Shaaban Robert ni mwandishi ambaye alikuwa na tabia ya kuwapa wahusika wake majina ya kipekee; majina ambayo yanaakisi tabia zao na hayatumiki katika maisha ya uhalisia.
Katika Kusadikika, kwa mfano, yupo Waziri Majivuno, Auni na Radhaa; kwenye Kufikirika, kuna Utubusara Ujingahasara, Mwerevu na Mjinga pia. Lakini wahusika hawa hawakupewa majina yao haya kwa bahati mbaya.
Yalikuwa ni mafumbo ambayo msomaji alipaswa kuyafumbua; kitendawili ambacho kilipaswa kuteguliwa. Kwenye kitabu chake cha Utubora Mkulima, mwandishi anamlazimisha msomaji kujiuliza, kwa nini mtu huyu aitwe Utubora na siyo Bwana Musa?
Jina la kitabu hiki, Utubora Mkulima, linaakisi mhusika mkuu wa kitabu, pamoja na wasifu wake. Mwandishi anaonesha jinsi gani jina la mtu huyu, Utubora, linashabihiana na tabia yake. Yeye ni kijana aliye “… mwaminifu kama mchana; na msiri kama usiku.” (uk 1).
Pia, mwandishi anamwelezea kama mtu ambaye “… alikuwa kama pumzi ya maisha kwa tajiri wake ambaye alikuwa hana mtu mwengine wa kutegemea” (uk 1). Zaidi sana, “.. alikuwa na tamaa ya ubora siku zote” (uk 27). Kama ilivyo kwa Karama katika Kusadikika, Utubora ni mhusika bapa, yaani mhusika katika simulizi ambaye amejengwa na sifa moja kuu na kusimamia dhana moja kuu.
SOMA ZAIDI: ‘Kusadikika’ ya Shaaban Robert na Nasaha Njema za Maisha
Si hivyo tu. Ukitoka dhana ya ‘utubora,’ ukulima nao umekuwa na nafasi kubwa ya kujenga uhusika na kuisogeza simulizi mbele. Kitabu hiki kiliandikwa wakati Watanzania wametoka tu kupata uhuru, mabadiliko mengi yakiwa yanaendelea kwenye jamii.
Japokuwa tunapokutana naye hakuwa akiishi kwenye miaka ya 1960, nafikiri kuwa Shaaban Robert alitaka kuakisi mabadiliko ya kijamii ya wakati huo na ndiyo maana Utubora alikuwa mkulima, kazi ambayo watu walikuwa wanaikimbia ili waende mijini kufanya kazi maofisini. Wakati dunia inaenda kulia, Utubora alikuwa anakwenda kushoto.
Hata hivyo, ukulima siyo kazi aliyoifahamu kabla sisi wasomaji kukutana naye. Tunapokutana naye kwa mara ya kwanza, maisha yake yamejaa simanzi nyingi. Amerudi kutoka vitani Burma, sasa Myanmar, ambako alikuwa ameenda kama askari kwenye Vita Vikuu vya Dunia.
Kufika nyumbani Dar es Salaam, anakuta mama yake ameaga dunia, na mchumba wake kipenzi, Sheha, ameolewa na mtu tajiri. Lahaula!
Kwa viashiria tunavyoviona, tunagundua kuwa yeye ni muathirika wa kile kinachojulikana leo hii kama Mkazo Baada ya Kiwewe, au Post-Traumatic Stress Disorder (PTSD) kwa kimombo, kabla hata hali hiyo haijapewa jina la kitaalamu.
SOMA ZAIDI: ‘Kufikirika’ ya Shaaban Robert na Uhalisia Usiyopitwa na Wakati
Sononeko la moyo wake linamsukuma kutaka kuondoka katika mazingira yale, na kwenda mbali kabisa ambako hakuna mtu anayemjua. Si tu kwamba alitaka kuhama, lakini pia alitaka kubadilisha aina ya kazi aliyokuwa akifanya awali, awe mkulima.
Kuipendeza nafsi yako
Mimi ni muumini wa nguvu aliyonayo mwanadamu kubadilisha njia anayoiendea. Wanasema, kama hupendi hali fulani, ibadilishe. Kama hupendi mazingira yako, yabadilishe, au hamia mazingira mapya. Wewe siyo mti kwamba umelazimishwa kukaa sehemu moja milele.
Ni kuhama huko ndiko kulikomkutanisha Utubora na mtu ambaye alimfahamu zamani aitwaye Makuu pamoja na mchumba wake, Radhia, watu ambao walikuwa na nafasi kubwa ya kumletea furaha katika maisha yake kwa namna tofautitofauti.
Kwa bahati mbaya, wapo watu wengi ambao wanaishi maisha ambayo hayawafurahishi wao wenyewe; wanaishi kwa ajili ya watu wengine. Wanaoa, na kujenga nyumba, na kufanya kazi katika tasnia ambazo haziwapi furaha mioyoni mwao.
Wanataka tu kutiki viboksi katika orodha iliyopo katika vichwa vyao kwamba wametimiza yale ambayo wanapaswa kutimiza kwa viwango vya wanajamii. Haikuwa hivyo kwa Utubora.
SOMA ZAIDI: Ni Wakati Tuitendee Haki Kumbukumbu ya Maisha ya Siti binti Saad
Hata pale ambapo watu wake wa karibu walipokuwa hawamwelewi, yeye alisimamia msimamo wake – alitaka kuifurahisha nafsi yake tu na si ya mtu mwengine yeyote, hata pale ambapo ilionekana kama ingekuwa hasara kwake.
Mwisho wa siku, msimamo wake unakuwa na manufaa kwake. Anapoondoka mjini na kufika kwenye kijiji kiitwacho Busutamu, alikozaliwa mama yake, inakuwa ni mwanzo wenye nuru mpya kwake.
“Nashukuru sana kuwa lazima ya kujisaga katika ofisi, kutwa kufanya kazi ninayoichukia, sinayo tena sasa… Nilikuwa sijui kuwa hai ilikuwa nini mpaka nilipokuja huku.” (uk. 32)
Pesa mambo yote?
Utubora ana mahusiano ya tofauti na pesa. Pesa ndiyo iliyomfanya akamkosa Sheha, na bado kidogo zimkoseshe nafasi ya kulijua penzi kwa mara ya pili. Kwa rafiki yake yule aitwaye Makuu, fedha ilikuwa ndiyo kila kitu.
Alimwambia Utubora siku moja kuwa, “Bila fedha, mwanamume hawezi kuoa hata mwanamke akampenda.” (uk. 38). Hata hivyo, pamoja na falsafa yake hiyo, na pamoja na kuwa na hizo pesa alizodhani ni mambo yote, mpenzi wake hakumpendea pesa hata kidogo, jambo ambalo lilimchanganya sana Makuu.
SOMA ZAIDI: Laiti Kama Ningepata Nafasi ya Kumhoji Shaaban Robert
Tena, kwa moyo wake mwema, Utubora alijitolea kufanya kazi za bustani kwa bibi mmoja aliyekuwa jirani yake. Watu hawakuelewa kwa nini anafanya kazi bila ya kudai malipo. Bibi huyu aliyefahamika kwa jina la Bimkubwa, alikuwa amebaki mwenyewe katika familia yake kwani wanafamilia wote walikuwa wamefariki.
Kama Utubora, alikuwa amejaa na majonzi. Hata hivyo, tofauti yao ni kwamba Utubora hakuruhusu majonzi hayo yajenge shina la uchungu ndani yake. Bimkubwa anamwambia Utubora, “Kutafuta furaha katika maisha ni kama kutafuta paka mweusi katika chumba chenye giza,” (uk. 50) – jambo ambalo Utubora hakukubaliani nalo.
Mwandishi anaonesha jinsi Utubora kuwa vitani kulimjengea taswira ya ulimwengu. “Vita vilimfundisha Utubora mambo mengi sana, vikamwonyesha vilevile maana mbalimbali za thamani ya maisha. Aliona dhahiri kuwa maisha yalikuwa si kitu cha biashara, alifahamu kuwa yalikwenda mbio, na kuwa hayakudumu.” (uk. 15).
Kwake yeye Utubora, vitabu vilikuwa ndiyo utajiri. “Robo ya mshahara ilikuwa inatumiwa siku zote kwa kununua vitabu hivyo.” (uk. 18)
Mapenzi
Ninaipenda hekima ya Utubora. Japokuwa Sheha alimuumiza sana, hakuacha kuyapa mapenzi nafasi nyingine tena. Na mama yake ana nafasi kubwa katika hili.
SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania?
Japokuwa mama yake alikuwa hayupo naye katika mwili, Utubora hakuacha kuendelea kuzungumza naye na kuchota katika hekima aliyompa enzi za uhai wake.
“… tangu Sheha alipovunja ada ya mapenzi, imani ya Utubora juu ya wanawake iliharibika. Walakini, kumbukumbu ya mama yake ilimwokoa katika kuingia katika kosa lile kubwa la kulaumu wanawake wote kama ilivyo desturi ya baadhi ya wanaume wenye malezi mabaya.
“Si kweli kabisa kuwa samaki mmoja akioza, wameoza wote. Samaki wengine huogelea na huzama baharini bafo; hawajavuliwa wala hawajaletwa sokoni kuuzwa.” (uk. 15)
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.