The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Wapendekeza Marekebisho Muhimu Yafanyike Katika Katiba ya Sasa Kuruhusu Kujiandaa na Uchaguzi

Sababu kubwa iliyotajwa juu ya maazimio haya ni kuwa muda uliopo mpaka kufikia uchaguzi ni mdogo sana kuweza kumaliza mchakato wa kupata Katiba Mpya.

subscribe to our newsletter!

Wadau wa masuala ya demokrasia wamependekeza leo Agosti 23,2023, kuwa Tanzania ifanye marekebisho muhimu katika katiba ya sasa ili kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2024 na 2025. Sababu kubwa iliyotajwa juu ya maazimio haya ni kuwa muda uliopo mpaka kufikia uchaguzi ni mdogo sana kuweza kumaliza mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Wadau hawa walikutana katika mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania, kikao kilichokutanisha serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo.

Akisoma maazimio hayo mbele ya washiriki takribani 200, Profesa Ibrahimu Lipumba, mwenyekiti wa sasa wa Kituo Cha Demokrasia, alieleza kuwa wadau watakuwa wakijidanganya ‘kudhani kuwa wanaweza tukakamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa [2024] na kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.’

“Kwa hiyo mkutano huu umejadili kwamba kuna umuhimu wa kuweza kufanya mabadiliko muhimu katika katiba iliyopo hivi sasa ili kuweza kutoa marekebisho ambayo yataruhusu upanuzi wa demokrasia, uwepo wa tume huru ya uchaguzi [na] ushiriki ulio mpana zaidi,” alielezea Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha CUF.

Marekebisho muhimu yaliyopendekezwa katika mkutano huo ni pamoja na kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi, kuruhusu uchaguzi wa Rais uweze kuhojiwa Mahakamani.

Marekebisho mengine ni kutaka kura zitakazofanya mgombea awe Rais ziwe walau asilimia 50 jumlisha 1. Kwa sasa Katiba inaruhusu mgombea yeyote aliyeongoza katika kura kwa kiasi chochote kutangazwa kuwa Rais.

Marekbisho haya yaliyopendekezwa sasa sio mageni, mwaka 2014 yalipendekezwa baada ya mchakato wa Katiba kuonekana haukupata muafaka. Hata hivyo baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vyote, mpango huu haukufanikiwa kutekelezwa kutokana na kukosekana makubaliano.

Hii ilipelekea kuingia kwenye uchaguzi kwa kutumia mfumo wa Katiba 1977 kama ulivyo sasa, baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani alieleza kuwa Katiba Mpya haikua kipaumbele  chake, kauli hii, pamoja na kufungika kwa uwanja wa siasa zikazima ndoto zote za mabadiliko ya endelevu ya kisiasa nchini.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kuingia madarakani, ameahidi kuhakikisha Tanzania inapata Katiba Mpya. Ahadi hii haikuja na tarehe kamili, jambo ambalo limewasukuma wadau kwa sasa kuhitaji maboresho muhimu ya Katiba wakati michakato mingine ikiendelea.

Wadau hawa kupitia Kituo cha Demokrasia, kinachoendeshwa na vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni wamependekeza miswada ya maboresho haya kuwasilishwa Bungeni katika kipindi cha Bunge kinachokuja cha Septemba 2023, huku wakishauri miswada ile ya tume ya uchaguzi na marekebisho ya Katiba kuwasilishwa kwa pamoja kama ilivyofanyika mwaka 1991.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *