“Unajua, sisi tuko vitani kimaisha,” anasema dereva mmoja wa daladala mwenye uzoefu mkubwa, akifafanua kwa kutaja changamoto nyingi zinazowakabili wafanyakazi wasio rasmi wa sekta ya usafirishaji Tanzania, ikiwemo kutokulipwa mishahara, saa nyingi za kazi, kutokulipwa kwa kuzidisha masaa yao ya kazi, huku wakiwa hawana ulinzi wowote wa kimaisha kama vile mafao ya uzeeni.
Hata hivyo, madereva wanaendelea kusonga mbele licha ya changamoto hizi: “Sisi sote ni watoto wa kimaskini. Tumejikwamua kwa nguvu zetu wenyewe.” Lakini nini kitatokea pale madereva hawa wakizeeka, wakiwa wameshachoshwa na kazi ngumu wanayoifanya? “Tutajikwamuaje?” Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa ushirika.
Anayeongea hapo juu ni mmoja kati ya viongozi watano wa Umoja wa Madereva na Makondakta Dar es Salaam—Msata (UMAMADARMS) niliowakuta wakiwa ofisini kwao kujadili historia ya kikundi chao hicho walichokiunda wenyewe kama ishara ya kutosubiri mtu aje awakomboe; ni “vita” walioamua kuipigana wenyewe, wanasema.
Manufaa yanayotokana na mapambano yanayoendeshwa na wanakikundi hawa ya kujikwamua kiuchumi yanatoa funzo muhimu kwa wavujajasho wengine, kwa watunga sera, na kwa yeyote yule mwingine anayetamani kuelewa namna watu wa hali ya chini wanavyoweza kutafuta “maisha mazuri.”
Kujikomboa kimaisha
UMAMADARMS ilianzishwa kwa njia isiyo rasmi mwaka 2003, ikiunganisha madareva na makondakta wanaofanya kazi kwenye njia ya Dar es Salaam mpaka mji wa Msata, mkoa wa Pwani, yenye umbali wa takriban kilomita 137.
Kama ilivyo kwa vikundi vingine vinavyofanana na UMAMADARMS, malengo ya awali ya kikundi hiki yalikuwa ni ya kawaida tu: kushughulikia mizozo inayotokea kazini na, kupitia michango ya wanachama, kusaidiana kwenye mahitaji yao ya kimsingi. Baadaye, hata hivyo, malengo haya ya kikundi yalipanuka.
UMAMADARMS ilisajiliwa rasmi mwaka 2011. Ingawaje imesajiliwa kama kama kikundi cha “kijamii” badala ya “ushirika,” kikundi hiki kimefanikiwa kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kiushirika, ikiwemo kuendesha biashara ya daladala, kununua ardhi na mengineyo inayosaidia kuboresha ustawi wa wanachama wake.
SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria
Baada ya jitihada kubwa za kuchangishana pesa, kikundi kilinunua gari lake la kwanza mwaka 2013. Kutoka hapo, kiliendelea kuhangaika kununua magari mengine mpaka kufikia magari matatu waliyonayo hivi sasa.
Ilipofika mwaka 2022, mapato ya chama yalikuwa Shilingi milioni 85.5. Leo hii biashara yao ya daladala huchangia zaidi ya asilimia 95 ya kiasi hicho, hali inayowafanya wanachama wake 53 kulazimika kulipia Shilingi 5,000 tu kama ada ya uanachama ya mwezi mmoja.
Ili kuwanufaisha wanachama wake, UMAMADARMS imeajiri watu sita miongoni mwa wanachama wake kama madereva na makondakta na inatoa malipo mazuri na maslahi bora zaidi kuliko ilivyo kawaida ya “matajiri” wengi, yaani wamiliki binafsi wa daladala.
Kwa mfano, wafanyakazi wote wa chama wana mikataba rasmi na mishahara ya Shilingi 200,000 kwa mwezi. Pia, wanachukua chochote kinachobaki baada ya kurudisha hesabu ya kila siku ya Shilingi 80,000 kwa chama. Hesabu hiyo ni ya chini kuliko ile ya Shilingi 100,000 na kuendelea ambayo matajiri wengi hudai tena bila ya kulipa mshahara wowote ule!
UMAMADARMS pia inaheshimu haki za msingi za wafanyakazi wake kama vile kuwapatia likizo zenye malipo, mapumziko yatokanayo na kuugua, kuwa na saa za kazi zinazoeleweka na zilizopangiliwa mapema.
“Chama kinasaidia sana,” anakiri mmoja wa madereva ambaye pia ni mwanachama wa UMAMADARMS. “Nilipata ajira. Nikikwama, kinasaidia kwa hali na mali. Chama kinatusaidia kiujumla. Kinabeba watu wengi sana.”
Pamoja na kuwaajiri watu, UMAMADARMS imelipia ada ili makondakta wake wote wapate mafunzo ya udereva kwenye vyuo vya VETA na madereva wote waende Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuongeza uzoefu. Baadhi yao wamenufaika kwa kupata kazi za udereva sehemu nyingine ambazo hulipa zaidi kuliko daladala, ingawa wanaendelea kuwa wanachama wa kikundi hicho.
SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni
Mpango mwingine wa kikundi unalenga kununua ardhi. Tayari chama kina shamba moja, na wanachama wanapanga kulima pamoja. Vilevile, kinanunua viwanja ili baadaye ivigawanye kwa wanachama wake wote. “[Ili] wajenge nyumba zao,” anasisitiza kiongozi mmoja. “Wasipange tena.”
Labda cha kushangaza zaidi, tangu mwaka 2015, UMAMADARMS imekuwa ikichangia kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili wanachama wake wote, wake zao na waume zao pamoja na watoto wao waweze kunufaika na bima ya afya. Kila mwezi, chama humlipia kila mwanachama wake Shilingi 20,000. Kwa mwaka 2022, jumla ya Shilingi 13.9 milioni ililipwa kwa NSSF.
UMAMADARMS pia inamchangia mwanachama wake akiwa na dharura, kwa mfano, msiba. Mwanachama mwenyewe akifariki, chama hakiitelekezi familia yake. Badala yake, kinaendelea kuchangia NSSF kwa ajili ya wategemezi wa marehemu na kusaidia watoto waende shule. Kwa sasa, kinasaidia familia tano kwa namna hii.
Yote haya yanaifanya UMAMADARMS kuwa “familia kubwa sana,” wanachama wake wanakiri, kikisaidia zaidi ya watu 400, wanachama wake pamoja na ndugu zao. Ni utashi huu wa wanachama wote wa kusaidiana kwa njia ya kujitegemea ambayo inaunga mkono ukuaji wa chama.
Tangu mwanzo, “tukaamua tujikomboe sisi wenyewe,” mmoja kati ya wanachama wakongwe wa chama hicho anasema. “Tunafanya sisi kama sisi kwa huruma zetu
,” mwanachama mwingine anaongeza. “Huruma hii hii [ndiyo] iliyotufanya tuwe hapa.”
Serikali ina jukumu gani?
Licha ya mafanikio haya, wanachama wa UMAMADARMS bado wanakabiliwa na vikwazo, mmoja mmoja na kama kikundi. Pia, wana malengo mengi ambayo hawajayatimiza bado. Kikundi kama hiki kinawezaje kupanuka zaidi?
Namna moja inayoweza kusaidia hilo kutokea ni kwa Serikali kuingilia kati na kuwaunga mkono, kitu ambacho wanachama wa kikundi hicho pia wanaafiki. “Sasa kwa huruma hii hii iliyotufanya tuwe hapa,” mmoja wa wanakikundi anasema, “Serikali itusaidie.”
SOMA ZAIDI: Sekta Isiyo Rasmi Yadaiwa Kutokuwa Rafiki Kwa Wanawake wa Kitanzania
Ushahidi kutoka nchi mbalimbali duniani unaonyesha kuwa uhusiano kati ya vyama huru vya kijamii au vya ushirika na dola ni uhusiano tata na siyo wa moja kwa moja. Hata hivyo, Serikali, ikiamua, inaweza kusaidia kuyabeba na kuyainua mashirika.
Yaani, inatakiwa kutengeneza mifumo ya kisheria, kitaasisi na kifedha inayoendana na mahitaji ya watu wa hali ya chini, wakiwemo wanaopambana katika maeneo ya mjini. Hata hivyo, historia ya Tanzania yenyewe inaonyesha kuwa wakati mwingine, juhudi za “uwezeshaji wa ushirika” zinaweza kugeuka kuwa njia ya kujipatia faida au kudhibiti.
Licha ya changamoto hizi, tukiangalia historia ya UMAMADARMS, tayari Serikali imeonyesha umuhimu wake, angalau katika hatua za awali, yaani chama kilisajaliwa kipindi kile Serikali ilipokuwa inahamasisha watu kuanzisha vyama. Serikali ikibaki na dhamira ile ile, inaweza kuleta mchango mkubwa kwenye ukuaji wa chama hicho.
Lakini tangu hatua hii ya kwanza, hata hivyo, msaada wa Serikali umebaki mdogo. Sasa hivi, viongozi wa UMAMADARMS wanadai kwamba ili wapate maendeleo, hatua zaidi kutoka kwa Serikali zinahitajika.
Mikopo isiyo na riba ndiyo kipaumbele kikuu. UMAMADARMS iliwahi kuchukua mkopo kwenye hizi benki za biashara. Mwaka 2022, kwa mfano, ilikamilisha urejeshaji wa mkopo kutoka Benki ya CRDB wenye thamani ya Shilingi milioni 37.7. Lakini viongozi wa kikundi wanasisitiza kwamba mkopo huo “umetuumiza.” Riba ilikuwa asilimia 24, na hivyo, “marejesho yalikuwa shida.”
Chama “kiliendelea kuwa hai” kutokana na “malengo” yake, lakini “vikundi vingi vinakufa kutokana na hali ya riba.” Vilevile, kuendelea kuwepo pia si sawa na mafanikio.
UMAMADARMS walipomaliza kulipa mkopo huo wa CRDB, gari waliyonunua kwa mkopo huo lilikuwa tayari “limeshachoka” na kuingia gharama nyingi. “Badala ya kupiga hatua, unabaki palepale, yaani, unawafanyia kazi wao [benki],” walieleza viongozi wa kikundi.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
Pamoja na masuala ya kifedha, viongozi wanatoa wito kwa Serikali kusaidia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanachama wao na raia kwa ujumla. UMAMADARMS inatamani kuwapa wanachama wake mikopo midogo midogo, lakini wanachama hao wanakosa ujuzi ambao ungewasaidia kuwekeza katika biashara zenye tija.
Sambamba na hilo, chama kingependa kujisajili kama SACCOS ili kujenga mifumo imara ya kukopeshana. Hata hivyo, viongozi wake wana wasiwasi kuhusu kanuni mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinazosimamia SACCOS ambazo wao wanadai ni “ngumu.” Kwa mfano, sasa SACCOS lazima zitumie mfumo wa uhasibu wa kielektroniki, ukiachilia mbali mahitaji mengine.
Masharti hayo labda zinaweza kumudu SACCOS za watumishi wa umma au wa makampuni binafsi, ambazo sasa ziko nyingi, hasa mijini. Lakini viongozi wa UMAMADARMS wanasisitiza, “Mfumo wa Serikali yetu ni mgumu kwa watu wa chini kama sisi.”
Kingine, wanachama wa UMAMADARMS, hata kama wameungana na watu wengi wanaohamia mjini, hawajasahau ndoto zao za kulima kwa pamoja, lakini viongozi wanaomba Serikali iwasaidie wakulima wadogo wadogo.
“Watalaamu washushwe ngazi ya kata” kiongozi mmoja anasisitiza. Kikundi kama chao kinahitaji msaada kidogo tu, anaongeza, ili baadaye kuwapa mfano mzuri vijana wengi zaidi ili na wao waende wakalime pia. Kimsingi, viongozi wanataka Serikali iwasikilize, itambue mchango wao, na isaidie kutimiza malengo yao.
“Serikali sijajua ni kwa namna gani sasa inashindwa kutembelea vile vikundi,” anasema kiongozi mmoja.“Kama tunaweza kuwa na mashamba, magari, tukalipia watu NSSF kwa nguvu zetu wenyewe, je, Serikali ikitutia nguvu kidogo tungefanya makubwa mangapi? Tungefanya makubwa mengi sana.”
Umuhimu wa mshikamano
Wakiwa wanasubiri msaada kutoka kwa Serikali, wavujajasho hawa wanatafuta njia mbadala za kujikwamua, ikiwemo kujenga umoja na mshikamano imara zaidi miongoni mwao. UMAMADARMS ni mfano mmoja tu, lakini hawako peke yao. Kuna vikundi vitano vya daladala kule stendi ya Mbezi.
SOMA ZAIDI: Bashiru Yuko Sahihi Kutaka Wakulima Waungane Dhidi Ya Wanaowadhulumu
Kwingineko jijini Dar es Salaam, vikundi kama UWAMAMAPO—wanaoendesha daladala kati ya Makumbusho na Posta—wanamiliki magari mawili kwa pamoja na wakatumia faida kununua viwanja na kuwagawia wanachama wao wote. Kikundi kingine kiko eneo la Tegeta chenye magari manane, na kimenunua viwanja vyake pia.
Wavujajasho wengi jijini Dar es Salaam – madereva na makondakta wa daladala, madereva wa bodaboda na bajaj, wamachinga, na wengineo – wamebuni mifumo ya kushirikiana kuweka akiba, kufanya biashara kwa pamoja, na kusaidiana kupata huduma za kijamii “kutoka chini.”
Vikundi hivi vinajenga umoja kwa ndani, lakini pia vinajenga mahusiano na vikundi vingine. Tena, UMAMADARMS ni mfano mzuri. Inashirikiana na vikundi vingine vya stendi ya Mbezi. Pia, viongozi wake wana mpango wa kusafiri kuvitembelea vikundi vingine huko Dar es Salaam na mikoa mingine ili kubadilishana na kujifunza kutokana na mafanikio yao.
Wakati huo huo, chama hicho tayari kimejiunga na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kilichozaliwa baada ya mgomo wa madereva wa mwaka 2015 na kinachoongozwa na madereva wenyewe.
Uhusiano kati ya UMAMADARMS na TADWU unaonyesha njia muhimu ya kusaidiana. Upande mmoja, TADWU husaidia uwakilishi na utetezi. Kwa mfano, kinafanya kazi kama daraja kati ya vikundi vidogo vya wavujajasho na maafisa muhimu wa Serikali.
Katika sekta ya usafirishaji binafsi ambayo imejaa mazingira ya unyonyaji, “Kazi ya TADWU ni kuhakikisha kuwa kila dereva anapata haki zake,” wanasema wanachama wa umoja huo.
Wakati huo huo, vyama kama UMAMADARMS ni nguzo za mapambano haya makubwa. TADWU “wanatutegemea sisi tuweze kuibeba kule juu,” wanasema viongozi wa chama hicho. Kupitia “maendeleo” ya kikundi na “huruma” yake ya kila siku, imeunganisha “familia” yake.
SOMA ZAIDI: Sakata la Uber, Bolt: Je, Ni Kweli Udhibiti Ni Hatari kwa Uchumi wa Soko Huria?
Familia hiyo hujiunga na “majirani,” yaani vikundi vidogo vingine, na vyote vinakutana ndani ya TADWU. Viongozi hao wanaendelea kusisitiza kwamba kutimiza malengo mengi zaidi kunawezakana, na kwa mtazamo wao, lazima yafikike.”UMAMADARMS inatamani ifanye vitu vyake kwa ukubwa kwa ajili ya kuwafurahisha wanachama wake, yaani tupate nguvu.”
Hivyo, swali muhimu linabaki: vikundi kama UMAMADARMS vinawezaje kuendelea kujenga umoja, kubaki vimeunganika vyenyewe wakati vikishirikiana na wengine? Vikundi hivi vinawezaje kupokea msaada kutoka nje utakaosaidia ukuaji wao bila kuhatarisha uhuru na uhai wao? Ni maswali tunayopaswa kutafakari kwa pamoja.
Michaela Collord ni Profesa Msaidizi katika Shule ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nottingham cha nchini Uingereza. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia Michaela.Collord@nottingham.ac.uk au kwenye mtandao wa X kama @MCollord.