Dodoma. Akina mama wenye watoto wadogo katika soko la Machinga Complex jijini hapa wameuelezea uamuzi wa jiji kutenga vyumba maalumu vya kunyonyeshea sokoni humo kama uamuzi wa busara sana, wakisema umewasaidia kuondokana na kadhia walizokuwa wakikabiliana nazo huko nyuma.
Kwenye soko hilo ambalo ujenzi wake ulikamilika Septemba 2022, likigharimu jumla ya Shilingi bilioni 9.53, ambapo kati ya hizo bilioni 6.5 zimetokana na mapato ya ndani ya jiji la Dodoma na Shilingi bilioni tatu zilitokana na fedha za mfuko wa mkopo wa dharura kutoka Shrika la Kimataifa la Fedha (IMF) ambayo Serikali ya Tanzania ilipatiwa.
Soko hilo lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 3,200, kuna vyumba viwili vilivyotengwa mahususi kwa ajili ya akina mama wanaonyonyesha kuwapatia watoto wao huduma hiyo muhimu kwa ustawi wao.
Mnamo Septemba 6, 2023, The Chanzo ilitembelea sokoni hapo na kwenda moja kwa moja kwenye moja ya vyumba hivyo vya kunyonyeshea ambapo ilimkuta mtoto mmoja akiwa chini kwenye kapeti, huku muda mfupi uliofuata wazazi wengine wakileta watoto wao walioonekana kuwa na umri kati ya miezi tisa na mwaka mmoja katika chumba hicho.
Kwenye chumba hicho, The Chanzo iliona picha za midoli zilizochorwa vizuri ukutani. Kwenye kuta za chumba hicho pia kuna michoro ya miti na wanyama mbalimbali kama vile twiga na simba. Sakafuni kumetandikwa kapeti lenye michoro ya midoli. Ukutani pia kuna ubao unaoweza kutumikia kufundishia.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
Kwenye chumba hicho pia The Chanzo iliona nepi za watoto ambazo hugawiwa bure kwa mama wa watoto hao. Pia, chumbani humo kuna viti viwili virefu vimewekwa kwa ajili ya wazazi kukaa na kunyonyeshea. Mazingira katika chumba hiki ni masafi sana, hali iliyofanywa kwa makusudi kulinda afya na ustawi wa watoto hao.
Mbali na kuhifadhi watoto wachanga wanaonyonya, vyumba hivyo pia huhifadhi watoto wadogo wanaosoma shule ambao baada ya kurudi shule hawawezi kwenda nyumbani kwani wazazi wao hushinda sokoni hapo siku nzima. Huduma zote wanazozipata akina mama hao kwenye vyumba hivyo zinatolewa bure na uongozi wa soko.
Ukombozi
Kwenye mahojiano yao na The Chanzo, akina mama wanaonyonyesha sokoni hapo walisema kwamba uwepo wa vyumba hivyo ni ukombozi kwao na watoto wao, kwani vinawasaidia kuweza kufanya biashara zao bila kuathiri wajibu wao kama walezi kwa watoto wao.
Wazazi wengi waligusia namna ambavyo vyumba hivyo vinasaidia “kuwasitiri” siyo tu watoto hao wadogo bali pia mama zao ambao vyumba hivyo vinawapa faragha katika utekelezaji wa wajibu wao muhimu kwa watoto wao, ule wa kuwanyonyesha.
“Inasaidia kutusitiri akina mama wakati wa kunyonyesha,” alikiri Fatuma Tesha, mmoja kati ya akina mama wanaotumia vyumba hivyo. “Vyumba hivi vinatusaidia kazi kufanyika kwa urahisi kwa sababu unakuwa huna muda wa kuanza kumuangalia mtoto yuko wapi.”
SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni
Fatuma aliiambia The Chanzo kwamba sokoni hapo kuna mambo mengi yanayoweza kuhatarisha afya na usalama wa watoto, akisema uwepo wa vyumba hivyo unasaidia kumlinda mtoto dhidi ya hatari hizo.
Mfanyabiashara mwingine sokoni hapo, Tuse Obokile, na ambaye ana mtoto mdogo, alisema kwamba uwepo wa vyumba hivyo umesaidia sana kuwalinda watoto wasipotee kama ilivyokuwa huko nyuma.
“Machinga ni soko kubwa sana kwa hapa Dodoma,” alisema Tuse. “Kwa hiyo, lina msongamano mkubwa sana wa watu. Kwa hiyo, hili soko linatusaidia sisi wamama ambao tuna watoto.”
