Tujipongeze, nchi yetu Tanzania imetimiza miaka 60 ya Muungano wake. Kwa kifupi tu ni kuwa Muungano huu ni wa kihistoria na umebaki kuwa Muungano pekee uliobaki kwa mtazamo wa vuguvugu la msukumo wa mawazo ya umajumui wa Afrika.
Tukiwa tunasherehekea Muungano huu leo Aprili 26, 2024, ningependa kuungana na wengine wanaojadili kuhusu hatma ya tukio hilo la kihistoria, nikifanya hivyo kwa kudurusu andiko la mwanamapinduzi wa Kitanzania, Abdulrahman Mohamed Babu, andiko ambalo, kwa maoni yangu, na kwa hakika, linapaswa kutufikirisha, na pengine kufanyiwa kazi na viongozi wa kizazi cha sasa ili kukamilisha ndoto, na maono, ya Muungano wetu huu.
Kwanza, yeye Babu ni nani? Kwa kizazi cha sasa, huyu ni mwanamapinduzi, Mzanzibari, mwanamajumui wa Afrika, msoshalisti, aliyewahi kuhudumu kama waziri kwenye Serikali ya awamu ya kwanza, aliyewahi kuwekwa kizuizini bila kusomewa mashtaka, na kuja kuielezea athari mbaya ya sheria hiyo.
Alipoachiwa huru, Babu akaenda kuishi ughaibuni ambapo, akiwa huko, akafanya kazi ya ualimu vyuo vikuu kadhaa na kama mwanafalsafa, na mwana-insha, aliyekuwa anaandika makala kila mwezi kupitia majarida ya Africa Now na Africa Event, na kutoa mawazo yake ya kiuchambuzi mahiri kuhusu mustakabali wa Afrika yetu kuanzia miaka ya 1980 mpaka 1990, kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Babu pia anatambulika kama mwanazuoni aliyeandika utangulizi kwenye chapa ya kwanza ya moja kati ya vitabu bora kuwahi kuandikwa kuhusu Afrika, kile cha How Europe Underveloped Africa, kilichoandikwa na mwanazuoni wa Kiguyana, Walter Rodney.
SOMA ZAIDI: Je, Zanzibar Inaweza Kuwa na ‘Mamlaka Kamili’ Ndani ya Jamhuri ya Muungano?
Babu, aliyefariki Septemba 5, 1996, London, Uingereza, aliishi ukimbizini barani Ulaya na Marekani, akifundisha, kama nilivyodokeza hapo juu, katika vyuo vikuu kadhaa.
Moja kati ya kazi zake za kiuwanazuoni zinazojulikana sana ni pamoja na kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1981, African Socialism or Socialist Africa?, kinachochambua, pamoja na mambo mengine, utegemezi kwa mfumo wa kibepari kwa mataifa mengi ya Afrika yaliyotoka kupata uhuru.
Babu, ambaye alitoa mchango mkubwa kwenye Mapinduzi ya Zanzibar ya Januar 12, 1964, alwahi kupewa udokta, siyo wa PhD, bali kwa mchango wake na mawazo yake, kama mwanafikra mahiri.
Mwanamapinduzi huyo, aliyekuwa swahiba wa karibu na mwanaharakati wa haki za binadamu wa Kimarekani, Malcolm X, ni moja kati ya wanazuoni wa kwanza wa Kiafrika walioona haja ya bara la Afrika kufanya mapinduzi kwa kujifunza kutoka kwa nchi za Mashariki mwa dunia, ikiwemo China na iliyokuwa Umoja wa Kisovyeti.
Abdulrahman Mohamed Babu akiwa na mwanaharakati wa haki za watu weusi, Malcom X, miaka ya 1960.
Itoshe tu kusema kwamba Babu ni jina kubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla, akitambuliwa na kuheshimiwa kwa mchango wake mkubwa katika kuchagiza fikra za ukombozi wa Afrika na wa mwanadamu kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: Jinsi Sakata la Ndizi Kuzuiliwa Kuingia Zanzibar Lilivyoibua Mjadala wa Muungano
Yeye ni mtu niliyevutiwa sana na mawazo yake kwa kusoma machapisho yake, na nafurahi kwamba katika uhai wake niliwahi kukutana naye, kwanza nchini Uganda, kisha hapa Tanzania.
Upekee, na nadhani umuhimu, wa Babu ni kwamba, ukimlinganisha na wenzake wa zama zake, ambao wengine walikuwa makamaradi wake wa siku nyingi, alikuwa na uwezo wa kuwakosoa watu hao pale walipokuwepo madarakani, kwa ujasiri na ukweli usiyokifani. Kingine muhimu n kwamba hakuna aliyeweza kumshutumu Babu kuwa wakala wa mabeberu, wengi wao wakiuchukulia ukosoaji wake kama mahiri na wa dhati.
Mkwamo wa Kaunda
Sasa, katika moja ya maandishi yake, Babu aliwahi kuchambua mkwamo, au njia panda, aliokutana nao Rais wa kwanza wa Zambia, Keneth Kaunda, ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu toka enzi ya kikao cha uanzishwaji wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika kwa nchi za Mashariki na Kati mwa Afrika (PAFMECA), kilichofanyika mwaka 1958, kwenye maktaba kongwe ya mji wa Mwanza.
Mwandishi wa makala haya akiwa katika ukumbi ulipofanyika mkutano wa PAFMECA Mwanza mwaka 1958.
Mkwamo huu ulihusu swali walilokuwa nalo wale waliokuwa na nia haswa ya kujiunga na Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar, lakini hawakuwa wanajua wanaweza kujiunga vipi na Muungano huo.
Kwa mfano, muundo wetu wa Muungano ni wa Serikali mbili, ya Jamhuri na ile ya Zanzibar, sasa nchi kama Zambia, ikitaka kujiunga kwenye Muungano huo, katika muktadha wa umajumui wa Afrika, itaingilia wapi?
SOMA ZAIDI: Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano
Je, Muungano wetu, ambao sasa unatimiza utu uzima wa miaka sitini, bado ni kitovu, au nucleus, ya muungano wa Africa? Hili ni swali muhimu kwa sababu hivi ndivyo tulivyoambiwa na kufundishwa sisi wazee wa leo wakati tukiwa watoto na vijana miaka ya 1960 na 1970.
Tuliwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili kumulika Afrika nzima. Kwa sasa ni muungano pekee uliobaki kwa mawazo yale ya umajumui wa Afrika, hali inayoufanya Muungano wetu kuwa mfano wa kuigwa na wengine ili kuendeleza mawazo na fikra hizo.
Mafunzo
Moja kati ya somo muhimu tunaloweza kuvuna kutoka kwenye historia hii ya miongo sita ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kwamba kumbe yawezekana Waafrika kuunda na kuudumisha muungano wao kitaasisi. Wetu umedumu, hicho ni cha kujipongeza na kujivunia. Huu, unaweza kusema, ndiyo uimara wa Muungano wetu.
Lakini kuna maswali kama hayo ya je, kwa mfano, upo uwezekano, na miundombinu, wa mtu wa tatu kujiunga na Muungano wetu huu? Nionavyo mimi hakuna. Hii ni kasoro ya kimuundo, na hivyo tunaweza kusema kwamba huu ndiyo udhaifu wa Muungano wetu huu.
Babu aliwahi kuandika kwamba Kaunda alitaka sana kujiunga na Muungano huu lakini angeichomeka wapi Zambia? Na baada ya ukombozi wa Msumbiji na wengineo, mbona na hao pia hawakujiunga? Unaweza kusema kwamba hii ni fursa iliyopotea.
SOMA ZAIDI: Nini Hasa Kilipelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
Rafiki yangu mmoja kutokana nchini Uganda, Dk Vukoni Lupa Lasaga, aliwahi kuniuliza, kifalsafa, kwa nini Mwalimu Nyerere alisita kuwa Mao Zedong wa Africa wakati tayari kwa ushawishi wake alishakuwa hivyo?
Pengine tungekuwa tayari tupo ndani ya muungano ambao nchi zingine zaidi, pengine tano, zingekuwa nasi. Ni vigumu kufikiri kuwa Samora Machel wa Msumbiji, Agostinho Neto wa Angola, Robert Mugabe wa Zimbabwe, Sam Nujoma wa Namibia, na Joseph Kabila wa DRC wasingekubali kujiunga na Muungano wetu.
Mfano wa kuigwa?
Hali ni tofauti kwengineko ambako miungano imefanyika. Katiba ya Marekani, kwa mfano, ina kifungu kinachoweka utaratibu wa nchi nyingine kujiunga na umoja huo wa mataifa 50 hivi sasa, kazi ambayo imekabidhiwa kwa Bunge la nchi hiyo. Nyerere alipenda kuwaita Wamarekani kama “marafiki zangu.” Je, tunaweza kuchukua kizuri hicho kutoka kwao?
Hapo juu umeona nikigusia uimara, udhaifu na fursa zilizopo kwa Muungano wetu. Lakini kuna tishio pia, na tishio lenyewe ni ukweli kwamba kama Muungano huu utaendelea kubaki na muundo huuhuu, basi kuna hatari ya kuvia.
Hiyo itakuwa ni bahati mbaya kwa sababu lengo la awali, kama kumbukumbu kutoka kwenye vikao vya PAFMECA zinavyoonesha, Muungano huu haukukusudiwa kuwa wa nchi mbili, bali mataifa yote yaliyoko kusini mwa Afrka, au yale yaliyo kusini mwa Jangwa la Sahara, au Afrika nzima.
SOMA ZAIDI: ‘Njia Bora ya Kutatua Kero za Muungano ni Kufufua Mchakato wa Katiba Mpya’
Ni rai yangu, leo hii tukiadhimisha miaka 60 ya Muungano, kwamba tufanye linalowezekana kulitimiza lengo hili. Wito huu nauelekeza kwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar, na kuwasihi watatue kasoro hii ya Muungano, hatua ambayo, kwa maoni yangu, itawasaidia kuweka alama kubwa za uongozi wao miongoni mwa watu wa Afrika.
Sehemu ya kuanzia inaweza ikawa ni marekebisho ya Katiba yetu ili iweke utaratibu ambao nchi nyingine ikitaka kujiunga na Muungano wetu iweze kuufuata.
Kitu kuwa wazo zuri, au wazo jema, peke yake haitoshi, yabidi kupiga debe la ushawishi ili watu wengi zaidi wajiunge nacho na kuwa na utaratibu utakaowawezesha kufanya hivyo. Lazima, kwa wazo hili la Muungano, kama ni wazo jema, kushawishi wengine nao wajiunge.
Heri ya Sikukuu ya Muungano!
Nsajigwa Nsa’sam Mwasokwa ni mwanafikra huru kutoka Mbeya, Tanzana. Kwa mrejesho, anapatikana kupita nsajigo60@gmail.com au +255 767 437 643. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.