The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Gumzo Ufungwaji wa Baa Maarufu Mwanza, TRA Yasema Haihusiki

Baa hiyo, ijulikanayo kama The Cask Bar and Grill, imefungwa kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni na kukwepa kodi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Hatua ya mamlaka za Jiji la Mwanza ya kuifungia baa maarufu jijini humo imezua gumzo miongoni mwa Watanzania, huku baadhi wakijiuliza endapo onyo lililotolewa na Serikali siku za hivi karibuni la kuzitaka mamlaka nchini kutokufungia biashara litakuwa limekiukwa.

Mnmao Agosti 16, 2023, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Kiomoni Kibamba, alitangaza kuifungia baa maarufu jijini humo ya The Cask Bar and Grill kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni za biashara, ikiwemo kufanya biashara ya matangazo.

“Tumeona ni busara kuanzia kesho [Agosti 17], bila shaka ilipaswa jioni hii ya leo [Agosti 16] awe amefunga biashara zake, mpaka hapo tutakapokuwa tumetatua changamoto hizo za ukiukwaji wa masharti ya leseni za biashara,” Kibamba alisema.

“Lakini busara imesema kwamba sasa hivi kuna vitu tayari ameshapika, na kwamba ikifungwa vitaharibika, tumemwambia mpaka kesho [Agosti 17] asifungue mpaka hapo atakapokuwa amejibu hizi changamoto za ukiukwaji wa masharti ya leseni ya biashara,” aliongeza.  

SOMA ZAIDI: ‘Hakuna Biashara’: Machinga Old Airport Mbeya Waeleza Masaibu Yao

Kwenye taarifa yake ambayo imeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Kibamba ameushutumu uongozi wa bar hiyo kuendesha biashara ya vileo bila kuwa na leseni ya kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka miwili, hali aliyodai imeipotezea Manispaa mapato kati ya Shilingi milioni 10 na 15.

Hata hivyo, hatua hiyo imezua gumzo mitandaoni, huku baadhi ya wachangiaji wakishuku kwamba motisha ya kufungwa kwa baa hiyo siyo ukiukwaji wa masharti ya leseni kama mamlaka zilivyodai bali ni kuonekana kwa tangazo linalopinga uwekezaji unaotarajiwa kufanyika katika bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya DP World.

Kwenye video fupi inayosambaa mitandaoni, anaonekana mtu mmoja akiwa ndani ya baa hiyo akiwa ameshikilia bango lenye maandishi yanayosema, ‘Okoa bandari zetu’ kwa herufi kubwa. Mjadala wa bandari umeendelea kushika kasi nchini, huku watu watatu wakishikiliwa na polisi kwa kile kinachohisiwa ni ukosoaji wao wa mkataba huo tata.

Moja kati ya wale waliohusisha uamuzi wa mamlaka jijini Mwanza wa kuifunga Cask Bar na tangazo hilo ni kiongozi mwandamizi wa chama cha upinzani CHADEMA Godbless Lema, ambaye amezitaka mamlaka nchini kuwa na huruma na watu wanaojitafutia kipato.

SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni

“Inaleta huzuni na majonzi sana,” Lema, ambaye amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), aliandika kwenye ukurusa wake wa Twitter. “Mnajua kama [huyu mfanyabiashara] ana mikopo benki au la? Mbegu mnayopanda ikikomaa hali itakuwa mbaya sana.”

Baadhi ya wachangiaji wamehoji inawezekana vipi kwa baa iliyoko mjini kufanya shughuli zake kwa kipindi cha miaka miwili bila kuwa na leseni ya biashara na kulipa kodi kama mamlaka zinavyodai, wakiashiria kwamba madai hayo ni visingizio tu kutoka mamlaka husika.

Taarifa za kufungwa kwa baa hiyo, hata hivyo, zimekuja wakati ambapo Serikali imeshaahidi hadharani kutokufungia biashara ya mtu yoyote kwa kudaiwa kwenda kinyume na taratibu, ahadi iliyotokana na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kwamba hatua hiyo haikuwa ikitenda haki.

Mnamo Juni 15, 2023, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba alitangaza kwamba kuanzia Julai 1, 2023, itakuwa ni marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ama ofisi, ama maeneo yoyote ya uzalishaji.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wafanyabiashara Wavutana Zanzibar Kuhusu Utoaji wa Stakabadhi Kielektroniki

“Napendekeza kuanzia Julai 1, 2023, iwe ni marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu,” Dk Nchemba alisema.

“Aidha, napendekeza sheria, na kanuni, na taratibu mbalimbali zirekebishwe ili kumchukulia hatua mwenye biashara kwa makosa ya biashara na siyo kuifunga biashara kwa makosa ya biashara,” alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (Chama cha Mapinduzi – CCM).

Hata hivyo, katika hali iliyoonekana ni kujitenga na uamuzi huo wa mamlaka za jiji la Mwanza, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitoa taarifa hapo Alhamisi, ikieleza kutohusika kwa namna yoyote na uamuzi wa kuifungia baa hiyo.

“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuujulisha umma kuwa, haijahusika kwa namna yoyote na ufungaji wa baa ya ‘The Cask’ iliyopo jijini Mwanza,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo. “Tunaomba wahusika na umma wawasiliane na mamlaka husika juu ya jambo hilo.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *