The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ujenzi wa Barabara kwa Hisani ya Watu wa Goba Wazua Gumzo Dar

Pengine kuna umuhimu wa kuweka mabango kwenye kila eneo ambalo wananchi wanajitoa ili taarifa hizo zikae kwa uwazi, na kuchochea uwajibikaji.

subscribe to our newsletter!

Picha ya bango la mradi wa ukarabati wa barabara ya Goba kwa Awadhi imesambaa kwa kasi sana kwenye mitandao ya kijamii, hasa makundi sogozi ya WhatsApp. Picha hii inaonesha bango mithili ya mabango ambayo huwekwa mwenye miradi ya ujenzi ikonesha taarifa za mradi. 

Bango hili linaonesha jina la mradi ambao ni Barabara ya Awadhi hadi Kanisa la KKKT yenye urefu kilometa mbili. Aina ya mradi ikiwa ni ukarabati na ujenzi wa mitaro na kuwa mfadhili wa mradi huo ni nguvu za wananchi wakazi wa eneo hilo. Pia, bango linaonesha muda wa mradi ambao ni mwezi Machi 2024 hadi Mei 2024. 

Tofauti na mabango mengine ambayo mara nyingi yamekuwa na ujumbe uliozoeleka kwamba UKIMWI unaua, bango hili limehitimishwa na ujumbe wa kibunifu wa Tuchange wote kujenga barabara yetu.

Kupitia ukarabati huu, wakazi wameazimia kujenga mitaro kwa kutumia zege, pamoja na kushindilia vifusi. Makadirio ya bajeti ni takribani Shilingi milioni 40 kutoka kwa wakazi 95 walioahidi. Tayari zaidi ya Shilingi milioni 16 zimeshakusanywa, na ujenzi umeshaanza. 

Hii siyo mara ya kwanza kwa jitihada za wananchi hawa kukarabati barabara hii ambayo ipo chini ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Awamu hii imekuwa ya kipekee kutokana na bango linaloendelea kuzua mjadala mkubwa. 

Barabara ya Anzuruni Goba kabla na baada ujenzi mwaka huu 2024

SOMA ZAIDI: Maendeleo Kutokea Chini? Hii ni Hadithi ya Ushirika wa Daladala Dar es Salaam

Mjadala huo umewaibua viongozi wa mtaa ambao waliwashawishi wananchi kuliondoa bango hili bila mafaniko. Msimamo wa wananchi ni kuwa endapo watalitoa, basi waitishe mkutano kuelezea barabara hiyo itatengenezwa lini. 

Utaratibu wa muda mrefu

Kwa maeneo ya Goba, suala la wananchi kuchangia ujenzi na ukarabati wa barabara zao siyo geni. Barabara nyingine za Goba ambazo nafahamu zimekuwa zikikarabatiwa kwa nguvu za wananchi ni pamoja na barabara ya Goba Hills yanye urefu wa kama kilometa moja na nusu. 

Barabara hii ambayo imekuwa ikikarabatiwa na wananchi, mwaka jana, 2023, wananchi hao walichanga zaidi ya Shilingi milioni 16, ambazo zilitumika katika kuweka vifusi na kujenga mitaro katika baadhi ya maeneo. 

Barabara nyingine ni ile ya Anzuruni inayopita kanisa la KKKT Goba kuelekea Shule ya Theresia ambapo wananchi walikarabati barabara yao kwa takribani Shilingi milioni 13. Bango na mjadala, vimewaibua pia TARURA ambapo wametembelea mtaa huo na kufanya mazungumzo na wananchi hao. 

Pengine kuna umuhimu wa kuweka mabango kwenye kila eneo ambalo wananchi wanajitoa ili taarifa hizo zikae kwa uwazi, na kuchochea uwajibikaji. 

SOMA ZAIDI: Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?

Ili kujiletea maendeleo, kuna umuhimu mkubwa sana wa jamii kukaa pamoja, kuchambua masuala yao  na hatimaye kushirikiana katika kutekeleza vipaumbele vyao. Ushiriki wa wananchi umeleta mafanikio makubwa sana kwenye maeneo mengi, na hii mifano ya Goba ni kwa uchache tu. 

Aidha, pamoja na matokeo mazuri ya ushiriki wa wananchi, bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi hao katika kufikia maendeleo endelevu. Moja ya changamoto ni kuwa siyo wananchi wote wapo tayari kujitolea, na hakuna namna ya kuwashurutisha.

Pili, ni juhudi hizi kufanywa na wananchi wasiyo na mamlaka wala dola husababisha mikwamo ya hapa na pale. Mfano, wakazi wengine wamekuwa wanaziba makusudi na waziwazi mitaro inayochepusha maji barabarani, na wengine kuzuia barabara zisipanuliwe kwa kiwango husika. 

Tatu, ni kukosekana na usimamizi na utaalamu madhubuti. Nne, ni kukosekana kwa taarifa za mipango ya Serikali kuhusu maeneo husika ili kuweze kuwa na mashirikiano na kufanya jambo zuri zaidi. Na tano ni kukosekana kwa ushirikiano wa viongozi wa Serikali wa maeneo husika katika kuisimamia na kuipa uhalali miradi hii ya kujitolea. 

Sera zihusike

Je, ni kwa namna gani sera zetu, mfano sera ya ugatuzi wa madaraka, zinaweza kuwasaidia wananchi kukabiliana na changamoto hizi ili kuwaongezea wananchi ari na kujiamini?

