Nimejitahidi kwa muda mrefu kufikiria kwa makini ni namna gani ya kumuenzi Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya pili aliyefariki dunia hapo Februari 29, 2024. Daima nimekuwa na hamu ya kutoa ziada kwa wasomaji wangu. Kutengeneza wasifu wa Mwinyi, ambaye anajulikana sana miongoni mwa Watanzania kama Mzee Rukhsa, kunaweza kuhusisha kuelezea historia yake tangu alipozaliwa hadi alipofariki.
Lakini swali langu ni jinsi gani haswa tunapaswa kumkumbuka mzee huyu? Nimefanya uamuzi wa kumuenzi kama mtumishi asiyekuwa na tamaa ya madaraka, ambaye alijitolea kwa dhati kwa ajili ya umma. Alikuwa na uwezo wa kusalimisha wadhifa wa uwaziri kutokana na uzembe wa wengine, na aligoma kugombea urais wa nchi, akiridhika kikamilifu na cheo chake cha urais wa Zanzibar. Hivyo, kwa kadri ya ufahamu wangu, nitajaribu kumwelezea Mwinyi kwa njia hiyo ya kipekee.
Siku moja mwezi Disemba mwaka 1970, wakati akihudumu kama Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Walima wa Karafuu, maarufu kama Clove Growers Association (CGA), Mwinyi alialikwa Ikulu na Rais Abeid Amani Karume.
Rais Karume alimweleza kwamba alipokea simu kutoka kwa Rais Julius Nyerere, ambaye alikuwa ameomba mapendekezo ya majina ya Wazanzibari wawili ambapo mmoja wao angechaguliwa kuingia kwenye Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa ya habari iliyotangazwa usiku huo ilithibitisha uteuzi wake kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais. Hapo ndipo safari ya kisiasa ya Mwinyi ilipoanzia.
Kujiuzulu uwaziri
Mwinyi alibakia kama waziri asiye na wizara maalum kwa kipindi cha mwaka mzima wa 1971 kabla ya uteuzi wake kuwa Waziri wa Afya katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ya 1972. Alihudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1975 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Ni wakati huu ndipo visa vya mauaji ya vikongwe viliibuka kwa nguvu katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kutokana na imani za kishirikina.
SOMA ZAIDI: Serikali za Majimbo na Ajenda ya Utaifa
Januari 24, 1976, aliyekuwa Waziri Mkuu Rashid Kawawa aliitisha kikao kujadili suala hilo. Wajumbe wa kikao hicho, kilichosimamiwa na Waziri Mkuu, kilimjumuisha Mwinyi katika nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; na Peter Siyovelwa ambaye alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais yenye dhamana ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Wengine walikuwa Peter Kisumo ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza; Marco Mabawa ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga; pamoja na maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Kikao hicho cha maamuzi muhimu kilikubaliana kuanzisha operesheni maalum iliyopewa jina la Operesheni Mauaji. Lengo kuu la operesheni hiyo lilikuwa ni kukamata na kuwahoji watuhumiwa. Hata hivyo, kwa kusikitisha, baadhi ya maafisa waliokuwa wakihusika na mahojiano walikiuka taratibu za kimaadili za kuhoji watuhumiwa.
Watuhumiwa walinyanyaswa kinyume cha sheria, na matokeo yake, wengi wao walipoteza maisha. Taarifa za visa hivyo ziliwasilishwa kwa Mwalimu Nyerere kabla ya kufikishwa kwa Mwinyi, ambaye kwa bahati mbaya alikuwa hajajulishiwa kuhusu vitendo hivyo.
Matukio haya yalisababisha hatua isiyo ya kawaida kuchukuliwa na Mwinyi, ambayo ni nadra katika utamaduni wetu. Kama waziri mwenye dhamana, Ali Hassan Mwinyi aliamua kuchukua uamuzi wa kipekee kwa kuandika barua kwa Mwalimu Nyerere ya Januari 22, 1977, akimuomba kujiuzulu kutoka kwenye nafasi yake.
SOMA ZAIDI: Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?
Baada ya Mwinyi kujiuzulu, Waziri Siyovelwa na wakuu wa mikoa Kisumo na Mabawa nao waliandika barua za kujiuzulu nafasi zao. Hatua hii ya Mwinyi ilikuwa ni uamuzi wa hiari, ukilenga kuhifadhi heshima ya Serikali na rais wake, Mwalimu Nyerere.
Ninaamini kwa moyo wangu wa dhati kwamba uamuzi wa kujitolea kujiuzulu ulimtengenezea Mwinyi heshima siyo tu miongoni mwa Watanzania, bali pia kwa kiongozi wao, Mwalimu Nyerere.
Ninaamini kwamba hatua hii ilikuwa ni mojawapo ya sababu zilizomwezesha baadaye Mwinyi kuinuliwa kama rais wa Zanzibar, na hatimaye, rais wa Tanzania. Hii ni somo muhimu kwetu sisi vijana, kuhimizwa kuishi kwa msingi na kanuni badala ya kushindana na kutamani vyeo vya uongozi.
Baada ya kujiuzulu, Mwinyi kwa mantiki iliyopo, alishushwa cheo na kuteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Misri. Baada ya kujiuzulu, Mwalimu Nyerere alimwita Mwinyi nyumbani kwake kumtaarifu kwamba baada ya mashauriano na Waziri wa Mambo ya Nje, Benjamin Mkapa, ameamua kumteua kuwa balozi nchini Nigeria.
Hata hivyo, baada ya muda mfupi, alimwita tena na kumuarifu kwamba, baada ya mashauriano zaidi na Mkapa, ameamua kumteua kuwa balozi nchini Misri. Mwinyi alitumikia kama balozi hadi mwaka 1981 aliporejeshwa nchini na kuteuliwa kama Waziri wa Maliasili na Utalii, na baadaye kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Muungano.
Urais wa Z’bar
Kuanzia Januari 24 hadi 30, 1984, kikao maalum cha Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kilifanyika kwenye Chuo cha Biashara Dodoma.
SOMA ZAIDI: Samia Azindua Tovuti ya Salim Ahmed Salim. Aagiza Tovuti ya Kumbukumbu Muhimu za Historia Ianzishwe
Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili suala la rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe, ambaye alikuwa ameshutumiwa na baadhi ya wajumbe kwa kosa la kujaribu kubadilisha katiba ya Zanzibar kinyume na taratibu ili kuipa Zanzibar mamlaka zaidi na kubadilisha muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu badala ya mbili, yaani Serikali ya Muungano, ya Tanganyika, na ile ya Zanzibar.
Ni muhimu kutambua kwamba kwa wale wanaomfahamu Mwalimu Nyerere, hata kwa kiwango kidogo, wanaweza kufahamu jinsi suala la Muungano lilivyokuwa nyeti kwake.
Matokeo ya kikao hiki yalikuwa ni kujiuzulu kwa Rais Aboud Jumbe kutoka nafasi zake zote za kiserikali na kichama hapo Januari 29, 1984.
Hii ilijumuisha nafasi yake kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Taarifa zakujiuzulu kwa Jumbe zilitolewa na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Daudi Mwakawago, kwa vyombo vya habari.
Katika kikao cha Kamati Kuu ya NEC kilichofanyika Januari 30, 1984, mapendekezo yaliyowasilishwa yaliweka jina la Ali Hassan Mwinyi kwa mbele. Hivyo, ndivyo safari ya Mwinyi ilivyoanzia kuhudumu kama Rais wa Zanzibar kuanzia Januari 31, 1984, hadi Oktoba 17, 1985.
Baada ya miaka saba tangu kujiuzulu kwake kutoka uwaziri katika wizara yenye umuhimu mkubwa na kushushwa daraja, Mwinyi alijukuta miongoni mwa viongozi wakuu wa Tanzania. Historia ya Aboud Jumbe kujiuzulu na kisha Mwinyi kuchukua nafasi yake ni ndefu kidogo ila kwa mantiki ya makala hii niishie kwa haya niliosema.
Urais Tanzania
Kama ilivyokuwa katika uongozi wa Zanzibar, ndivyo hivyo ilivyokuwa katika uongozi wa Tanzania. Mwaka 1985, Mwinyi alitarajia kuendelea kutumikia kama Rais wa Zanzibar, lakini mapenzi ya Mwenyezi Mungu yalikuwa na mipango tofauti kwa ajili yake.
SOMA ZAIDI: Viongozi Hawa Kumi wa Tanzania Watakuhamasisha Kupenda Kusoma Vitabu
Kwa mujibu wa mfumo wa CCM wa wakati huo ambao ulikuwa unazingatia chama kimoja, Mwenyekiti, ambaye wakati huo alikuwa Mwalimu Nyerere, alipendekeza majina kwa ajili ya mchakato wa mahojiano na upigaji kura. Mwalimu Nyerere alileta majina matatu: Salim Ahmed Salim, Rashid Mfaume Kawawa, na Ali Hassan Mwinyi.
Baadaye, Kawawa aliamua kujitoa katika kinyang’anyiro hicho, akiamini kwamba mrithi wa Mwalimu Nyerere anapaswa kutoka nje ya kundi la wapiganiaji uhuru. Pia, lengo la Mwalimu Nyerere la kutaka rais ajaye atoke Zanzibar linaweza kuwa moja ya sababu zilizomshawishi Kawawa kujiondoa.
Kwa hivyo, majina mawili ya Wazanzibari yaliendelea kubaki, yaani Salim na Mwinyi. Mwalimu Nyerere aliwashirikisha wazee wa chama kutoka Zanzibar, lakini kwa bahati mbaya, wajumbe hao hawakutaka kusikia jina la Salim kutokana na tuhuma mbalimbali zisizo na msingi dhidi yake.
Pamoja na changamoto zote, majina ya Salim na Mwinyi yalijadiliwa kwa kina na vikao vya CCM husika, ambavyo vilijumuisha viongozi kutoka Tanganyika na Zanzibar. Wengi wa wajumbe waliona kuwa Mwinyi ndiye mgombea anayefaa zaidi, na hivyo jina lake likateuliwa kugombea urais.
Mwinyi mwenyewe alikiri kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na upendeleo kwa Salim, lakini mwishowe, kudra za Mwenyezi Mungu zikamuangukia yeye.
SOMA ZAIDI: Maswali ya Msingi Kuhusu Sanamu ya Mwalimu Nyerere Iliyozinduliwa na Umoja wa Afrika
Kama ilivyokuwa desturi katika mfumo wa chama kimoja, mgombea mmoja alipigiwa kura na wanachama, na kisha wananchi kupiga kura ya ndiyo au hapana. Uchaguzi ulifanyika Oktoba 27, 1985, na matokeo yalitangazwa tarehe Novemba 1 katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Adam Sapi Mkwawa, alimtangaza Mwinyi kuwa mshindi kwa kura 4,778,114, sawa na asilimia 93.01 ya kura zote zilizopigwa. Kwa manufaa ya historia, mwaka 1980 ni Watanzania 6,910,555 tu ndiyo waliojiandikisha kupiga kura. Waliopiga kura ni 5,181,999 na vituo vya kupigia kura vilikua 30,000.
Mwinyi alihudumu kama Rais wa pili wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 1985, hadi Novemba 23, 1995, alipomkabidhi kijiti kwa kiongozi wake wa zamani, Benjamin William Mkapa, aliyekua waziri wake wakati akiwa balozi.
Hii ni historia fupi sana ya safari ya kisiasa ya Hayati Ali Hassan Mwinyi. Makala yangu ililenga kutoa mtazamo tofauti kidogo na kuelezea kwa undani zaidi safari yake ya kisiasa. Maisha yake ya kisiasa yananikumbusha kauli nzito ya Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini, Togolani Mavura: “Kila mtu kwa karama yake, kadri yake na kudra yake.”
Hakuna haja ya kufanya mambo kuwa magumu sana, kwani mapenzi ya Mungu ndiyo hushinda kila mara. Na hili ni somo kubwa sana kwetu Watanzania wa sasa. Tunamuombea Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi!
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.