Inasemekana, hapo mwanzo, enzi za Agano la Kale, Shetani alipata ufunuo mbadala wa kuanzisha hekalu lake kama taasisi kamili.
Pamoja na kujaliwa wafuasi kemkem, ongezeko la sadaka za fungu la kumi, kufunuliwa ujuzi na miujiza kedekede sambamba na kuwa na upeo wa kutoa mapepo bubu, bado Shetani alijisikia mdhaifu na duni kwa kukosa heshima na utambulisho mbele ya jamii.
Aidha, kwa muda mrefu alifedheheka kwa kupakwa sifa mbaya na alichoka kuendeleza utume wake mafichoni, ilhali yeye binafsi hana sifa mbaya kama wamnenavyo wanadini na ndimi zao. Alidhamiria, iwe kwa dua au dau, kumiliki kanisa lake kamili hadi utimilifu wa dahari.
Shetani bin Ibilisi, hakuridhika tu na mkate wa kila siku, aliona fursa adimu ya kujiimarisha kimfumo na kimkakati zaidi. Aliona wivu vile jinsi na jinsia Mungu ilivyo tamalaki halaiki na katika milki tukufu na enzi zake takatifu.
Hivyo, ilimbidi Shetani kuandaa hati za kiliturujia, herakia, katiba yake mintarafu na mitaguso mbalimbali.
“Kwa nini nisimiliki na kusimika nyumba yangu ya ibada?” alijitafakarisha tena na tena. Alitaka kutumia vizuri ule uwanja wa kidemokrasia na uhuru wa kuabudu uliokuwepo. Hivyo, kwa muktadha na mustakabali huu, Kanisa la kishetani, lingekuwa ni njia mahsusi ya kupambana na uzushi dhidi yake, kuepusha ushindani wa kidini, lakini zaidi kuyapoteza, au kuyapotezea, kabisa maadui wa kiroho.
Kwa karama, kudra na kadri ya mang’amuzi ya nyakati hizo, dunia ilikuwa ni uwanja wa vita isiyoisha kati ya ubaya na uzuri, kati ya mrengo wa kulia na kushoto na kati ya pepo na jehanamu. Enzi hizo, sera ya kutofungamana na upande wowote haikuwepo.
“Ndiyo, ni vita kati ya misaafu dhidi ya misaafu, ni mawindo ya roho za kikafiri, ni ishara za utabiri na biashara za utabibu wa magonjwa ya kisasa kama ugumba, upweke, afya ya akili na sonono,” shetani alimwaga sera zake.
“Nitakuwa muombezi kwa kila nafsi, mkate na divai vitapatikana kwa wote, ibada zangu fupi bila tozo wala michango isiyoisha, mahubiri yanayogusa mihemko na mahitaji ya sasa ya watu, tofauti na makanisa mengine, nitaweka wazi mapato na matumizi ya sadaka zenu, pia huduma ya usomaji wa nyota zenu itakuwepo, naleta church of feeling free,” alihubiri Shetani.
SOMA ZAIDI: Profesa Mussa Assad: Ufisadi Umeshamiri Kwa Sababu Mafisadi Hawaadhibiwi
Mara nyingi huyu Shetani ilimbidi avae kama mwanakondoo ili kuwavuta na kuwateka watu, walakini ndani ni mbwa-mwitu. Alibobea sana katika ushushushu na ule unaitwa ushunuzi jamii.
Ebwana eeh, alijua sana kuwachota na kuwalaghai watu, hasa kwa kucheza na hisia zao, alimtaja taja sana Mungu wa majeshi. Alisisitiza unyenyekevu wake, na namna tambo na agenda yake ni dhihirisho la mkono wa Mungu.
Punde si punde, Shetani aliomba faragha na Mungu ili kumtaarifu azma yake hiyo. Hii ilidhihirisha duniani na mbinguni kuwa Shetani na Mungu siyo maadui, kumbe wana tofauti tu za kiteolojia na kiitikadi. Ndiyo maana, hata katika kile kitabu cha Ayubu (1, 7-12), Shetani anamshawishi Mungu aruhusu mabaya yampate Ayubu, mtumishi wake, ili kumpima ukomavu wa imani yake.
Kwa hiyo, Shetani alifunga safari kwenda kumwona Mungu. Alijipanga kwa ushawishi na uzengezi wa kila aina kama ule wa nyoka aliyewadanganya akina Adamu na Hawa kule bustani ya Edeni.
Mazungumzo
Basi, Shetani alibisha hodi kwa Mungu naye, bila kufura, alimkarimu kwa furaha na mbawazi.
“Karibu sana swahiba, kulikoni mbona ghafla ujio wako?” Mungu alinena juu ya mimbari yake. “Kuna jema au tafrani tu duniani?”
“Hapana, usiogope, siyo ujio wa dharura,” alijibu Shetani, huku akimwaga tabasamu tele, akivuta kiko mdomoni na mkono kwenye kikoi.
SOMA ZAIDI: John Heche: Ugonjwa Unaoitesa Tanzania ni Uongozi M’bovu
Baada ya kusabahiana mubashara, tena kwa bashasha na busu takatifu, Shetani aliongeza, “Nimekaa katika maombi na kutafakari kwa muda mrefu kuhusu misheni zetu huko duniani, hasa juu ya hatma ya huyu mwana wa adamu, nimeona ni vyema tukutane na kubadilishana uzoefu.”
Shetani aliongea kwa imani na imla, akisema, “Utaafikiana nami kwamba bei na madai yako ya kwenda peponi yapo juu mno hivyo unakosa wateja. Wewe una amri ngumu, utitiri wa sheria na utii mno. Labda hujawahi kujiuliza, je, hizi sheria zako nyingi zinazaa dhambi zaidi au dhambi zaidi ndizo hupelekea sheria zaidi?
“Kwa upande wangu nazidiwa na idadi kubwa ya wateja na sina pa kuwaweka, ndiyo maana nahitaji taasisi ya kuhimili. Wengi waja kwangu kwani njia yangu ni nyepesi, ni njia ya mnato na mkato bila makato.
“Hivyo, nimekuja kukutaarifu azimio langu la kufungua kanisa kubwa, mfano wa hospitali ambayo itapokea watu wote bila masharti shurutishi, bila ubaguzi wala ulanguzi. Naomba ruhusa na usaini haya makubaliano,” alimalizia Shetani kwa msisitizo huku akipiga magoti.
“Mmmh!” Mungu alivuta pumzi bila pupa na kujibu, “Mwanadamu siyo mdori wa kuchezewa huku na kule. Aliumbwa kwa sura yetu na kupewa hadhi ya uhuru. Hivyo, Uhuru Uendelee. Siafikiani nawe katika hilo, sikubaliani na mkataba wako huo ila upo huru kusimika madhabahu yako.”
Ukimya
Baadaye, ulifuata ukungu wa ukimya mzito uliotanda pande zote. Mungu hakuongea zaidi, mithili ya tembo, hakuzozwa tena na kelele za chura. Ukimya wake ulikuwa gumzo, fumbo na ulipata tafsiri nyingi.
Lakini, malaika na walimwengu wengi walijawa jazba na kukosa ustahimilivu. Walitamani Mungu atoe tamko na onyo kali kwa shetani. Lakini wapi!
Naam, walisahau kuwa Maanani ni mwingi wa subra na, kadri ya midrash-mapokeo ya kiyahudi, ana sifa kuu mbili zinazotegemeana: ni mwingi wa haki na huruma.
SOMA ZAIDI: Twaha Mwaipaya: Rais Samia Hawezi Kukwepa Hitaji la Katiba Mpya
Maana kama tungeumbwa tu kwa haki, nani angesimama mbele yake, na kama tungeumbwa tu kwa huruma, wengi tungeikufuru. Hivyo, hizo tunu mbili ni namna ya kuweka uwiano au mizania.
Basi, pasi na shaka, Shetani akaenda zake na njiani aliendelea kueneza sera zake mithili ya yule mpanzi wa biblia (Lk 8:5-14). Mahubiri yake yalijikita katika kubatiza ubaya kuwa uzuri, kutumikia kuwa kutumikiwa, haki kuwa fadhila na fedheha kuwa fadhila na umaskini ulikuwa siyo uadui tena bali mtaji wa kiroho na kisiasa.
“Ndiyo, mimi ndiye Shetani,” alirudia rudia. “Nitawapa fahari na falme zote, budi mniabudu. Mimi nipo karibu yenu zaidi, najua mahitaji na shida zenu zote.”
Ni kweli, kadri ya mapokeo ya zamani katika tamaduni na dini nyingi, Shetani na Mungu, wapo karibu nasi waja. Yaani, ndani mwetu tuna chembe-chembe za umungu na ushetani.
Ni nguvu mbili pinzani rohoni na mwilini mwetu. Ile falsafa ya Yin-Yang ya Wachina. Hizi nguvu kinzani zipo vitani siku zote. Daima inayoshinda ni ile ambayo mwanadamu anailisha na kuipatia kipaumbele zaidi.
Mafunzo
Tunapolia juu ya uhuru wetu bendera, tunapolalamika juu ya ombwe la ‘maadili na mila zetu,’ tunaposaga meno juu ya kukithiri vitendo vya rushwa, kuongezeka kwa umaskini, tunaponyoosheana vidole juu ya mikataba ya miumbi pamoja na kukosekana kwa haki ni kwa sababu sisi wenyewe ni sehemu ya tatizo na tumeruhusu hayo mabaya yatokee na kutamalaki.
SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini
Watawala na majahili wao wa kimataifa wamefanikiwa, kwa kiasi kikubwa, kutugawa na kusaliti juhudi zote za kujikomboa. Uzalendo leo umekuwa ni kuimba mapambio ya watawala, ni uchawa na unafiki fulani tu.
Hata Katiba Mpya tunayohitaji haitakuwa mwarobaini wa matatizo yetu kama hakutakuwa na mikakati binafsi na ya kitaasisi ya kubadili tamaduni, fikra, tabia na mazoea yetu mabaya.
Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au Twitter kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.