The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Matatizo ya Nishati Tanzania ni Matokeo ya Sayansi Kuburuzwa na Siasa

Siasa zitumike kuongoza, ila kila uamuzi wa kisiasa sharti utafsiriwe na wataalamu.

subscribe to our newsletter!

Makadirio ya hifadhi ya gesi asilia Tanzania ni futi za ujazo trilioni (tcf) 57. Hii ni kwa mujibu wa kitabu Mining for Change: Natural Resources and Industry in Africa, kilichochapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford, Februari 13, 2020.

Taasisi ya Kimataifa ya Uongozi wa Biashara (ITA), mwaka 2017, ilitoa ripoti kuwa matumizi ya mafuta Tanzania yalikuwa pipa 35,000 kwa siku. Ripoti ya mtandao wa takwimu ulimwenguni, Worldometers, umeandika kuwa matumizi ya sasa ni pipa 72,000.

Maana yake ni kuwa ndani ya miaka sita, ongezeko la matumizi ya mafuta Tanzania ni zaidi ya maradufu. Ni tafsiri kuwa nchi inakua, shughuli za kiuchumi zinapanuka, matumizi ya nishati yanaongezeka kwa kasi, na mipango ya nchi haiendani na kasi ya ukuaji.

Maendeleo endelevu ya nchi hujengwa vema pale mambo matatu yanapokutana kwa usawa na kuachiana nafasi: siasa, sayansi na uchumi.

Siasa inaongoza nchi, lakini mipango ya maendeleo lazima ijengwe kiuchumi na kisayansi. Pale siasa inapoongoza, kisha mipango ikaandaliwa kisiasa, taifa lazima likwame au liingie mtaroni.

Hakuna wakati siasa peke yake ilifanikisha matokeo bora pasipo ushiriki wa sayansi na uchumi. Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema maendeleo ya nchi yanahitaji ardhi, watu na siasa safi.

Bila shaka, Mwalimu Nyerere aliposema nchi inahitaji siasa safi, alimaanisha siasa inayoheshimu sayansi na uchumi. Siasa safi ni wanasiasa kutambua na kuheshimu wataalamu.

FDR na Dili Mpya

Rais wa 31 wa Marekani, Herbert Hoover, alitaka kuivusha nchi kisiasa, nyakati za mdororo mkubwa wa kiuchumi, au great depression. Alifeli! 

Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt, au FDR kama anavyojulikana, aliingia na mipango ya kisayansi. Alitambulisha mpango alioupa jina la Dili Mpya, au New Deal, uliojengwa na R tatu.

SOMA ZAIDI: Ukombozi wa Tanzania Unahitaji Kwanza Mapinduzi ya Maarifa

R ya kwanza ilikuwa Relief, au nafuu, kwa wasio na ajira na maskini. R ya pili ni Recovery, au uhuishaji, wa uchumi mpaka kiwango cha kawaida. Na R ya tatu ni Reform, au mageuzi ya mfumo wa kifedha na kudhibiti kutojirudia kwa msukosuko wa uchumi wa viwanda.

Mipango ya kisayansi ndani ya New Deal iliivusha Marekani kwenye mdororo wa kiuchumi kutoka mwaka 1933 mpaka 1939. Na kutokana na uimara wa mipango ya kisayansi, Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilipoanza, Marekani, badala ya kutikisika, ilizidi kuimarika.

Ni sababu FDR kuchaguliwa mara nne, hivyo kuweka rekodi ya kuwa Rais wa Marekani aliyeshinda uchaguzi mara nyingi, vilevile aliyeongoza kwa kipindi kirefu zaidi. FDR alifanya siasa safi. Siasa yenye kuheshimu sayansi na mipango ya kiuchumi.

Ulaya ilibomoka wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, miundombinu iliharibiwa kwa mabomu. Majiji makubwa yakawa taabani. Mpango wa kisayansi wa Marshall Plan, au Mpango wa Marshall, ndiyo uliiwezesha Ulaya kujengeka upya na kuwezesha mataifa makubwa kurudi kwenye miguu yake haraka.

Brazil na sayansi ya uchumi

Kisha, tuitazame Brazil, taifa linaloshika nafasi ya 11 duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa, likiwa ndilo taifa lenye uchumi imara kuliko mataifa yote ya Amerika Kusini na Amerika ya Kati.

SOMA ZAIDI: Kukosekana Mwendelezo Serikalini Kunaigharimu Tanzania

Mwaka 1992, Brazil ilitisha ulimwenguni kwa mfumuko wa bei. Mwaka 1994, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Itamar Franco, alimteua Fernando Henrique Cardoso, au FHC, kuwa Waziri wa Fedha.

Chini ya urais wa Itamar, FHC alianzisha kampeni iliyoitwa kwa Kireno, Plano Real, yaani Mpango Halisi. Kipindi hicho mfumuko wa bei ulipaa mpaka kufikia zaidi ya asilimia 1,110 mwaka 1992 kisha mwaka 1993 ukapaa kwa kasi hadi kufikia 2,400. Ila Plano Real iliumaliza na nchi ikawa salama bila mfumuko wa bei.

Safari ya kuijenga Brazil yenye uchumi mkubwa ilianzia pale Itamar alipomteua FHC kuwa Waziri wa Fedha. Mwaka 1995, FHC alichaguliwa kuwa Rais wa Brazil na kuzidi kuifanya nchi hiyo kuwa imara zaidi kiuchumi.

Brazil leo ipo mbali kwenye uchumi wa viwanda duniani, huku Pato la Taifa (GDP) la nchi hiyo likiwa imara. Vita yao ya sasa ni kukuza na kujenga uwiano mzuri wa GDP na mchango wa kichwa kwa kichwa (GDP per capita).

Hapa kwetu Tanzania, kila baada ya miaka 10 nchi inafanya sensa ya makazi na watu. Lengo ni kuhakikisha nchi inaweka mipango mizuri ya maendeleo, yenye uwiano na ongezeko la idadi ya watu.

Kupatwa kwa sayansi

Miaka 62 ya uhuru, changamoto zinaongezeka. Mapya yanayoletwa na ongezeko la watu pamoja na teknolojia, yanakutana na matatizo ya tangu ujima. Matatizo ya mafuta yanaongezeka badala ya kupungua. Shida ya umeme haipati ufumbuzi. Sababu ni moja, sayansi inapatwa na siasa.

Taifa lenye kiwango kikubwa cha gesi, mipango ya kiuchumi na kisayansi haitekelezwi ili nchi iwe na umeme wa gesi, vilevile magari yatumie gesi, kuondokana na adha ya uagizaji mafuta ambayo yanatesa nchi.

SOMA ZAIDI: Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia

Umeme ni tatizo la zama zote tangu uhuru. Suluhu yake imekuwa matamko ya kisiasa. Nafuu inaonekana kwa muda mfupi kwa sababu ya tamko. Matatizo ya kimsingi yapo palepale.

Bila kuruhusu mipango ya kisayansi kuchukua nafasi, faida ya utajiri wa gesi haitaonekana. Siasa zitaendelea kuinyanyasa sayansi. Mateso ya nishati yataendelea kuwa janga sugu, utawala hadi utawala.

Kujenga mradi mkubwa wa umeme wa maji wa Julius Nyerere wakati mvua si uhakika, wakati una gesi ya kutosha ni matokeo ya siasa kuiburuza sayansi. 

Yapo maeneo yenye hali bora ya kuzalisha umeme wa upepo. Nchi ina urani ya kutosha ambayo ni elementi tajiri kwa uzalishaji wa nishati. 

Uhaba wa umeme uliopo sasa, bei ya mafuta inavyoitesa nchi, utajiri wa gesi uliopo nchini, uwepo wa urani na rasilimali mbalimbali zenye kutosheleza kuzalisha umeme, ni matokeo ya kushughulikia mambo kisiasa badala ya kisayansi na kiuchumi.

Mataifa makubwa yote, viongozi wa kisiasa huruhusu mawazo yao yachakatwe kisayansi na kiuchumi kwa kutumia wataalamu. Changamoto wanaziwekea mipango ya kisayansi na wanazimaliza.

SOMA ZAIDI: Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?

Hapa kwetu Tanzania, sayansi inaburuzwa na siasa. Wachumi wanapokea maelekezo kutoka kwa wanasiasa kwa mambo yanayohusu uchumi. Taifa linahitaji siasa safi ili kupiga hatua na kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za muda mrefu.

Siasa safi ni kuheshimu sayansi. Siasa zitumike kuongoza, ila kila uamuzi wa kisiasa sharti utafsiriwe na wataalamu. Vinginevyo, mwendo utakuwa wa kusuasua.

Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), zilikamilisha uhuru wake kutoka kwa Mwingereza mwaka 1971, miaka 10 baada ya Tanganyika, na miaka saba kutoka Mapinduzi ya Zanzibar. UAE ilikuwa jangwa tupu ilipokabidhiwa uhuru wake.

Mipango ya kisayansi imeibadili UAE ndani ya miaka 50. Ni matajiri wenye kila kitu. Taifa la Tanzania linahitaji sayansi na mipango madhubuti ya kisayansi, kufika mahali UAE ilipo.

Ni aibu kupitwa na UAE. Ni fedheha kuendelea kuona uduni wa nishati nchini kama changamoto juu ya uwezo. Inaumiza zaidi kufikiria kuwa kila kitu kinawezekana kama uzalendo na sayansi vitapewa nafasi na siasa kufungwa minyororo kwenye mambo yenye kuhitaji utaalamu.

Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *