The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?

Mara nyingi waandishi wa habari hudhani kwamba changamoto wanazopitia, kama kukosekana kwa uhuru, ni mpya. Kitabu hiki kinatuonesha kwamba changamoto hizi si mpya na zimekuwepo siku zote.

subscribe to our newsletter!

Nimelifahamu jina la Ben Mtobwa tangu nikiwa shuleni. Riwaya yake ya Zawadi ya Ushindi ilimpa umaarufu mkubwa miongoni mwa wanafunzi kwani ilisomwa katika mfumo wa NECTA. 

Zaidi ya kitabu hicho, nilikuwa sijasoma vitabu vyake vingine mpaka hivi karibuni nilipokikuta kitabu hiki, Mhariri Msalabani: Siku Mia Moja na Hamsini za Mateso katika Maisha Yangu kwenye duka la vitabu la Kase, mjini Arusha; nilifurahi sana.

Enzi za uhai wake, Ben Mtobwa alikuwa mwandishi wa habari. Ndani ya kitabu hiki kilichochapishwa mwaka 2000, Mtobwa anaelezea jinsi ambavyo siku moja aliingia matatizoni kwa sababu ya kazi yake kama mwandishi wa habari. Mtobwa aliheshimika kama Mhariri Mtendaji na mmiliki wa gazeti la Heko, pamoja na kampuni ya uchapishaji ya Heko Publishers. 

Katika kitabu hiki kidogo, chenye takriban kurasa 62 tu, Mtobwa anatupeleka kwenye miaka ya tisini na kutuonesha, japo kwa kifupi sana, hali ya uandishi wa habari ilivyokuwa katika muktadha wa kusimamia haki za binadamu na utawala bora.

Shutuma za wizi

Tunapokutana na Mtobwa ni Julai 30, 1999, akiwa ana umri wa miaka 41. Katika mwaka huo, Mtobwa anakamatwa kwa kosa ambalo ukilisikia haiingii akilini: anashutumiwa kwa wizi wa vifaa vya ofisini. Mahakama ndiyo inayoweza kuamua kama aliiba au la, na kwa hakika, alipelekwa huko mahakamani. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Kama ilivyo ada, wanaanzia kwanza kituo cha polisi. Humo ndani anatupwa ‘shimoni,’ sehemu ambayo, kwa maelezo mafupi anayoyatoa mwandishi, yanakupa picha kuwa si sehemu ambayo ungependa kuingia hata kwa nusu sekunde. 

“Baada ya nusu saa,” Mtobwa anaandika kwenye ukurasa wa tano wa kitabu chake, “ilipatikana idadi ya kutosha ya wahalifu. Tukaongozwa na polisi mmoja kupelekwa shimoni, suruali zikiwa zimelegea kwa njaa na kukosa mikanda, miguu ikiwa wazi, huku tukichungwa kama mifugo. Nilijiona kama niliyeanza safari ya ahera, iliyojaa mateso na aibu.”

Kama hayo hayatoshi, anasema: “Umenyang’anywa viatu vyako bila maelezo yoyote, huku ukilazimika kutembea juu ya ujiuji wa kitu ambacho hujui kama ni maji, mkojo au matapishi na kulazimika kwenda hivyo chooni ambako ni bahari ya mkojo unaonuka vibaya tokea mlangoni, unaanza kupata hofu kama utatoka humo ukiwa hai.”

Kama ilivyo kwa mwandishi yeyote mdadisi, Mtobwa alitumia tukio hili kama fursa ya kudadisi mfumo wa haki na sheria unavyofanya kazi. Anahamahama kutoka kutumia nafsi ya kwanza katika simulizi yake kwenda nafsi ya pili, ambayo huwa haitumiki sana, kana kwamba anajaribu kuweka umbali kati yake na kile kilichomtokea. 

Kwa maneno yake mwenyewe, Mtobwa anaandika kwenye ukurasa wa tano: “Umekuwa ukiandika vitabu, umekuwa ukichapisha majarida, kazi ambayo taifa linahitajika kuithamini na hivyo, kukuthamini wewe pia, badala ya kukuchukulia kama kibaka yeyote yule, pengine mwenye hadhi ndogo kuliko mwuzaji wa madawa ya kulevya.”

Siyo mara ya kwanza

Haikuwa mara yake ya kwanza kuingia shimoni, anakiri hivyo yeye mwenyewe. Mara ya kwanza ilikuwa kwa sababu ya habari iliyoandikwa na Godfrey Mhando kwenye jarida la Mwanamama kuhusu biashara ya picha za wanawake wasio na nguo iliyoshamiri jijini Dar es Salaam wakati huo. 

SOMA ZAIDI: Zubayda Kachoka Lakini Ally Saleh Anaendelea Kupambana Zanzibar

‘Wakubwa’ hawakuifurahia habari hiyo. Kwa kuwa Heko ilichapisha jarida hilo, Mtobwa naye akaswekwa ndani. Heko iliwahi pia kufungiwa na Serikali kwa madai kuwa ilifanya ‘uchochezi’ kwa kuchapisha maoni ambayo ‘yangeweza kuhatarisha amani.’

Lakini kuhusu mashitaka haya yaliyompa mateso mpaka akayaandikia kitabu, Mtobwa hakuelewa kwa nini yalikuzwa kwa jinsi yalivyokuzwa. Kama ni stakabadhi ya malipo, alikuwa nazo; ushahidi mwingine uliohitajika, aliutoa. Hata hivyo, bado alionekana mwenye makosa. 

Kilichomshtua zaidi ni pale ambapo hakimu mmoja alimuuliza, “Vipi, kwani kesi hii ni ya uhaini?” Swali hili lilitokana na masharti magumu ya dhamana aliyokuwa amepewa Mtobwa.

Bila shaka kumekuwa na maendeleo makubwa katika tasnia ya habari nchini Tanzania kati ya wakati Mtobwa alipokuwa akifanya kazi na sasa. Zimetungwa sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya 2016; pia, kumekuwa na maboresho mbalimbali ya sheria hiyo, na zingine zinazotumika na wanahabari. 

Hata hivyo, tafakuri ya Mtobwa kutokana na alichokipitia inaendelea kuwa na hoja leo hii, zaidi ya miaka 20 baadaye.

Nafasi ya uandishi

Mtobwa anadadavua nafasi ya uandishi wa habari kwa kueleza mchango wake na wa gazeti lake nchini Tanzania, akiandika: “[Kwa] kujenga daraja la kisiasa mara tu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini na kuwapa uwanja mpana wanaoitwa wapinzani huku chama tawala wakiendela kupata haki yao.” 

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Mtobwa anaonesha jinsi mwandishi wa habari anaweza kuisababisha Serikali kubadilisha msimamo wake juu ya mambo yanayoathiri nchi. Anasikitishwa na waandishi waliokuwa wakiandika kuhusu yaliyomkuta kwa kuangazia upande mmoja; na kusema kuwa “mwandishi anaelezewa kama kioo cha taifa, sio tarumbeta au kasuku wa taifa.”

Ni rahisi kudhani kwamba changamoto tunazoziona katika tasnia zilianza na sisi. Tunadhani kwamba changamoto za uhuru wa vyombo vya habari zimeibuka tu sasa, na pengine huko nyuma kulikuwa na ahaueni; lakini ni muhimu kujifunza kutokana na historia kwani kila kitu kilichowahi kuwa, kitakuwa.

Mtobwa hakuishia ‘shimoni’ tu, alifika hadi gerezani huko Mwanza. Akiwa huko anakutana na mengi ambayo huwa hayafahamiki kwa urahisi nje ya gereza. Mtobwa anaangazia haki za wafungwa kwa kina – jinsi ambavyo hali zao za kiafya huzorota kwa lishe duni, hali ya uchafu, kupigwa, na manyanyaso mengine. 

Anaandika: “Katika gereza hili, kinyume na matarajio yangu ya awali, kuwa mfungwa anafundishwa maadili mema na kupatiwa mafunzo ili akitoka aweze kuachana na uhalifu na kuanza maisha mapya, mfungwa wa mahabusu anaingizwa katika genge la hatari, ambalo linamkaribisha katika dunia ya uhalifu na kumlea katika mazingira ya aina hiyo, akisubiri siku ya kutoka ili kwenda kuendeleza kile alichofundishwa.”

Nimefurahi sana kwamba Mtobwa aliandika yaliyomtokea. Ni wito kwa waandishi wa habari wa leo kufanya hivyo pia. Ni muhimu sana kuandika vitabu kuhusu kazi zetu katika muktadha wa kisiasa, kiuchumi na kijamii tuliopo. 

Yawezekana simulizi zetu zikaakisi mambo magumu, au mepesi. Cha msingi ni kwamba, tunachangia katika kutunza historia yetu kwa mtazamo wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts