu – mara nyingi maamuzi hubakia baina yao watoto na walezi au wazazi wao.
Iwapo mzazi au mlezi utaamua kumpa mtoto simu, basi ni vyema kuzingatia yafuatayo:
Muda wa kutumia simu: Ni vyema kama mzazi au mlezi ukazungumza na mtoto juu ya muda na wakati sahihi wa kutumia simu. Kwamba pawepo na kiwango cha muda wa matumizi. Kwa mfano, mwaweza kukubaliana kwamba kwa siku atumie simu muda wa saa mbili na isizidi hapo. Hii humpa muda wa kufanya mambo mengine mbali na simu, ikiwemo kujisomea ama kucheza na wenzake.
SOMA ZAIDI: Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua
Mahala pa kutumia simu: Matumizi ya simu yawe na mipaka, kwa mfano asiende nayo shuleni, kanisani, nakadhalika.
Wajue anaowasiliana nao: Ni vyema kama mzazi kuwa na tabia ya kuchunguza aina ya mawasiliano afanyayo mtoto wako ili kuhakikisha kuwa mtoto wako yuko salama katika matumizi yake ya simu. Ni wajibu wa mzazi kuhakikisha kuwa anamlinda mtoto wake, hasa kwa kuwa ni rahisi mtoto huyo kufanyiwa ukatili kwa njia ya simu.
Udhibiti wa matumizi ya mitandao ya kijamii: Ni vyema kuweka mipaka juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii hasa kwa mtoto. Mitandao ya kijamii si salama kwa watoto kwani mazungumzo na maudhui yake ni ya watu wazima. Mjengee subira kwani umri sahihi ukitimia atajiunga.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?
Udhibiti juu ya tovuti za kutembelea: Si kila tovuti ni salama kwa mtoto kutembelea, hivyo ni wajibu wa mzazi kuwa na udhibiti wa tovuti ambazo mtoto atatembelea. Na kama mzazi utashidwa kuzuia, ama kufuatilia, ni vyema kuweka kidhibiti, au parental control kama inavyojulikana kwa kimombo.
Kama mzazi unatakiwa kuwa makini kuhakikisha matumizi ya simu hayangiliani na ratiba za mtoto za kulala, kupumzika, kucheza, kuhusiana na marafiki familia pamoja na kujisomea.
Makala hizi za maelezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.