The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tuzo za Uandishi Bunifu Tanzania: Bahati Nasibu au Kamari?

Kama lengo la tuzo hizi ni kukuza uandishi bunifu na usomaji nchini, basi ni muhimu sana kuwa na mpango mkakati usiopishana njia na malengo hayo. Kwa sasa, mpango mkakati umeshindwa kulenga shabaha hiyo.

subscribe to our newsletter!

Kwa mara ya kwanza, mwaka jana 2023, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, walitoa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu katika tanzu za riwaya na ushairi kwa waandishi nchini Tanzania. 

Mbali na tuzo hii, pia kumekuwepo na tuzo nyingine kutoka nchini Kenya, iitwayo Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika. Kwa hakika, hii ni hatua kubwa mno katika kukuza uandishi wa vitabu, na hatimaye usomaji, nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Serikali imesema kwamba moja kati ya malengo ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni kukuza uandishi bunifu na usomaji nchini. Kama hivyo ndivyo, basi ni muhimu sana kuwa na mpango mkakati usiopishana njia na malengo hayo. Kwa sasa, walau kwa mtazamo wangu, mpango mkakati umeshindwa kulenga shabaha hiyo. 

Masharti ya ushiriki kwa waandishi, kukosekana kwa mkakati wa kuzikuza tuzo hizi, pamoja na kasoro zingine zinaelekea kudumaza ubunifu wa kiuandishi, na hatimaye kushindwa kuchochea hamu ya usomaji. Katika makala haya, nitagusia maeneo kadhaa ambayo binafsi siioni dhamira ya kulenga shabaha iliyokusudiwa.

Moja kati ya maeneo haya ni masharti magumu ya ushiriki yanayopelekea kuaachwa nje ya shindano kwa waandishi wengi wenye vipaji, nia na sababu za kushiriki. Na hata baadhi ya waandishi waliobahatika kutuma miswada yao, wameshindwa kuonesha vipaji vyao itakikanavyo kutokana na masharti magumu.

Kuchapishwa kwengine

Moja kati ya masharti haya ni kwamba muswada unaotakiwa kuwasilishwa ni lazima uwe haujachapishwa mahali popote. Waandaaji hawataki kupokea riwaya, au shairi, ambalo limekwishachapishwa kitabu, au hata mtandaoni tu. Nimekuwa nikijiuliza, kuna tofauti gani katika kuisoma na kuihukumu kazi ambayo haijachapishwa mahali popote na ile ambayo imechapishwa kitabuni au mtandaoni? 

SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?

Kuna hofu gani miongoni mwa majaji na waandaaji wa tuzo kuruhusu kazi ambazo zimeshachapishwa na kusomwa na wasomaji wengi huko mtaani? Mimi nilidhani tuzo zingeongeza raha na hamasa endapo wasomaji wangekuwa wamepata kuzisoma kazi zinazoshiriki. 

Tunajua kwamba, mshindi wa tuzo atapatikana kwa maamuzi ya majaji, lakini hilo halipaswi kuzuia wasomaji kutokusoma kazi hizo. Hivyo ndivyo tuzo nyingi kubwa duniani zinavyoendeshwa.

Kuna hatari kubwa endapo kazi za uandishi zitaishia kusomwa na majaji peke yao halafu wasomaji tukabaki washangiliaji wa matokeo ya ushindi ilhali wakati wa mchakato tulifunikwa gunia machoni. Kwa mtazamo wangu, huo utakuwa ni mchezo wa bahati nasibu!

Ni sawa na kuchezesha ‘korokoro’ chini ya boksi halafu hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuchungulia, zaidi ya kusubiri kumshangilia mshiriki aliyebahatika kulamba bingo.

Kumekuwa na hoja kwamba, waandaji wanataka miswada ambayo haijachapishwa popote, wakiamini kwamba kufanya hivyo ni kuwanyanyua waandishi wachanga. Kama kweli hoja hii inatoka kwa waandaaji, basi ni muhimu wakautangazia umma kwamba tuzo hizi ni kwa waandishi wachanga tu—na waweke wazi sifa zitakazowatofautisha waandishi wachanga na waandishi wakubwa. 

Bila kufanya hivyo, waandishi wengi wataendelea kubaki katika njia panda kwa sababu, kwa hali ya kawaida tu, uchanga wa mwandishi haupimwi kwa kazi ambayo haijachapishwa. Wako waandishi wachanga na wameshachapisha kazi zao. 

Pia, kuna waandishi wakubwa tu ambao wameshachapisha vitabu kadhaa na bado wanayo miswada mingi ambayo haijachapishwa mahali popote. Kwa maana hiyo, hao wanaweza kuituma miswada hiyo na wakaonekana ni waandishi wachanga kwa kigezo hicho.

SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar

Kama hivyo sivyo, na kwamba lengo ni kutowaacha nyuma waandishi (wachanga) ambao hawajapata kuchapisha miswada yao bila kuwaathiri wale ambao wameshachapisha kazi zao mitandaoni, na hata kwenye vitabu, basi ingeruhusiwa washiriki wote kutuma kazi zao kwa namna yoyote ilivyo.

Kimsingi, waandishi hawapaswi kuandika kwa ajili ya tuzo, bali kwa msukumo uliomo ndani yao, kwa ajili yao na jamii zao. Kisha tuzo zinakuja kutolewa kwa wale waliofanya vizuri zaidi. Hivi ndivyo tuzo kubwa kama Nobel Prize in Literature, Booker Prize, Pulitzer Prize, namna zitolewavyo.

Idadi ya maneno

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-cornell wanataka mswada wa riwaya wenye maneno si chini ya 50,000, wakati tuzo yaTaifa ya Mwalimu Nyerere wanataka si chini ya maneno 60,000. 

Lakini mara kadhaa nimesikia majaji wa tuzo hizi wakisema wamesoma miswada mingi mizuri na iliyobora kabisa ya waandishi, yaani washiriki, lakini mwishoni wanagundua hadithi nyingi zilikuwa imekwishafika mwisho kabla ya kutimia kwa maneno hitajika, ila waandishi wanaharibu kwa kujaribu kujaza maneno ili kukidhi idadi inayohitajika katika tuzo.

Kama majaji wanakiri kuwa kazi fulani zilikuwa nzuri sana, lakini ziliharibiwa kwa juhudi za waandishi kutaka kukidhi sharti la idadi (kubwa) ya maneno, maana yake wanakiri kwamba sharti la idadi kubwa ya maneno linachangia kupoteza kazi nyingi bora ambazo zingeliifaa jamii kama isingelikuwa idadi hiyo ya maneno. 

Kutokuwa na sharti la idadi kubwa ya maneno hakupunguzi sifa za uandishi bora. Hata waandishi wakubwa pamoja na walimu wa uandishi bunifu duniani wanakubaliana kuwa, kadri mwandishi anavyotumia maneno machache ndivyo anavyoonesha umahiri wake zaidi. 

Na hata wengi wao, vitabu vyao bora na mashuhuri vilivyojizolea tuzo nyingi, havikubanwa na masharti ya idadi kubwa ya maneno.

Kutuma mswada kwa barua pepe

Kuna sharti pia la washiriki kutuma kazi zao kwa njia ya barua pepe, sharti lililowekwa kwa sababu ya uwepo wa lile sharti mama la kutaka miswada iwe haijachapishwa mahali popote. 

Mwandishi anatuma nakala laini ya kazi yake kwa barua pepe kwenda kwa waandaaji, kisha waandaaji nao wanawatumia majaji hiyo nakala laini, halafu miswada itakayoshinda nayo inatumwa kwa njia ileile ya nakala laini kwenda kwa mchapishaji. 

SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?

Huko kote kazi ya mwandishi ikiwa katika nakala laini inabaki katika barua pepe zao. Je, ni kwa namna gani tumejihakikishia usalama wa kazi hizi? 

Siku akitokea mtu mmoja katika mnyororo huo akakosa uaminifu, akaichapisha kazi ya mwandishi kimagendo, au hata akawatumia marafiki zake kwa njia hiyohiyo ya nakala laini, atajulikanaje? 

Kama ingelikuwa kazi inayoshiriki tuzo ni ile iliyokwishachapishwa, kidogo matumaini ya usalama yangekuwepo.

Maendeleo ya mwandishi

Tuzo hizi za uandishi bunifu, pamoja na mambo mengine, zinatarajiwa kuwakuza waandishi kiuandishi pamoja na kuwafungulia milango ya fursa za kiuandishi. Mwandishi anapotangazwa kushinda tuzo fulani, hapaswi kubaki vile alivyokuwa kabla ya tuzo. 

Lakini washindi wengi wa tuzo hizi mbili hawabadilishwi na tuzo hizi mbili, hali inayowafanya wabaki vilevile kabla na baada ya kupokea tuzo. Unajua ni wasomaji wangapi wa vitabu wanaoweza kuwataja walau waandishi watano tu walioshinda tuzo? Kumi kwa mmoja. Sasa hili ni kosa la kiufundi. 

Kurekebisha mapungufu haya, waandaaji walipaswa kuwekeza nguvu katika maeneo mbalimbali, moja wapo ikiwa ni kushirikiana na vyombo vikubwa vya habari, vya ndani na vya nje ya nchi, ili kuzinadi tuzo husika kwa ukubwa unaotakikana, pamoja na kuwanadi na kuwapatia vipindi vya mahojiano waandishi walioshinda tuzo. 

Kwa kufanya hivyo, watasaidia wasomaji kuwatambua washindi hawa na kuzitambua kwa kina kazi zao, kitu ambacho kitakuza majina na hadhi za waandishi pamoja na kazi zao. Walakini hali ilivyo hivi sasa, ni kinyume chake. Si redioni wala runingani ambako waandaaji wa tuzo wamewapeleka kwa wingi waandishi walioshinda tuzo.

SOMA ZAIDI: Tamasha la Vitabu Zanzibar: Kitovu cha Vipaji Vipya?

Katika kuzieneza kazi zilizoshinda tuzo, waandaaji wa tuzo wanapaswa pia kuzitafutia masoko kazi za waandishi kwa kuziingiza kwenye mitaala ya elimu. Kwa kufanya hivyo, tutazipa hadhi tuzo husika pamoja na washindi wenyewe. Walau hili, kwa tuzo za Mwalimu Nyerere, Serikali iliahidi kulifanyia kazi, ingawaje sifahamu utekelezaji wake umefikia wapi.

Kumekuwa na utamaduni wa kufuata maprofesa vyuo vikuu ili kuwatumia kama majaji wa tuzo za uandishi bunifu. Si jambo baya kabisa. Lakini pamoja na weledi wao katika fasihi, ni muhimu sana tukatambua kwamba, maprofesa wengi wa fasihi, kutokana na umri wao na elimu zao, wameondokea kuwa wapenzi wa uandishi wa namna ile ya akina Euphrace Kezilahabi, Shaaban Robert, Ndyanao Balisidya, Shafi Adam Shafi, na kadhalika. 

Wapenzi wa namna hii ya uandishi si rahisi sana kuuelewa uandishi wa kisasa na kuujaji. Sina hakika ni maprofesa wangapi wa fasihi ya zama hizo wataelewa pale mhusika wa riwaya hizi za kisasa, maarufu kama riwaya-pendwa, atakapoita Uber, au Bolt, badala ya teksi, au pale atakapom-DM mtu huko Instagram, au pale ambapo mume atakapomghadhabikia mkewe kwa kosa la kum-blue tick WhatsApp na kisha kukaa kimya. 

Ni muhimu sana jopo la majaji kuzingatia waandishi, walimu wa fasihi na wachambuzi wa fasihi ya kisasa.

Hafla ya utoaji tuzo

Hafla ya utoaji tuzo ndiyo kilele cha shughuli nzima ya tuzo husika kwa mwaka husika. Kwa sababu hiyo, macho ya wadau mbalimbali huelekezwa hapo ili kuona mafanikio na mwelekeo wa tasnia kwa ujumla. 

Hivyo, waandaaji wanapaswa kuwa wabunifu ili kuandaa hafla ambayo itaamsha ari ya uandishi na usomaji, na haitawachosha na kuwachukiza waandishi pamoja na wasomaji. 

Lakini katika tuzo zetu kumekuwa na uangalifu hafifu mno katika maeneo mengi ambayo ningetamani waandaaji wangefanya marekebisho, moja ikiwa ni itifaki za kisiasa.

SOMA ZAIDI: Maswali ya Msingi Kuhusu Sanamu ya Mwalimu Nyerere Iliyozinduliwa na Umoja wa Afrika

Kumekuwa na kasumba ya kutumia majukwaa ya kisanaa na kitaaluma kwa minajili ya kisiasa. Utamaduni huu umekuwa chachu ya kuviza na kuzorotesha ukuaji na ufanisi wa matukio mengi ya sanaa. Kama hili tumeshindwa kabisa kulikwepa, basi walau tulipunguze kidogo. Nitoe mifano michache kudhihirisha hili.

Kwenye hafla ya utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, mwaka 2023, mgeni rasmi alikuwa ni Rais Mstaafu wa Msumbiji, mzee wetu Joaquim Chissano. Sasa hebu jiulize, Chissano anakuja kuongeza hamasa gani kwenye suala zima la uandishi wa vitabu nchini Tanzania? 

Tunatambua mchango mkubwa wa mzee Chissano katika kukipigia chapuo Kiswahili duniani, kama alivyofanya miaka ya nyuma katika Baraza la Umoja wa Mataifa. Na kwa kuwa tunamuheshimu sana, basi katika hafla kama ile ya utoaji tuzo, tungeweza kumwomba ahudhurie kama mwalikwa na si kama mgeni rasmi. 

Ukitaka kuielewa hoja yangu, nenda kasikilize hotuba ya mzee Chissano katika utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, mwaka 2023. Alitumia muda mwingi kuongelea historia yake binafsi pamoja na makomredi wenziye katika harakati za kudai uhuru. Hafla ya utoaji tuzo ikafunikwa na simulizi za FRELIMO na TANU!

Idadi kubwa ya wazungumzaji, au watoa hotuba, kama Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar; Waziri wa Sanaa na Michezo; Katibu Mkuu Wizara ya Elimu; Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Sanaa, Utamaduni, na Michezo; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET); Kamishna wa Elimu; Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, na wengine wengi haikuwa na tija. 

Mengi katika mambo waliyohutubia, pengine hayakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na uandishi bunifu, au mazungumzo yao yalifanana. Ingetosha kuwa na wazungumzaji wachache kwa niaba ya wengi. Hafla ya tuzo haipaswi kuwa uwanja wa kumridhisha kila msemaji wa taasisi fulani.

Kwenye hafla ya utoaji tuzo ya Mabati Safal-Cornell, mwaka 2019, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, alipopewa nafasi ya kuzungumza, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisimama na kuanza kumdhihaki na kumkebehi kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, aliyekuwa amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Kama haitoshi, aliwashukia wadhamini wa tuzo hizo, kampuni ya utengezaji mabati ya Alaf na kuwatishia, kwa sababu aliwahi kuwaomba mchango wao wa mabati lakini hawakumpatia. Hafla inayohusu usomaji na uandishi wa vitabu inahusianaje na vimbwanga hivi vya kisiasa? 

Hii yote inasababishwa na waandaaji wenyewe kuifanya hafla ya vitabu kuwa uwanja wa siasa.

Kwenye hafla ya utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere pia, paliandaliwa mjadala wa vitabu kutoka kwa maprofesa na wadau wa vitabu. Mjadala huu ni matokeo ya kukosa ubunifu unaokwenda na wakati. Hebu fikiria, kila mzungumzaji mmoja alipaswa kutumia dakika kumi ‘kuhutubia.’ 

Maana yake, kwa wazungumzaji saba hizo ni dakika 70. Zaidi ya saa nzima tunasikiliza mjadala usioendana na tuzo za uandishi. Basi bora wangetumia dakika hizo hizo sabini tu, lakini kilichotokea, kutokana na uzito wa CV zao, mwendesha mjadala alilazimika kutumia kati ya dakika tano mpaka saba kumtambulisha kila mwanajopo mmoja. 

Dakika tano kwa watu saba ni dakika 35, yaani zaidi ya nusu saa zilitumika kwa ajili ya utambulisho pekee!

Jingine nililoliona kwenye Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ni lile lililohusu washindi kushindwa kutoa neno la shukrani. Tukio ni utoaji wa tuzo ya uandishi bunifu. Washindi wa tuzo hizo wamehudhuria ukumbini. Lakini wamekosa japo dakika mbili tu kwa kila mmoja kutoa neno la shukrani. 

Hawa waandishi washindi ndiyo waliotukusanya ukumbini, hivyo jukwaa hili lilipaswa litumike kuwanadi na kuwakuza zaidi wao. Mnashindwaje kutenga japo muda wa dakika 20 kwa washindi kutoa neno la shukrani tu halafu mnawapa wanajopo zaidi ya dakika 100 kuzungumza?

Jingine ni lile linalohusu utolewaji wa orodha fupi na orodha ndefu za washiriki wa tuzo fulani, utamaduni wa kawaida kabisa, ambapo baada ya waandishi kuingia kwenye kinyang’aniro cha tuzo, majaji husoma miswada yao na kuchagua washindi, ambapo waandaaji wa tuzo hutangaza majina ya waandishi waliofanikiwa kuingia katika orodha ndefu, au Longlist

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Hakuna Kiswahili Kimoja

Na baada ya muda mfupi hutangazwa tena majina yaliyopenya katika orodha fupi, yaani Shortlist. Baada ya hapo mshindi hutangazwa. Lakini hali ni tofauti huku kwetu. 

Mathalani, katika mchakato mzima wa utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2023, hapakuwa na orodha ndefu wala fupi iliyotangazwa, mpaka siku ya tukio ukumbini ndipo wakatangazwa washindi moja kwa moja. 

Kutangaza orodha ndefu na fupi huwaongezea tashiwishi waandishi na wasomaji kufuatilia yanayoendelea kujiri kabla ya tukio husika. Lakini pia huwafanya wasijihisi kufunikwa gunia jeusi machoni mpaka siku ya kutangazwa washindi.

Majaji wa miswada

Wataalamu wa uandishi wanaochaguliwa kuisoma miswada husika na kuihukumu ni watu muhimu sana, ambao sifa zao hazipaswi kuwa na mawaa japo chembe. Katika eneo hili, kuna mengi ya kujadili. 

Kwa mfano, suala la Jaji Mkuu wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2023, kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kwa mwaka huohuo wa 2023, lilinitafakarisha sana, na nadhani, kama nilivyosema, linahitaji mjadala mpana. 

Huko ‘duniani’ tumeona mara kadhaa mwandishi anakosa tuzo fulani na anakwenda kushinda tuzo sehemu nyingine kwa mswada uleule, kwa sababu majaji wanatofautiana fikra na ufahamu, kwa hivyo majaji wa tuzo moja wanaweza kuamua tofauti na wale wa tuzo nyingine. 

Lakini katika tuzo hizi za Safal-cornell na Mwalimu Nyerere, ambapo jaji wa kule anakuja kuwa jaji wa huku, inaondoa ladha ya kuwa na tuzo mbili tofauti kwani matarajio ya washiriki yanakuwa ni yaleyale.

SOMA ZAIDI: BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania

Kwa kuhitimisha, niseme tu kwamba duniani kote, miongoni mwa mambo yanayokuza hadhi na thamani ya tuzo ni pamoja na umri wa tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake na thamani ya tuzo hiyo kwa maana ya pesa. 

Huku kwetu Afrika, si ajabu kukuta thamani ya tuzo ni Shilingi milioni 500, lakini washindi wote kwa ujumla wanaondoka na si zaidi ya Shilingi milioni kumi tu. Hizo nyingine ni maposho, anasa, na maandalizi yasiyo na ulazima wowote. 

Sijajua kwa tuzo hizi mbili, yaani ile ya Kenya na hii ya Tanzania, thamani halisi ni ipi na matumizi yake yanatumikaje kuwatuza walengwa. Tunapaswa kulichungulia.

Nimeona waandaaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere wameshatangaza kuwa Aprili 13, 2024, ndiyo siku ya kuwatuza washindi wa tuzo hiyo. Ni matarajio yangu watachukua ushauri wangu na kuufanyia kazi ili kuboresha tuzo hizo. 

Nawatakia kila la kheri!

Maundu Mwingizi ni mwandishi wa riwaya na hadithi fupi kutoka Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI). Kwa mrejesho, anapatikana kupitia maundumwingizi@gmail.com au @maundumwingizi kwenye mtandao wa X. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *