Iwe ni katika ubepari au ujamaa, nchi inahitaji dira, au falsafa, ya maendeleo ili kuwezesha uratibu wa mipango, mikakati na sera katika mwelekeo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii utakaopelekea kujenga jamii mpya inayotazamiwa na umma, au ideal society kwa kimombo.
Historia inatufundisha kwamba tangu kuibuka kwa dola za kisasa, hususani jamhuri, tangu mwishoni mwa karne ya 18, nchi nyingi zilizofanikiwa kujikomboa kutoka hali duni ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ni zile ambazo mipango na mikakati yao ilijidhatiti katika falsafa fulani ya maendeleo iliyoeleweka kwa umma.
Licha ya migongano na misuguano inayotokana na mahusiano ya kijamii-uchumi, mataifa hayo yaliyojikomboa katika hali duni na unyonge yameweza kudumisha hali ya utaifa wao na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika uzalishaji mali na kutanua wigo wa fursa na uwezekano wa kuboresha hali za maisha ya mwananchi mmoja mmoja.
Marekani, China
Chukulia mfano taifa la Marekani, nchi ambayo imekuwa ikitolewa sana mfano na wasomi na wanasiasa wetu wengi wa sasa, ambayo nayo inayo falsafa ya maendeleo iliyoongoza mafanikio yake kwa takribani karne mbili.
Si lengo lango kujadili kwa undani falsafa yao ya maendeleo, lakini ieleweke kwamba msingi mkubwa wa falsafa ya maendeleo ya Marekani tuionayo leo imejengeka juu ya mawazo na mijadala ya Alexander Hamilton na Thomas Jefferson, moja ya waasisi wa taifa hilo, baada ya mapinduzi ya taifa hilo ya kibwanyenye ya kati ya mwaka 1775 na mwaka 1783.
SOMA ZAIDI: Haya Ndiyo Yaliyofanya Dira ya Taifa ya 2025 Isifanikiwe Kikamilifu. Mchakato wa Dira ya 2050 Waanza
Tuchukulie mfano mwingine wa China, dola lililokuwa na historia kubwa ya ustarabu wa binadamu, baada ya kupitia hali ya muda mrefu ya utengano na kudhalilishwa kutokana na uvamizi wa mataifa ya Ulaya, ilibadili gia ya mwendo wa kimaendelo kuanzia mwaka 1949.
Tangu wakati huo hadi hii leo, China, chini ya falsafa ya maendeleo yao wenyewe, ambayo inaeleweka vema kwa umma, na hasa kundi la tabaka tawala, wameweza kufanya maajabu makubwa sana katika historia ya binadamu kwa kuwaondoa mamilioni ya wananchi wake katika lindi la umasikini ndani ya kipindi kifupi.
Hivyo basi, kwa taifa lolote makini linalotaka kutoka katika hatua moja kwenda hatua nyingine, ili liweze kufanikiwa linahitaji kuwa na dira, au falsafa, ya maendeleo inayoeleweka, vinginevyo jitihada zozote zitakazofanyika bila ya dira fasaha haziwezi kuleta matokeo kama ilivyokusudiwa.
Tunajenga taifa la namna gani?
Sasa, mwaka huu wa 2024 inatimia miaka 60 tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukiwa katika mchakato wa kutengeneza dira mpya ya taifa ya maendeleo kama tulivyotangaziwa, swali linalopaswa kutuongoza katika mchakato huu linatakiwa kuwa tunataka kujenga nchi ya namna gani?
Ni jamii ya namna gani tuitakayo kuishi sisi tuliopo leo na tungependa vizazi vijavyo navyo viishi?
SOMA ZAIDI: Wadau wa Elimu Wahoji Ukimya wa Dira ya Taifa Katika Kutambua Nafasi ya Kiswahili Kwenye Elimu
Swali hili ni muhimu, na linatakiwa kujibiwa na dira, au falsafa, ya maendeleo ya taifa kwa kuwa jamii tuitakayo ndiyo chachu ya matumaini ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa lao.
Ni ngumu sana kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye juhudi za maendeleo ya taifa kama hakutakuwepo na tumaini linaloeleweka kwao vizuri.
Tanzania hivi sasa tunacho kitu kinachoitwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 ambayo kipindi chake kinaisha mwakani ambayo mchakato wake wa kuiandika ulianza mwaka 1995 na utekelezaji wake ukaanza mwaka 2000.
Leo hii ukiwauliza Watanzania, au kundi la tabaka tawala, juu ya dira yetu, au falsafa yetu, ya maendeleo tuliyonayo sasa lengo lake ni kujenga jamii ya namna gani, kwa uzoefu wangu wa kufuatilia mijadala ya maendeleo, sidhani kama utaweza kupata jibu moja linaloeleweka.
Dira ijitafsiri
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, kwa kiwango kikubwa, haikuweza kujitafsiri kwa wananchi na haikuweza kueleweka kwa wananchi kama ilivyokuwa kwa tunayoweza kuiita dira ya kwanza ya taifa hili ambayo ilikuwa kujenga nchi ya Ujamaa na Kujitegemea.
SOMA ZAIDI: Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti
Dira hii ya sasa inayoisha mwakani, 2025, kwa mtazamo wangu, iliandikwa kama mpango wa mendeleo wa taifa wa miaka 25, haikutupa kwa ufasaha falsafa yetu ya maendeleo hasa ni ipi na jamii itamaniwayo na Watanzania ni ipi.
Makosa haya hatupaswi kuyarudia tunapoelekea kuunda dira mpya ya maendeleo hapo mwakani. Pamoja na jitihada zinazofanywa hivi sasa za kupata maoni ya kila mwananchi, ni muhimu sana kuhakikisha inafanyika mijadala ya kina ambayo mwisho wa siku itatupa dira na falsafa ya maendeleo itakayoeleweka kwa umma.
Mchakato huu wa kuandika dira usihamasishwe katika namna ya kwamba tupo kwenye mchakato wa kuunda mpango wa maendeleo. Tunahitaji kuwa na dira, au falasafa, ya maendeleo kwanza ndiyo tupate mipango ya maendeleo ya muda mrefu na mifupi itakayoakisi dira hiyo.
Joel Ntile ni mwanamajumui wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @JoelNtile. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.