SOMA ZAIDI: Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti

Ili kuongeza ari ya wananchi kushirikiana katika kujiletea maendeleo, kuna umuhimu wa Serikali kutambua na kuunga mkono jitihada zao. Pale wananchi wanapoanzisha jitihada za kujiletea maendeleo, basi Serikali, kupitia ngazi za mitaa na kata, wawe wepesi kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha jitihada zao zinaleta tija. 

Je, haiwezekani wahandisi walioajiriwa na Serikali na kulipwa na kodi za wananchi, kusaidia katika kushauri na kusimamia juhudi za wananchi? 

Kwa kuwa changamoto za barabara hutokea mara kwa mara, hasa wakati wa misimu ya mvua, je, halmashauri haiwezi kuwa na greda, kisha wananchi wachangie gharama za vifusi na mafuta? 

Lakini pia, mikutano ya wakazi wa mitaa wameonekana kutokuwa na uwezo wa kutatua kero za maeneo mbalimbali ya mitaa. Kwanza, mahudhurio ya wananchi huwa ni hafifu sana na ajenda mara nyingi hazigusi mahitaji halisi ya kila mwananchi. 

Hivyo, Serikali ihakikishe viongozi, kama wajumbe, wanaitisha mikutano ya maeneo yao ili wananchi waweze kuibua na kuchambua kero zao mahususi, na kupanga namna ya kuzitekeleza. 

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu

Kata, au mtaa, ni eneo kubwa sana, na kwenye kila eneo kuna vipaumbele na mahitaji yake tofauti, hivyo ni muhimu kila eneo lichukuliwe kwa utofauti wake. 

Na muhimu zaidi ni kuhakikisha taarifa mbalimbali, hasa za mipango na bajeti, zinawafikia wananchi kwa uwazi. Tunapaswa kufahamu barabara zote ambazo zipo chini ya TARURA na ambazo hazipo. Aidha, ni mchakato gani unatumika ili barabara iwe chini ya TARURA. 

Pale ambapo barabara zipo chini ya TARURA, wananchi wafahamu bajeti na mipango ya kila mwaka ya barabara hizo, ili kama bajeti haitoshi, au mwaka huo haipo, waweze kujipanga kuongeza nguvu ili barabara ziwe kwenye hali nzuri wakati wote. 

Upatikanaji wa taarifa utaongeza kuaminiana kati ya wananchi na viongozi wao na kuboresha mashirikiano katika kutatua kero za wananchi na kuleta maendeleo. 

Richard Temu ni Afisa Mwandamizi wa Programu ya Ushiriki wa Wananchi kutoka Twaweza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia rtemu@twaweza.org na 0719275323. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

8 Responses

  1. Hao watu wamejitambua
    Sasa Serikali ikienda hapo kazi yao ni moja tu KUBORESHA KIWANGO CHA HIYO BARABARA INAYOTENGENEZWA sio kuingilia mchakato mzima,
    Kuna mambo mengi wananchi wakipewa support wanaweza kuleta mapinduzi chanya kulika kufuata urasimu na taratibu nyingiiii ambazo zingine zinachelewesha maendeleo na zingine ni mianya tu ya kuwaibia wananchi

    1. Kwanza niwapongeze wananchi wa Goba kwa wazo na kitendo walichokifanya.Kikubwa wananchi hawa wapatiwe wataalam wa kuwaongoza vizuri namna bora ya ujenzi wa Barabara.
      Sioni tatizo katika swala la wananchi kujitolea ujenzi wa Barabara maana barabara hizo ni zao ndio maana zipo chini ya Mamlaka ya serikali za mitaa.

  2. Hii inaonesha kwa kiasi gani Tarura wanahitaji kujitathmini kama serikali imeqeza ouchangia zaidi ya mion 500 kusupport clabu za michezo na mengine mengi hata hili pia ni jukumu lqo na ndio maana tunalipa kodi
    binafs mm nonasio kosa kujitolea lkn tuwekwe wazi kabla ya wqo kufikia hatua hiyo niyapi yalikua majibu ya Tarura

  3. Mama wananchi hawa wanaojitengeneza barabara ya mtaa wa awadhi Goba tunaomba Serikali yako iwapatie lami kama timu za Simba na Yanga zinavyopewa Mamilioni ya hela. Na wananchi hawa wa Goba ndio magoli yao ya Maendeleo. Barabara ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

  4. Mama wananchi hawa wanaojitengeneza barabara ya mtaa wa awadhi Goba tunaomba Serikali yako iwapatie lami kama timu za Simba na Yanga zinavyopewa Mamilioni ya hela. Na wananchi hawa wa Goba ndio magoli yao ya Maendeleo. Barabara ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

  5. Mradi kama huu upo pia Bunju A, Burumawe, hawa jamaa nao wamehangaika sana Kwa michango na ukarabati wa Barabara Yao..huku wakikabiliwa na changamoto ya malori ya mchanga yanayoharibu hiyo Barabara.

  6. Hapa Goba Barbara za mitaani imekuwa ni changamoto hasa wakati huu wa mvua zinazoendelea kunyesha, maeneo mengine kama una usafiri wako, pikipiki au gari mvua ikinyesha tu, huondoki hapo maana shughuli yake ni pevu, utaikokota pikipiki baadae ya mvua kukatika au utalisahau gari Hilo kwa siku kadhaa sababu ya udongo huu wa mfinyanzi. Yaani ni keto KUBWA.

    HONGERENI wenzetu kwa hatua hiyo, binafsi nawapongeza sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *