Morogoro. Wadau wa maji wameshauriwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kueleza changamoto zinazojitokeza kwenye maeneo yao, hususan za uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ili mamlaka husika ziweke kuchukua hatua kwa urahisi.
Ushauri huo umetolewa Julai 6, 2023, mkoani Morogoro na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Shahidi wa Maji, Abel Dugange, katika mafunzo ya siku moja yaliyowakutanisha wadau hao yaliyolenga kuhakikisha vijana, wanawake, na watu wengine kwenye jamii wanawajibika katika kutunza mazingira.
“Ukizungumzia mitandao ya kijamii, vijana wengi wako huko, vingozi na taarifa nyingi za kiserikali zinatolewa huko,” alisema Dugange wakati akiongea na The Chanzo pembezoni mwa mafunzo hayo. “Kwa hiyo, tunaamini mitandao ya kijamii inawateja wengi, tukianzia wale wanaofanya maamuzi, lakini pia wanaotakiwa kutekeleza maamuzi yanayofanyika.”
Mkurugenzi huyo alisema kwamba mitandao ya kijamii inatoa fursa pana kwa wananchi kuchochea maendeleo kwenye maeneo yao husika, akitaja eneo la kuhimiza uwajibikaji wa viongozi wa umma kama jambo linaloweza kufanikishwa vizuri na matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Ukipeleka barua, mtu anaweza kukaa nayo, majibu yanatagemea hapo hapo awe na mamauzi ya kukujibu au kutokujibu,” alisema. “Na tumekuta changamoto za hivyo kwamba tumepeleka barua hatujajibiwi. Lakini kwenye mitandao inamanisha hata asipojibu yeye mtu mwingine ataona, atamkumbusha.”
SOMA ZAIDI: Maji Yanavyoinyima Raha Makao Makuu ya Nchi
Akiongea kwenye mafunzo hayo, Mshauri wa Masuala ya Teknolojia na Mdau wa Maendeleo wa Shirika la Mashahidi wa Maji mkoani Morogoro, Thimo Pazza, alisema, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vinaweza kuchukua nafasi kubwa kwa wao kupaza sauti zao na mwisho wa siku matatizo yanayowakabili yakatatuliwa kwa urahisi.
“Dunia ilivyo kwa sasa hivi asilimia kubwa ya watu wanatumia mitandao ya kijamii,” alisema Pazza. “Lakini pia, ukianza kuangalia vyombo vya habari, kwa mfano, uko kwenye daladala, utasikia redio, unaweza ukawa sehemu ya kula chakula ukawa unatazama televisheni.”
“Kwa hiyo, ukiweka maudhui yako kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inakuwa ni rahisi kuwafikia watu wengi zaidi na kwa haraka,” aliongeza mshauri huyo.
“Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inaweza ikasaidia kuhakikisha kwamba watumiaji wanaweza kutoa sauti zao zinazohusiana na masuala ya mazingira na maji kwa kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinatunzwa.”
SOMA ZAIDI: ‘Hayatibu Ugonjwa Wowote’: Zanzibar Yatahadharisha Unywaji wa Maji ya Chemchemi Pemba
Miraji Simba, mkazi wa Dar es salaam na mshiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa aliwahi kutoa taarifa za umwagikaji wa maji safi katika bomba kubwa la sukita kupitia mtandao wa Whatsapp, na kwambabaada ya taarifa yake kuonekana Wizara ya Maji ilikuchukua hatua kwenda kurebisha tatizo hilo.
“Baada ya kuitoa hiyo taarifa Wizara ya Maji ilipata taarifa, DAWASA walipata hiyo taarifa na wote wakaja kulishughulikia hilo tatizo kwa kiwango kinacho stahili lakini si kwa kumaliza kabisa,” alisema Simba.
Zahara Mzee kutoka kata ya Kivule, Dar es Salaam, alisema wakati mwingine tukio linapotokea na inahitajika kufanyiwa kazi, mwandishi wa habari anakuwa hayupo kwa wakati huo.
“Anapokuwa na shughuli nyingine inapelekea kutokuwa na ule ukaribu [hivyo taarifa kushindwa kutoka],” alisema. “Na kitu kingine naona bado hatujajenga ile nguvu ya pamoja lakini kwa mafunzo haya tumetengeneza ushirikiano na nguvu ya pamoja.”
SOMA ZAIDI: ‘Mazao Yetu Yote Yamesombwa na Maji.’: Njaa Inavyowanyemelea Waathirika wa Mafuriko Mtwara
Naye Omary Ngosha, mkazi wa Morogoro alisema pamoja na kuwahi kutumia vyombo vya habari kwenye utatuzi wa changamoto za maji, lipo suala la ukosaji wa bajeti linaloichangia kushindwa kushirikisha vyombo vya habari kwenye matukio yanayojitokeza.
“[Kuna wakati] nataka nimuite mwandishi wa habari sehemu, kumbuka mimi sina bajeti,” alisema. “Hata wewe unaangalia huyu anakaa katikati ya mji , wakati mwingine tunajikuta kuna baadhi ya vitu tunavikosa hasa yale matukio ya wakati husika kwa sababu sina bajeti.”
Akizungumzia mafunzo hayo, Nantaika Maufi, mshiriki kutoka Dar es Saalam alisema mafunzo hayo yamempa mwanga wa namna ya kutumia mitandao ya kijamii kuwasilisha changamoto zinazojitokeza.
“Nina uelewa kiasi [kuhusu mitandao], siyo sana, maana kuna upana zaidi ndiyo maana kwenye hili darasa limesaidia kuona jinsi gani ya kutumia mitandao,” alisema Maufi. “Maana unakuta unajua kupokea [simu] na kuzungumza lakini sasa kuingia kiundani kidogo leo nimepata mwanga.”
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Tanzania ina watumiaji wa intaneti milioni 29 mpaka kufika Juni 2021, sawa ya asilimia 49 ya Watanzania.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.
One Response
Hakika jamii kwa ujumla inahitaji kuelimishwa na kuonyeshwa nguvu ya mitandao ya kijamii ili kuleta uwajibikaji na mabadiliko chanya kwenye jamii zetu hasa masuala mazima ya utunzaji maji na vyanzo vyake.
#bombasiomaji