Kifo huibua hata yale yaliyofichikana katika maisha ya mtu. Wasiomjua wakamjua, wasiyofahamu matendo na mchango wake chanya au hasi kwa jamii, wakaanza kufahamu.
Mtu huyo ataelezewa kwa ubaya hata asiyoutenda, maana hayupo akajitetea; atasifiwa kwa mazuri hata akthari ya alivyotenda, maana hayupo akathibitisha au pengine akajifakhiri.
Hata hivyo, mara nyingi aliyekufa husifiwa kwa mazuri. Yale mabaya na aibu husitiriwa, maana si vyema kumkashifu marehemu, wakati mwenye kukashifu bado yu hai; haijui hatima yake.
Mtu husifiwa kwa mazuri kwani ndiyo maelekezo ya dini; au kwa wingi wa mema aliyotenda na mawanda yake kiwakati, kimahali na watendewa, hadi kufunika ubaya wake; au pengine kwa sababu mara nyingi husifiwa na watu wa karibu – familia, wapenzi, taasisi au mfumo aliyoutumikia.
Haya yanasadifu kwa Hayati Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa rais wa awamu ya tatu wa Zanzibar na awamu ya pili kwa Tanzania. Kifo chake cha Februari 29, 2024, kimemgusa kila aliyemfahamu wakati wa utumishi wake, na hata waliyomshuhudia uzeeni mwake.
Nyoyo za wakubwa kwa wadogo; waume kwa wake; watawala kwa watawaliwa; familia na watu baidi; mashuhuri na wasiyojulikana, zilitikiswa kwa simanzi la ajabu. Akili zikapigwa na butwaa, vichwa kusikitika huku vikiinama kuruhusu machozi ya huzuni na majonzi yatiriirike, yasidhuru.
Kauli yake ya hekima – Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni. Basi ewe ndugu yangu, kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa– ikaanza kutafsirika kivitendo. Vinywa vya mashekhe na maimamu vikimiminika kauli njema na dua za kheri ya anakokwenda.
SOMA ZAIDI: China Ilikuwa na Deng, Tanzania Ikapata Mwinyi
Mikono ya maamuma ikiwa juu kuomba kabuli ya muombwaji. Sauti za waliomfahamu vyema zikinguruma katika vyombo mbalimbali vya habari. Zikisimulia ushujaa, ujasiri, uadilifu, hekima, busara na utu wake.
Zikithibitisha wema wa moyo wake mkunjufu. Historia za makuzi, malezi, elimu na utumishi wake zikiangaziwa katika mwelekeo chanya uliyozaa tija kwa jamii na taifa.
Mwinyi na Kiswahili
Waliyo wengi walidhukuru juu ya uwezo wa Mwinyi wa kimaamuzi na kimageuzi, hususan kisiasa na kiuchumi. Mwanademokrasia, mwanamageuzi na Mzee Rukhsa, zikawa lakabu zilizomganda katika uhai wake; na kubaki vinywani mwa waliomfafanua nyuma yake.
Hata hivyo, Mwinyi anatajwa pia kama nguli wa Kiswahili na utamaduni wake. Bila ya shaka tulistafidi ulimi wake fasaha, tulistaladhi lafudhi adhimu na kuburudika na uteuzi wake bora wa msamiati.
Kwa kawaida, watu wengi wasiyo na asili ya pwani huathiriwa na lugha za kikabila katika utamkaji na ufasaha wa Kiswahili. Kwa Mwinyi, hali haikuwa hivyo. Kama ilivyoelezwa na wengi kuwa baba yake alimhamishia Zanzibar ili kuroanisha ulimi wake na kuwa mwanazuoni mkubwa Afrika Mashariki.
Hivyo, ulimi wake ulilainishwa kwa misingi ya lugha ya Kiarabu, iliyochavuliwa na mafunzo ya Qur-an tukufu na masomo mengine ya dini ya Kiislamu. Lugha ya Kiarabu ilichavua ufasaha wake wa Kiswahili na ubora wa lafudhi yake.
Hii ni kwa sababu lugha ya Kiswahili imeathiriwa mno na Kiarabu katika nyanja nyingi, zikiwemo za kimsamiati, fonimu na hata baadhi ya misemo, nahau na tamathali zake.
Wasomi wengi, hasa wenye umahiri wa lugha zaidi ya moja, hujikuta wakichomeka misamiati ya lugha nyingine katika uzungumzaji wa lugha moja. Kwa mfano, wengi huingiza maneno ya Kiingereza wanapotumia Kiswahili.
SOMA ZAIDI: Rais Mwinyi, Aliyefariki Feb. 29, Hakuwahi Kujutia Uamuzi wa Kujiuzulu Uwaziri
Pamoja na kuwa Mwinyi alikuwa mmahiri wa lugha za Kiarabu, Kiingereza na Kiswahili, alibaki katika ufasaha wa lugha anayoitumia kwa wakati husika pasi na kuchanganya na lugha nyengine. Na kwa namna hiyo alikuwa mwenezi mzuri wa Kiswahili fasaha ndani na nje ya Afrika.
Mpangilio wa maneno
Pamoja na ufasaha wa lugha na lafudhi nzuri, Hayati Mwinyi anatajwa kuwa mwandishi mzuri anayejua kuzingatia taratibu za uandishi, mantiki ya tungo, mpangilio wa maneno, sentesi na vifungu vya habari.
Binafsi yake, ameandika kitabu kikubwa cha zaidi ya kurasa 400 kinachozungumzia maisha yake, kwa lugha ya Kiswahili. Angeliweza kukiandika kwa Kiingereza na kupata soko kubwa huko ughaibuni. Hili linaonesha mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili na umahiri wa uandishi wa lugha hiyo.
Mwinyi hakupenda uandishi tu, bali aliwapenda waandishi pia. Pamoja na kuwa mfasaha wa lugha, mwandishi mzuri na mwalimu wa Kiswahili, alitoa mchango mkubwa kwa waandishi wengine wa lugha na fasihi.
Kwa mfano, diwani nyingi za marehemu Muhammed Seif Khatib ziliandikiwa dibaji na Hayati Ali Hassan Mwinyi. Mfano wa dibaji bora kati ya hizo ni ile ya diwani ya Wasakatonge.
Kuandika dibaji ya vitabu vya fasihi hakuthibitishi mchango wake katika uandishi pekee, bali pia kunaashiria umilisi wake wa lugha ya Kiswahili na fasihi yake. Si rahisi kwa mtu asiye mmilisi wa lugha na fasihi kukiandikia dibaji kitabu kizima, hasa kile cha fasihi.
Weledi wa mpangilio mzuri wa maneno na ustadi wa uteuzi wa msamiati kulingana na mada, mahali na mhusika anayezungumza naye, ulimsaidia kuimarisha matumizi bora ya lugha. Hapa nitanukuu baadhi ya maneno yake katika hotuba aliyoitoa mbele ya Rais Msataafu, Hayati John Magufuli katika hafla maalumu ya SCOUT.
SOMA ZAIDI: Nitakavyomkumbuka Mwinyi, Mzee Rukhsa Asiyekuwa na Tamaa ya Madaraka
“Nataka usadiki, kwamba mambo unayoyafanyia nchi hii, yananigusa moyo wangu sana. Hiki ndicho kiigizo. Ndiyo igizo la urais. Rais afanye hivyo unavyofanya wewe. Wewe unamudu kufanya, wengine wanatamani kufanya; na kutamani na kumudu ni vitu viwili mbalimbali.”
Katika nukuu hii, maneno kama usadiki; unamudu; kutamani; na mbalimbali, akimaanisha tafauti, yameteuliwa kutoka bahari pana ya Kiswahili fasaha. Utakubaliana nami kuwa maneno hayo ndiyo yanayoipamba zaidi nukuu hii.
Upangiliaji rudufu wa tungo kuanzia “Rais afanye hivyo unavyofanya wewe….” hadi mwisho wa nukuu hii, umeifanya nukuu hiyo kutoa ujumbe mzito kwa msikilizaji, licha ya kuwa pambo lisilo shaka.
Kila msemaji hutoa ujumbe. Lakini ili ujumbe upokewe kwa uzito zaidi, hutegemea sana uteuzi wa maneno na mpangilio wa tungo, licha ya hali ya msemaji na usemaji. Haya yote yalikusanyika kwa pamoja kwa Ali Hasasan Mwinyi wakati wa kutamka maneno hayo.
Kukiinua Kiswahili
Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya taifa mara baada ya uhuru, mwaka 1961, huku kikiteuliwa kuwa lugha ya kufundishia elimu ya msingi na kama somo la lazima katika elimu ya msingi na sekondari.
Kadhalika, kufundishwa katika vyuo mbalimbali. Haya yote yaliimarishwa na kuendelezwa katika asri ya utawala wa Rais Mwinyi. Aidha, matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha katika hotuba zake na kubaki katika utamaduni wa ‘Mswahili’ hata alipofanya kazi nje ya nchi, ni ishara ya kukithamini, kukikuza na kukieneza Kiswahili duniani.
Mnamo mwaka 1968, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lilianzishwa. Mwinyi, licha ya kushiriki kikamilifu katika uandaaji wa misingi bora ya uanzishwaji na uendeshwaji wa baraza hilo, akateuliwa kuwa mwenyekiti wake wa kwanza.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunahitaji Kusoma Vitabu Vingi Zaidi vya Kiswahili?
Kama tujuavyo, kiongozi wa kwanza wa taasisi ana jukumu zito la kuisimamisha taasisi hiyo na kuiweka katika barabara iliyonyooka.
Kwa takriban mika kumi, Hayati Mwinyi alifanikiwa kuliongoza baraza hilo na kulisimamisha imara. Maendeleo ya BAKITA yanayoshuhudiwa leo ni matokeo ya misingi imara iliyojengwa chini ya usimamizi, uangalizi, busara, hekima na uongozi wa hayati Mwinyi.
Februari 2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Kiswahili, kilimuomba Mwinyi kushiriki kuanzisha Taasisi ya Kiafrika ya Mifumo ya Maarifa Asilia, au African Institute of Indigenous Knowledge System (AIIKS), huko Afrika Kusini katika Chuo Kikuu cha Kwazulu Natal mjini Durban.
Katika taasisi hii lugha za kiafrika zilitumiwa kama moja ya maarifa asilia. Kiswahili nacho, kama lugha ya Kiafrika, kikapenya. Wajumbe wa mkutano huo walimuomba Hayati Ali Hassan Mwinyi kuwa mlezi wa kwanza wa taasisi hiyo, naye akakubali.
Akiwa mgeni rasmi, akatoa hotuba iliyosisitiza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili Afrika kwa kutumia lugha za kiafrika. Kwa mfano, tunapofundisha Kiswahili Nigeria tusitumie Kingereza. Badala yake, tutumie Kihausa, Kiurba, nakadhalika. Badala ya kutumia Kifaransa kufundishia Kiswahili Congo, tutumie Kilingala, Chiluba, Kikongo.
Kwa kufanya hivyo kutawezesha kufufua na kuendeleza lugha za asili na wakati huohuo kukiendeleza na kukijenga Kiswahili. Lugha za kiafrika zinapotumika kufundishia Kiswahili ni rahisi Waafrika kujiona katika lugha hii adhimu.
Kadhalika, Kiswahili kitabeba msamiati mwingi kutoka katika lugha nyingi za Kiafrika. Hivyo, itakuwa rahisi kukikuza Kiswahili na kuifanya kuwa lugha ya Afrika.
Tunazienzi vipi juhudi hizi?
Mara nyingi anapoondoka mtu mwenye hadhi kubwa katika jamii kwa kufariki au kustaafu nafasi yake, kauli ya kuyaenzi aliyoyafanya hutamalaki. Tafsiri ya kauli hii hubaki kwenye kuyaheshimu, kuyasifia na kuyapa hadhi mema aliyoyatenda.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?
Busara zangu zinaniamuru kusisitiza kuwa njia kuu ya kuenzi juhudi na mema ya aliyetangulia, ni kuvuka hatua alizozifikia au kukamilisha malengo aliyoyakusudia.
Kama kweli tunakusudia kuitunza, kuikuza, kuiinua na kuihifadhi lugha hii, kama ishara ya kuenzi jitihada za walioifikisha ilipo leo, akiwemo Hayati Ali Hassan Mwinyi, basi ni kufanya maamuzi ya kuipa nafasi ya kudhibiti na kuendesha mfumo mzima wa elimu yetu.
Kuanzia uandaaji wa vyanzo vya marifa kama vile mitaala, mihutasari, miongozo, vitabu nakadhalika; mafunzo ya ualimu; ufundishaji; upimaji na mchakato wa tathmini.
Tunashuhudia Kiswahili kinavyopasua anga za kimaeneo, kimatumizi na idadi ya watumiaji. Kiswahili ni lugha rasmi katika mataifa mengi ya Afrika. Ni lugha inayofundishwa duniani kote. Ni lugha ya uandishi na utangazaji katika vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Afrika.
Kiswahili ni lugha rasmi ya jumuia za kimataifa za Kiafrika, zikiwemo Umoja wa Afrika (AU) na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Mwaka 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO liliipitisha rasmi Julai 7 ya kila mwaka kama siku maalumu ya Kiswahili duniani.
Ukizingatia hadhi hii ya Kiswahili na kwamba ndiyo lugha ya taifa la Tanzania, unaweza kujiuliza ni kipi hasa kinachozuia lugha hii kupewa hadhi yake katika taifa la Tanzania, hususan katika mifumo ya utoaji maarifa? Huku hoja zote za kuikinza lugha hii kuendesha mfumo wa elimu yetu zimeshindwa kusimama na kujitetea kila zinapotolewa.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili
Vipi tunaweza kuitakidi kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa huku ikifunikwa na lugha ya Kiingereza katika uendeshaji wa shughuli muhimu na rasmi za kitaifa, kama mfumo wa elimu na uandaaji wa baadhi ya nyaraka za Serikali na taasisi nyingine?
Ni jambo lisilokubalika katika milango ya akili na utambuzi. Ni wakati wa kutanabahi sasa kabla jua halijachwa, na haliko mbali kuchwa.
Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.