The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo

Viwanja vyetu vya michezo vinapaswa kuwa chini ya taasisi itakayojikita kusimamia viwanja tu badala ya kuwa chini ya wizara ambayo husimamia sera.

subscribe to our newsletter!

Pamoja na ukweli kwamba baadhi ya michezo nchini kama mpira wa wavu, wa mikono, netiboli na baadhi ya michezo ya riadha imedorora, umuhimu wake hauwezi kukwepeka, hasa wakati huu ambao sekta hiyo inazidi kuvuta mamilioni ya watu duniani.

Hapa kwetu Tanzania, soka, mbio za marathoni na mpira wa kikapu ndiyo inayoonesha uhai na kufuatiliwa na wengi, ingawa kwa marathoni ni pale tu wanamichezo wetu wanaposhinda.

Zile nyakati za kujazana Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kushuhudia Michezo ya Taifa ya Riadha, au pale Relwe Gerezani kushuhudia michuano ya taifa ya netiboli, au pale DDC Kariakoo kushuhudia mashindano ya taifa ya ngumi za ridhaa, haupo tena wakati huu.

Ni mchezo wa soka pekee ndiyo unaweza kukusanya kuanzia watu 5,000 hadi 60,000 na wengine wakabaki nje kwa kukosa tiketi.

Mchezo wa pili kwa umaarufu, netiboli, sasa hausikiki kabisa na unaonekana kuishia katika mashindano ya mashirika ya umma au yale ya shule za sekondari. Leo hii ni vigumu kujua klabu bingwa ya taifa, na hata kama ipo ni kwa wale wadau hasa na si mashabiki.

SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu

Mpira wa kikapu bado unavuta vijana wengi na tukio la hivi karibuni la kuanza kuvutia wanamichezo maarufu, linaweza kurudisha mwamko wa mchezo huo.

Michezo muhimu

Lakini kufifia kwa michezo mingine hakumaanishi kuwa haina umuhimu unaotakiwa ufanyiwe kazi ili kurudisha hamasa na hatimaye kurudia tena kuanza kutoa ajira kwa vijana na watu wengine wengi, kama ambavyo ngumi za ridhaa zinavyozidi kuchanja mbuga.

Riadha ina michezo mingi, ukiachana na mbio za marathoni ambazo zina wanamichezo wachache wanaong’ara duniani. Leo hatuna wanariadha wa mbio fupi kama enzi za akina Norman Chihota, Mwalimu Ally, Mwinga Mwanjara, Nzael Kyomo, huku zile za umbali wa kati zikitoa nyota kama Filbert Bayi, Lwiza John, Zakia Mrisho, Clever Kamanya na Samuel Mwera.

Bado mbio za marathoni zinatamba kwa kuwa hazihitaji miundombinu ya gharama sana ukilinganisha na nyanja kama mbio za mita 100, 200, 400, 5,000 na 10,000 ambazo ni lazima zifanyike kwenye viwanja vyenye zulia maalum na si lami kama ilivyowekwa Uwanja wa Uhuru.

Bado michezo mingine kama kuruka juu, kurusha tufe, kurusha mshale, kuruka viunzi na kupokezana vijiti, pia zinahitaji maeneo na vifaa maalum ambavyo vimekuwa adimu kuonekana katika viwanja vyetu vya michezo.

Ni Uwanja wa Amaan na wa Benjamin Mkapa tu ndiyo inayoweza kuwa na sifa za kuandaa michezo hiyo mingine ya riadha, ukiacha marathoni ambazo sasa zimekuwa ni wimbo wa kila kampuni au taasisi, ingawa hazizalishi wanariadha nyota wa mchezo huo.

Mashindano ya AFCON

Hatua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipa haki Tanzania kuwa moja ya nchi tatu zitakazoandaa fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2027 (AFCON 2027) inatupa wasaa wa kuanza kufikiria upya viwanja vyetu vingi vilivyojengwa kwa viwango vya olimpiki, lakini havina hadhi hiyo kutokana na wamiliki kutoweka nguvu katika kumalizia ili vifikie viwango hivyo.

SOMA ZAIDI: Tufurahie Uenyeji AFCON 2027 Tukisuka Mikakati

CAF wanaweza kufurahi kama Tanzania pamoja na Uganda na Kenya zitajenga viwanja vya mpira wa miguu, tofauti na Moi Kasarani, Mandela Namboole na Benjamin Mkapa wa Dar es Salaam kwa kuwa shughuli yao kubwa ni soka.

Lakini sioni Serikali hizi tatu zikifikiria kujenga viwanja vya soka pekee, bali kujenga viwanja vya kiwango cha olimpiki.

Hatujui Kenya na Uganda wanaendeshaje viwanja vyao, lakini hapa kwetu ni lazima viwe chini ya Wizara ya Utamaduni, Michezo na Sanaa kama ulivyo Uwanja wa Mkapa na Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa), huku vingine kama Sheikh Amri Abeid na Nyamagana vikiwa chini ya halmashauri.

Viwanja vingine vingi vinavyotumika viko chini ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) na vichache chini ya taasisi au watu binafsi.

Kumekuwa na tatizo kubwa katika uendeshaji wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru, na wakati fulani wakati wa ukarabati wa Uwanja wa Uhuru iliteuliwa kamati ya tofauti, wengine wakiwa hawana ufahamu wowote wa uendeshaji viwanja wala uhandisi na matokeo yake yakawa ni kuweka lami kwenye eneo la kukimbilia.

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Uzio ukajengwa wa vyuma kana kwamba mashabiki ni wanyama wa mwituni, hali inayoweza kuhatarisha maisha yao iwapo kutatokea dharura kubwa inayohitaji watu wakusanyike sehemu maalum kwa haraka ili kujiokoa.

Uwanja wa Mkapa ulikuwa unaelekea kudhoofika eneo la kuchezea hadi CAF ilipoingilia kati na kuomba upumzishwe ili nyasi zipumue. Bado kuna maeneo mengi kwenye Uwanja wa Mkapa ambayo hayajaanza kutumika, huku runinga ikitumika kwa nadra wakati ni moja ya nyenzo nzuri za kutoa taarifa za mechi na mambo mengine.

Uendeshaji wa miundombinu hiyo kisiasa unasababisha hadi uongozi wa uwanja kuyumba na hivyo kukosa watu wenye mikakati ya muda mrefu ya kuboresha uwanja.

Kwa kifupi, bado uwanja haujawa huru kujiendesha, kujitafutia masoko, fedha na masuala mengine muhimu, huku mchezo wa soka pekee ukipata nafasi kubwa kuliko mingine kwa kuwa ndiyo unaoingiza zaidi fedha.

Wakala wa viwanja

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na wazo la kuanzishwa kwa Wakala wa Viwanja vya Michezo nchini, kama ilivyo kwa ofisi nyingine kama TANROADS. Wazo hili bado halijafanyiwa kazi na hatujui ni kwa sababu gani.

SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani

Kuviondoa viwanja vya michezo chini ya Wizara ya Utamaduni, Michezo na Sanaa na kuviweka chini ya wakala huru wa viwanja vya michezo au mamlaka kunaweza kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa si katika uendeshaji wake tu, bali hata katika kufufua michezo mingine.

Ni dhahiri kuwa ofisi huru ya wakala wa viwanja itajikita zaidi katika kuhakikisha kuwa viwanja vinatumika kwa ufanisi, vinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, vinaingiza fedha zinazotakiwa zirudi Serikalini, na inaajiri watendaji na wasimamizi wenye taaluma na wanaopata mafunzo mara kwa mara kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na vinakuwa na uongozi usiobadilishwabadilishwa kwa matakwa ya kisiasa au kutolewa kafara.

Kama Serikali itaongeza viwanja viwili kwa ajili ya AFCON 2027, maana yake usimamizi utatakiwa uwe mkubwa zaidi na unaojitegemea ili uweze kupanga mipango yake kulingana na mahitaji ya michezo.

Hivi sasa uendeshaji wa uwanja huo hutegemea fedha zinazotengwa kwa wizara hiyo, ambayo kwa kweli fungu la maendeleo huwa ni dogo sana. Hata uwanja changamani ambao ungekuwa katika awamu ya pili ya ujenzi wa Uwanja wa Mkapa, bado haujajengwa na hakuna matumaini hayo.

Chombo imara

Tunahitaji chombo imara cha kusimamia viwanja vya michezo vya Serikali kitakachokuwa kinabuni mikakati thabiti ya kuviendeleza, kuendeleza nguvu kazi na kuweka teknolojia inayotakiwa, kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Mamlaka ya Bandari, ambazo zimeajiri watu kulingana na taaluma zinazotakiwa na si kutafuta watu ndani ya wizara na kuwapa majukumu ya usimamizi.

SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?

Kwa hiyo, ni muhimu wakati huu ambao tunafikiria kuandaa fainali za AFCON 2027, kuanza kufikiria pia uendeshaji wa viwanja vyetu vya michezo kama unastahili kuendelea kuwa chini ya wizara, ambayo kwa kawaida hujishughulisha zaidi na kusimamia sera, au kuwa chini ya taasisi itakayojikita kusimamia viwanja tu.

Kama ungeniuliza, ningekwambia huu ndiyo wakati muafaka wa kuanzisha chombo hicho maalum cha kuendesha na kusimamia viwanja vya michezo wakati huu tunajiandaa kuikaribisha Afrika hapa nchini.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts