Dar es Salaam. Awamu ya pili ya utolewaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ilifanyika jijini hapa hapo Aprili 13, 2024, katika ukumbi wa The Super Dome Tanzania, Masaki, huku burudani, furaha na hamasa vikilisindikiza tukio hilo muhimu ambalo mgeni wake rasmi alikuwa ni mshindi wa Tuzo ya Nobel wa mwaka 2021 kwa upande wa fasihi, Abdulrazak Gurnah.
Jumla ya washindi 30 walitangazwa wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya watu, wakiwemo maafisa waandamizi wa Serikali, mabalozi, na wale wanaotoka kwenye tasnia ya uandishi nchini, kumi wakiwa ni waandishi bunifu kwenye tanzu ya riwaya, kumi wengine wakiwa ni washairi na kumi wengine wakiwa ni waandishi wa hadithi za watoto, ingizo jipya kwenye tuzo hizo.
Hafla hiyo ilianza kwa wahudhuriaji wake kutangaziwa washindi wa kumi mpaka wa saba kutoka kwa kili tanzu, ambao wote walitambuliwa kwa kupewa vyeti vilivyotambua ushiriki wao. Hili lilifuatiwa na kuwekwa hadharani majina ya washindi wa tatu na wa pili kutoka kwa kila tanzu, ambao walijishindia vyeti na fedha taslimu Shilingi milioni tano kwa washindi wa tatu na Shilingi milioni saba kwa washindi wa pili.
Kiu ya wahudhuriaji wa hafla hiyo iliyodumu kwa takriban masaa nane, kuanzia saa 11 jioni hadi saa sita usiku, ilikatwa baada ya majina ya washindi wa kwanza kutoka kila tanzu kuwekwa hadharani – Laura Pettie Kisswaka (riwaya), Blandina Isabela Lucas (hadithi za watoto) na Mohamed Omar Juma (ushairi) – ambao walizawadiwa vyeti, ngao na fedha taslimu Shilingi milioni kumi.
Mbali na zawadi hizo, washindi hao wa kwanza pia watashuhudia Serikali ikigharamia uchapishwaji wa miswaada yao na vitabu vitakavyotokana na miswaada hiyo vitasambazwa kwenye shule na maktaba zote zinazomilikiwa na Serikali nchi nzima. Serikali hutafuta mchapishaji kwa utaratibu wa kutangaza zabuni ambapo wachapishaji wanaokizi vigezo huomba na kuchaguliwa.
SOMA ZAIDI: Tuzo za Uandishi Bunifu Tanzania: Bahati Nasibu au Kamari?
Katika hafla hiyo ya Jumamosi, Taasi ya Elimu Tanzania (TET), ambao ndiyo wasimamizi wa tuzo hizo, walimtangaza mchapishaji mashuhuri nchini Tanzania, Mkuki na Nyota, kama mchapishaji aliyeibuka mshindi kwenye utafutaji wa mchapishaji na msambazaji atakayefanyia kazi miswaada ya riwaya na ushairi, ambaz zilikuwa tanzu pekee zilishoshindaniwa, iliyoibuka mshindi mwaka 2023.
Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ilizinduliwa rasmi mwaka 2023 kama sehemu ya jitihada za Serikali za kuchochea hamu ya uandishi na usomaji nchini pamoja na kufufua tasnia ya uchapishaji ambayo imedaiwa kuwa katika hali mbaya inayotishia uhai wake. Imepewa jina la Mwalimu Julius Nyerere kumuenzi baba huyo wa taifa la Tanzania, ambaye, mbali na kuwa kiongozi wa nchi, alikuwa mwandishi mzuri pia.
Uandishi bunifu ni aina ya uandishi ambapo mwandishi hubuni dunia yake katika kuelezea mawazo yake kuhusiana na mambo yanayoendelea katika jamii yake. Aina hii ya uandishi huonekana kwenye kazi kama vile riwaya, ushairi na tamthiliya ambazo uandishi wake hutofautiana na ule unaohusu matukio ambayo yapo kwenye uhalisia wa kidunia.
Kuhifadhi historia
Katika hotuba yake kama mgeni rasmi wa shughuli hiyo iliyofanyika hapo Jumamosi, Gurnah, ambaye aliondoka Zanzibar kwenye miaka ya 1960 na kwenda kuishi Uingereza, alisema kwamba uandishi bunifu una umuhimu sana kwa taifa na dunia kwa ujumla kwani hutumika katika kuhifadhi historia, uchumi, siasa na utamaduni wa watu wenyewe, ambayo yote husaidia kujenga jamii thabiti kimitazamo na kitabia.
“Vilevile, maandiko bunifu huelimisha, huburudisha, na kuliwaza kulingana na nyakati tofauti ambazo jamii inapitia,” alihutubia Gurnah ambaye moja ya kazi zake bunifu, riwaya ya Paradise, imetafsiriwa kwa Kiswahili na Ida Hadjivayanis na kuitwa Peponi.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili
“Maandishi bunifu pia ni kichocheo cha kuchokonoa fikra yakinifu za watu kuhusu hali ya jamii.”
Gurnah, aliyezaliwa Disemba 20, 1948, kwenye iliyokuwa Zanzibar ya Kisultani, aliwaambia washiriki wa hafla hiyo kwamba jamii zote ulimwenguni kote huchagizwa kwa maandiko yaliyoandikwa kwa lugha ya jamii husika, akitambua juhudi zinazotekelezwa na Serikali katika kukuza, kuendeleza na kuhifadhi maandiko bunifu ya Tanzania, hali aliyosema inasaidia “kufumbata” uhai wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
“Natoa raia kwa waandishi wenzangu kutumia kalamu zetu ili kulifaa taifa letu la Tanzania,” Gurnah, ambaye kazi zake nyingi zinahusu madhila ya ukoloni na hatma ya wakimbizi wa Afrika barani Ulaya, aliwaasa waandishi wenzake. “Waswahili husema, kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Waandishi wenzangu, ikumbukwe kuwa uvumilivu na ustahimilivu wenye kuchochewa na kupenda kujifunza ndiyo msingi wa mafanikio katika tasnia ya uandishi bunifu.”
Gurnah alizungumza kuhusu kukua kwa lugha ya Kiswahili duniani, akisema lugha hiyo imekuwa “tunu” barani Afrika na “mwezi mchanga unaochomoza mataifani na viungani mwao,” hali inayoweka ulazima wa upatikanaji wa machapisho mengi zaidi yaliyopo kwenye Kiswahili, hali itakayoitambulisha lugha hiyo na kuipaisha zaidi.
Mwandishi Nyerere
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi aongee na wahudhuriaji wa hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alielezea mantiki ya tuzo hizo kupewa jina la Mwalimu Nyerere, akisema hatua hiyo imefanyika kumuheshimisha kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania huru anayejulikana kwa kupenda kwake sana kusoma na kuandika.
SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar
“Kweli, Mwalimu [Nyerere] alikuwa na mahaba na vitabu,” Profesa Mkenda, ambaye pia ni Mbunge wa Rombo (Chama cha Mapinduzi – CCM), alisema. “Alivisoma na alivichambua, na zaidi, alivitafsiri na aliviandika. Tunajua pia alitafsiri pia kitabu cha [mwanafalsa wa Kigiriki] Plato, ambacho tunatumaini tutakiona, tutazungumza na familia yake.”
“Leo [Aprili 13] tunaadhimisha kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere na tunamuenzi kwa kutoa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu,” aliongeza Mkenda. “Hii ni tuzo kubwa sana inayozingatia umahiri na umaarufu wa Mwalimu Nyerere.”
Mbali na hotuba, hafla hiyo ilipambwa kwa burudani kedekede, ikiwemo utumbuizaji uliofanywa na msanii Mrisho Mpoto na bendi yake, vichekesho vilivyotumbuizwa na mchekeshaji Eliud Samwel, pamoja na usomaji wa mashairi, riwaya na hadithi za watoto.