The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuongeza Ubora wa Elimu Inayotolewa Tanzania

Ni vyema tukafahamu kwamba hatima zetu zipo juu ya mikono yetu wenyewe, na kwamba elimu bora ndiyo itakayotufikisha kwenye nchi ya ahadi.

subscribe to our newsletter!

Mtakubaliana na mimi kwamba malengo makuu ya elimu, duniani kote, ni kuandaa rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo yao binafsi, lakini, zaidi, kwa ajili ya maendeleo ya taifa lao kwa ujumla.

Kazi kubwa ya elimu ni kuwajengea uwezo wanafunzi na kuwafungua fikra kiasi cha kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha. Lengo la elimu siyo tu kuzalisha watu waliosoma, au wasomi, na kufaulu kwa viwango vya juu. 

Elimu pia inapaswa kuzalisha watu wenye ujuzi na maarifa makubwa yatakayokuwa msaada kwa ukuaji wa taifa kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kuwa na taasisi na mamlaka za elimu zinazotimiza majukumu yao ipasavyo ni takwa la msingi kabisa na la lazima kwa taifa lolote linalohitaji maendeleo madhubuti.

Kila nchi inatoa elimu kwa wananchi wake, lakini si kila taifa hutoa elimu bora. Nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania kwa miaka mingi, zinatoa elimu isiyo na ubora na kupelekea kupata wataalamu wengi wasio na uwezo kabisa, ama wenye uwezo mdogo. Wengi watakua wanajiuliza, kwani elimu bora ni ipi haswa?

Kwa mtazamo wangu, elimu bora hupimwa kwa kiwango chake cha uhalisia ilichobeba; elimu bora lazima ibebe kiwango kikubwa, kama si chote, cha uhalisia wa maisha ya watu wake.

Elimu bora

Elimu bora huwafundisha watu wake historia ya kweli ya taifa lao na siyo historia bandia; huwapa habari za mashujaa wao wa kweli na kuwapandikiza ushujaa huo. Elimu bora huwaonesha, na kuwasaidia, wanafunzi kufahamu misingi ya jamii yao na tamaduni zinazowatofautisha wao na wengine.

SOMA ZAIDI: Uchambuzi wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kwa Mwaka 2024/25

Elimu bora huwaambia ukweli wanafunzi kuhusu hali ya taifa lao kisiasa na kiuchumi na kuwapandikiza ari ya upambanaji kwa ajili ya kuleta mabadiliko. Elimu bora huwaonesha wanafunzi aina ya taifa nchi husika inalolihitaji, na kuwaonesha njia za kupita ili kufika huko.

Elimu bora hujikita kuwafundisha wanafunzi juzi mbalimbali zitakazowawezesha kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, au taifa, husika. Kwa mfano, kama kwenye taifa husika kuna tatizo la magonjwa, elimu bora itajikita kufundisha watu wake namna ya kutengeneza tiba sahihi na baadaye kinga ya kuzuia magonjwa hayo.

Hiyo itapunguza, kama siyo kumaliza, vifo vitokanavyo na magonjwa husika na zitakazobakia watauza kwa mataifa mengine ambapo hiyo itakuza uchumi wa nchi na kuongeza pesa za kigeni nchini.

Elimu bora hujikita kufundisha wananchi wake namna bora zaidi ya kutumia rasilimali zilizopo kwenye jamii, au taifa, husika kwa faida yao na jamii, au taifa, nzima. 

Mfano, kama kwenye jamii husika kuna madini, wanafunzi watafundishwa namna bora ya kuyatumia madini hayo kwa faida yao na ya taifa zima; watafundishwa namna ya kufanya biashara ya madini na namna ya kuchakata madini kuwa bidhaa.

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Elimu ya Afrika, ikiwepo Tanzania, imejikita kwenye ufundishaji kwa njia ya nadharia – kusoma, kuona picha, kukariri, na kadhalika –ambapo imetupatia wataalamu wengi wasio na uwezo na ushindani mdogo kwenye soko la ajira, tofauti na mataifa ya wenzetu ambayo wanafunzi husoma kwa vitendo na kuona zaidi.

Rasilimali nyingi

Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache yaliyobarikiwa rasilimali nyingi, lakini ajabu kwenye mfumo wa elimu, hususan shule, wanafunzi hawafundishwi namna ya kuzitumia kwa faida yao na ya taifa kwa ujumla; ni ajabu sana kuona kwamba tunazalisha wataalamu wengi ambao hata sisi wenyewe hatuwezi kuwatumia!

Elimu yetu imekua ikifundisha wanafunzi vitu vingi visivyo na maana na kuacha vile vyenye maana. Fikra zangu mara nyingi zimekuwa zikiniambia pengine elimu hii ilikua na manufaa makubwa miaka ya nyuma, na siyo katika miaka hii.

Kwa nini hatutaki kubadilika? Kwa nini tunawafundisha wanafunzi vitu tusivyovihitaji? Tunawafundisha kwa manufaa ya kina nani? Kwa mfano, ni kwa nini unazalisha wakandarasi halafu zabuni za mabarabara unawapa Wachina au wageni wengine?

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuja na wazo zuri kwenye mitaala ya amali, lakini swali ni je, tumejipanga vya kutosha kuhakikisha inatekelezeka na kuleta matokeo tarajiwa? 

Kwa akili yangu ndogo ya miaka 19 ya kuzaliwa, naona kabisa kwamba kwa hili Serikali imekurupuka na kwamba sioni ikileta yale matokeo ambayo wengi tunayatamani.

SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi

Kwa nini? Kwa sababu kwanza kwenye mchakato wa mabadiliko hayo wananchi, ambao ndiyo walengwa, hawakushirikishwa vya kutosha. Wananchi wanapaswa kuulizwa aina ya elimu wanayoitaka wenyewe ili ilete manufaa kwao na siyo viongozi kukaa na kuwapangia wanayoitaka wao.

Ni vyema kama taifa tukakaa chini na kujadili aina ya elimu tunayoihitaji, itakayokidhi matakwa ya wananchi wa taifa hili na vizazi vyao; ni vyema tukafahamu kwamba hatima zetu zipo juu ya mikono yetu wenyewe, na kwamba elimu bora ndiyo itakayotufikisha kwenye nchi ya ahadi. 

Mabadiliko hayajawahi kuwa kitu kirahisi rahisi; mabadiliko ni vita kubwa ambayo inabidi tukubali kuipigana kwa ajili ya vizazi vyetu, vya sasa na vijavyo.
Brayan Silayo ni mdau wa elimu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia brayansilayo14@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. “Ni vyema kama Taifa tukakaa chini na kujadili aina ya elimu tunayoihitaji,itakayokidhi matakwa ya wananchi wa Taifa hili na vizazi vyao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *