Mengi yanasemwa kuhusu vijana hapa nchini kwetu kiasi ya kwamba wimbo huo sasa unaanza kuchosha kwenye masikio ya baadhi yetu. Vijana wa Kitanzania wanatupiwa kila aina ya sifa mbaya: wavivu, walevi, legelege, hawana maadili, hawafikirii maisha ya baadaye, nakadhalika.
Lakini tukichukua muda na kutafakari, hata kidogo tu, tutagundua kwamba vijana wanawajibika kwa kiwango kidogo sana kwenye mambo yanayoathiri ustawi na mwelekeo wa nchi hii, ambayo, kwa tathmini yangu, kwa kiasi kikubwa huchangiwa na wazee wetu.
Tujaribu kujiuliza maswali haya: wezi wakubwa wa fedha za umma hapa nchini kwetu ni akina nani, wabadhirifu wakubwa ni akina nani? Wanafiki wakubwa ni akina nani? Wakatili wakubwa ni akina nani?
Nani wanaongoza kutongoza binti wadogo na kuwaacha na mimba? Wanaodai rushwa kwa kijana ili apate ajira wakati hana kitu zaidi ya elimu yake? Wanaoimba nyimbo za kinafiki kabisa, na kudhihirisha uchawa uliokubuhu?
Wanaowazuia vijana wasizungumze kwenye mikutano ya mitaa na vijiji ni akina nani? Wanaowapendelea ndugu zao wasio na sifa na kuwaacha vijana kusota? Je, wanaorudi nyumbani wakiwa wamelewa na kuanza kutembeza vichapo kwa wenza wao ni akina nani?
SOMA ZAIDI: Je, Ni Kweli Ushirikishwaji wa Vijana Kwenye Uongozi Tanzania Ni Hafifu?
Sisemi vijana ni watakatifu wakati wazee ni ibilisi, la hasha! Hoja yangu hapa ni kwamba kama wazee wanataka kutumia mifano ya vijana wavivu kuwasema vijana wote, basi na vijana wajibu mapigo. Vijana wa siku hizi ni zao la wazee wa siku hizi!
Mkinzano wa vizazi
Hata hivyo, suala hili halishangazi hata kidogo kwa ni ni jambo la kawaida kwa vizazi vilivyotangulia kuvilaumu vizazi vilivyofuatia.
Wazee wa leo wanaolaumu mavazi ya vijana wa siku hizi ndiyo waliovaa mabugaluu, mapekosi, sketi fupi, nakadhalika wakiwa vijana hadi wazee wa enzi zile wakaanza operesheni ya kuhimiza mavazi ya heshima.
Binafsi nawafahamu baadhi ya wazee wa siku hizi niliowafundisha wakiwa vijana. Najua nani walitoroka shule na kwenda kulewa hadi kiranja mmoja alifichwa nyuma ya darasa kwani alikuwa hawezi hata kutembea!
Ilibidi viranja wenzake wawafukuze wale wa vidato vya chini waende kulala ili wambebe mwenzao hadi bwenini na kumbwaga. Najua waliotoroka kwenda kusikiliza Tabora Jazz enzi zile usiku kucha.
Najua walioweka konyagi pori kabla ya mdahalo ili waweze kuondoa aibu mbele ya dada zao na wapenzi wao watarajiwa. Nawajua waliopata mimba wakiwa shuleni.
SOMA ZAIDI: Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe
Wote hawa walikuja kuwa maprofesa, walimu mashuhuri, wafanyakazi bora na hata ‘waheshimiwa.’
Sijui kwa nini mtu akivuka ujana na kuingia ujuzi, au uzee, anapatwa na ugonjwa wa kusahau alikotoka, maana katika kuwalaumu vijana wanajilaumu wenyewe!
Naam, na wale waliowalaani wanabugaluu nao walilaaniwa na wazazi wao kwa kuacha mila zao na kuvaa suti na tai.
Ndiyo waliosaliti utamaduni wao, si tu wa mavazi bali pia kwa kukosa heshima wakirudi nyumbani, wakitamba mbele ya wazee na kuwalaumu eti wamepitwa na wakati. Mkinzano huu wa vizazi ni wa kudumu!
Mabaki ya ukoloni
Lakini ni mkinzano wa kudhuru na kudhulumu pia ambao, kwa sehemu, unaweza pia kuwa ni mabaki ya ukoloni.
Kutokana na kusoma, pamoja na kuongea na wazee sana sehemu mbalimbali za nchi, nimegundua kwamba kabla ya wakoloni kuja na mfumo dume wao, wavulana na wasichana wa Kiafrika walikuwa na nafasi kubwa kwenye kuamua hatma za jamii zao husika.
Wakoloni ndiyo waliowatenganisha vijana, hasa wale walioenda shule, na jamii zao, na kujazwa itikadi, dini, mitazamo, na tabia tofauti ili watumikie dola la kikoloni. Na kwa njia hiyo walijenga uhasama zaidi kati ya wazee na vijana.
Lakini vijana wa enzi zile waliweza kuwageuzia wakoloni kibao, kwa kuongoza mapambano ya kupata uhuru, na walirithi nafasi za wakoloni na nafasi kibao nyingine zilizotokana na upanuzi wa dola na vyombo vyake wakiwa vijana.
SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu
Na wamekaa nazo miaka yote. Sasa iweje wawalaumu vijana wanaotaka kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao na wao?
Kwa kweli, naamini kwamba wazee wamekuwa wajanja. Wanajua kwamba vijana wanawazidi katika elimu ya shule, katika kujua mambo mengi, katika matumizi ya teknolojia, nakadhalika.
Sasa wamebaki na nini ili waendelee kushika nafasi zao vizuri? Umri tu, na kwa wanaume wazee, udume, basi!
Ndiyo maana unawasikia wazee wakisisitiza, “Oh, vijana hawana heshima. Lazima watuheshimu. Mila na hila. Tuendelee na salaam za kitumwa!”
Naam. Waheshimiwe hata kama hawana heshima! Binafsi napenda kumheshimu yule anayejiheshimu.
Hakuna mtetezi
Na watetezi wa vijana ni akina nani haswa, Idara ya Vijana? Naamini wanajitahidi lakini ni kakijiidara kamoja ndani ya wizara yenye jina reeeeeeeefu na kabajeti kafupi. Au ni Umoja wa Vijana wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (UVCCM)?
SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani
Unaweza kuniambia ni wakati gani wamesimama kutetea haki za vijana wenzao? Wamewatetea Machinga? Wasichana wa kazi? Bodaboda? Wale wanaohukumiwa kwenda kwenye shule za ukata –majengo bila elimu–, wanaonyonywa hata wakipata kazi kwa kisingizio cha “kujitolea?”
Umoja huu wa vijana haupo kwa ajili ya vijana wenzao, bali kwa ajili ya kulinda wazee wao, ili na wao wapate nafasi ya kulindwa baadaye. Ndiyo maana watu wanalalamika kwamba vijana hawafai katika uongozi.
Vijana si wa aina moja na hawa ni vijana wa aina fulani tu, labda tuwaite vijachawa. Vijana wote wasihukumiwe kwa matamko na vitendo vya kundi hili dogo.
Vipi kuhusu umoja wa vijana wa vyama vingine je, vijana wao wamesimama kiasi gani kutetea vijana wasio nacho katika jamii?
Tuchukue nafasi za ushiriki wa vijana wa kawaida, kwa mfano, mitaani na vijijini. Tuliwahi kufanya utafiti takribani miaka kumi iliyopita kuhusu nafasi ya vijana katika jamii, tukiangazia vijiji vinne katika wilaya nane, vijiji 32 kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa
Katika vijiji 31, vijana walisema hawapewi nafasi za kuongea kwenye mikutano, wanadharauliwa na kubezwa pale wanapojaribu kuongea, vipaumbele vyao havipewi nafasi, fursa za vijana zinatolewa kwa watoto wa viongozi, nakadhalika.
Katika kijiji kimoja walikuwa wanachapwa hata viboko wakijaribu kutoa wazo lao. Sana sana wanahesabiwa kama nguvu-kazi ya bure katika miradi ya kijiji. Si kwamba hawataki kushiriki katika miradi hii lakini daima hawaulizwi, wanaamuliwa tu.
Kwa mfano, inaamuliwa waje Jumamosi saa fulani, ama sivyo watapigwa faini. Lakini Jumamosi ni siku yao maalum ya biashara zao, hivyo ni hasara kubwa kwao lakini lazima wakubali au faini na kunangwa.
Kwa kuwa ni nguvu kazi ya kijiji, kwa nini wasiulizwe na wao ni wakati gani ni bora kwao kufanya kazi hiyo? Sasa hapo tunashangaashangaa nini kama vijana hawataki kujihusisha na mambo? Wengi wamekata tamaa!
Vijana watambuliwe
Na wanaokata tamaa zaidi ndiyo wanaoingia kwenye ulevi wa aina mbalimbali. Lakini wangepewa mafunzo kidogo na nafasi wangefanya mambo makubwa sana.
Vijana ni waelimishaji, ni waraghbishi, ni watafiti, wanaweza kusaidia kuandikisha watoto na kufanya kazi nyingi za jamii ili mradi watambuliwe na kupewa uwezo wa kujikimu tu.
SOMA ZAIDI: Mama Samia Kuna Haya Mengine Kwa Vijana
Upande wa elimu sitaki hata kugusia. Utabaka umeweka mizizi hadi kuta za elimu zimeporomoka halafu tunashangaa kwa nini vijana hawaoni umuhimu wa kwenda kwenye shule ili wapigwe muhuri wa ‘KAFELI.’
Hawa vijana, kati ya miaka 15 na 35, ni asilimia 37 ya watu wote Tanzania; ni nguvu kazi ya taifa, na akili kazi, na ubunifu kazi, na jitihada kazi ya taifa.
Uzoefu wangu baada ya kufanya kazi na vijana katika sehemu nyingi ya nchi hii ni kwamba vijana wakipewa fursa walio wengi wanaikamata kwa mikono yote miwili na miguu hadi kucha la mwisho.
Siri ya maendeleo ya nchi yetu imelala kwa vijana, lakini lini watapewa vipaumbele, lini watapewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao?
Ukiangalia nchi nyingine, vitu kama maendeleo, ubunifu, na uvumbuzi vinaletwa na vijana, lakini hapa kwetu vijana wakija na wazo jipya wanaambiwa hawana heshima, wawasikilize wazee, na ubunifu huo unapotea moja kwa moja.
Hatuendelei kama taifa kwa sababu hatuwapatii nafasi vijana walete maendeleo. Kama hamniamini, wapatie fursa muone miujiza!
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.