Septemba 29 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Moyo Duniani kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu afya ya moyo na magonjwa ya moyo, na kuongeza juhudi za kuzuia, kutambua, na kutibu magonjwa ya moyo kwa wakati.
Kwa mwaka huu wa 2023, dunia imesherehekea siku hiyo chini ya kauli mbiu isemayo Tumia Moyo Kulinda Moyo. Hapa kwetu Tanzania, magonjwa ya moyo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana sambamba na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Kwa mfano, tafiti zinaonesha kwamba wagonjwa milioni 1.5, sawa na asilimia 49 ya wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza, walihudhuria vituo vya huduma za afya nchini mwaka 2022 kwa sababu ya shinikizo la juu la damu, kutoka asilimia 34 iliyorekodiwa mwaka uliopita, 2021.
Miaka 30 ilyopita, ni asilimia tano tu ya wananchi walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu. Shinikizo la juu la damu ni moja ya vichochezi vikuu vya magonjwa ya moyo.
Hii yote inamaanisha kwamba mpango kazi bora wa kupambana na magonjwa ya moyo ni muhimu kwa taifa. Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba Tanzania haina mpango kazi, au Action Plan, huo wa kupambana na magonjwa ya moyo.
Mtindo wa maisha usiofaa
Sababu kuu za magonjwa ya moyo kwa watu wazima ni mtindo wa maisha usiyofaa, ikiwemo matumizi ya tumbaku, unywaji pombe, lishe isiyofaa, haswa ulaji wa chumvi kupita kiasi kinachoshauriwa, na kutokufanya mazoezi.
SOMA ZAIDI: Wanaoishi na Kisukari Mtwara Wafurahia Kufikiwa na Huduma Nafuu za Matibabu
Kuongezeka kwa shinikizo la damu, unene wa kupitiliza na kisukari, ni vichochezi muhimu kwa magonjwa ya moyo. Vichochezi hivi vinaweza kutambuliwa na kudhibitiwa mapema kupitia huduma bora za afya ya msingi katika ngazi za zahanati na vituo vya afya, ikiwemo kuviepuka kupitia elimu ya kinga kwa watu walio kwenye hatari ya kupata na vichochezi hivi.
Hii inatasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo yangeweza kusababisha vifo au gharama kubwa za matibabu.
Kwa watoto, sababu kuu ya kusumbuliwa na magonjwa ya moyo ni matatizo ya ukuaji kabla ya kuzaliwa, yanayosababisha kasoro kwenye maumbile ya moyo.
Mara nyingi, mtoto asipopata matibabu mapema huweza kumsababishia kifo, au matatizo makubwa ya moyo ya kudumu kwa kipindi chote cha uhai wake.
Matibabu ya operesheni za kurekebisha kasoro za maumbile ya moyo huepusha madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na magonjwa ya moyo, matibabu haya, hata hivyo, yana gharama kubwa.
Watoto ambao matatizo yao ya moyo hutambuliwa mapema na kupatiwa huduma za matibabu mapema ni wachache. Tafiti zinafanyika kugundua chanzo kikuu cha kutokea kasoro hizi.
SOMA ZAIDI: Soma Hapa, Unaweza Kuwa na Uraibu wa ‘Energy Drinks’
Lakini matatizo ya mama, kama vile kisukari cha ujauzito na shinikizo la juu la damu la ujauzito, yanaweza kusababisha mtoto kuzaliwa na ugonjwa wa moyo.
Njia bora ya kudhibiti magonjwa haya ni kupitia huduma bora za mama mjamzito karibu na mama, yaani katika zahanati na vituo vya afya.
Matatizo ya moyo yana athari kubwa kiafya na matibabu yake yana gharama kubwa, na hivyo huathiri uchumi kwa familia zinazopitia changamoto hizi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mfumo usiofaa
Mfumo usiofaa wa kugharamia huduma za afya uliopo hapa nchini kwetu unasababisha mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu kwa watu wenye magonjwa ya moyo kwa watu wasio na kipato kikubwa.
Taarifa ya Hali ya Uchumi ya 2022 inaonesha kwamba watu wachache sana wana bima ya afya.
Mnamo mwaka 2022, mifuko miwili mikuu ya bima ya afya, yaani Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) na Mfuko wa Bima ya Jamii (iCHF), ilikuwa na wanachama milioni 5.1, idadi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya watu nchini ya milioni 63.3.
SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?
Aidha, makusanyo yaliyotokana na kulipia kadi za uanachama wa bima ya afya 2022 yanaonyesha karibia nusu ya wanachama wa iCHF walikuwa si wanachama hai.
NHIF imefanya mabadiliko kwenye usajili wa Bima ya Watoto ya Shilingi 50,400 kwa mwaka, yaani TOTO Afya. Utaratibu mpya unawapa nafasi wazazi kusajili watoto wao kwenye TOTO Afya kupitia shule badala ya usajili wa mtoto mmoja mmoja.
Kutokana na mabadiliko haya, wazazi waliojiajiri, wanaotaka kupata bima ya NHIF kwa watoto wao wenye umri wa miaka chini ya mitano na wasiokidhi vigezo vya kupata Bima ya Afya shuleni, watatakiwa kusajili watoto wao kupitia vifurushi vya familia vya NHIF ambapo bei ya chini kabisa ya kifurushi ni Shilingi 312,000 kwa mwaka.
Utaratibu huu unaathiri ugharamiaji wa huduma za afya kwa watoto wa watu waliojiajiri na wenye kipato kidogo, na watoto wanaotegemea msaada wa jamii kupata bima ya afya.
Sera ya huduma ya afya bure kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano haitekelezeki kwani huduma za afya bure zinazotolewa kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya vya Serikali hazina ubora.
Mara nyingi, mzazi hujikuta akigharamia matibabu kwa kununua dawa au kwenda kwenye vituo vya huduma za afya vya binafsi.
SOMA ZAIDI: Wazazi wa Watoto Njiti Bahi Wafurahia Kufikiwa na Huduma za Watoto Wao
Kwenye ngazi za hospitali za rufaa, wazazi wengi wasio na bima hujikuta wakilipia wenyewe gharama za matibabu, wenye kipato wakipata athari kubwa za kuingia kwenye umaskini.
Watoto wadogo wenye magonjwa ya moyo wanaweza kuathirika zaidi na utaratibu mpya wa usajili wa kadi ya Toto pale ambapo mzazi hana uwezo wa kulipia bima ya familia wala matibabu.
Uhaba wa huduma bora
Tatizo la upatikanaji wa huduma bora kwenye zahanati na vituo vya afya vya Serikali,
pamoja na umuhimu mkubwa wa huduma bora za afya kuwa karibu na jamii katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo magonjwa ya moyo, linatia mashaka sana.
Kuna uhaba wa huduma za kuzuia, kutambua, na kutibu mapema magonjwa ya moyo kwenye ngazi za afya ya msingi, yaani zahanati na vituo vya afya, hivyo kusababisha vifo na athari za kiafya na kiuchumi kwa watu wenye magonjwa ya moyo.
Pamoja na ongezeko la ujenzi wa vituo vya huduma za afya, idadi iliyopo bado haikidhi mahitaji ya umma.
Watu wanaoishi vijijini na wenye kipato kidogo wanaathirika zaidi kwani vituo vya afya na zahanati nyingi zipo mjini zaidi ya vijijini. Pia, hawawezi kumudu gharama kwenye vituo vya huduma za afya vya binafsi.
SOMA ZAIDI: Hospitali ya Benjamin Mkapa Kutafiti Sababu ya Ongezeko la Tatizo la Mawe ya Figo Kanda ya Kati
Vituo vya afya ya msingi vilivyopo vina uhaba wa huduma bora, ikiwa ni pamoja na upungufu wa dawa, vifaa, huduma za kulaza wagonjwa, na idadi ndogo ya wafanyakazi wa afya wenye mafunzo.
Kwa mfano, uwiano wa chini kabisa wa wafanyakazi wa afya, yaani madaktari na wauguzi waliosajiliwa, na wagonjwa, unaohitajika ili kuweza kutoa huduma ya afya ya msingi kwa jamii ni wafanyakazi 2.5 kwa watu 1000.
Lakini, mpaka kufikia Machi 2022, jumla ya madaktari 26,090 walikuwa wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, ikiwa ni idadi ya madaktari 0.4 kwa kwa watu 1000.
Jumla ya wauguzi na wakunga waliosajiliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania ni 47,973, au wakunga 0.8 kwa watu 1000.
Aidha, kuna tatizo la mgawanyiko wa wafanyakazi wa afya, zahanati na vituo vya afya vijijini na maeneo ya pembezoni vikiwa na uwiano mdogo zaidi wa idadi ya wafanyakazi wa afya na wagonjwa kulinganisha na hospitali na vituo vya vingine vya huduma ya afya vilivyopo mijini.
Serikali itimize wajibu
Sisi ACT-Wazalendo tunaitaka Serikali iweke kipaumbele kwenye kuimarisha huduma za afya ya msingi ili kuzuia, kutambua mapema, na kudhibiti vihatarishi vya magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Serikali inaweza kufanya hivi kwa kuweka kipaumbele kwenye matatizo ya upungufu wa vituo vya huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya, ukosefu wa dawa, ukosefu na upungufu wa wafanyakazi wa afya wenye mafunzo.
SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Njia Bora Ya Kukabiliana Na Magonjwa Yasiyombukiza
Pia, Serikali inapaswa kuimarisha huduma za elimu ya kuzuia na kupambana na magonjwa yasiyoyoambukiza kwenye ngazi ya jamii, kupitia zahanati, na vituo vya afya. Juhudi hizi ziende sambamba na urekebishwaji wa mfumo wa kulipia huduma za afya.
ACT-Wazalendo pia tunaitaka Serikali ikamilishe mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote, kwa kuimarisha mfumo wa hifadhi ya jamii ili bima ya afya iwe fao la mfuko wa hifadhi ya jamii.
Mwisho, ni muhimu kwa Serikali kuweka mpango kazi utaoweka kipaumbele kwenye masuala makuu manne kwa magonjwa ya moyo: kuzuia, kutambua, na kudhibiti mapema vichochezi; huduma za utambuzi na matibabu; huduma kwa watu walioathirika na magonjwa ya moyo; na tafiti.
Dk Elizabeth Benedict ni mtaalamu wa afya ya jamii na Msemaji wa Sekta ya Afya ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia elizabethbenedict2013@gmail.com au X (Twitter) kama @DrBSanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.