Mwanza. Hali ya sintofahamu imeigubika Kambi ya Chinangali, mkoani Dodoma, ambako jumla ya vijana 268 wamekusanywa na Serikali kupitia Programu ya Kuwezesha Ushiriki wa Vijana Katika Kilimo Biashara (BBT- YIA) inayokusudiwa kuongeza ajira za vijana milioni tatu na kuongeza ukuaji wa kilimo nchini hadi kufikia asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.
Hali hiyo inatokana na dhana waliyonayo vijana hao kwamba Serikali imewatelekeza na kukiuka ahadi ilizotoa awali zilizowafanya vijana hao washawishike kujiunga na programu hiyo, huku lawama zaidi zikielekezwa kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anayeshutumiwa kuwatolea kauli nzito vijana hao pale wanapomueleza masaibu yao.
Juhudi za kupata majibu kutoka kwa Bashe hazikufanikiwa baada ya Mbunge huyo wa Nzega Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM) kutokujibu maswali tuliyomtumia kwenye nambari yake ya simu. The Chanzo ilitaka kufahamu ni juhudi gani Serikali inachukua kutatua kero hizo zilizoibuliwa na wanufaika takriban kumi wa programu hiyo tuliozungumza nao.
Wanufaika hao, ambao The Chanzo imeamua kuficha majina yao kulinda usalama wao, walieleza kusikitishwa kwao na kukiukwa huko kwa makubaliano yao na Serikali, hali wanayodai imewafanya waishi kwa “tabu na mateso” kambini hapo, huku hatma yao na ile ya familia zao walizoziacha nyumbani zikiwa katika mashaka makubwa.
“Kiukweli hakuna kinachoendelea hapa [kambini] ndugu yangu,” mmoja wa wanufaika wa mradi huo alimwamba mwandishi wa habari hii. “Tumerundikwa hapa, na Serikali haitaki kusikia chochote kutoka kwetu. Tunatishiwa kwamba tunaweza kufukuzwa muda wowote na wakaletwa vijana wa JKT na sisi hatuna mchango wowote kwa [chama tawala] CCM. Hiyo siyo sawa kabisa.”
“Bashe amekuwa akifika hapa na kutoa kauli zisizostahili kabisa,” alidokeza mnufaika mwingine wa programu hiyo. “Wewe fikiria, mtu anawaambia [vijana hapa kuwa] wazazi wenu hao masikini mbona hawakuwaandalia mazingira mazuri? Bashe anafikia hatua ya kusema kwamba sisi tumeokotwa mtaani, kweli jamani?” Bashe hakupatikana kujibu shutuma hizi.
Madai ya kutelekezwa
Madai haya ya vijana kutelekezwa na kulazimishwa kuishi kwa mateso yalishawahi kuibuliwa mwezi Januari mwaka huu na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee, ambaye, akiandika kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, alihoji masuala kadhaa kuhusiana na programu hiyo, hususan kutokuwepo kwa ulinganifu kati ya kile Serikali iliahidi na kile kinachofanyika kambini huko.
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
“Mwaka jana [2023] wakati wa Bunge la Bajeti, tuliambiwa Wizara [ya Kilimo] imepanga kufikia 2025 kuwa na ekari 2,500,000 kwa ajili ya kuwapatia vijana na wanawake,” aliandika Mdee kwenye moja ya maandiko yake. “Leo 2024, ekari 600 kuzisafisha, kupima, kusawazisha mashamba pamoja na kuweka miundombinu ya umwagiliaji tumeshindwa. Tukiri tulikurupuka ili tujisahihishe.”
Mdee hakuwa tayari kufanya mahojiano na The Chanzo kuhusiana na sakata hili, akisema hawezi kufanya hivyo kwa sasa kwani ana mgonjwa hospitalini anayemuuguza. Ukosoaji mkali wa Mdee dhidi ya programu hiyo ulimuibua Asia Msuya, kijana aliyejitambulisha kama mnufaika mwa programu hiyo, aliyekanusha madai ya Mdee kwamba vijana hao wanapitia hali ngumu ya kimaisha.
Kwenye video iliyochapishwa kwenye mtandao wa X hapo Februari 1, 2024, na ambayo kwa sasa haionekani kwa kila mtu, Msuya aliyaita madai yaliyoibuliwa na Mdee “uzushi,” akisema kwamba yeye kama mnufaika wa mradi huo yuko tayari kukabiliana na changamoto zozote kwenye mchakato wa kufanikisha programu hiyo.
Msuya, hata hivyo, amekuwa sura muhimu kwenye kampeni zinazoendeshwa na Serikali kuhusiana na programu hiyo, akionekana kwenye mabango ya Serikali akimsifu Rais Samia Suluhu Hassan “kwa kuhamasisha vijana na wanawake kushiriki katika kilimo kwani kilimo ni biashara.”
Ukiukwaji wa ahadi
Lakini vijana waliopo Kambi ya Chinangali wameiambia The Chanzo kwamba hali kambini hapo haipo kama vile wengi wanavyofikiri, wakilalamikia hatua ya Serikali kwenda kinyume na makubaliona mengi ya awali ambayo yaliwashawishi vijana kushiriki kwenye programu hiyo.
Kwa mfano, vijana hawa wanadai kwamba Serikali iliwaahidi kuwagawia ekari tano kwa kila mmoja pamoja na kuanzisha miundombinu ya umwagiliaji. Badala yake, vijana wote 268 wanalazimika kulima shamba la ushirika linalokadiriwa kuwa na ekari zisizozidi 200, The Chanzo imeelezwa.
“Wewe fikiria, hakuna mtu aliyepewa shamba hapa, halafu waziri anajinadi kuwa watu wamepewa mashamba,” alisema kijana mmoja. “Tunalazimishwa kulima alizeti kwenye shamba la pamoja na hapo hatujui kitakachopatikana kitakuwa kiasi gani. Hatukuja hapa kulima alizeti, tulikubaliana kuwa Chinangali kutakuwa na kilimo cha mboga mboga.”
SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Waziri Bashe Juu ya Mradi wa ‘Ujenzi wa Kesho Njema’
Taarifa hii kutoka kwa mnufaika wa progrmu hii, hata hivyo, inakinzana na ile ya Serikali ya Januari 22, 2024, iliyohusu hatua ya waziri anayehusika na masuala ya vijana, Joyce Ndalichako, kukabidhi mashamba na zana za kilimo kwa vijana 268 wa programu hiyo, akiitaja programu hiyo kama “kati ya miradi ya kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita.”
“Hakuna chochote ambacho Serikali imetimiza,” kilisema chanzo chetu kingine cha habari. “Watu wanalazimika kwenda kulima vibarua kwa wakazi wa maeneo jirani na wengine tunalazimika kuchimba mitaro ili tupate hela ya kujikimu. Mimi mwenyewe hapa nimetoka kupalilia karanga za mtu muda si mrefu. [Hii] ni aibu kwa Wizara [ya Kilimo].”
Wanufaika pia wamelalamikia vigezo na masharti ya umiliki wa ardhi na uendelezaji ambavyo wameviita kama vya “kinyonyaji” na ambavyo vinaenda kinyume na misimamo na ahadi za awali za Serikali.
Umiliki wa mashamba
Kwenye barua yake ya Januari 22, 2024, ya kukabidhi mashamba kwa wanufaika hao, ambayo The Chanzo imefanikiwa kuona nakala yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, anaambatanisha masharti ya kuendeleza shamba ambayo kila mnufaika anapaswa kuyatekeleza.
Moja kati ya masharti hayo ni sharti kwamba mazao yatakayozalishwa yatauzwa kwa mnunuzi atakayekubalika kwa mujibu wa taratibu za Chama cha Ushirika wa Vijana BBT, sharti ambalo vijana wanasema liliwashangaza kwani halikuwepo kwenye makubaliano ya awali.
Masharti hayo yanasema pia mnufaika atamiliki shamba hilo kwa miaka 33 tu ambapo baada ya kipindi hicho masharti ya umiliki au upangishaji yatabadilika. Miaka hii ni pungufu mara mbili ukilinganisha na miaka 66 inayotajwa kwenye mwongozo wa utekelezaji wa programu, pamoja na ahadi ya Rais Samia mwenyewe.
SOMA ZAIDI: Bajeti Wizara ya Kilimo Inaakisi Umuhimu wa Kilimo Tanzania?
Ingawaje barua hiyo inadai kuwapa wanufaika ekari tano za ardhi, wanufaika hao wameiambia The Chanzo kwamba kilichofanyika kimsingi ni vijana hao “kubananishwa” wote kwa pamoja kwenye shamba la ekari 200 wanalolazimika kulilima bila kuwa na miundombinu yeyote.
Malalamiko haya, pamoja na kushindwa kwa Serikali kuyapatia ufumbuzi kwa wakati, yameharibu uhusiano uliopo kati ya uongozi wa wanufaika na Serikali, hali iliyoilazimu Serikali kuingilia kati na kuvunja uongozi uliokuwepo na kuunda uongozi mwingine.
Machi 1, 2024, Vumilia Zinkankuba, ambaye ni Mratibu wa programu hiyo, alifika katika Kambi ya Chinangali na kumuamrisha Mwenyekiti wa Vijana wa BBT Chinangali, Hans Mlelwa, aachie nafasi ya uongozi, akimshutumu kutoa taarifa za programu nje ya kambi. Juhudi za kumpata Zinkankuba kuelezea sakata hili hazikufanikiwa.
“Tulishtukia tu kwamba mwenyekiti na wasaidizi siyo viongozi tena na [Zinkankuba] akadai kuwa hayo ni maelezo kutoka kwa Bashe,” alisema mnufaika mmoja. “Haiwezekani kabisa, mwenyekiti ndiye mtu pekee aliyekuwa akitutetea na kutupambania. Tushajua njama zao ni kutaka tuendelee kusota hapa.”
Uamuzi wa kuvunjwa kwa uongozi huo ulikuja siku chache baada ya uongozi huo kumuandikia Bashe ukimuomba kukutana na yeye kujadiliana naye masuala ya msingi yanayotokea kambini hapo bila mafanikio yoyote.
Inaumiza
“Inaumiza pale Serikali inaposema sisi tunaishi maisha mazuri [huku kambini],” alisikitika mmoja wa wanufaika wa programu hiyo. “Wake zetu wamekimbia hawataki kuamini tunachowaambia kwamba tunapitia wakati mgumu. Wao [wake zetu] wakiona picha za Bashe wanajua tumetoboa tayari. Mimi mke wangu kakimbia familia anadai nimefika huku nimetelekeza familia.”
Gibson Mulokozi, mshauri mwelekezi huru wa kilimo-biashara, aliiambia The Chanzo kwamba namna pekee Serikali inaweza kuboresha mahusiano yake na wanufaika wa programu hiyo, na hivyo kuhakikisha kufanikiwa kwake, ni kuhakikisha kuna uwekezaji na uwazi wa kutosha kwenye utekelezaji wake.
SOMA ZAIDI: Simulizi ya Kijana wa Mjini Aliyetaka Kupata Utajiri wa Haraka Kupitia Kilimo
“Hakuna kitu kingine cha ziada,” Mulokozi, ambaye huandikia chapisho hili mara kwa mara, alisema kwenye mahojiano maalumu. “Pesa ya kutosha inahitajika kwenye mradi kama ule, na utekelezaji uwe wa wazi. Tofauti na hapo, kile kilichotarajiwa hakitaonekana.”
Mdude Nyagali, mwanaharakati ambaye amekuwa akiikosoa programu hiyo ya BBT kwa muda sasa, hususan kwa kile anachodai ni kutokuwepo kwa uwazi na uwajibikaji unaoridhisha, aliiambia The Chanzo kwamba namna pekee ya kutatua malalamiko haya ya wanufaika ni kwa mradi kusitishwa kwa muda na kupisha tathmini mpya kufanyika.
“Serikali isiposhtuka mapema, pesa zote zitapigwa,” alionya Nyagali. “Kwa upande wangu, [Serikali] wasimamishe mradi [halafu] usimamiwe upya. Mradi hauna uhalisia.”
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.
6 responses
Serikali iache ubabaishaji yani sipendi hiyo njia wanayotumia kuwalaghai na kuwadanganya yani kama inatafuta vibarua wa kuwatumikisha vile kama wameshindwa waache vijana wakapambane sio kuleta habari tofauti na inavyotakiwa
Ni utapeli tupu wa ccm. Wanavizia kura Kwa kutumia kisingizio Cha kuinua vijana,ukweli wanapiga! Ni no kosa kuwaamini ccm!
CCM OYEEEEEEE! Mitano tena
Wajinga wakubwa, mmeshindwa kujisaidia hadi mkasaidiwe na serikali? Bila Shaka ninyi ni Green Guard, sasa mnataka mtelezo. Mtasubiri sana. Rudini nyumbani mkalime na familia
Selikali hii ya ovyo sana
Dah ni hatari
Wawe wavumilivu serikali yetu sikivu itawasikiliza kile wanachodai na mambo yataenda Sawa Tu,uzuri wanakula haijawahi wakalala njaa,familia zao nazo zijitume Tu Kwa kadri wawezavyo ,mvua zinanyesha kila mahali watu walime watapata mazao