The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kirumba, Mwanza: Biashara ya Ngono Yafanyika Katika Eneo la Shule ya Msingi, Mabaki ya Kondomu Yazagaa

Katika uchunguzi uliofanywa na The Chanzo kwa siku tofauti uwanjani hapo majira ya asubuhi iligundua kuzagaa kwa kondomu zilizotumika katika maeneo mbalimbali kando ya uwanja huo ikiwemo viunga vya shule za msingi Kitangiri.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Ni jambo ambalo halikutarajiwa na wengi na isivyo bahati, uwe mgeni ama mwenyeji hapa mjini Mwanza ukipita pembezoni mwa mazingira ya shule za msingi Kitangiri A na C zilizopo pembezoni mwa uwanja wa CCM Kirumba kuanzia majira ya saa moja jioni utakutana na makundi ya wanawake wanaofanya biashara ya ngono.

Wakazi wa eneo hili wamechoshwa na hali hii kwani licha ya wao kuona ni kinyume na maadili, vitendo hivi vinavyofanyika kwenye eneo la shule wanaona ni jambo la hatari kwa afya na malezi ya watoto.

Mariam James, 28, mama wa watoto wawili na mmiliki wa mgahawa eneo la uwanja wa CCM Kirumba yeye anadai kuwa watoto wake wanaosoma shuleni hapo na anaona wapo kwenye hatari ya kukumbana na magonjwa kwani inapofika asubuhi mabaki ya kondomu hutapakaa kwenye viwanja vya shule.

“Wale ni wadogo, hawezi kuelewa wanaweza kuokota na kuanza kuchezea, hapo ndio utakuwa mwanzo wa kupata maambuzi ya ajabu ajabu,” anasema Mariam, “ Siyo suala zuri hata kidogo, Serikali iliangalie kwa upana wake.”

Mariam anaamini  kuwepo shughuli hizo kwenye eneo la makazi na shule kunapelekea kuwaweka kwenye hatari kubwa wasichana wadogo ya kujiingiza kwenye biashara ya ngono kwa kuwa itafika kipindi itaanza kuonekana ni jambo la kawaida.

SOMA ZAIDI: Aliyemwingilia Shemeji Yake Kwa Madai ya Kumpa Dawa ya Utasa Jela Miaka 30

Jumanne ya Aprili 23, 2024, Mbunge wa Ilemela Dkt Angelina Mabula alilifikisha suala hili bungeni na kuitaka Serikali kujenga uzio katika Shule hizo ili kuokoa maisha ya watoto ambao wanachezea kondomu zilizotumika na kutupwa katika eneo la shule.

Mbunge huyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi alisema kuwa eneo hilo lenye shule mbili pamoja limekuwa likitumika vibaya na wanawake wanaojiuza.

“Ni lini serikali itaweka uzio katika shule hizi ili kuokoa maisha ya watoto ambao wanachezea mipira (kondomu)? “ Alihoji Dkt Mabula.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilemela kutembelea shule hiyo na kufanya tathimini ya hali ilivyo.

Mohammed Ramadhani ambaye pia ni mkazi wa Kirumba anaamini kuweka uzio sio mwarobaini wa changamoto wanayokumbata nayo wakazi wa eneo hilo kwa kuwa uzio utaleta ahueni kwa shule tu na sio wakazi wote. 

“Uzio utazuia tu pale shuleni, lakini wanafunzi watatoka watapita kwenye mazingira ya jirani, wataona ile mipira, watakanyaga. Unadhani hapo watakuwa wamesaidia kitu?” Anasema Mohammed.

Mkazi huyu wa Kirumba na dereva bodaboda anadai kuwa Serikali inafanya uzembe kulishughulikia suala hili kwani athari zake ni kubwa ambazo hawawezi kuziona kwa sasa lakini kwa baadaye tatizo litakuwa kubwa sana. 

Licha ya shule hizi kuwa na walinzi lakini bado vitendo hivi vinaendelea huku uongozi wa shule, bodi ya shule na uongozi wa Serikali ya Mtaa umekuwa ukifumbia macho kwa muda vitendo mrefu hivyo katika mazingira ya shule.

“Kuna wakati ukipita pale Serikali wakichachamaa hukuti mtu kabisa, kweupe. Lakini wanachachamaa kwa muda tu halafu wanaishiwa makali, mimi nina uhakika hili jambo linaweza kumalizwa kabisa iwapo Serikali ikalivalia njunga”, aliongeza.

Katika uchunguzi uliofanywa na The Chanzo kwa siku tofauti uwanjani hapo majira ya asubuhi iligundua kuzagaa kwa kondomu zilizotumika katika maeneo mbalimbali kando ya uwanja huo ikiwemo viunga vya shule za msingi Kitangiri. 

Wakati The Chanzo ilipotembelea maeneo hayo majira ya usiku iligundua kuwepo kwa wanawake  wasiopungua 100 wanaojiuza mahali hapo.Uchunguzi pia umebaini kuwa wengi wanaojiuza ni kuanzia umri wa miaka 17 hadi 50 wakiwa wanajipanga kando na jengo la uwanja  ili kutega wateja. 

Na mara baada ya kupata wateja, wale ambao hawamudu kukodisha vyumba kwenye nyumba za wageni hulazimika kutafuta maeneo ya kificho ambapo ndipo wengine huingia katika maeneo ya shule.

“Hapa wanagawana, unawaona hao, hao ni wa elfu mbili kuanzia kwenye mlango huu hadi mlango huu hapa. Sasa kuanzia hapo kwenda hivi utawapata wa elfu tatu na kule mwisho ni wa elfu tano. Yaani huu uwanja wamegawana vilivyo na hawana aibu kabisa”. Alieleza mmoja wa vijana ambao The Chanzo ilimkuta eneo hilo akiomba jina lake lisitajwe.

SOMA ZAIDI: Kumi na Tatu Wakamatwa Kwa Udhalilishaji wa Watoto Wa Kiume Zanzibar

“Kiukweli ni dada zetu ila wanakera, hawa hapa ndio huwa wanaenda kumalizana na wateja wao kule kwenye uwanja wa shule na vyoo hivyo hapo vya shuleni,” aliongeza.

Juhudi za jeshi la Polisi

Kutokana na malalamiko hayo ya baadhi ya wananchi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa aliieleza The Chanzo kuwa Jeshi la Polisi Mwanza wanatambua na wanafahamu kuwepo kwa malalamiko ya watu kugeuza maeneo ya uwanja huo kuwa kama danguro.

“Ni kweli tunakiri kupokea malalamiko ya baadhi ya wakazi wa maeneo kuwa wanawake baadhi kujihusisha na vitendo vya ukahaba, kujiuza katika eneo hilo. Kwa ujumla wake vitendo hivyo siyo vizuri kimaadili,” alieleza  Mutafungwa.

Mtafungwa anaendelea kufafanua: “Wakati mwingine vitendo hivyo vimekuwa vikichochea uhalifu, wakati mwingine wanawake hao wanafanya vitendo hivyo wakiwa wamejipanga kuwapora hao wanaume wanakubaliana nao, pia hivyo hivyo kuna wanaume wao wanaenda kwa lengo la kuwafanyia uhalifu wale wanawake.” 

Mutafungwa alieleza kuwa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza wamekuwa wakifanya doria na msako kwenye maeneo hayo na kuwakamata wanawake wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafIkisha mahakamani.

Jeshi la Polisi limesema kuwa kwa mwezi wa nne peke yake mwaka 2024 waliwakamata wanawake 18 na kuwafikisha mahaka ya wilaya ya Ilemela, lakini bado tatizo limekuwa likiendelea maana wanawake hao wanapoachiwa hurudi tena kuendelea na biashara hiyo.

Katika orodha ya wanawake 18 waliokamatwa na Jeshi la Polisi mwaka 2023  The Chanzo ilibahatika kupata nakala ya kesi inaonyesha kuwa wanawake hao ni kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya mji wa mwanza.

Pamoja na juhudi hizo, Mutafungwa aliieleza The Chanzo kuwa tataizo hilo haliwezi kumalizwa na Polisi peke yako bali jamii kwa ujumla.

Kuna watu wamelikombatia suala hili?

Wesa Juma ni diwani wa kata ya Kirumba, aliiambia The Chanzo kuwa jambo hili ni kero na yeye kama mwathirika mkuu anadai kuwa limefikishwa Baraza la Madiwani mara kadhaa lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.

“Hili tumeliongea mara kadhaa kwenye Baraza la Madiwani,” amesema Wesa, “Mabula alikuwa na halali ya kulifikisha bungeni” 

SOMA ZAIDI: Mtanzania Akamatwa Malaysia Akidaiwa Kuwaingiza Wenzake Kwenye Ukahaba

“Kuna kukosekana nguvu ya pamoja, hili linaisha kabisa japo linaweza lisiwe la usiku mmoja. Kuna kipindi wakati wa sherehe za Mei Mosi, walikaa wanajeshi wanne tu, hapa wawili na kule juu wawili, hapakuwa na mwanamke aliyeonekana hapa” aliongeza.

The Chanzo ilimtafuta pia Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza ambao ni wamiliki wa uwanja wa CCM Kirumba, ndugu Omary Mtuwa ili kujua iwapo wanaijua kero hii.

Katika mazungumzo yake na The Chanzo alifafanua kuwa wana taarifa ya kuwepo kwa kero hiyo katika eneo la uwanja huo na kama wamiliki wana mpango wa kuweka taa nje na ndani ya uwanja ili kuwepo na mwanga kuzuia watu wanaotumia giza kujificha kufanya biashara hizo.

“Tulifanya ziara pale usiku kama mara mbili hivi ili kuweza kujua kinachopelekea wao kufanyia matendo yao pale. Chama kinachukua hatua na wakati wowote utaona taa hapo taa zitawekwa , ndani ya mwezi mmoja utaona taa ziko pale.” 

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *