Ukatili umetapakaa na kuenea sana katika jamii zetu, na dunia kwa ujumla, kiasi ya kwamba kujizuia kutokuuzoea pekee naweza kusema ni kitendo cha kijasiri sana, na hata cha kimapinduzi!
Kukataa kwamba hali tuliyonayo ndivyo jinsi hali inavyopaswa kuwa, na kuendelea kuwa na matumaini kwamba dunia tofauti, iliyo bora na ya haki, zaidi kuliko hii iliyopo inawezekana, ni mtazamo mgumu, lakini wa lazima, kuwa nao kulingana na jinsi hali ya mambo ilivyo.
Kukataa kuuzoea ukatili unaofanyika kwenye jamii zetu, ambao kwa kiwango kikubwa huelekezwa kwa makundi dhaifu ambayo badala ya kudhulumiwa yangepaswa kuhifadhiwa, ni sehemu muhimu ya mchakato wetu wa kuthibitisha utu na ubinadamu wetu mbele ya uso wa dunia, mchakato ambao unazidi kuwa mgumu kutokana na ubinafsi tunaosukumiwa na hali ngumu ya maisha.
Kuuzoea ukatili huu ni kujikatia tamaa kama wanadamu ambao uwezo wa kubadilisha mazingira yetu upo ndani mwetu, na kujikatia tamaa kwa mwanadamu ni adhabu ambayo uzito wake unafanana tu na ile ya mtu kuchukua uhai wake mwenyewe.
Kuishi, tujiulize, kutakuwa na maana gani kama hakutajumuisha kushiriki kikamilifu kwenye kuifanya dunia yetu iwe bora zaidi, mchakato ambao utajumuisha kukataa, katakata, kuizoea hali isiyotufurahisha?
Tuwatetee wanawake
Hatuwezi kuutazama ukatili unaoelekezwa kwa wanawake na watoto, wa kike na wale wa kiume, kama kitu cha kawaida tusichokuwa na uwezo wa kukibadilisha.
SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022
Vipigo, na muda mwingine mauaji ya kikatili, yanayoelekezwa kwa wanawake, muda mwingi kutoka kwa wapenzi, au waume, zao, si jambo tunaloweza kuruhusu akili yetu ilizoee na kulikuchukulia ni la kawaida. Kufanya hivyo itakuwa ni kukiri kushindwa kwetu na hali ambayo tunaweza kuidhibiti.
Ukatili wanaoendelea kufanyiwa watoto wetu, ukijumuisha vitendo vya ubakaji, ulawiti, na kuchomwa moto eti ameiba Shilingi 5,000, haupaswi kuzoeleka na kuingiza katika akili zetu mawazo kwamba hatuwezi kufanya kitu kurekebisha hali mbaya sana ya mambo inayoitia aibu jamii yetu na sisi wanachama wake.
Kama hatuwezi hata kuwahakikishia watoto wetu ulinzi wanaostahiki ili waweze kukua kama inavyopaswa, tunaanzaje kujiita wazazi, walezi, au hata ‘viongozi,’ na kujipiga vifua eti tunatimiza wajibu wetu kama inavyotupasa?
Lazima tusimame imara na kupaza sauti zetu pale tunaposhuhudia mawakala wa dola, wakiwemo askari wa jiji na maafisa wengine wa mamlaka za Serikali, wakiwasumbua wafanyabiashara wadogo, maarufu kama wamachinga, kwa kuwakamata kiholela, kuwaweka ndani na kuwaharibia , au kukamata, biashara zao, biashara wanazozitegemea kuendesha familia zao zinazokabwa koo na ugumu mkubwa wa maishaa.
Ni wajibu wetu kusimama na wamachinga na kuikumbusha Serikali kwamba haina haki ya kuwapangia kitu cha kufanya watu iliyowaacha bila msaada wowote.
SOMA ZAIDI: Kuna Ugumu Gani Kwa Serikali Kuwasikiliza Wamachinga?
Hatupaswi kuiruhusu Serikali na mawakala wake waharibu biashara za watu ambao watahitaji fedha kwa ajili ya kupata huduma zote za msingi za kijamii, ikiwemo maji, afya, na elimu, huduma ambazo Serikali ilipaswa kuwapatia bure wananchi wake kustahiki jina la ‘Serikali.’
Tusimame na Wamasai
Tunapaswa kusimama na Wamasai na wenyeji wengine wa Ngorongoro wanaopambania haki yao ya msingi ya kubaki katika makazi yao ya asili, makazi waliyoishi kwa karne na karne, haki ambayo iko hatarini kupokwa na Serikali ambayo viongozi wake wanaonesha kutoa kipaumbele zaidi kwenye kujilimbikizia mali kwa njia za kifisadi na haramu badala ya kujali maisha ya watu wake.
Ingawaje wanarudia madai hayo mara kwa mara, wakitegemea mwisho wa siku yatatuingia akilini, ni lazima tukatae utetezi finyu unaotolewa na mawakala wa dola unaokusudiwa kuhalalisha uhamisho huo wa wenyeji kwenda kwenye maeneo wasiyokuwa na historia nayo, ikiwemo madai kwamba zoezi hilo linafanyika kwa “hiyari.”
Tunapaswa kuieleza Serikali kwamba zoezi haliwezi kuwa la “hiyari” katika mazingira ambayo huduma za msingi za kijamii zinakatwa, hali inayowafanya wenyeji wasiwe na chaguo lingine lolote kama bado wangependa kuishi bali kuhama maeneo hayo; zoezi haliwezi kuwa la “hiyari” wakati ambapo wawakilishi wa wenyeji wanatishiwa uhai wao na maeneo mengi zaidi yanamegwa kwa kisingizio cha “uhifadhi.”
Hatupaswi kuhadaika na madai kwamba zoezi husika linalenga kuimarisha “uhifadhi” katika mazingira ambayo hakuna ushahidi wowote umewekwa hadharani wa uwepo wa wenyeji hao, na kuongezeka kwa idadi yao, na kuhatarishwa kwa uhifadhi. Hatupaswi kuamini madai haya wakati ambapo uhamishwaji wa wenyeji unaambatana na mipango ya ujenzi wa hoteli za kifahari kwenye maeneo hayohayo.
SOMA ZAIDI: Uhamisho wa Wafanyakazi Wazawa Ngorongoro Unaacha Maswali na Mashaka Makubwa
Kwa ufupi, hatuwezi kuruhusu thamani ya mwanadamu mwenzetu ionekane ni ya chini zaidi kuliko ile ya mnyama wa porini. Ni binadamu ndiyo anapaswa aamue hatma ya mnyama pori na siyo kinyume chake, na tutakuwa hatujitendei haki tukiruhusu mawakala wa Serikali watushawishi kwamba hata tunapaswa kuwa na huo mjadala.
Wanaoonewa
Tusimame na wafanyakazi wanaojitokeza na kulalamikia maslahi duni pamoja na uimla wa waajiri wao; tuwaunge mkono wanafunzi wanaolalamikia adhabu ya viboko iliyothibitishwa kuathiri maendeleo yao; na tuwaamini wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokerwa na kukithiri kwa vitendo vya rushwa ya ngono vinavyoendekezwa na wahadhiri wao.
Tusimame na wafungwa katika harakati zao za kulinda utu, heshima na haki zao, ikiwemo ile ya kushiriki kweye michakato ya kidemokrasia, kama vile kupiga kura; tuwapazie sauti wale waliopo mahabusu ambao kesi zao zimeendelea kwa miaka bila ya kuwepo kwa dalili zozote za kuhitimishwa; na tuzifariji familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na vitendo vya askari wa Jeshi la Polisi pamoja na kuwasaidia kuhimiza uwajibikaji.
Tusimame na Wapalestina wanaopambana na itikadi hatari ya kizayuni ambayo utekelezaji wake umekuwa ukisababisha maafa kwa zaidi ya miaka 70 na tuwafariji ndugu zetu kutoka Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako mapigano kati ya walafi wa madaraka yanaendelea kuathiri maisha ya mamilioni.
Tunapaswa tuikemee Indonesia kwa ukatili inaotekeleza dhidi ya raia wake huko West Papua; tuendelee kuyataka mataifa ya magharibi kuwaachia watu wa Haiti nchi yao ili wajitawale wenyewe; tuiambie Morocco tunalaani kitendo chake cha kuendelea kuikalia kwa mabavu Sahara Magharibi; na China iache ukandamizaji wake dhidi ya raia wake wa Xinjiang.
SOMA ZAIDI: Je, Dunia Inaweza Kupata Suluhu ya Kudumu ya Mgogoro wa Israel na Palestine?
Hatupaswi kuuzoea ukatili, hususan ule unaotokea mbele ya macho yetu, na tukiwa tunafurahia siku hii muhimu ya Eid Al Fitr, ni matumaini yangu kwamba tutapata muda wa kutosha wa kutafakari juu ya mustakabali wa dunia na jamii zetu na kujiuliza endapo kama tunatimiza wajibu wetu ipasavyo kwenye kuzifanya kuwa bora zaidi, ikiwemo kwa kupinga ukatili unaoendelea, hususan dhidi ya makundi yanayotutegemea kuyapa hifadhi.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.