“Unakuta uko bize na kazi, kwa hiyo unakuta yule mtoto anaanza kufanya nini, kuzurura, mwisho wa siku mtoto anapotea ndani ya soko kwa sababu soko ni kubwa,” aliongeza mama huyo. “Ni ngumu kwa mtoto mdogo kuweza kutambua kwamba ofisi ya mama iko pale, kwa sababu mazingira yote ya vizimba yako sawa.”
Upotevu wa watoto
Veronica Tarimo ni Meneja wa soko hilo ambaye alikiri kwenye mahojiano yake na The Chanzo kwamba huko nyuma, tatizo la upotevu wa watoto sokoni hapo lilikuwa kubwa, akiitaja hiyo kama moja wapo ya sababu zilizolisukuma Jiji la Dodoma kutenga vyumba hivyo maalumu sokoni hapo.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Veronica alisema kwamba kabla ya kuanzishwa kwa vyumba hivyo, uongozi wa soko uliripoti kupotea kwa watoto wapatao nane. Tangu kuanzishwa kwa vyumba hivyo, hata hivyo, hajapokea taarifa yoyote ya mtoto kupotea, alisema meneja huyo.
SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni
“Jiji lilijali zaidi namna ya kumsitiri mama na mtoto, hasa pale mama anapotoa huduma ya mtoto wakati wa kunyonyesha,” alisema Veronica wakati akiongea na The Chanzo ilipomtembelea ofisini wake. “Wamama wengi wanatoa ziwa sehemu yoyote pasipo mazingira ambayo ni mazuri.”
Ester Mwaipopo ni moja kati ya wasimamizi wa vyumba hivi sokoni hapo ambaye aligusia kwamba vyumba hivyo haviwanufaishi wafanyabiashara wanawake tu bali pia wateja wanawake wanaotembelea sokoni hapo kufata mahitaji mbalimbali wakiwa na watoto wao wachanga.
“Kuna wateja ambao wanapita na watoto, wanapata sehemu nzuri ya kupumzika,” alieleza Ester. “[Mteja] anakaa, ananyonyesha mtoto wake, kisha anaendelea na manunuzi.”
Miundombinu rafiki
Kwa siku nyingi, wadau wa maendeleo ya wanawake na watoto nchini wamekuwa wakizitaka halmashauri nchini kote kuweka miundombinu rafiki kwenye masoko itakayowasaidia wanawake kushiriki kikamilifu kwenye biashara hizo.
Wito huu unatokana na ukweli kwamba wanawake hapa nchini Tanzania wamekuwa wakishiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za biashara, huku ripoti zikionesha kwamba takribani asilimia 48 ya biashara zote nchini ni biashara zinazomilikiwa na wanawake, wengi wakiwa kwenye sekta isiyo rasmi.
SOMA ZAIDI: UN Women Yataka Ushiriki Zaidi wa Wanawake Kwenye Siasa, Uchumi
Ripoti pia zinaonesha kwamba wanawake wengi nchini Tanzania wenye umri kati ya miaka 25 na 34 hutumia muda wao mwingi, takriban masaa sita kwa siku, kufanya kazi zisizopokea ujira wowote ule, wakati wanaume wenye umri sawa na huo hutumia muda wa mwingi, masaa matano kwa siku, kwenye ajira.
Kukosekana kwa miundombinu rafiki, kama vile vyoo na vyumba vya kunyonyeshea kwenye masoko, kulitajwa kama moja ya changamoto ambazo wafanyabiashara wanawake masokoni wanakabiliana nazo kwenye utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Equality for Growth mwaka 2009.
Jane Magigita, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo linalopigania usawa wa kijinsia kwenye sekta nyingine za uzalishaji mali, ameiambia The Chanzo kwamba soko kuwa na eneo la kunyonyeshea na kulea mtoto ni jambo la muhimu kwani mtoto anahitaji huduma nyingi, ikiwemo usafi wake.
“Soko ni eneo la kazi, na kama maeneo ya ofisi yanaweza kuweka vituo, au huduma, maalumu ili kulea watoto, hasa hao wadogo chini ya miaka mitatu, ni muhimu sana katika kuimarisha malezi ya watoto, na kupunguza mzigo wa kazi nyingi kwa mwanamke, ikiwemo hawa wanaofanya kazi au kutoa huduma maeneo ya umma,” alisema Magigita.
“Halmashauri zetu zitenge maeneo [kwenye masoko kwa ajili ya kunyonyeshea] na bajeti,” alipendekeza Magigita ambaye amekuwa akipigia kelele sana suala hili. “Kila soko linaweza kutafuta namna ya kulifanyia kazi hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackiline@thechanzo.com.
One Response
Maelezo yako yanatia moyo kuhusiana na huduma ya watoto wa wazazi wa kike wanaofanya kazi ya biashara ndogo za soko la bidhaa za rejareja.