Dodoma. Wakati Serikali ikipongezwa kwa juhudi zake zilizopelekea kushuka kwa vifo vinayotokana na uzazi nchini Tanzania, wadau wameendelea kusisitiza umuhimu wa hudumu wa afya kufanya kazi zao kwa weledi na umakini kuepusha vifo vinavyoepukika wakati wa mchakato wa kujifungua.
Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, iliyozinduliwa hapo Oktoba 28, 2023, inabainisha kwamba vifo vinavyotokana na uzazi kwa akina mama vimepungua kutoka 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/2016 hadi kufikia 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.
Lakini wadau wanaamini kwamba endapo kama juhudi za kupunguza zaidi idadi hii hazitahusisha kusimamia umakini na weledi wa watoa huduma, akina mama wengi wanaojifungua wanaweza kuwa katika hatari ya kupoteza maisha yao au yale ya watoto wao kutokana na watoa huduma kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
Zaidi ya mara moja Watanzania wameshuhudia wazazi, na muda mwingine na watoto wao, wakifariki wakati wa mchakato wa uzazi katika hali ambayo inahusishwa na uzembe wa watoa huduma.
Mnamo Novemba 19, 2023, kwa mfano, Serikali mkoani Tanga ilitangaza uchunguzi kufuatia tukio la mjamzito na kichanga chake kufariki katika Kituo cha Afya cha Kabuku, wilayani Handeni, mkoani humo, vifo vilivyokuja kuthibitishwa kutokea kutokana na uzembe wa watoa huduma.
SOMA ZAIDI: Simulizi ya Mapambano ya Mama Mwenye Ulemavu: Uzazi Katika Umri Mdogo, Kazi, Mapenzi, Familia na Ndoa
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Serikali kuingilia kati kufuatia malalamiko kwamba watoa huduma wamesabisha kifo cha mama mjamzito au mtoto wake kwani mnamo Mei 10, 2022, mamlaka mkoani Songwe walichukua hatua kama hiyo baada ya wauguzi katika Kituo cha Afya cha Tunduma, wilayani Momba kutuhumiwa kusababisha kifo cha mtoto aliyezaliwa kituoni hapo.
Baadhi ya wananchi waliopoteza wapendwa wao katika mazingira kama hayo wameiambia The Chanzo kwamba dhamira ya Serikali kuokoa maisha ya mama mjamzito na mtoto wake wanazitambua, lakini iongeze nguvu katika kuhimiza umakini zaidi miongoni mwa watoa huduma ili kuepusha vifo vinavyoepukika.
Moja kati ya watu hawa ni Rajab Athuman, mkazi wa Dodoma ambaye alimpoteza mke wake mwaka 2021, aliyefariki punde tu baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na kile kilichokuja kubainika ni kukosekana kwa umakini kwenye kumbeba baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.
“Inavyosemekana [wahudumu] walikuwa wameshamaliza kumfanyia upasuaji na mtoto alimuona,” Athuman, 34, alieleza kwenye mahojiano na The Chanzo. “Kumtoa kwenye kitanda cha upasuaji, kumuweka kwenye machela ili wampeleke wodini, pale kulikuwa kuna tatizo. Aliyekuwa amembeba kwenye mikono ya juu mikono yake iliteleza, [mke wangu] alipigiza kichwa chini” na kufariki.
“Wawe makini zaidi,” alisema Athuman alipoulizwa atoe wito wake kwa watoa huduma. “Kwa sababu yeye [muuguzi] anapopokea mshahara huwezi jua anatatua vingapi. Anapookoa maisha ya mtu huwezi jua anasaidia watu wangapi. Kwa hiyo, waongezewe ujuzi na wawe makini. Bila wao hatuwezi kuwa sisi.”
Uwekezaji
Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya kitabibu aliyeiambia The Chanzo kwamba juhudi za kuondokana na ule unaoitwa uzembe katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini ni lazima ziende sambamba na kuongezwa kwa madaktari katika hospitali na vituo vya afya pamoja na kuongezewa maslahi kwa watu wa kada hizo.
SOMA ZAIDI: Wadau Wahimiza Ufikishwaji Elimu ya Uzazi kwa Vijana Wenye Ulemavu
Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa madaktari, huku tatizo hilo likionekana kuwa kubwa zaidi vijijini kuliko mijini. Hata kwa wale wahudumu wa afya waliopo nchini, maslahi yao yametajwa kuwa ni yasiyoridhisha, hali inayopelekea baadhi yao kuondoka nchini na kwenda kutafuta maslahi mazuri zaidi nje ya nchi, au kuacha kazi za udaktari.
Hivi karibuni, kulikuwa na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ikihusisha wafanyakazi katika sekta ya afya, ambapo watu wengi waliokuwa wanafanyakazi kwenye sekta hiyo walitangaza kuwa wamelazimika kuondoka kwenye sekta hiyo, wakitaja maslahi yasiyoridhisha, ikiwemo malipo hafifu yasiyoendana na kuongezeka kwa gharama za maisha, kama sababu za kuacha kazi.
“Mtu akiwa anafanya kazi ambazo zilitakiwa zifanywe na watu watatu, na anafanya peke yake, atakuwa na msongo [wa mawazo] na kuna kipindi hajali tena,” Dk Kisowile alisema kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Huo upungufu wa rasilimali watu mtu anajua kwamba hata nifanyeje mimi ndiyo nipo.”
Dk Kisowile, ambaye huandika mara kwa mara kwenye The Chanzo, alisema kwamba Serikali haina budi kuongeza watumishi kwenye sekta ya afya, pamoja na kuongeza maslahi kwa wale waliopo kazini, akisema kwamba kuridhika kwa mtoa huduma kuna uhusiano wa moja kwa moja na kuimarika kwa huduma inayotolewa.
“Kitu kingine ni kuongeza mafunzo kwa wafanyakazi waliopo kazini,” aliongeza mtaalamu huyo. “Kuna vitu vipya vinaibuka kila siku jinsi gani ya kumsaidia mama ili vifo visitokee. [Pia,] kuboreshwa mazingira ya kazi, ikiwemo vitendea kazi, dawa pamoja na mishahara ya watumishi wa huduma za afya. Pia, urahisishaji wa mfumo wa rufaa. Kina mama wengi wanafariki kwa sababu rufaa imekuwa ngumu.”
SOMA ZAIDI: ‘Nakuwa Baba Kamili’: Wanaosindikiza Wake Zao Kliniki Waeleza Uzoefu Wao
Wito huu unaungwa mkono na Rabia Saad, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Action Girls Foundation, linalojihusisha na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana, ambaye ameiambia The Chanzo kwamba kuondokana na uzembe kwenye vituo vya afya kutahitaji “kuimarishwa [kwa] mifumo ya afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakina mama wajawazito.”
Serikali yanena
Dk Mzee Masumbuko Nassoro ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, kutoka Wizara ya Afya, aliiambia The Chanzo kwamba Serikali inayachukulia kwa uzito mkubwa malalamiko ya uzembe unaopelekea vifo vya mama na mtoto, na Serikali haisiti kuchukua hatua dhidi ya wahusika pale inapobainika uzembe kweli umetokea.
Dk Nassoro alisema kwamba wanaobainikia kufanya uzembe hufikishwa kwenye vyombo husika, kama vile Baraza la Madaktari na Baraza la Wauguzi, na mtu akipatikana na hatia hatua stahiki huchukuliwa dhidi yake.
“Hatua hizi ni pamoja na kusimamishwa kazi,” alisema afisa huyo mwandamizi wa Serikali. “Mtu asipowajibika vizuri basi kuna hatua za juu zinachukuliwa kwenye mabaraza yao, na tunaamini hizi zitasaidia katika kupunguza uzembe unaotajwa na kuokoa maisha ya akina mama na watoto wengi zaidi.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.