The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maswali ya Msingi Kuhusu Sanamu ya Mwalimu Nyerere Iliyozinduliwa na Umoja wa Afrika

Sanamu hiyo haijakidhi vigezo vyote vya kitaalamu vinavyohusu sanamu yenye hadhi ya kimataifa kama vile mfanano wa muhusika, kuibua haiba, au character na mkao, au posture.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Februari 18, 2024, Umoja wa Afrika (AU) ulizindua sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere mjini Addis Ababa, Ethiopia. Shughuli hiyo ilihudhiriwa na marais kadhaa, akiwemo Samia Suluhu Hassan, pamoja na wageni wengine wengi mashuhuri barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Hata hivyo, punde tu baada ya sanamu hiyo kuzinduliwa, Watanzania wengi walitoa maoni yao, wakisema kwamba sanamu hiyo haifanani na Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania aliyehudumu kama Rais wa taifa hilo kuanzia 1964 mpaka 1985.

Kitaalamu, sanamu yenye hadhi ya kimataifa kama hii inapaswa kuwa na matokeo matatu: mfanano wa muhusika kama hadidu za rejea zilivyotaka, kuibua haiba, au character na mkao, au posture

Hivi ni baadhi ya vitu muhimu katika kujiridhisha na ubora wa sanamu na vyote vitatu, kwa mtazamo wangu, havikutimizwa kwenye sanamu hii ya Nyerere. Maeneo mengine yanaweza kuwa mavazi, urefu, unene, nakadhalika. 

Mkao wa Mwalimu katika sanamu hii yenye mkono ulionyooka kama Papa anabariki watu, kwa mfano, haikuwa alama bora ya kumuwakilisha Mwalimu.

Mchoraji ni nani?

Jambo moja lililonishangaza katika shughuli hiyo ya uzinduzi ni kutotajwa mahala popote kwa msanii aliyefanikisha utengenezaji wa sanamu hiyo. Taarifa ya AU iliyotolewa kwa waandishi wa habari unaweza kusema ilimsahau aliyesanifu na kuchonga sanamu hiyo. 

SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar

Iko hivyo pia kwa vyombo vya habari kadhaa vilivyoripoti tukio la uzinduzi wa sanamu hiyo.

Lakini turudi nyuma kidogo kabla ya kulichambua suala hilo kwa undani zaidi. Akizungumza Bungeni Juni 6, 2023, aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana, alisema kuwa kampuni ya Epitome Architects Limited iko mbioni kukamilisha ujenzi wa sanamu hiyo. 

“Mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 205,942 unajengwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Sekretarieti ya SADC, Mameneja Mradi kwa kushirikiana na familia ya Mwalimu Nyerere na kwa mujibu wa Mkataba uliopo, inatarajiwa kukamilika Disemba, 2023,” alisema Dk Chana kwenye hotuba yake ya bajeti.

Kiasi hiki cha fedha, hata hivyo, kinatofautiana na kile kilichotajwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, ambaye amehudumu kama meneja wa mradi huo wa sanamu, Emmanuel Ishengoma, aliyenukuliwa hapo Mei 6, 2020, akisema kwamba gharama rasmi za mradi huo ni Dola za Marekani 267,992.60.

Ukweli ni kwamba Epitome Architects Limited, kama inavyojitangaza kwenye tovuti yake, ni kampuni ya uchoraji ramani za majumba, au architects, kama jina lao linavyooelekeza. Kampuni hiyo pia hufanya usanifu wa ndani, uongozi wa mikataba, usuluhishi, pamoja na kazi nyingine. 

SOMA ZAIDI: Ni Miaka 61 ya Uhuru Kweli?

Nilipopita kwenye tovuti yao niligundua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Epitome Architects Limited ni Nuru Nyerere-Inyangete, mwanafamilia wa Mwalimu Nyerere na mtoto wa hayati Joseph Nyerere.

Maswali mengi

Mtoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kusimamia ujenzi wa sanamu hiyo, amedai kuwa sanamu hiyo imepitia vigezo vyote vya kisheria na kitaalamu mpaka kufikia kuruhusiwa kupandishwa katika ofisi za AU. Kauli hii ya Madaraka Nyerere inazua maswali mengi.

Kwa mfano, ni kwa vipi kamati ilimpa kazi yenye hadhi ya kimataifa mwanafamilia ya Nyerere ambaye hafahamiki popote kama mchongaji, au sculptor? Je, Madaraka Nyerere aliwezaje kushiriki katika kinyang’anyiro cha kusimamia uchaguzi na usimamizi wa kazi iliyokuwa ikifanywa na kampuni ya mdogo wake bila mgongano wa kimaslahi?

Kwa kuwa kampuni ya Epitome Architects Limited siyo kampuni ya kuchonga, je, walipataje kazi hii? Hadidu za rejea za utengenezaji wa kazi hii zilitaka sanamu, au prototype, ipelekwe Dodoma kukaguliwa kwanza kabla ya ujenzi wa sanamu ya mwisho ili isimikwe Adis Ababa. Je, jambo hili lilifayika?

Kwa nini sanamu hii haikufanyiwa pre-testing? Je, kamati ilimtembelea msanii, au sculptor, kuona maendeleo ya kazi? Kampuni ya SAMCRO ya Afrika Kusini ilishinda zabuni ya kutengeneza sanamu ya Mwalimu Nyerere. Je, ni kwa nini haikufanya kazi hii na hivyo kupelekea kurudiwa kwa zabuni hii?

SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?

Mradi ulikuwa ni wa shilingi ngapi? Je, ni Dola za Marekani 267,992.60 kama Ishengoma alivyoripotiwa na vyombo vya habari Mei 6, 2020, au ni Dola za Marekani 205,942 kama ilivyotajwa na Dk Chana Bungeni mwaka 2023?

Kwa kuwa Ishengoma ndiye aliyekuwa meneja wa mradi – hapakuwa na mameneja wa mradi kama lilivyoelezwa Bunge– na pia mteja, au client, je, Serikali haikuona kuwa kwa kufanya hivyo kunaondoa uwezo wake wa kuukagua mradi na kwa hiyo kuleta mgongano wa kimaslahi?

Kwa kuwa kampuni iliyoshinda zabuni ilikuwa ya Kitanzania yenye ofisi zake jijini Dar es Salaam, je, wale Wazungu walioonekana Adis Ababa wakisimika sanamu ile walikuwa ni akina nani na wanatoka wapi? Je, historia yao katika kutengeneza eneo hili ikoje?

Historia za waasisi

Sheria ya Waanzilishi wa Taifa, au Honoring Founders Act, ya 2004, na kanuni zake za 2005, inaitaka Serikali kuunda chombo kinachoitwa Founders of the Nation Centre katika kifungu cha 4(1). 

Chombo hiki ndiyo kinapaswa kuwa na mamlaka ya kusimamia kazi, historia na mambo mengine yahusuyo Baba wa Taifa na Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar. Ni wakati muafaka wa kufuta ombwe la usimamizi na kutunza historia ya waanzilishi wa taifa letu kwa Serikali kuanzisha chombo hicho.

SOMA ZAIDI: Je, Serikali Inaifahamu Dhana ya Utamaduni Anuai?

Kimsingi, kwenye jambo hili, kama nchi, tumejidharaulisha mbele ya jumuiya ya kimataifa. Katika muktadha wa Tanzania na Afrika, Mwalimu Nyerere siyo mtu mdogo kabisa na ‘tusimchukulie poa,’ kama wanavyosema vijana. 

Pia, tukumbuke uwepo wa mradi huu haukutokana na wazo au bidii yetu sisi Watanzania bali aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, hayati Robert Mugabe, aliyelipigania kwa nguvu mwaka 2015, akisisitiza umuhimu wa Mwalimu katika bara la Afrika.

Kwa sababu Watanzania na walimwengu wengi wameikataa sanamu hii, ni vyema kwa Serikali kuchukua jukumu la kuitengeneza upya kwa gharama zake kwani gharama za mradi mpaka sasa ziligharimiwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Tanzania haitakuwa ya kwanza kuchukua hatua hiyo. Mnamo Januari 23, 2023, Rais Hakainde Hichilema wa Zambia alilazimika kuiondoa hadharani sanamu ya Rais wa kwanza wa taifa hilo, Keneth Kaunda, baada ya Wazambia wengi kulalamika kuwa sanamu hiyo haifanani na mwasisi huyo wa taifa hilo la kusini mwa Afrika. 

Je, Rais Samia Suluhu naye atafuata njia hiyo?

Kwa kumalizia, ni muhimu kukumbushana kwamba hadidu za rejea zilitaka mwonekano wa Mwalimu Nyerere katika sanamu hiyo uwe kama alivyokuwa kati ya miaka ya katikati ya 1960 na katikati ya 1980. Kwa mtazamo wangu, Mwalimu Nyerere hakuwahi kuwa na taswira hii iliyowekwa Adis Ababa katika kipindi chochote kile cha maisha yake. 

Pia, mtu anaweza kusema kwamba kama familia imeridhika, sisi tuhoji kama nani? Napenda ifahamike kuwa muonekano wa Mwalimu Nyerere siyo haki binafsi, au exclusive right, ya wanafamilia na ndiyo maana, kama taifa, tumeshiriki kwenye mchakato wa kuitengeneza. Kama raia wa nchi hii, tuna haki ya kuhoji.

Naomba tujibiwe maswali yetu ya msingi.

Robert Mwampembwa ni msanii, mwandishi na Mkurugenzi wa taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT). Kwa maoni, anapatikana kupitia ‎robert@ubunifu.co.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Naunga mkono hoja ya kufanyiwa kazi kwa Sheria ya Waanzilishi wa Taifa, au Honoring Founders Act, ya 2004, na kanuni zake za 2005, inaitaka Serikali kuunda chombo kinachoitwa Founders of the Nation Centre katika kifungu cha 4(1).

    Tukio kama hili ni mara ya pili limetokea kuna wakati kiongozi mkuu wa nchi alikabidhiwa kitu kisichofanana na Mwalimu ikidaiwa kuwa ni sanamu ya Mwalimu.

  2. MATAKWA YA WATANZANIA NI YA JUU ZAIDI KULIKO MATAKWA YA MADARAKA NYERERE AU FAMILIA:

    Sanamu inayodaiwa ni “mfanano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere” haifai na IBOMOLEWE mara moja na KUUNDWA UPYA. Ni kashfa kwa Watanzania na haistahili kubaki hivyo hivyo kama ilivyo katika eneo la Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU).

    Kasoro zinazoonekana wazi:-
    1. Uso wote Kwa ujumla (macho, pua midomo Kati ya mengine.
    2. Mwonekano (wajihi) hauakisi (depict) vitendo vya Mwalimu kwa umma wa Watanzania ama matukio ya kimataifa. Mfano wa wazi ni usimamaji wa Mwalimu wakati Wimbo wa Taifa unapoimbwa wakati wa sherehe za kitaifa au ziara za kimataifa. Kwa kipindi cha mwaka 1960 hadi 1980, sanamu hiyo walau ingeonyesha Mwalimu amesimama wima na mkono wake wa kushoto umeshika kifimbo chake cha mpingo chenye rangi nyeupe kwenye incha zake (both ends).
    3. Haijawahi kutokea katika utumishi wake wa umma, kitaifa au kimataifa Mwalimu akionekana hivyo, sio tu katika kipindi cha utawala wake wote bali hata wakati wa uhai wake wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *