The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Hatari Kwa Nchi Kuwa na Vijana Wanaodhani Wanaweza Kuishi kwa Kusifia Wengine Badala ya Kufanya Kazi

Tusikubali kamwe kujenga taifa la vijana wavivu wa kufikiri na kutenda wanaotegemea kusifia ili wapate kula.

subscribe to our newsletter!

Miaka ya nyuma kidogo, chawa walijulikana kama wadudu waharibifu, na mara walipoweka makazi yao kwenye nguo ya mtu, mtu huyo alifanya haraka sana kumwondoa. Kwa lugha rahisi, chawa walikua ni uchafu, na binadamu hakuwa na matumizi nao. Lakini katika karne hii ya 21, chawa wamekua si uchafu tena, bali viumbe muhimu sana kwenye maisha.

Vijana wengi, baadhi yao hujita wasomi, ndiyo wamekuwa chawa wakubwa kwa watawala ili waweze kutimiza haja zao. Ilianza enzi zile za profesa mmoja wa chuo kikuu aliyemshukuru rais kwa kumtoa ‘jalalani’ na kumteua waziri. Profesa huyu alizidiwa na mihemko kiasi kwamba alimwita bosi wake ‘Mheshimiwa Mungu.’ Hivi juzi, nimemwona chawa mmoja akimuweka kwenye kundi la utukufu Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Yesu Kristo na Mtume Muhammad!

Sina maana ya kuwakataza kusifia pale mnapojisikia kufanya hivo, ila Wazungu wana msemo usemao, Too much is harmfull, ambao tumeutafsiri kwenda Kiswahili kama Sana ikizidi sana, si nzuri sana. Ndiyo, chochote, hata kama ni kizuri kiasi gani, kikizidi huchukiza, kukera, na kugeuka kuwa madhara.

Hata hivyo, mimi wala sina shida na hawa wasifiaji, bali wale wanaosifiwa. Niliwahi kusikia kwamba Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa Tanzania, aliwahi kukataa waziwazi kusifiwa, akijua kwamba ni sumu kubwa kwenye utawala wake. Je, hawa watawala wa leo, hawaoni shida kusifiwa? Je, hawaoni kwamba wanajitengenezea laana kukubali kufananishwa hadi na mitume?

Nilitegemea kwamba wangekuwa watu wa kwanza kutoka hadharani na kulikemea hili, lakini imekua tofauti. Tena nasikia kwamba wapo baadhi wanawalipa hao chawa ili washinde kutwa kuwasifia.

Tunajenga taifa gani?

Kabla ya kuwaza kuleta maendeleo, ni sharti tujiulize kwanza tunataka kujenga taifa la namna gani? Je, litafananaje? Je, watu wake wawe na sifa zipi? Je, wafanye nini na kwa kiwango gani?

SOMA ZAIDI: Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuongeza Ubora wa Elimu Inayotolewa Tanzania

Tusikubali kamwe kujenga taifa la vijana wavivu wa kufikiri na kutenda wanaotegemea kusifia ili wapate kula. Tujenge taifa la vijana wakorofi na wadadisi kama alivyotaka Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere; taifa ambalo watu wake wanauelewa wajibu wao na kuutimiza bila ya kukumbushwa.

Tujenge taifa ambalo viongozi watatuongoza na siyo kugeuka kuwa watawala na miungu watu; taifa ambalo viongozi watajali maslahi ya wananchi wake na siyo kuwadhihaki kama wanavyofanya sasa.

Tujenge taifa la watu imara na jasiri wanaoweza kudai haki zao pale zinapokandamizwa na watawala na siyo kukaa na kulalamika vijiweni. Tujenge taifa ambalo wananchi wote, pamoja na watawala, wanaelewa kwamba haki ndiyo msingi wa nchi yenye amani na maendeleo.

Tujenge taifa ambalo upinzani hautoonekana uadui mbele ya macho ya watawala; taifa ambalo watu wema mithili ya Godlisten Malisa hawatateswa na kuonewa na wasio na haki kwa kutumia mgongo wa Jeshi la Polisi.

Tujenge taifa ambalo viongozi wetu watakua na uthubutu na ujasiri wa kukemea wizi, rushwa na ubadhirifu wa vigogo Serikalini hadharani. Tujenge taifa ambalo fursa zitagawiwa kwa watu wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, hali zao za elimu, kijamii, na kadhalika.

SOMA ZAIDI: Watanzania Tupo Kwenye Hali Nyerere Alitutahadharisha Nayo: Utii Ukizidi Unakuwa Woga, na Uoga Huzaa Unafiki na Kujipendeza

Tujenge taifa lenye mifumo huru ya kiuendeshaji wa taasisi. Tuwe na vyombo huru vya dola visivyoingiliana. Tuwe na Bunge huru linalotetea maslahi ya wananchi, na siyo maslahi ya Serikali, Bunge ambalo litapitisha sharia zisizo kandamizi kwa wananchi, Bunge ambalo halitapitisha mkataba wa kuuza rasilimali za nchi kwa kumwogopa Rais.

Tuwe na Mahakama huru isiyo na ubia wowote na Serikali wala Bunge. Mahakama yenye uwezo wa kumwajibisha Rais na Spika pale wanapokosa. Mahakama ambayo itaweza kutengua matokeo ya uchaguzi pale itakapotakiwa kufanya hivo.

Mahakama ambayo jaji wake hapatikani kwa huruma ya Rais wala Serikali. Mahakama ambayo haitegemei fedha za kupiga magoti wizarani kujiendesha. Mahakama ambayo ina uwezo wa kumwajibisha na kumhukumu kiongozi yoyote wa umma bila ya kumwonea haya. Tupate Mahakama ambayo maskini atapata haki yake mbele ya mwenyenacho.

Tupate Tume ya Uchaguzi iliyo huru, siyo kwa jina, bali katika muundo wake wa kiuendeshaji. Tume yenye uwezo wa kumtangaza mshindi halali bila kujali itikadi ya chama chake. Tume ambayo Rais hawezi kuamka na kuwafukuza kazi kwa utashi wake.

Tupate mifumo bora ya elimu itakayotuzalia viongozi bora na wawajibikaji, elimu itakayowapa vijana wetu ujuzi na maarifa itakayowatoa kwenye utegemezi.

Tukemee ukatili

Tujenge taifa la watu wenye ujasiri wa kukemea ukatili bila ya kujali nani na wapi unapofanyika ukatili huo. Tuungane pamoja kuwatetea ndugu zetu Wamasai ambao wanalalamika kufukuzwa kwenye makazi yao huko Serengeti na Ngorororo. Tusimame pamoja kutetea ndugu zetu wanaopotea kila leo na kupatikana wakiwa wamefariki.

SOMA ZAIDI: Tutawezaje Kubuni Katika Mazingira ya Uhuru wa Mashaka?

Tusimame pamoja kuwatetea vijana ambao wamekumbwa na msongo wa mawazo kwa kukosa ajira. Kukaa bila kazi ni ukatili ambao vijana wanafanyiwa na Serikali.

Tusimame pamoja kama taifa na kutoa kauli moja dhidi ya ndugu zetu nchini DRC ambao wanateseka kwa sababu ya utajiri wao Mungu aliowajalia. Tusimame pamoja kuwatetea ndugu zetu Wapalestina na kukemea kwa nguvu unyama wanaofanyiwa na Israel kwa kisingizio cha kuwa Taifa teule.

Wakati mkipinga wale wanaomsema Rais, msisahau pia kupinga wale wanaowatesa ndugu zetu Wasudani sambamba na ndugu zetu wa Kamongo huko Tarime. Tujenge taifa letu kwenye misingi ile aliyoitaka Mwalimu Nyerere ya kuheshimiana na kujaliana bila kukandamizana.

Wahenga walisema, Kujikwaa sio kuanguka. Tumekosea njia, hatuna budi kujitafakari na kurudi kwenye reli. Upumbavu ni kujua unakosea njia na kuendelea kutembea mbele. Tusiwe wapumbavu!

Brayan Silayo ni mdau wa elimu kutoka Kilimanjaro, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia brayansilayo14@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts