The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukombozi wa Tanzania Unahitaji Kwanza Mapinduzi ya Maarifa

Bila mageuzi ya fikra, taifa litaendelea kukuza roho ya ufisadi ambayo itaitesa nchi karne nyingi zijazo.

subscribe to our newsletter!

Jarida la Encyclopédie, lililotoka katikati ya karne ya 18, lililoandikwa na mwanafalsafa Denis Diderot, mwanahisabati Jean le Rond d’Alembert na wengine 150 ni nguzo muhimu ya Zama za Maarifa, au Enlightenment Age kama wanavyosema kwa kimombo, zama zinazotambulika kama mhimili wa historia ya matokeo makubwa ya maendeleo ya kisayansi barani. 

Zama za Maarifa zinajumuisha mitazamo na kazi za kifalsafa za Francis Bacon, John Locke mpaka Sir Isaac Newton. Ukiachana na Encyclopédie, pia kuna chapisho la Discourse on the Method la Rene Descartes la mwaka 1637, kama nguzo nyingine muhimu ya Zama za Maarifa barani Ulaya. Kwa kifupi sana, chapisho hilo linaeleza kuwa fikra za mtu ndiyo msingi wa mtindo wa kuishi.

Maarifa, au enlightenment, ni majumuisho ya mawazo ambayo kitovu chake ni msingi wa furaha ya binadamu, msako wa maarifa yenye kupatikana kwa njia ya kuhoji, na uthibitisho wa kifikra. Inakwenda mbele zaidi na kugusa sheria asilia, uhuru, maendeleo, uvumilivu, undugu, Serikali ya Kikatiba, na mgawanyo kati ya dola na dini.

Kuanzia tafsiri ya Zama za Maarifa mpaka maudhui ya jarida la Encyclopédie, Diderot alifafanua kuwa msingi wake mkubwa ulikuwa kubadili namna watu walivyofikiri, kuwafanya wajielimishe wenyewe, na kujua mambo mengi.

Maarifa na ufisadi

Miaka 400 imekatika tangu Zama za Maarifa – Karne ya 17 mpaka 21 –, misukosuko mingi imeikumba Ulaya, vita za dunia, ya kwanza na ya pili, ila ukipitia ripoti ya kimataifa ya Kielelezo cha Mtazamo wa Rushwa, au Corruption Perceptions Index (CPI), Ulaya ina afadhali kubwa kwa vitendo vya rushwa kuliko mabara mengine.

Nchi ya Denmark, kwa mfano, inaongoza duniani kwa kutokuwa na matendo ya rushwa. Mataifa mengine ya Ulaya – New Zealand, Finland na Norway – yanafuatia. Singapore ndiyo nchi pekee kwenye 10 Bora kutoka nje ya Ulaya, yenye unafuu wa rushwa.

SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: Je, Ufisadi Unatokana na Udhaifu wa Serikali au ni Tatizo la Kijamii?

Mataifa mengine ndani ya 10 Bora, yenye matendo machache ya rushwa ni Sweden, Uswis, Uholanzi, Ujerumani, Luxembourg na Ireland. Taifa la Marekani, licha ya kutofanya vizuri kwenye vielelezo vya rushwa, lina mifumo imara yenye kudhibiti rushwa na haonewi mtu aibu.

Hazijapita siku nyingi tangu Seneta wa New Jersey, Bob Menendez na mkewe, Nadine Arslanian, wafikishwe mahakamani kwa kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara watatu, Wael Hana, Jose Uribe, na Fred Daibes.

Menendez alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Marekani kabla ya kuibuka kwa kashfa hiyo. Anatuhumiwa kupokea maelfu ya Dola za Kimarekani na dhahabu ili kuwasaidia wafanyabiashara hao kwa kutumia mamlaka yake ya useneta.

Hivyo ndivyo mifumo ya Marekani inavyofanya kazi na adhabu ni kali kwa wala rushwa. Pamoja na hivyo, nchi hiyo haimo hata ndani ya 20 bora miongoni mwa mataifa yenye unafuu wa rushwa. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya CPI 2022, iliyochapishwa Januari 2023.

China ni hatari sana. Wananyonga wala rushwa. Pamoja na hivyo, haimo hata katika nchi 60 bora duniani zenye afadhali ya rushwa. Mantiki hapa ni kuwa maambukizi ya namna bora ya kufikiri ni tiba kubwa kuliko sheria kali!

SOMA ZAIDI: Profesa Mussa Assad: Ufisadi Umeshamiri Kwa Sababu Mafisadi Hawaadhibiwi

Ulaya waliamua kushughulikia kwanza namna ambavyo mtu mmoja-mmoja anapaswa kufikiri, anavyoweza kusaka maarifa, na anavyoyaendea mabadiliko ya kimaisha. 

Unaweza kusema hata walivyosafiri kutoka kwenye nchi zao na kukomba rasilimali za Afrika, Asia na Amerika, kisha kuzigeuza nchi za mabara mengine kuwa makoloni, halafu rasilimali za mabara mengine wakazitumia kuijenga Ulaya yao, ni matunda ya kufikiri tofauti kwa watu wa bara Ulaya.

Ujamaa au ubepari?

Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere ilipiga hatua kubwa katika kujenga watu kufikiri kijamaa. Watoto waliandaliwa tangu darasa la kwanza kuishi kijamaa. Mitaa ikapokea. Taifa likaelewa falsafa.

Tamati ya muongo wa tisa, Karne ya 20, ilikuja na mabadiliko. Tanzania, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ikahama kutoka kwenye itikadi ya Ujamaa na kuchepukia uchumi wa soko. Nchi ilihama pasipo kuwaandaa Watanzania kufikiri tofauti. Hiki, kwa maoni yangu, ndicho kinachoitesa nchi yetu hivi sasa. 

Kwa miaka 29, nchi inaimbishwa wimbo kuwa ubepari ni dude hatari. Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa kwaya, Watanzania ndiyo wanakwaya. Taifa likaimba kwa sauti za kupanda na kushuka.

SOMA ZAIDI: Mfumo Wetu Wa Uchumi Na Dhana Ya Ukosefu Wa Ajira

Mwandishi wa Marekani, William Arthur Ward, aliyefariki dunia mwaka 1994, anatambulika sana kwa nukuu yake kuhusu mwalimu bora, inayosema: “The mediocre teacher tells. The good teacher explains. The superior teacher demonstrates. The great teacher inspires.” 

Kwa tafsiri isiyo rasmi, anamaanisha mwalimu wa kawaida husema, mwalimu mzuri hufafanua, mwalimu bora huonesha kwa mifano, mwalimu aliyetukuka huhamasisha.

Mwalimu Nyerere alitimiza kila sifa ya mwalimu katika kuhakikisha Ujamaa unaeleweka na unakolea kwenye fikra za Watanzania. Fikra zilichakatwa. Walimu walinolewa. Yeye mwenyewe aliandika vitabu.

Nyerere alitafsiri kitabu cha The Merchant of Venice cha William Shakespeare hadi kuwa Mabepari wa Venisi, ongeza machapisho mengine mengi yenye kulaani ubepari.

Nchi ilipohama mhimili wa Ujamaa, ilikosa wafundishaji mahiri mithili ya Mwalimu Nyerere. 

Matokeo yake, nchi ina rangi mbili. Wapo wenye mitazamo ya kijamaa na wanatetewa na Katiba, inayosema Tanzania bado ni taifa la kijamaa. Wengine wameshahama kiakili na wameuendea ubepari kwa pupa. Nchi ina fikra mchanganyiko. 

Nchi ya kitu kidogo

Rushwa na ufisadi vinastawi katikati ya fikra mchanganyiko. Taifa likaangukia kuwa Nchi ya Kitu Kidogo kama alivyoimba Eric Wainaina, sasa imestawi, imekuwa taifa la roho ya ufisadi.

Mfanyabiashara anawaza kukwepa kodi. Mtumishi wa umma hesabu zake za kujikomboa kimaisha ni kuiba. Wanasiasa walishafika mbali kujaribu kuhalalisha rushwa ya uchaguzi kwa kuiita ‘takrima.’

SOMA ZAIDI: Ufisadi Kama wa TPA Utakomeshwa na Mikataba ya Manunuzi Serikalini Kuwekwa Wazi

Tumekuwa nchi ya kutoaminiana. Mwananchi anamtafsiri mwanasiasa ni mwizi. Mbunge anamwona waziri ana fedha nyingi. Rais kila uchwao anapokea taarifa za ukweli na nyingine za uzushi kuhusu wasaidizi wake kukwapua fedha kifisadi.

Nchi ya roho ya ufisadi. Zabuni hazitolewi kwa vigezo mpaka kwanza rushwa. Mla rushwa anamwaga fedha kumchafua mla rushwa mwenzake, ni nongwa kwamba wa pili hali vizuri na wenzake. Anajimegea “minyama” peke yake.

Mwingine si mla rushwa ila hapendwi kwa sababu anaweka “kauzibe” kwa wapigaji. Vita zinapiganwa Serikalini mpaka wakati mwingine Rais anachanganyikiwa. Anashindwa kumtambua nani mwovu na yupi hana hatia.

Wananchi nao wanaimbishwa nyimbo zenye majina ya mafisadi. Ushahidi dhidi ya wanaosemwa ni mafisadi hauwekwi wazi na hatua za kisheria hazichukuliwi. Ndivyo roho ya ufisadi inavyoendesha nchi. Fisadi anaweza kumzushia msafi, tena akihonga wanahabari na wana-mitandao ya kijamii maarufu.

Wenye mamlaka Serikalini wanasaini mikataba chini ya ushawishi wa rushwa. Wakati mwingine mikataba inayosainiwa ni salama kwa nchi, ila inapigwa vita kali na wataalamu wa mgawo wa asilimia, kwamba waliosaini wamekula peke yao.

Mapinduzi ya maarifa

Tulipo, Tanzania inahitaji mapinduzi ya maarifa. Watanzania wabadili aina yao ya kufikiri na jinsi ya kutazama mambo. Enlightenment Age iliwafanya Wazungu Ulaya kupora rasilimali Afrika na mabara mengine, wakajenga nchi zao na bara lao. Tanzania, watu kwa ubinafsi, wanakula rushwa na kuacha wageni wanaiibia nchi yake.

SOMA ZAIDI: Maafisa Waandamizi wa Serikali Wadaiwa Kuhongwa Mabilioni ya Fedha na Iliyokuwa Acacia

Tunahitaji sayansi mpya ya kufikiri kuhusu nchi na namna Mtanzania na Mtanzania wanavyoweza kutazamana kama ndugu. Hivi sasa hali ni mbaya. Roho mbaya imezalishwa ndani ya roho ya ufisadi. Utu unatoweka. Yupo Mtanzania anaona sawa wenzake wafe ili yeye apate.

Bila mapinduzi ya maarifa, nchi itaendelea kubaki palepale. Zitajengwa barabara chini ya kiwango zenye kukarabatiwa mwaka kwa mwaka au kujengwa upya kila baada ya miaka mitano kwa sababu hakuna fikra za kujenga miundombinu ya kuishi zaidi ya karne.

Miaka 62 ya uhuru, maji na umeme vinaendelea kuwa mateso kwa sababu hakuna maarifa ya utatuzi wa kudumu na kama yapo basi yanapigwa vita. Bila mageuzi ya fikra, taifa litaendelea kukuza roho ya ufisadi ambayo itaitesa nchi karne nyingi zijazo.

Rene Descartes katika katika chapisho lake la Discourse on the Method anaeleza kwamba fikra ndiyo msingi wa mtindo wa kuishi, ananisaidia kuhitimisha kuwa ufisadi unaitesa Tanzania kwa sababu ya namna Watanzania wanavyofikiri. 

Hata kusuasua kwa maendeleo, chanzo ni fikra!

Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *