Dodoma. Katika kuzitatua changamoto za kujifunza na kukuza ujuzi zinazowakabili mabinti Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, serikali ya Canada imetangaza kutoa msaada wa dola milioni 25 za Canada, takribani bilioni 46 za Kitanzania zitakazotumika katika mradi wa elimu uitwao ‘Kila Binti Asome’
Mradi huu ambao upo chini ya Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF unalengo la kuwawezesha mabinti wenye umri wa miaka 10-19, kujifunza na kuongeza ujuzi wao kuendana na mahitaji ya soko ya sasa na baadaye nchini Tanzania.
Akitangaza msaada huo Julai 20, 2023 wakati wa ziara iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa na Waziri mwenye dhamana ya Shirika la Maendeleo ya Uchumi la Pasifiki la Canada Harjit Sajjan, alisema msaada huo umelenga pia kutoa fursa za upatikanaji wa njia bora za kujifunza kwa mabinti wajawazito na wasichana waliojiufungua ambao wameenguliwa kwenye mifumo rasimi ya elimu.
SOMA:Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi
“Wasichana wajawazito na mabinti waliojifungua wanastahili kupata elimu, stadi za maisha, ujuzi wa malezi na mafunzo ya ujuzi.” alisema. “kisha wanaweza kuendelea na masomo yao, kupata fursa sawa ya ajira yenye staha na kuvunja mzunguko wa umaskini ambao kina mama wengi wadogo wanaangukia.”
Alisema kuna haja ya kuwa na mbinu bora itakayo saidia kuondoa changamoto zinazo wakabili mabinti hao. “Canada imekuwa mshirika wa muda mrefu wa Tanzania katika elimu. Tumeshirikiana kuboresha viwango vya elimu, na upatikanaji kwa shule zote za msingi na sekondari kwa wasichana na wavulana.” aliongeza.
SOMA ZAIDI:Harakati za Kudai Katiba Mpya Ziende Sambamba na Kudai Mabadiliko Kwenye Mfumo wa Elimu’
Katika Kipindi cha miaka 14 iliyopita, Canada ilitoa zaidi ya dola milioni 250 kwenye mfumo wa elimu. “Niko hapa kuthibitisha Canada kwamba itaendelea kuisaidia jitihada za elimu nchini Tanzania. Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyosema ‘Elimu siyo njia ya kuukimbia umaskini, ni nyenzo ya kupambana nao’.
Kwa upande wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Profesa Adolf Mkenda alisema, ziara hiyo inawakumbusha mahusiano mazuri ambayo yapo kati ya Canada na Tanzania katika sekta ya elimu.
“Sisi hapa tumekuwa na Watanzania wengi wamesoma Canada kwa kusaidiwa na Serikali ya Canada.” alisema Prof. Mkanda. “Tunafurahi mahusiano yetu katika sekta ya elimu yanaendelea kukua na kuimarika sana. Mahusiano hayo tutaendelea kuyaimarisha”
Mkenda alisema Tanzania inaendelea na mageuzi makubwa katika elimu, moja ya eneo ikiwa ni miaka ya lazima ya mtoto kukaa shuleni. Kwa sasa umri huo ni miaka saba hali ambayo Profesa Mkenda anaeleza kwamba watoto wengi wanamaliza wakiwa na miaka 13, umri ambao si wa kuingia kwenye soko la ajira.
SOMA PIA:Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe
“Kwa hiyo hatua ya kwanza ya mageuzi hayo, ni kuwa na elimu ya lazima ya miaka 10 badala ya kuwa na miaka 7,” alieleza Mkenda. Waziri Mkenda amefafanua kwamba tayari mchakato huo umeanza na Wizara inakaribia kupata kibali cha mwisho na tutakuwa tunatekeleza hatua kwa hatua.
Profesa Mkenda pia ameeleza kwamba Wizara inategemea kuanzisha utaratibu ambapo baada ya shule ya msingi kutakuwa na mikondo miwili, mkondo wa elimu ya jumla na mkondo wa elimu ya amali.
Ambapo elimu ya jumla itakuwa na mafunzo ya amali, lakini mfunzo mengi zaidi darasani. Mkondo wa elimu ya amali itakuwa na mafunzo mengi ya elimu ya amali na masomo machache ya darasani.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.