Hatimaye, wawakilishi wa Tanzania waliosalia katika michuano ya soka ya klabu barani Afrika, Simba na Yanga, wamejua wapinzani wao watakaokutana nao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hii ni baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupanga makundi hayo Ijumaa na baadaye kutoa ratiba ya mechi hizo za kutafuta timu nane zitakazoingia robo fainali, hatua ambayo hakuna klabu ya Tanzania imewahi kuvuka tangu zianze kushiriki.
Simba na Yanga, kwa nyakati tofauti, zimefanikiwa kufika robo fainali kabla ya muundo huo haujabadilika na baada ya kubadilika, lakini imekuwa ni changamoto kubwa kwenda nusu na baadaye fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Tangu kutolewa kwa mgawanyo wa makundi hayo, kumeibuka mijadala yenye hoja za kujenga hofu na mingine kujenga matumaini kuwa moja ya klabu hizo mbili haitaweza kusonga mbele na nyingine ina kazi rahisi ya kuvuka makundi kutokana na rekodi na ushiriki wa timu hizo huko nyuma.
Simba imepangwa Kundi B pamoja na klabu za Jwaneng Galaxy ya Botswana, Wydad Casablanca ya Morocco na Asec Mimosa ya Ivory Coast, timu ambazo ameshakutana nazo kwenye michuano hiyo misimu ya karibuni na kupata matokeo tofauti.
Yanga imepangwa Kundi D pamoja na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri, Medeama ya Ghana na CR Bellouizdad ya Algeria.
SOMA ZAIDI: Huu ni Wakati Muafaka Kuanzisha Wakala wa Viwanja Vya Michezo
Kundi la Yanga lina mabingwa watupu kwenye nchi zao, na kibaya zaidi Al Ahly ndiye bingwa mtetezi aliyemfunga Wydad Casablanca katika fainali ya msimu uliopita, jambo ambalo limeleta hoja nyingi kuwa safari ya Yanga kutoka nje ya Ligi ya Mabingwa imeshafika kwa kuwa mbali na vigogo hao wa Afrika, ina mtihani mwingine mgumu mbele ya Belouizdad, bingwa wa Algeria kwa misimu mine mfululizo, huku Medeama akianza kuchomoza barani Afrika licha ya umri wake mdogo.
Ukuaji wa soka
Lakini katika miaka michache iliyopita, soka la Afrika kwa ngazi ya klabu limekuwa likikua kwa kasi maeneo mengi kutokana na programu za maendeleo za nchi hizo au uwekezaji unaofanywa na watu binafsi, kiasi kwamba zile timu kubwa zenye mashabiki wengi na zinazoendekeza utamaduni wa kale, zimeanza kufifia.
Usingetegemea jina kama Medeama kuwa kigogo wa soka nchini Ghana ambako kuna wakongwe kama Asante Kotoko na Accra Hearts of Oak ambazo zimeshatetemesha soka la Afrika huko nyuma.
Hata huko Algeria, Belouizdad, ambayo imeshatwaa ubingwa wa nchi hiyo mara nane, imeibuka kuwa hatari barani Afrika kwa miaka takriban minne iliyopita wakati wakali wanaojulikana kutoka taifa hilo la kaskazini mwa Afrika ni kama MC Alger.
SOMA ZAIDI: Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu
Klabu hiyo ilitwaa Kombe la Shirikisho msimu uliopita kwa ushindi wa sheria ya bao la ugenini dhidi ya Yanga na baadaye kutwaa Super Cup kwa kuizamisha Al Ahly na ES Setif, ambazo pia zimetwaa ubingwa mara nane kila moja.
Pengine timu inayoonekana kuwa kubwa katika makundi yote ni Al Ahly Sporting Club, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika, Afrika mara 11, ubingwa wa Misri mara 43 na Kombe la Misri mara 38 huku ikitwaa Super Cup mara 13. Ndiyo klabu yenye mafanikio makubwa barani Afrika.
Simba itakutana na Wydad Athletic ambayo ilishika nafasi ya pili nchini Morocco, lakini ambayo ni kubwa kuliko zote kwenye taifa hilo, ikiwa imeshatwaa ubingwa mara 22, makombe tisa ya Morocco na manne ya Elite Cup. Imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara tatu, Kombe la Washindi mara moja na Super Cup mara moja.
Timu nyingine ni Asec Mimosas, klabu yenye mafanikio kuliko zote nchini Ivory Coast ikiwa imetwaa ubingwa wa nchi mara 29 huku ikitwaa kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ambao Yanga ilishiriki pia. Inasifika kwa kuzalisha nyota wengi wa nchi hiyo wanaosakata soka barani Ulaya.
Jwaneng Galaxy ndiyo pekee inayoonekana kuwa si mbabe wa soka kimataifa, ikiwa ndiyo kwanza ina miaka tisa tangu ilipozaliwa mwaka 2014. Hata hivyo, imekuwa na mafanikio makubwa katika umri wake mdogo baada ya kutwaa ubingwa wa Botswana mwaka 2020 na 2023 huku ikishika nafasi ya pili mwaka 2017, 2018 na 2019, hali inahyoonyesha kukua hatua kwa hatua.
SOMA ZAIDI: Tufurahie Uenyeji AFCON 2027 Tukisuka Mikakati
Ilifika kwa mara ya kwanza hatua ya makundi msimu wa 2021-22 ilipoiondoa Simba katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, ikipata ushindi usiotarajiwa wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kwao.
Rekodi za klabu hizo pinzani kwa Simba na Yanga ndizo zinafanya mashabiki na baadhi ya wachambuzi kutabiri kuwa safari ya Watanzania imefika ukingoni au mmoja tu ndiyo anaweza kuchomoka na kutinga robo fainali.
Soka linabadilika
Lakini soka linabadilika kila mara. Haikutarajiwa Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita baada ya kuondolewa na Al Hilal katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na baadaye kukutana na kigogo wa Tunisia, Club Africain katika kuamua timu ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Lakini safari ikawa tofauti baada ya Yanga kushinda ugenini dhidi ya Watunisia na baadaye kupoteza mechi moja ya hatua ya makundi, huku ikishinda mechi za robo na nusu fainali pamoja na moja ya fainali, lakini ikaangushwa kwa sharia ya bao la ugenini, ambayo imeshawekwa kapuni barani Ulaya.
Kila mara klabu za Tanzania zinapopangiwa na za Afrika Kaskazini kama Tunisia, Algeria na Misri huchukuliwa kama zimeshatolewa kutokana na rekodi za Waarabu, na hasa ujanja binafsi wa wachezaji na ari ya ushindi wanayokuwa nayo wakati wote wa mchezo.
SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga
Rekodi za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ubabe wao unapungua na klabu kutoka kanda nyingine za Afrika zinazidi kuanza kufika hatua za juu za mashindano ya barani Afrika.
Ni kweli fainali tatu zilizopita za Ligi ya Mabingwa zilizikutanisha timu tupu za Afrika Kaskazini, lakini kuna mabadiliko makubwa katika kanda nyingine yanayoonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwavua ubabe Waarabu hao.
Katika miaka minane tangu 2016, Mamelodi Sundowns imefika nusu fainali mara mbili na kuishia robo fainali mara nne, ikiwa ni maendeleo makubwa kwa klabu iliyoanzishwa miaka 53 iliyopita.
Mwaka jana ndiyo klabu iliyokuwa ikivutia zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa na hakuna aliyetarajia kuwa ingeishia nusu fainali, ambako ilitolewa na Wydad.
Maendeleo kwa timu kama Mamelodi, Medeama, Jwaneng Galaxy, Simba na Yanga katika miaka ya karibuni yanaonesha kuwa muda wa kuhofia klabu za Afrika Kaskazini haupo tena.
Wakati Simba iliporudi hatua ya makundi miaka mitano iliyopita, ilikutana na vipigo vya kutisha katika mechi za ugenini, hali imekuwa ikizidi kuwa nzuri kwa gtimu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi kadri miaka inavyokwenda. Hali kadhalika Yanga ambayo ilitikisa soka la Afrika msimu uliopita ilipofika fainali.
SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani
Mafanikio hayo yanaonyesha kuwa hakuna hofu tena ya kucheza Misri, Algeria wala Tunisia kwa klabu zimefanikiwa kupunguza ule ushindi wa kishindo ulipokuwa ukipatikana awali.
Na hali haiwekani ikaendelea kuwa hiyohiyo ya kuondolewa kwa tofauti ndogo ya mabao na timu hizo za kaskazini kama kweli klabu zetu zinapiga hatua thabiti kama ilivyoonekana katika miaka michache iliyopita.
Na ukiziweza timu za Afrika Kaskazini, huwezi kusumbuliwa sana na timu kutoka kanda nyingine kama Afrika Magharibi, Afrika ya Kati au Kusini mwa Afrika. Na hilo pia limedhihirika katika miaka ya karibuni wakati timu kama Rivers, Nkana Red Devils, Marumo Gallants na Horoya ya Guinea zilivyokutana vipigo mbele ya vigogo hao wa Tanzania.
Simba na Yanga zikijidhatiti, lolote linawezekana!
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.