Search
Close this search box.

Dar Mpaka Gaza, Krismasi Hii Itukumbushe Umuhimu wa Amani, Upendo

Ni dhahiri, katika sherehe ya Krisimasi, tunaadhimisha upendo wa Mungu kwa waja wake na viumbe vyake.

subscribe to our newsletter!

“Nitarejea nyumbani msimu huu wa sikukuu,” alisikika baba mmoja akiongea kwenye simu yake katika kimoja ya vijiwe vya kahawa vilivyopo hapo Namanga, jijini Dar es Salaam, akionekana kufurahia sana mazungumzo aliyokuwa akifanya.

Kama vile kicheko, maongezi yake siyo tu yaliniambukiza na kuniteka kihisia, bali pia yaliamsha dhamira ndani yangu ya kutaka kurudi kijijini kwetu kama ilivyo desturi miongoni mwa Watanzania walio wengi msimu huu wa sikukuu.

‘Kurudi nyumbani’ ni kauli ambayo hata huko mitaani na kwenye mabango, au vyombo vya habari, tunaisikia. ‘Rudi nyumbani kumenoga,’ linasema tangazo moja; ‘wanaita Afrika, mimi naita nyumbani,’ linasema jingine. Naam, zile hekaheka bin pilikapilika na shamrashamra za sikukuu zimeshaanza kutamalaki.

Unajua, haijalishi tupo wapi na tumetingwa na kazi kiasi gani, kuna hulka na haiba fulani ambayo inatutaka tukutane kama familia, au marafiki, ili kula karamu na salamu pamoja. Kuna hisia na hamasa fulani zinazoambatana na kurudi nyumbani, hasa pale tulipozaliwa na kukulia.

Ni zaidi ya mahali-kijiografia; ni kumbukumbu hai tunayotembea nayo, inayotupa hisia ya umiliki na mtazamo wa maisha ambao hutupa uimara na mwelekeo sahihi wa maisha yetu. Nyumbani ni mahali rejea unapojivunia, haijalishi papoje. La sivyo, wahenga wasingenena kuwa, mkataa kwao mtumwa.

SOMA ZAIDI: Mvutano Kati ya Mungu na Shetani Unaweza Kueleza Hali ya Sasa Tanzania?

Basi, juzi hapo katika pitapita zangu mjini, nikakutana na Mzee Chalamila (siyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), ambaye tunatoka kijiji kimoja cha Mapogoro, huko Iringa. Hatujaonana kitambo. Ile kukutana tu, akaanza kunisuta eti kwa nini simtembelei kwake. Ni kweli, sijaenda kwake kwa muda mrefu sasa. 

Nilisingizia kukosa muda na kusongwa kazini, ni kitubio. Ni kawaida na ada, kila tukikutana tunapiga soga na kukumbushana mengi, hasa yale wachunuzi wanaita intergenerational gap and crisis. Licha ya umri kumtupa mkono, mzee huyu bado ana mwenendo na mwonekano wa kijana. Ama kweli, utu uzima una siha na busara zake!

Kutegemeana

“Kila msimu una mizimu yake pia,” Mzee Chalamila alianzisha mada, huku nikimsikiliza kwa umakini. “Kipindi hiki cha Krismasi na kuelekea mwaka mpya, ni wakati muafaka wa kukutana pamoja kama familia na majirani. Udugu wetu umeunganishwa, siyo tu na damu na ukoo, bali na mfumo mzima wa maisha wa kutegemeana na kuhusiana.”

Mzee Chalamila alimeza fundo la mate na kuongeza, “Mwisho wa mwaka angalau jipe likizo. Jilipe, mwanangu! Ni nafasi nzuri ya kupumzisha nafsi, kujitafakari ulipotoka, unakokwenda na kujiwekea malengo mapya. Usiogope kujisikiliza.” 

SOMA ZAIDI: Msimu Huu wa Sikukuu, Tukumbuke Vitu vya Kuzingatia Tunaposafiri na Watoto

Kwa maneno hayo alinigusa roho hadi nikasugua kichwa.

Huenda kagundua kuwa siku hizi nakimbizana na mambo mengi sana, hasa yale yanayohusiana na umri wangu kama kijana. Ni nadra kukaa kimya na bure. Kufanya taamuli, au meditation, hatuenzi tena. 

Tunaogopa upweke kama vile ugonjwa fulani. Yamkini mfumo huu geugeu wa kibepari unatugeuza kama chapati jikoni. Unatufanya watumwa wa kazi na ujira kama maroboti. Tunaishi nyakati ombwe na mtanziko mkubwa!

Wakati anaongea juu ya Krismasi, mimi nilitaharuki na kuhama kidogo. Kimwili nilikuwa pale, lakini nilisafiri kifikira hadi Mashariki ya Kati. Naam, kule Gaza na Bethlehemu, Palestina, alikozaliwa mtoto Yesu, ambako hadi sasa mauaji ya halaiki yanaendelea, yakihalalishwa rasmi mbele ya macho yetu. 

Simanzi imetamalaki na mioyo imezizima. Tuseme sera yetu ya uhusiano wa kimataifa, jumuiya za kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vimeshindwa kazi yao. Ni fedheha na aibu kubwa!

SOMA ZAIDI: Je, Dunia Inaweza Kupata Suluhu ya Kudumu ya Mgogoro wa Israel na Palestine?

Binafsi niliwaza na kuwazua, jinsi Noeli ya Mariamu, Yusufu na mtoto Yesu ilivyokuwa. 

“Walifanana na sisi Waafrika-Wakristu kwa mambo mengi,” Mzee Chalamila alichangia. “Labda walitamani mwanao azaliwe kwao Nazareti kijijini, lakini waliishia Bethlehemu kama wakimbizi, maskini! Fikiria, Yesu, mwana wa Mungu, kuzaliwa pangoni, katikati ya wanyama na wachungaji.  Naye baba yake Yusufu, fundi seremala na mama yake Mariamu, binti mdogo, alipata mimba katika mazingira tatanishi.”

Fumbo la imani

“Tukio la Krismasi ni fumbo la imani, ni ushahidi dhahiri wa upendo wa Mungu kwa wanadamu. Na kipaumbele kiwe ni kumbukizi ya mtoto Yesu, siyo Papa Noeli au mti wa Krismasi,” aliongeza.

Nami naafiki fika kuwa hii ni kumbukizi nzuri, tuitumie ipasavyo. Namfahamu Mzee Chalamila kama mcheshi na mcha Mungu sana.

“Kila ninapowaza simulizi ya Noeli huwa najiweka katika nafsi ya kwanza ya Mungu, yaani navaa uhusika wa Mungu,” Mzee Chalamila aliongeza, huku akisafisha miwani yake. 

SOMA ZAIDI: Waraka wa Maaskofu Katoliki Kupinga Mkataba Bandari Wasomwa Makanisani Tanzania

“Kama Mungu, ningefanya mambo tofauti kuanzia kutungwa mimba mpaka kuzaliwa kwa mtoto Yesu,” aliendelea. “Nisingekubali tukio hili kubwa na la kipekee, la mtoto wangu aliyezaliwa bila kuumbwa, liwe la kienyeji vile. Vilevile, nisingekubali azaliwe tarehe ile ya kipagani, Dies Natalis Solis Invicti kama waimbavyo Walatini.”

 “Lakini mapenzi na matakwa ya Maanani ni tofauti na yetu, mzee wangu,” nilidakia. Ni dhahiri, katika sherehe ya Krisimasi, tunaadhimisha upendo wa Mungu kwa waja wake na viumbe vyake. 

Tena tunaimba mithili ya malaika na milki kuu Zaburi katika Novena kuwa, Bwana karibu atafika, njoni kumwabudu. Mbingu ifurahi nayo dunia ishangilie, nanyi milima pigeni vigelegele.

Kwa lugha nyingine ni katika sura hii ya mtoto mchanga, Mungu alifika na akajifanya sawa nasi, akawa nasi, akakaa nasi; ndiye Emanueli, Mungu pamoja nasi. Tuwe macho! Kristo yu aja, ujio wake umekaribia. Kwa maana, Mungu ndiye mhujaji amejaa haja na tija ya wanadamu. Alhamdulillah!

Thamani ya hadithi

“Kumbuka mtoto Yesu, alizaliwa katika familia na kaya kama zetu,” Mzee Chalamila alirudia na kudadavua. “Alipewa haki ya kuishi utoto wake na kusimuliwa zile hadithi kama vile sisi tulifundishwa chini ya miti pale kijijini kuhusu historia na falsafa ya uduara ‘ya Kiafrika’ ambayo ilidai kuwa maisha na historia vimo katika mzunguko radidi wa kuwapo na kuwa usio na mwisho lakini wenye kudakizana. 

SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

“Kupitia hadithi kemkem, tungo za kale kama inkishafi, visasili, michezo mbalimbali na methali, tulijitambua, kuaminiana na kufahamiana zaidi,” Mzee Chalamila aliongea kwa ari na umahiri sana.

Hali kadhalika, wanadamu tunaishi kwa kusimuliana. Sisi ni simulizi hai zinazotembea. Tena tunafikiria zaidi kupitia fasihi simulizi kuliko katika dhana, takwimu na namba. 

Hivyo, hata katika msako wa ukweli na vuguvugu zetu za ukombozi, ziwe za fikra au maendeleo endelevu, simulizi zina nafasi adimu sana katika kukuza akili tunduizi, ubunifu na udadavuzi, pamoja na utamaduni wa kujadiliana ambao, pasi na shaka, unaanzia nyumbani, hasa utotoni.

Ni jambo murua na mbawazi familia zinapokutana kusherehekea, kuumega mkate, kuimba tenzi za roho, kuwasha mishumaa na kufanya ibada za shukrani. 

Ni kile ambacho gwiji wa fasihi Chinua Achebe aliwahi kusema: “Ndugu anapowaita wenzake kwenye sherehe, hafanyi hivyo ili kuwaokoa na njaa. Wote wana chakula kwao nyumbani. Tunapokusanyika pamoja kama jamaa siyo kwa sababu ya kuona mbalawezi, kila mmoja anaweza kuiona mwake. Tunakuja pamoja kwa sababu ni vizuri kwa ndugu kufanya hivyo.”

SOMA ZAIDI: Fanya Hivi Kujenga Uhusiano wa Karibu na Mtoto Wako Pindi tu Anapozaliwa

Tuliagana na Mzee Chalamila, tukitakiana kheri na fanaka ya Krismasi ndani ya nyoyo zetu na chini ya paa zetu. Nikutakie na wewe, msomaji wangu, kheri ya Krismasi na Mwaka Mpya!

Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au Twitter kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

One Response

  1. Andiko zuri kabisa linatukumbusha muhimu wa tamaduni zetu tulizoishi tulipokuwa watoto ni dhahiri Sasa tunapaswa kuziambukiza kwa kizazi chetu. I’m motivated to go back home. “turudi nyumbani”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *