The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simba Iongeze Muda wa Maoni Marekebisho ya Katiba

Taarifa iliyotolewa na kamati Disemba 26 inashukuru wanachama kwa kutoa maoni yao na kueleza kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni Disemba 31.

subscribe to our newsletter!

Klabu ya Simba iko kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba yake baada ya kupewa maelekezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na pia kukosolewa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA).

Ni takriban miaka sita tangu klabu hiyo kongwe ya michezo ilipopitisha marekebisho ya katiba kwa ajili ya kubadili mundo wa umiliki na uongozi, lakini ikakumbana na vikwazo kadhaa vilivyotokana na kanuni za sheria ya umiliki wa kampuni, kiasi cha Tume ya Ushindani (FCC) kuzuia kwa muda kuendelea na mchakato na baadaye klabu kulazimika kubadili muundo wa umiliki, kutoka asilimia 51 za hisa zinazotakiwa zimilikiwe na mwekezaji hadi asilimia 49 za hisa zinazokubaliwa kikanuni.

Mbali na kasoro hizo za kiufundi kumekuwepo na kutofautiana kuhusu uendeshaji wa klabu, huku baadhi wakihoji kama mwekezaji ameshaingiza Sh. Bilioni 20 alizotakiwa kulipa kununua asilimia 49 ya hisa.

Lakini mwekezaji amekuwa akiongea mara kwa mara kuwa anatoa fedha za usajili zinazofikia shilingi bilioni, nje ya fedha ambazo anadai ameshaweka kwa ajili ya kununua hisa hizo.

SOMA ZAIDI: Kelele kwa Mangungu ni za Kukariri, Tatizo ni Kubwa Simba

Pia katika uendeshaji, pamoja na kwamba mwekezaji anatakiwa amIliki asilimia 49 za hisa, yeye ndiye ameishika bodi ya wakurugenzi, akiteua mtu wake kuwa ndiye mwenyekiti tofauti na utaratibu wa kawaida unaoupa upande ambao unamiliki hisa nyingi haki ya kuteua mwenyekiti katika bodi hiyo.

Pia kumekuwepo na mgongano au hali ya kutoeleweka katika uendeshaji klabu, na hasa timu ya mpira wa miguu, upande mmoja wanachama wakiona kuwa mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu ndiye anayekwamisha timu kufanya vizuri, huku wengine wakimtuhumu mwenyekiti wa bodi, Salim Try Again kuwa ndiye sababu na wachache wakiamini kuwa wote wawili hawastahili kushika hatamu.

Mambo yasingekuwa magumu zaidi kama timu ya mpira wa miguu isingekuwa na matokeo yasiyoridhisha uwanjani na hakuna siri kwamba kipigo cha mabao 5-1 walichopoewa na watani wao wa jadi, Yanga, kilikuwa kama kutia petroli katika moto uliokuwa unafifia.

SOMA ZAIDI: Mamelodi Wametoa Somo kwa Yanga, Simba

Hata hilo la kurudishiwa katiba ili ifanyiwe marekebisho kulingana na sheria za nchi limetoka kirahisi baada ya matokeo hayo mabovu, la sivyo lingechukuliwa kuwa ni hujuma kama timu ya soka ingekuwa inafanya vizuri.

Ni jambo jema kwamba Serikali inalirudisha suala la marekebisho ya katiba kwa wenyewe ili lifanyiwe marekebisho na wahusika, lakini uongozi umeligeuza suala hilo kama giza kubwa mbele ya wanachama.

Kamati iliyoundwa kushughulikia marekebisho hayo imetoa maelekezo kwa wanachama kutoa maoni yao kuhusu marekebisho ya katiba bila ya kueleza kwa mapana kasoro zilizoanishwa na serikali na zile zilizosumbua Rita, ili wanachama wawe na mwanga wakati wanapotoa maoni yao kuhusu marekebisho hayo.

Kwa sasa ni kama wako kwenye dimbwi kubwa wakiogelea bila ya kujua wanatakiwa waende wapi. Hawana mwongozo unaowaambia kuwa katika marekebisho yanayofanyika, maeneo muhimu yako katika suala gani, kwa sababu walishashiriki kutoa maoni kuhusu katiba nzima, takriban miaka saba iliyopita. 

Leo wanatoa maoni yao kuhusu jambo gani hasa au lolote wanalodhani ni muhimu waliseme tu, hata kama katiba imeshalishughulikia na lina majibu tayari.

Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo Disemba 26 inashukuru wanachama kwa kutoa maoni yao na kueleza kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni Disemba 31, yaani Jumapili na kwamba masuala hayo yatajadiliwa katika mkutano wa wanachama utakaofanyika Januari.

Taarifa hiyo inaitaja BMT na RITA lakini haielezi taasisi hizo zilikosoa nini na zimetoa maelekezo gani.

SOMA ZAIDI: Simba, Yanga Hazina Haja Tena ya Kuhofia Yeyote Ligi ya Mabingwa

Katika hali kama hii, kamati ya marekebisho ya katiba ndiyo ingechukua jukumu la kuongoza utoaji maoni. Yaani ingeanisha maeneo ambao yamo kwenye katiba ya sasa na ambayo yanatakiwa yafanyiwe marekebisho na kutoa sababu ili wanachama wajue kuwa sehemu muhimu ni ipi na hivyo wajikite katika maeneo hayo, labda tu kwa vipengele ambavyo wanadhani ni muhimu lakini havikuzingatiwa wakati wa marekebisho ya awali.

Na ndio utaratibu unaotumiwa na taasisi nyingi kuongoza marekebisho ya katiba. Kwamba Serikali imekataa kipengele fulani kwa sababu fulani na inataka kisomeke kwa namna nyingine ambazo zinaweza kuwa na mambo matatu ambayo wanachama watachagua lipi ndio lipite.

Ni kwa njia hiyo kunaweza kukawa na maoni ya kutosha ya wanachama ambayo yataipa kamati wigo mkubwa wa kujadili maoni hayo na baadaye kupeleka kwenye mkutano mkuu kile ambacho kimependekezwa na wengi ili uamue kitu kimoja.

Marekebisho ya katiba ni lazima yaongozwe ili kutoruhusu maoni ambayo si muhimu kwa wakati huo na pia kutoa fursa kwa wanachama wengi kutoa maoni kuhusu jambo ambalo wanalijua kuliko kuwaambia tu watoe maoni bila ya kujua kinachotakiwa kwa wakati huu ni nini na kilichokwamisha mchakato kutokamiliki ni nini.

Kama mwekezaji, Mohamed Dewji analalamika mara kwa mara kwamba kuna baadhi ya viongozi ndio wanakwamisha mchakato na kuna wakati atawataja, huu ni wakati wa kuweka bayana hoja wanazosimamia hao wanaoonekana wanakwamisha mchakato ili zijadiliwe na kupatiwe ufumbuzi.

SOMA ZAIDI: Timuatimua ya Makocha Imekuwa Mtindo Ligi Kuu

Ni vizuri kwamba marekebisho hayo yamekuja kipindi ambacho hakina mafanikio kwa timu ya soka na hivyo kutokuwepo na zile kelele za kupinga maoni ya wanachama wanaonekana kuwa tofauti na wengi. 

Kwa kawaida mafanikio ya timu za soka za klabu za Simba na Yanga huwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa kuwa hoja yoyote inayoibuka ni lazima ichangiwe kwa maoni chanya. 

SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa

Tukiwa tofauti, hata kama ni mazuri kiasi gani, yatachukuliwa kwamba ni ya wasaliti na wanaohujumu timu na historia zao zitafuatwa hadi huko nyuma kama waliwahi kumshabikia mgombea ambaye hakushinda ili kuthibitisha kuwa mawazo yake yanalenga kuihujumu timu.

Ni muhimu wanachama na viongozi wa Simba wakalichukulia suala hili kwa umuhimu mkubwa na ikiwezekana kamati itoe mwongozo kwa wanachama kuhusu vipengele vinavyotakiwa vifanyiwe marekebisho na si vibaya kama itaomba muda zaidi wa kukusanya mapendekezo yanayotokna na maelekezo.

Kila la heria Simba katika marekebisho ya katiba.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts