The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simba Bado Ina Nafasi kwa Al Ahly Kama Timu Itaandaliwa Vizuri

Maandalizi yasiwe ya kimbinu tu, bali kisaikolojia pia ili wachezaji waweze kujitambua kuwa wanaweza kupata ushindi katika mazingira magumu.

subscribe to our newsletter!

Mashabiki wengi walitoka uwanjani Ijumaa wakiwa na hasira, wasijue lawama wamtwishe nani baada ya klabu yao ya Simba kukubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya Al Ahly katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa soka Afrika.

Ni wazi kuwa kumbukumbu zilizowajia baada ya mchezo huo ni timu yao kushindwa kuvuka hatua ya robo fainali na kwamba kipigo hicho kimeondoa matumaini yoyote mbele ya Al Ahly ambao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa vigogo hao wa soka wa Tanzania.

Simba haijawahi kuiondoa Al Ahly kwenye mashindano hayo wala mengine yoyote ya Afrika, lakini imekuwa ikijifariji na matokeo ya ushindi wa nyumbani ambao huwa hauinufaishi katika matokeo ya jumla kwa kuwa vigogo hao wa soka barani Afrika hupata ushindi mzuri nyumbani na hivyo kila mara kuiondoa Simba mashindanoni.

Na safari hii, klabu hiyo ya Misri imevunja utamaduni huo wa kupoteza mchezo wa ugenini ambao huiweka katika hali ngumu wakati ikijiandaa kwa mechi ya marudiano.

Kama kawaida ya timu kutoka Afrika Kaskazini kutafuta bao la mapema, Al Ahly ilianza kwa nguvu kwa lengo la kupata bao ambalo lingewapa ahueni. Ikafanikiwa kupata bao ndani ya dakika tano za kwanza na hivyo kucheza dakika zilizosalia bila ya wasiwasi mkubwa.

Makosa

Haikuwa ajabu kwamba Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, ikimiliki mpira kwa zaidi ya asilimia 60 kwa takriban dakika 80 zilizosalia za mchezo huo. Simba ilitawala sehemu ya kiungo na kitu kizuri ni kwamba ilimiliki mpira ndani ya nusu ya Waarabu, lakini haikuweza kutumia nafasi ilizotengeneza.

SOMA ZAIDI: TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars

Kama Kibu Dennis, Sadio Kanoute na Saido Ntibanzokiza wangekuwa makini katika kipindi cha kwanza, Simba ingeweza kuwa inafurahia matokeo tofauti na haya ya kufungwa bao 1-0 nyumbani. Maana yake ni kwamba nafasi yoyote inayopatikana katika mechi kubwa kama hiyo, ni lazima itumike kikamilifu na kwa umakini mkubwa.

Kibu ndiye angeweza kufungua milango ya Al Ahly baada ya kuburuziwa pasi ndefu na akawazidi mbio mabeki wa Ahly. Lakini akapoteza utulivu katika umaliziaji. Wakati alitakiwa aubetulie mpira juu ya kipa aliyekuwa akitoka golini, Kibu aliamua kupiga shuti kubwa na mpira kupaa juu ya lango.

Makosa hayo pia yalifangwa na Kanoute na Saido licha ya kwamba nafasi walizopata hazikuwa na uhakika sana.

Kwa kawaida, mbele ya timu kutoka Afrika Kaskazini, matokeo kama hayo ni mwisho wa safari, lakini mpira wa miguu unaongoza duniani kwa kutotabirika matokeo ukilinganisha na michezo mingine.

Ndiyo, Al Ahly wanaweza kuwa walificha makali yao na pengine ubora wao haukuwa wa kiwango cha kawaida kwa sababu baadhi ya wachezaji wao tegemeo kama Percy Tau ndiyo kwanza walikuwa wametoka kupona majeraha yao, lakini hilo halifai kuwa jambo la kuikatisha tamaa Simba.

Nafasi bado ipo

Simba bado ina nafasi ya kubadili matokeo na kuondoa mwiko wa kutovuka hatua ya robo fainali.

SOMA ZAIDI: TFF, TPLB Ziamke, Azam Media Siyo Mfadhili

Ukweli kwamba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, ilitengeneza nafasi zaidi ya tatu za wazi, ilimlinda kipa wake asisumbuliwe mara kwa mara, unatoa matumaini kuwa kuna kitu Simba inaweza kufanya kama ilivyokuwa mwaka 2003 ilipoivua Zamalek ubingwa wa Afrika kwa kuiondoa kwa ushindi wa penati kwao nchini Misri.

Iliwahi kufanya hivyo kwa Mufurila Wanderers ilipogeuza kipigo kibaya cha mabao 4-0 nyumbani kwa kushinda kwa mabao 5-0 ugenini.

Si rahisi kumshinda Al Ahly kwa mabao 2-0 nyumbani kwao Misri, lakini inawezekana kama timu itaandaliwa vizuri, si tu kimbinu, bali kisaikolojia ili wachezaji waweze kujitambua kuwa wanaweza kupata ushindi katika mazingira magumu.

Na kisaikolojia ni pamoja na mashabiki kuonyesha kuwa wana matumaini na kikosi chao. Haya mahojiano yanayofanywa kwa mashabiki na vyombo vya habari vya mitandaoni yanaweza pia kuwa na athari kwa wachezaji.

Wengi wanaonyesha kuwa wameshakata tama kwamba timu haiwezi kusonga mbele. Katika mazingira hayo, unategemea wachezaji watajionaje kuwa wanaweza kugeuza matokeo? Ni nadra sana kwa maelezo kwamba “safari ndiyo imeishia hapo” kuwa hamasa kwa wachezaji labda yasemwe na timu pinzani.

SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?

Kwa hiyo, maandalizi pia yanahusisha matumaini waliyonayo viongozi, mashabiki na wanachama kwamba kuna jambo linaweza kufanyika ugenini, achilia mbali mbinu na mikakati ya kocha na benchi lake la ufundi.

Mchezo wa soka hutoa nafasi ya timu kujiuliza na ndiyo maana hata lile bao la dhahabu liliondolewa. Wakati ule, dakika zikiongezwa na timu ikapata bao ndani ya muda wa nyongeza mechi ilikuwa inaishia hapo. Lakini huu ulikuwa ukatili ambao mchezo wa soka haukuutaka.

Na Simba ina nafasi hiyo ya kujiuliza ndani ya wiki moja. Na jibu ikiwa inawesekana, basi lolote laweza kutokea Misri. Simba bado ina nafasi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *